Ijumaa, 10 Shawwal 1445 | 2024/04/19
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali

Ni Nini Kilitokea na Kinatokea Nchini Jordan?

(Imetafsiriwa)

 Swali:

"Kamati ya utetezi wa wafungwa katika kesi ya kile kinachojulikana kama "uchochezi" nchini Jordan ilielezea kutoridhika kwake na kile ilichoelezea kama hatua ya mamlaka "kuwanyimwa" haki za kimsingi ... na kuwataka waruhusiwe kukutana nao wajue uchunguzi unaofanywa nao." (London Arabi 21, 19/4/2021).

"Serikali ya Jordan ilikuwa imesema kuwa washtakiwa wote watafika mbele ya mahakama, pamoja na Mkuu wa zamani wa Mahakama ya Kifalme, Basem Awadallah, isipokuwa Mwanamfalme Hamzah, ambaye mzozo wake utasuluhishwa katika mfumo wa familia tawala ya Hashimiya ... ”(London Arabi21, 14/4/2021).

Swali ni: Je! Ni nini kilitokea na kinatokea nchini Jordan? Je! Ni jaribio la kumpindua Mfalme Abdullah II? Je! Haya ni matokeo ya mzozo wa ndani kwa ndani wa familia inayotawala, kwa sababu Mwanamfalme Hamzah ndiye kiongozi wa mtuhumiwa, au ana uhusiano wa kigeni, kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan alivyotangaza? Na asili yake ni nini?

Jibu:

Ili kufafanua ukweli wa kile kilichotokea, tunakagua yafuatayo:

1- Ingawa maafisa wa Jordan, na ipasavyo, vyombo vya habari vya Jordan na njia nyingi za setilaiti za Kiarabu, ziliepuka kuyaita matukio nchini Jordan kuwa jaribio la mapinduzi, na kuiita njama ya kudumaza usalama na utulivu wa Jordan, ingawa mazingira yote yanaonyesha jaribio la mapinduzi ambalo lilitibuliwa katika dakika za mwisho za maandalizi yake nchini Jordan. Kinachoonyesha kuwa hii ilikuwa katika nyakati za mwisho ilikuwa kupelekwa kwa vikosi vya usalama katika maeneo kadhaa ya mji mkuu, kumaanisha hofu na kutarajia harakati zinazokaribia za sekta zingine za jeshi ambazo zinapaswa kuwa waaminifu kwa majina yaliyotajwa hapo juu, haswa Mwanamfalme Hamzah. Walakini, kushindwa kutangaza kutiwa mbaroni kwa maafisa wa jeshi na kuthibitisha hili, kunaashiria kuwa jambo hilo lilikuwa likiandaliwa na kutafakari juu ya suala la wakati unaofaa wa utekelezaji. Kuzungumzia juu ya njama hii kubwa hakuwezi kufanyika bila maafisa wa jeshi.

2- Siku ya kwanza, 3/4/2021, ya matangazo haya yaliyotolewa na serikali ya Jordan, Mwanamfalme Hamzah alitangaza, kupitia video iliyorekodi habari yake, kwamba alikuwa amezuiliwa nyumbani ("Mfalme Mtarajiwa wa zamani wa Jordan, Mwanamfalme Hamzah Bin Al Hussein, alithibitisha, mnamo Jumamosi, habari za kuzuiliwa kwake na kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani, baada ya kukana rasmi hilo katika kipindi cha operesheni ya kukamatwa kwa Mkuu wa zamani wa Mahakama ya Kifalme, Basem Awadallah, na watu wengine ...” (Shirika la Anadolu, 3/4/2021)). Serikali na matangazo yake yaliaibika kumshtaki Mwanamfalme Hamzah moja kwa moja kwa kuhusika katika njama hii, ili kutodhoofisha "heshima" ya familia ya kifalme huko Jordan, na sio kuwaanika washiriki wake wakifanya njama dhidi yao, lakini siku iliyofuata, matangazo rasmi yalikuwa wazi katika kumshtaki Mwanamfalme Hamzah kwa hili:

(Naibu Waziri Mkuu wa Jordan na Waziri wa Mambo ya Nje, Ayman Safadi, alithibitisha katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo kwamba vikosi vya jeshi na Idara ya Ujasusi zilifuatilia shughuli na hatua za Mwanamfalme Hamzah, Sharif Hassan Bin Zaid na Basem Awadallah wakilenga usalama na utulivu wa Jordan. Safadi aliongezea kwamba vyombo vinavyohusika vilifuatilia mawasiliano kati ya watu waliotajwa hapo juu na vyama vya nje kuhusu wakati unaofaa zaidi wa kutekeleza mpango wa kudumaza nchi na usalama wake.” (BBC, 4/4/2021)). Inawezekana kwamba kujadili suala la "wakati unaofaa zaidi" inamaanisha kuwa suala hilo lilikuwa katika hatua ya maandalizi, lakini serikali iliogopa kuwa ilikuwa karibu, kwa hivyo iliamua kuruka na kukamata.

3- Kuhusu "vyama vya kigeni," sio jambo lililofichika, bali hutamkwa na matangazo rasmi ya Jordan, na kile kilichosemwa kwa maneno ya Waziri wa Mambo ya Nje Safadi kwamba ("uchunguzi uligundua mawasiliano ya Mwanamfalme Hamzah na pande za kigeni ya kudhoofisha usalama wa nchi"…." Walimwona mtu aliyekuwa na mawasiliano na vyombo vya usalama vya kigeni na mke wa Mwanamfalme Hamzah na wakampa nafasi ya kupata ndege ili atoke nje ya nchi, na harakati zilizotajwa hapo juu zilidhibitiwa kabisa, na usalama wa Jordan umemakinika na uko imara." (I24, 4/4/2021)). (Safadi alielezea kwamba Mkuu wa Wafanyikazi alikutana na Mwanamfalme Hamzah, na akamuomba asimamishe harakati zinazolenga usalama wa nchi, na kwamba mwanamfalme huyo alikataa kujibu ombi la kukomesha harakati hizi, na kumjibu vibaya, kulingana na usemi wa Safadi ... Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan aliendelea, akisema kwamba uchunguzi wa awali ulionyesha kwamba Mwanamfalme Hamzah alikuwa katika mawasiliano ya mara kwa mara na Mkuu wa zamani wa Mahakama ya Kifalme, Basem Awadallah, kuhusu hatua zake ...” Safadi pia alisema kuwa "tulifuatilia uingiliaji na mawasiliano na pande za kigeni kuhusu wakati unaofaa zaidi wa kuanza hatua za kuleta mtafaruku Jordan, "na kuongeza kuwa kuna juhudi za kudhibiti hali hiyo ndani ya familia ya Hashimiya, na "hakuna aliye juu ya sheria" (Al Jazeera Net, 4/4/2021), na kwa haya matangazo ya kushikwa na kuzuiliwa, ambayo hayajawekwa wazi bado, utawala wa Mfalme Abdullah II, aliyeungana na Waingereza, alikuwa karibu na jaribio la mapinduzi lililoongozwa na kaka yake, Mwanamfalme Hamzah.

4- Ama habari kuhusu ni zipi pande hizi za nje, viashiria vinaashiria uhusiano wa Amerika na matukio yanayojiri Jordan, na hii inadhihirika kutoka kwa yafuatayo:

a- Mwanamfalme Hamzah Bin Hussein, Mfalme wa zamani wa Jordan, ni mtoto wa raia wa Amerika Lisa Najib Al-Halabi, ambaye Mfalme Hussein alimuoa na kujulikana kama Noor Al Hussein. Baada ya kifo cha mumewe, Mfalme, mnamo 1999, alirudi Amerika, na alikuwa na shughuli kadhaa zilizoonyesha masilahi yake kama raia wa Amerika, ingawa hakukata uhusiano wake na Jordan na alikuwa na ikulu huko anakoishi wakati yuko Jordan. Alikuwa na ushawishi kwa Mfalme Hussein wakati, kabla ya kifo chake, alimwondoa kaka yake Hassan kutoka nafasi ya Mfalme Mtarajiwa na kumteua mtoto wake Abdullah kama Mfalme Mtarajiwa kuwa mfalme baada ya kifo chake, na kisha Hamzah akawa Mfalme Mtarajiwa mpya .. Hii ndio ilifanyika wakati Abdullah alikuwa mfalme na Hamzah akawa Mfalme Mtarajiwa mnamo 1999. Ilibainika kuwa Wamarekani walimlinda na kumsimamia na kuwasiliana naye moja kwa moja, kwa hivyo uaminifu wake kwa Amerika ulionekana. Kwa sababu hii, Abdullah II alimfukuza kaka yake Hamzah kutoka wadhifa wa Mfalme Mtarajiwa mnamo 2004, ambayo ilimfanya ajutie kupoteza nafasi ya kuwa mfalme na kumjengea roho ya kulipiza kisasi dhidi ya kaka yake. Na nafasi ya Mfalme Mtarajiwa ilibaki wazi hadi Abdullah II akamteua mtoto wake Hussein katika nafasi hii mnamo 2009. Kwa hivyo mzozo uliofichwa uliibuka ndani ya familia inayotawala. Wamarekani waliweza kununua mmoja wao kutoka ndani yake, kama ilivyotokea katika nchi za Najd na Hijaz wakati Wamarekani walipofanikiwa kumnunua Salman na mtoto wake katika familia ya Saudi, ambayo ilinyonyeshwa kutoka kwa maziwa ya Waingereza, wakalelewa mikononi mwao, na kuingia madarakani kupitia wao wakati walipoasi serikali ya Khilafah iliyoshirikishwa na Waingereza.

b- Inaonekana kana kwamba Mfalme Abdullah na Waingereza nyuma yake walikuwa wameona uhusiano mzuri wa Wamarekani na Mwanamfalme chipukizi Hamzah, haswa kupitia mama yake, Lisa "Noor", kwa hivyo mfalme alimwondoa kwenye wadhifa wa Mfalme Mtarajiwa mnamo 2004 bila kuteua badala yake, lakini kwa maana ya ufalme, mtoto wa kwanza wa mfalme ni Mfame Mtarajiwa, ambayo ilithibitishwa na amri ya kifalme mnamo 2009, na hii iliongeza hamu ya Hamzah kuleta mabadiliko ya sheria kwa mtindo wa Saudia kwa kukanyaga nyuma ya Amerika badala ya kuendelea kufuata Uingereza; kwa hivyo Hamzah alianza kufanya kazi kuunda vikundi nyumbani na nje ya nchi kwa msaada na mwongozo wa Amerika… Ni vigumu kwa mfalme kumkamata Hamzah, akiogopa kuanzisha shinikizo la Amerika juu yake, kwa hivyo ujanja wa Kiingereza ulikuwa nyuma ya kitendo ambacho kiliaibisha Amerika kutokana na kuingilia kati dhidi ya mfalme wakati alipomkamata Hamzah na kundi lake. Kitendo hiki kilikuwa makubaliano ya ulinzi ya pande zote, kwa hivyo mfalme aliyahitimisha pamoja na Amerika na akaipa kila kitu inachotaka na akachapisha katika Gazeti Rasmi hata kabla ya kuwasilishwa kwa Baraza la Wawakilishi, kama ilivyo kawaida katika makubaliano kama haya!

c- (Makubaliano hayo yalitiwa saini tarehe 31 Januari iliyopita, serikali iliidhinisha mnamo Februari 17, amri ya kifalme ilitolewa kuidhinisha ichapishwe katika Gazeti Rasmi na iweze kufanya kazi, bila kuwasilishwa Bungeni, kwa manaibu pamoja na waheshimiwa ... Chini ya makubaliano; Jordan inatoa maeneo ya kipekee kwa vikosi vya Amerika, pamoja na maeneo 15, ambayo ufikiaji wake unadhibitiwa na upande wa Amerika, na vikosi hivi vinaweza kumiliki na kubeba silaha katika eneo la Jordan wakati wa kutekeleza majukumu yao rasmi. Iliidhinisha utumiaji wa wigo wa redio na mawasiliano ya simu bila ufuatiliaji wa Jordan ... Makubaliano hayo yalisema kwamba muda wake ni miaka 15, isipokuwa utakapobatilishwa na mmoja wa pande hizo mbili kwa taarifa iliyoandikwa mwaka mmoja mapema kwa chama kingine kupitia njia za kidiplomasia ... (Arabi21, Ijumaa 19/3/2021)). Arabi21 hakutaja tarehe ya kuchapishwa katika Gazeti Rasmi ... lakini ilitajwa katika CNN kwa Kiarabu mnamo 21/3/2021: [(Serikali ya Jordan ilikuwa imeidhinisha makubaliano mnamo tarehe 17 Februari iliyopita, na amri ya kifalme ilitolewa kuidhinisha na kuchapisha uamuzi juu yake katika Gazeti Rasmi mnamo Machi 16, baada ya kutiwa saini tarehe 31 Januari iliyopita.) [Pia imenukuliwa na ammannet.com mnamo 18/3/2021: [(Mkataba wa Ushirikiano wa Ulinzi kati ya Serikali ya Ufalme wa Hashimiya wa Jordan na Serikali ya Amerika). Ambayo ilichapishwa katika Gazeti Rasmi katika Toleo Nambari 5706 la tarehe 16/3/2021 ...)] Ni wazi kutokana na hilo kwamba uharaka wa kuchapisha makubaliano katika Gazeti Rasmi, ulikuwa udharura wa ajabu!

d- Kisha serikali ilianza kumkamata (kumzuilia) Hamzah na kundi lake mnamo tarehe 3/4/2021, na ndipo makubaliano hayo yalileta aibu kwa Amerika kuingilia kati dhidi ya mfalme, mwenza wake katika makubaliano ya pamoja ya ulinzi, ambaye aliipa, kulingana na makubaliano, kile ilichotaka, hata zaidi ya kile ilichotaka! Ni kana kwamba Amerika ilitambua hili baada ya kukamatwa kwa kikundi hicho na Hamzah kuzuiliwa nyumbani kwake! Ilichelewesha taarifa yake juu ya tukio hilo hadi tarehe 7/4/2021: (Ikulu ya White House ilitangaza kuwa "Rais Biden wa Amerika amezungumza leo" 7/4/2021 "na Mfalme Abdullah II wa Jordan kuelezea msaada mkubwa wa Amerika kwa Jordan ... ( AFP 7/4/2021)), inaisaidia Jordan, sio mfalme, kwa hivyo jibu la Amerika kwa tukio hilo lilichelewa, na sauti yake inatofautiana na sauti ya jibu la Uingereza: (Uingereza ilitangaza nia yake juu ya utulivu wa serikali ya Jordan, kwa hivyo Waziri wa Kigeni wa Uingereza wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini James Clevery aliandika kwenye Twitter mnamo 4/4/2021 akisema: "Tunafuatilia kwa karibu matukio nchini Jordan ... Jordan ni mshirika anayethaminiwa sana kwa Uingereza. Tunamuunga mkono kikamilifu Mfalme Abdullah.”

e- Amerika imefichua katika magazeti yake juu ya hatua za utawala nchini Jordan. The New York Times ilisema mnamo 6/4/2021 ("Mkuu wa wafanyikazi wa Mwanamfalme Hamzah, Yasser Majali, na binamu wa Bwana Majali, Samir Majali, bado wanashikiliwa katika eneo lisilojulikana, kulingana na familia yao, ambayo inatoka kwa mmoja wa Makabila makuu ya Jordan… Lakini hali ya shauku siku ya Jumanne kuhusu alipo Majalali na mwanamfalme mwenyewe kulidokeza kuwa mivutano haikuisha kabisa.”)

Mnamo tarehe 3/4/2021, Washington Post ilikuwa ya kwanza kufichua matukio haya huko Jordan na kwamba Mwanamfalme Hamzah amezuiliwa nyumbani au gerezani. Kulazimisha mamlaka za Jordan kutangaza kinachotokea. Waziri wa Mambo ya Ndani au Waziri Mkuu hakutangaza, lakini Waziri wa Mambo ya Nje Ayman Safadi alisukumwa kutangaza hili katika mkutano na waandishi wa habari, akisema, "Idadi ya watu waliokamatwa Jumamosi (3/4/2021) ilikuwa kati ya 14 na 16, na hakuna kiongozi yeyote wa kijeshi aliyekamatwa. Harakati zilizoongozwa na Mwanamfalme Hamzah zilizingirwa na uchunguzi bado unaendelea, na kwamba kuna majaribio ya kudhoofisha Jordan, na kwamba huduma za usalama zilifuatiliwa katika kipindi cha mwisho cha mawasiliano ya duru ya karibu ya Mwanamfalme Hamzah na pande za kigeni, pamoja na upinzani wa Jordan nje ya nchi, wakiutuhumu kwa kupanga njama ya kuleta mtafaruku Jordan. Uchunguzi umekuwa ukiendelea tangu zamani, na mamlaka zilichukua hatua baada ya washukiwa kumaliza hatua ya kupanga ili kuamua wakati wa kuchukua hatua” (Shirika la Petra la Jordan , 4/4/2021).

f- Na baada ya kuzima jaribio hilo, Abdullah II alielekeza mnamo tarehe 7/4/2021 siku tano baada ya tukio hilo, akisema ("Mwanamfalme Hamzah leo yuko na familia yake katika ikulu yake chini ya uangalizi wangu, na kuhakikishia kuwa ugomvi umekoma, na kwamba Jordan yetu iko salama na imara kwa uamuzi wa watu wa Jordan na kujitolea kwa jeshi na huduma za usalama. Changamoto ya siku zilizopita hazikuwa ngumu sana au hatari zaidi kwa utulivu wa nchi yetu, lakini zilikuwa chungu zaidi, kwa sababu vikundi vya ugomvi vilikuwa ndani na nje ya nyumba yetu moja. Hakuna kitu kilichokaribia kile nilichohisi cha mshtuko, maumivu na hasira, kama kaka na mlinzi wa familia ya Hashimiya na kama kiongozi wa watu hawa. "Alitaja kwamba" Mwanamfalme Hamzah alijitolea mbele ya familia kufuata njia ya baba na babu, kuwa mwaminifu kwa ujumbe wao, na kuweka masilahi ya Jordan, katiba yake na sheria juu ya mambo mengine yoyote.”)

Hitimisho:

1- Mfalme aliweza kukwamisha mpango wa Amerika wa kuleta mabadiliko katika serikali kwa kumwondoa Mfalme Abdullah na kumchukua Hamzah badala yake, na hiyo ilikuwa kupitia makubaliano ya ulinzi wa pande zote na kuipatia Amerika kile inachotaka kutokana na unyakuzi wa ardhi ya nchi hiyo na anga. Aliiaibisha Amerika na akakomesha kuingilia kati kwao kumuunga mkono Hamzah dhidi ya mwenzake katika makubaliano, mfalme mwenyewe.

2- Inawezekana kusema kwamba utulivu katika mzozo wa Uiingereza na Amerika utatokea huko Jordan, lakini utakuwa wa muda, kwani Amerika inajiona kuwa mrithi wa ukoloni wa Uingereza katika eneo hilo, na haiwezekani kwamba Amerika itatumia makubaliano hayo kwa kusudi tofauti na kusudi ambalo Mfalme aliharakisha kulimaliza!

3- Mapambano ya kimataifa katika nchi za Kiislamu kugawanya utawala na ushawishi hayaishii isipokuwa kwa mabadiliko ya kweli, ambayo ni kuanza tena kwa maisha ya Kiislamu na kusimamishwa kwa Khilafah Rashidah yenye kuheshimu Uislamu na Waislamu na kuondoa ushawishi wa makafiri.

[وَيَقُولُونَ مَتَى هُوَ قُلْ عَسَى أَنْ يَكُونَ قَرِيباً]

“…na watasema: Lini hayo? Sema: A'saa yakawa karibu!” [Al-Isra’: 51]

7 Ramadhan Al-Mubarak 1442 H

19/4/2021 M

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu