Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Vipi Khilafah Itakavyo Unda Familia Imara

• Nguvu na utulivu wa familia ya Waislamu wakati mmoja iliwahi kuwa sifa ya kipekee ya Ummah huu wa Kiislamu. Gaston Jezz, profesa wa Kiswizi wa kanuni ya familia aliye zuru Jamhuri ya Uturuki kufuatia kuvunjwa kwa Khilafah Uthmaniya alisema kuwa utulivu wa imani za kidini katika ardhi hii, “ulizalisha nyumba za familia imara zaidi ulimwenguni, na umbile hili liliasisi maisha ya umma ambayo kamwe hayajawahi kuonekana katika historia ya taifa lolote.”

• Lakini, leo kuna mgogoro unaoathiri umoja wa familia ya Waislamu kutokana na mazingira ya maadili na sheria zisizo kuwa za Kiislamu zinazo tuzunguka sisi na jamii zetu chini ya nidhamu tunazoishi nazo kwa sasa na serikali zisizo kuwa za Kiislamu zinazo tutawala juu yetu. Nidhamu na serikali hizi zimemomonyoa vibaya ndoa, kuvuruga cheo cha mama, na kuchochea kuvunjika kwa familia kupitia sheria na sera zao haribifu.

• Hivyo basi, ili kujenga familia imara, yahitaji mabadiliko ya mizizi na matagaa ya nidhamu za kisiasa katika ardhi zetu, na mageuzi kamilifu ya msingi, maadili na sheria ndani ya mujtama zetu, kupitia kusimamisha dola inayo tambua umuhimu mkubwa wa kulinda utukufu wa ndoa, kunyanyua hadhi ya cheo cha mama na kujenga na kuhifadhi familia nzuri. Hili lapaswa kujitokeza kupitia misingi, sheria na nidhamu zake ambazo zitaileta kivitendo ruwaza hii njema katika uhalisia. Ruwaza hii kubwa yaweza kupatikana pekee kupitia dola iliyo jengwa juu ya msingi safi wa Itikadi ya Kiislamu inayo tabikisha kwa ukamilifu sheria ZOTE za Kiislamu – kwani ni Mwenyezi Mungu (swt) pekee, Mjuzi wa kila kitu, Mwenye hekima, Anayejua vizuri zaidi namna ya kupangilia mambo ya wanaume na wanawake, haki na majukumu yao katika njia itakayo leta furaha na mafanikio kwa familia na wanafamilia wake wote. Mwenyezi Mungu (swt) asema, 

إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا وَأُوْلَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴿

“Haiwi kauli ya Waumini wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumetii! Na hao ndio wenye kufanikiwa.” [An-Nur: 51]

• Dola hii iliyo jengwa kwa msingi safi wa Uislamu na inayo tabikisha imani, maadili na sheria zake zote ni Khilafah kwa njia ya Utume – Nidhamu ya Mwenyezi Mungu (swt). Uongozi huu wa Kiislamu utageuza misingi na sheria tukufu za kijamii na kifamilia za Kiislamu kutoka kwa mkusanyiko wa majukumu na hukmu zinazo fuatwa na Waislamu wachache wachamungu hadi kwa mkusanyiko wa maadili na sheria ambazo zitakuwa ndio ada ya mujtama mzima, zinazo tabanniwa na wengi miongoni mwa watu, na sheria ambayo watu binafsi wanaishi kwayo katika maisha yao ya kila siku. Hili hupatikana kupitia taasisi na nidhamu zake zinazo kuza, kutabikisha, kupigia debe, kutekeleza na kulinda maadili na sheria za familia ya Kiislamu ndani ya mujtama.   

 (1) Khilafah ambayo imejengwa juu ya msingi safi wa Uislamu, itakuza TAQWA – uchamungu – ndani ya mujtama mzima kuliko kutafuta matakwa na matamanio ya kibinafsi yenye madhara kama yanavyo pigiwa debe kupitia uhuru ulio pitiliza na usawa wa kijinsia. Taqwa ndio msitari wa mbele wa ulinzi na kiungo muhimu zaidi cha kukuza na kulinda familia imara kwa sababu ndio msukumo mkuu wa matendo mema, kutimiza majukumu ya Mwenyezi Mungu (swt), na utiifu kwa Mipaka na Sheria Zake.

Taqwa humsukuma mtu binafsi kuingiliana na jinsi ya pili kwa Haya, kujifunga kwa sheria zote za kijamii katika makutano yao nao – ima iwe hadharani, faraghani au mtandaoni, kutafuta ndoa ili kuchunga shahwa, na kujiweka mbali kutokana na kitendo chochote au hali yoyote inayo karibia haramu ili kulinda heshima yao. Ni hili ndilo linalo punguza mahusiano nje ya ndoa katika mujtama. Ni Taqwa pia ndio inayomshajiisha mtu binafsi kutafuta mwenza kwa msingi wa Dini na tabia njema ili kuifanya ndoa kuwa fungamano la usuhuba. Na ni Taqwa ndio gundi inayo gandisha pamoja familia yenye mafanikio kwani humsukuma kila mwanafamilia kutekeleza majukumu yao na haki za wengine kwa uvumilivu, uangalifu na upole na kushirikiana juu ya wema na uchamungu, kuepuka uchoyo na ubinafsi na kutenda kile kilicho bora kwa maisha yao ya ndoa na familia. Hii hujumuisha kufanya kila kilicho muhimu ili kupata utulivu katika ndoa na kuepuka talaka. Hivyo, humshajiisha mwanamume kumtendea wema mkewe, kufanya bidii kutoa mahitaji ya familia yake na kutekeleza dori yake kama msimamizi kwa mapenzi, uangalifu, upole na huruma badala ya hofu na ghasia. Humshajiisha mwanamke kuwa mtiifu kwa mumewe, kutekeleza majukumu yake ya nyumbani kuzingatia uangalifu mkubwa, wakati na umakinifu katika kuwalea watoto wake. Na huwashajiisha watoto kuwaheshimu, kuwatii na kuwachunga wazazi wao na wakubwa zao … ikijenga maisha mazuri na familia yenye utulivu.   

Khilafah hukuza Taqwa ndani ya mujtama kupitia utabikishaji wake kamili wa Uislamu. Nidhamu ya Elimu ya Khilafah kwa mfano itakuza maadili na ufahamu sahihi wa hukmu za kijamii na majukumu ya Kiislamu katika raia wake, kiasi ya kuwa mujtama kwa jumla utashikamana na sheria kupitia ukinaifu na mapenzi ya hukmu zake na kupinga tabia chafu na fisidifu kwa aina zake zote. Utekelezaji wa hukmu za Kiislamu kupitia nidhamu za kisiasa na mahakama za Khilafah zitaadhibu wale watakao kiuka mipaka ya Uislamu. Na Sera ya Vyombo vya Habari ya Khilafah itasaidia maslahi ya Uislamu, ikiwemo kupambana na fikra zozote fisidifu na kulingania kila kilicho kizuri. Magazeti, majarida, runinga, redio, mitandao ya kijamii, makongamano na mbinu nyenginezo zitatumiwa ili kufikia lengo hili. 

(2) Khilafah itaupangilia mujtama juu ya msingi wa mtazamo sahihi wa mahusiano kati ya wanaume na wanawake unaoazimia ushirikiano baina ya jinsia hizo mbili huku pia ikilinda familia. Kupitia nidhamu yake ya elimu, vyombo vyake vya habari na utabikishaji wake kamilifu na utekelezaji wa maadili na hukmu za nidhamu ya kijamii ya Kiislamu, Khilafah itauelekeza mtazamo wa jamii juu ya uhusiano kati ya wanaume na wanawake kando na kupagawa na upande wa ngono na starehe kwa kile kilicho sambamba na lengo halisi la ghariza ya kijinsia na manufaa yake kwa mujtama – ndoa na kizazi. Hii ni kuongezea kupigia debe mtazamo wa wanawake kama heshima na umuhimu wa haya na kujistiri. Hivyo basi, itaharamisha kasumba mbovu ya kuwapa sura ya ngono wanawake na mujtama au kupigia debe mahusiano yoyote machafu ima katika unadi wa bidhaa, vyombo vya habari, fasihi au mtandaoni. Pamoja na hili, Khilafah itatabanni hijabu (khimar) na jilbab kama vazi la nje la mwanamke – awe Muislamu au asiyekuwa Muislamu – ikiharamisha kuonyesha uchi au mapambo katika maisha ya nje, ikisaidia kudumisha mahusiano safi baina ya wanaume na wanawake na kulinda sitara yao.

Dola pia itakomesha uchanganyikaji huru na faragha (khulwah) kwa wanaume na wanawake ulioko leo katika mashule, vyuo, vyuo vikuu, mabaa na vilabu, na sehemu nyinginezo na majumbani na ambao aghlabu hupelekea mahusiano nje ya ndoa, badala yake kutabikisha utenganishaji wa wanaume na wanawake sana iwezekanavyo katika maisha ya nje – ima katika taasisi zake za elimu, nidhamu yake ya usafiri, makazini, mahospitali na maeneo mengine.  

“Kimsingi wanaume na wanawake hutenganishwa, na hawatangamani pamoja isipokuwa kwa ajili ya haja ambayo sheria imeiruhusu na imeruhusu kutangamana kwao ajili yake, kama vile biashara na hajj.”

Kifungu cha 113, Kielelezo cha Katiba ya Al-Khilafah cha Hizb ut Tahrir

“Hairuhusiwi kwa mwanamke kuwa peke yake na mtu asiyekuwa mahram yake. Hairuhusi kwake kuonyesha mapambo (Tabarruj) yake na uchi (‘Awrah) wake mbele ya wanaume wa kando.”

Kifungu cha 118, Kielelezo cha Katiba ya Al-Khilafah cha Hizb ut Tahrir

Pamoja na hili, Khilafah itashajiisha pakubwa na kusaidia ndoa, ikiwemo kifedha ikihitajika. Khalifah wa karne ya 8, Umar bin Abdul Aziz, kwa mfano, aliagiza mali ya dola kupewa wale waliohitaji kuoa. Fauka ya hayo, Uislamu umeweka adhabu kali ya zinaa inayo ashiria umakinifu ambao kwao Uislamu hutazama ulinzi wa ndoa na familia.

(3) Nidhamu za Khilafah zitasaidia utekelezaji wa dori za ndoa na familia za Kiislamu, na majukumu na haki za wanaume na wanawake ili kupatikane utulivu katika maisha ya ndoa na familia. Nidhamu yake ya elimu na vyombo vya habari zitajenga ufahamu safi wa hukmu za kisheria za Kiislamu ndani ya vijana na raia wake zinazo husiana na majukumu ya kibinafsi ya jinsia hizi mbili ndani ya maisha ya familia. Kwa mfano, katika masomo ya fiqh ya Kiislamu katika mtaala wake wa elimu, dola itakuza mtazamo sahihi wa majukumu na sifa za mwanamume kama msimamizi wa familia ambaye anapaswa kuwa na huruma, upole na uchungaji juu ya mkewe na watoto wake. Masomo haya pia yatajenga ufahamu wa umuhimu na majukumu ya wanawake katika dori yao msingi kama kina mama na wake pamoja na wachangiaji wakubwa wa maendeleo na ufanisi wa jamii na mujtama. Zaidi ya hayo, katika kiwango cha elimu ya shule ya upili, wanafunzi wa kike, mbali na kusoma masomo jumla kama vile thaqafa ya Kiislamu, hesabu na sayansi, watapewa vilevile chaguo la kuchukua Somo la Nyumbani litakalo wawezesha kupata taaluma katika nyanja za uangalizi na usimamizi wa watoto katika maisha ya nyumbani.  

Khilafah haitaelimisha tu raia wake hukmu zinazo husiana na maisha ya familia pekee, bali itawasaidia kivitendo katika kutekeleza dori na majukumu yao. Kwa mfano, Kifungu cha 153, cha Kielelezo cha Katiba cha dola ya Al-Khilafah cha Hizb ut Tahrir, “Dola itadhamini kazi kwa raia wake wote wanaobeba uraia wa Dola.”

Jukumu hili juu ya Khilafah limejengwa juu ya Hadith ya Mtume (saw), «وَالإِمَامُ رَاعٍ وَمَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ» “Imamu (Khalifah) ni mchungaji na ataulizwa kuhusu raia wake.” Hivyo basi, Khilafah itamsaidia kila mwanamume kutekeleza jukumu lake la kukimu mahitaji ya familia yake, ikiwemo kupeana pesa kutoka katika hazina yake, kupeana ardhi yake ya ukulima, na kuandaa mafunzo kwa wale wanao yahitaji kwa ajili ya ajira, na kuwawezesha kukimu maisha. Yote haya hupatikana kutokana na umbile sahihi la nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu inayo zalisha uchumi fanisi.  

Vilevile, Khilafah itawawezesha wanawake kutekeleza dori yao msingi kama kina mama kupitia kuhakikisha kuwa daima wanaangaliwa kifedha na kamwe hawalazimishwi kulegeza msimamo kwa majukumu yao msingi kwa watoto wao kutokana na shinikizo la kiuchumi ili kupata ajira. Hivyo basi, mahakama za Khilafah zitamsaidia mwanamke yeyote ambaye mumewe amekataa kumkimu na watoto wake, na kumlazimisha kutekeleza jukumu lake hili kwa mujibu wa uwezo wake au kukabiliwa na adhabu endapo atakataa. Maandishi kutoka katika vitabu vya sheria vya wanazuoni wa Kiislamu wakati wa Khilafah ya Abbasiya, kwa mfano, yanaeleza namna gani wanawake walikuwa wakipeleka malalamishi yao kwa makadhi dhidi ya waume waliokuwa hawawakimu kwa masrufu ya kutosha na namna makadhi hao walivyo lazimisha malipo. Katika hali ambayo mume wa mwanamke ni masikini au hana ndugu wa kiume wa kumkimu, basi ni jukumu la Khilafah kufanya hivyo, kwani Mtume (saw) amesema, (رواه مسلم) «مَنْ تَرَكَ مَالاً فَلأِهْلِهِ وَمَنْ تَرَكَ دَيْنًا أَوْ ضَيَاعًا فَإِلَيَّ وَعَلَيَّ» “Yeyote anaye acha mali ni ya jamaa zake, na yeyote anaye acha deni au wanao mtegemea ni kwangu mimi na juu yangu.” Yote haya pia yatahakikisha kuwa watu binafsi hawatashinikizwa kupanga familia zao kwa kuhofia ufukara. Bali, Khilafah itashajiisha familia kuwa na watoto wengi kwa kutambua kuwa daima watapewa mahitaji yao.

“Moja wapo ya sifa nyingine nzuri ya tabia ya Waturuki ni ukarimu na heshima yao kwa Muumba wao … mama ni mshauri; hutafutwa ushauri wake, husitiriwa, husikizwa kwa heshima na utiifu, hukirimiwa hadi mwisho wake na kukumbukwa kwa mapenzi na majonzi kaburini mwake.”

Julie Pardoe, Mwanahistoria na Msafiri wa Kiingereza wa karne ya 19, akizungumzia kuhusu hadhi ya mama chini ya Khilafah Uthmaniya katika kitabu chake ‘Mji wa Sultan na Mienendo ya Kijamii ya Waturuki mnamo 1836’

Pamoja na yote haya, nidhamu ya kimahakama ya Khilafah itacheza dori muhimu katika kudumisha umoja na utulivu wa maisha ya ndoa na familia. Kamwe haitavumilia ghasia za kinyumbani, na kuwaadhibu vikali wahalifu wake. Itasimama kama mlinzi dhidi ya ndoa za lazima na kukabiliana vikali na vitendo vyovyote na mitazamo yoyote mengine ya kitamaduni isiyo kuwa ya Kiislamu inayo dhuru familia. Na itahudumu kama mwamuzi muhimu katika kutatua barabara na kwa haraka mizozo ya kindoa na familia ili kuzuia kukua kwa matatizo – kupitia kuhakikisha ufikiaji haki ni wa haraka, adilifu na huru. 

• Hivyo basi, Khilafah itahudumu kama ngome halisi ya familia, ikiimarisha na kuilinda kutoka pembe zote. Hii ndio sababu mwanachuoni maarufu Imam Ghazali (RM) alisema, “Dini ndio msingi na Sultan ndiye mlinzi. Kitu kisicho kuwa na msingi huporomoka na kitu kisicho kuwa na mlinzi hupotea.” 

ثُمَّ جَعَلْنَاكَ عَلَى شَرِيعَةٍ مِّنَ الْأَمْرِ فَاتَّبِعْهَا وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاء الَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ﴿

“Kisha tukakuweka wewe juu ya Sheria ya mambo yao, basi ifuate, wala usifuate matamanio ya wasio jua kitu.” [Al-Jathiya: 18]

Imeandika kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Dkt. Nazreen Nawaz
Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 12 Aprili 2020 07:43
Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.