Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Ubepari Huwatelekeza Wazee, Lakini Uislamu Huwajali

Habari:

Siku ya Ijumaa tarehe 07 Mei 2021, Raisi Samia Suluhu Hassan alihutubia wazee wa jiji la Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Wazee waliwasilisha matatizo yanayowakabili ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za afya kwao, kuchelewa kwa posho za kujikimu, kukosekana kwa sheria ya kuwalinda nk.

Maoni:

Wazee waliwasilisha changamoto zao kuu wakiwa na matumaini baada ya Raisi Samia kuahidi kuyatafutia ufumbuzi katika kipindi chake cha utawala. Utamaduni huu wa kuongea na wazee wa jiji la Dar es Salaam ulianza tangu kipindi cha awamu ya kwanza ya utawala wa Mwalimu Nyerere, lakini bado matatizo ya wazee yamezidi kuongezekea siku hadi siku bila matumaini ya kutatuliwa

Kuhusu upatikanaji wa huduma za afya kwa wazee, serikali ilikwishatoa kadi za matibabu ya bure kwao lakini inaonekana wazi kuwa bado wanapata changamoto nyingi katika huduma ya afya. Wazee walithibitisha kuwa hawapati vipimo kwa ukamilifu na madawa, na kadi za matibabu walizopewa haziwaruhusu kupata matibabu katika hospitali za rufaa na hospitali za mikoa. Waliiomba serikali kuongeza wigo wa matumizi ya kadi hizo ili waweze kupata matibabu katika hospitali zote

Wazee wa jiji la Dar es Salaam ambao wanawakilisha wazee wa nchi nzima walionesha masikitiko yao makubwa kuhusu posho za kujikimu, ambapo serikali ilijibu kuwa ipo tayari kuanza kupitia upya suala hilo, lakini kama kawaida serikali ikaja na kisingizio cha kuporomoka kwa uchumi kutokana na athari za janga la Covid-19

Kuhusu kukosekana kwa sheria ya kuwalinda wazee, serikali ilikiri kuwa Sera ya Wazee ya mwaka 2003 ndiyo sera pekee inayohusu wazee mpaka sasa, hivyo itatunga sheria kutokamana na sera hiyo ili kuboresha hifadhi kwa wazee

Hali hii haioneshi kingine zaidi ya uhalisia wa serikali za kibepari za kidemokrasia, Tanzania ikiwa miongoni mwao, kuwa haziwajali wazee. Ukitazama kwa makini utaona kuwa matatizo yote ambayo wazee waliwasilisha kwa serikali ili yapatiwe ufumbuzi, hakuna hata moja lililopata ufumbuzi inavyostahiki isipokuwa ahadi tu.

Nchi ambayo inayosemwa kuwa huru kwa miaka 60 sasa, iliyotunikiwa rasilimali nyingi sana ikiwa ni pamoja na rasilimali muhimu kama gesi asili, mafuta na madini imeshindwa hata kutoa huduma za afya bora, posho za kujikimu na usalama kwa jamii yake ndogo ya wazee wachache.

Jambo hili linaashiria ukweli wa mambo mawili: awali, ni uwepo wa ukoloni, ambapo rasilimali zilizopo haziwanufaishi walio wengi na badala yake zinaporwa na Wakoloni kupitia makampuni yao ya kikoloni kwa jina la uwekezaji.

Ukweli mwingine unaodhihirika ni namna walivyo wanasiasa chini ya serikali za kidemokrasia. Lengo lao kuu ni maslahi yao binafsi na maslahi ya mabwana zao wakoloni Wamagharibi huku wakiwatelekeza watu wao hususan wazee.

Uislamu umeamrimsha kuwajali, kuwaheshimu na kuwahurumia wazee. Ni namna ya kuonesha na kulipa fadhila kwa wazee, ni heshima, baraka na muhimu zaidi ni amri kutoka kwa Muumba, Mwenyezi Mungu (SWT).

Amesema Mtume (SAW):

«ليس منا من لم يرحمْ صغيرَنا ، ويُوَقِّرْ كبيرَنا»

 “Si katika sisi (Si Muislamu) asiyewahurumia watoto na kuheshimu wazee” (Tirmidh)

Pia Abu Mussa al-Ash`ari (ra) amesimulia kuwa Mtume (SAW) amesema:

«إِنَّ مِنْ إِجْلاَلِ اللَّهِ إِكْرَامَ ذِي الشَّيْبَةِ الْمُسْلِمِ»

“Hakika katika kumtukuza Mwenyezi Mungu kunahusu kuwaheshimu wazee Waislamu” (Abu Dawud)

Zaidi ya hayo, wanafamilia ni faradhi kuwajali na kuwatunza wazazi wao kama ambavyo Quran imesisitiza suala hili mara nyingi:

[وَقَضَى رَبُّكَ أَلاَّ تَعْبُدُوا إِلاَّ إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِنْدَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلاَهُمَا فَلاَ تَقُلْ لَهُمَا أُفٍّ وَلاَ تَنْهَرْهُمَا وَقُلْ لَهُمَا قَوْلاً كَرِيمًا * وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنْ الرَّحْمَةِ وَقُلْ رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا]

“Na Mola wako amehukumu kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili kuwafanyia wema. Kama mmoja wao akiwa mzee au wote wawili basi usiwaambie hata Ah! Wala usiwakemee, na useme nao kwa lugha ya heshima. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma na useme: Mola wangu! Wahurumie wazazi wangu wawili kama walivyonilea mimi nilipokuwa mtoto"    [TMQ 17: 23-24]

Endapo wazee watakuwa hawana watoto na ndugu wa karibu kuwalea na kuwatunza, au watoto na ndugu hao pia ni masikini basi serikali ni lazima iwahudumie kwa mahitaji yao msingi na mahitaji yao muhimu. Haya yalitokea katika kipindi chote cha utawala wa Kiislamu wa Khilafah.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.