Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa

Amiri wa Hizb ut Tahrir

Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Katika Ukurasa Wake wa Facebook

Jibu la Swali:

Yeyote anayepata Rikaz (Hazina Iliyozikwa) Khumusi Moja Inapaswa Kutolewa

Kwa: Abu Ahmad

(Imetafsiriwa)

Swali:

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimshukie bwana wetu Ahmad. Assalam Alaikum Wa Rahmatullah Wa Barakatuh. Ninatoka Palestina, na wapo wanaotafuta madini ya thamani katika ardhi ya wengine. Lau atapata faini za Uthmaniya ambazo zilifichwa na Utawala wa Uthmaniya mwaka 1916 na hawezi kuzirudisha kwa Waturuki sasa, basi je ni mwenye kupata mali akipata ana fungu au ni mwenye ardhi pekee - ujira wa kuhifadhi hazina hiyo katika ardhi yake? Je, ile mali ambayo asili yake ni milki ya dola serikali, itapeanwa yote kwa maskini, au ni khumusi pekee? Nawashukuru, Mwenyezi Mungu akunusuruni na akulindeni nyinyi na wenye ikhlasi.

Jibu:

Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuh.

Tayari tumejibu swali kama hilo zaidi ya mara moja, na nitakunukulia kutoka kwake:

1- Kutoka kwa Jibu la Swali 8/11/2013:

(…Ama sehemu ya pili ya swali kuhusu Al-Rikaz (hazina zilizozikwa, yeyote atakayeipata Rikaz (hazina iliyozikwa), khumusi moja yake lazima ikabidhiwe kwa Dola ya Kiislamu ili kuiweka kwa maslahi ya Waislamu, na khumusi nyengine nne ni kwa wale wanaoipata, mradi tu mawe ya madini hayo hayapatikani katika ardhi ya mtu mwingine.

Lakini kama dola ya Kiislamu haipo kama ilivyo leo, basi yule anayeipata Al-Rikaz anatoa khumusi moja kwa ajili ya masikini na mafukara na maslahi ya Waislamu... na kutafuta haki ya hayo, na inayobaki ni yake.

Ushahidi wa hilo ni:

A- Al-Rikaz ni mali iliyozikwa chini ya ardhi iwe dhahabu, fedha, vito, lulu au silaha. Hizi zinaweza kuwa hazina za watu wa kale kama Wamisri, Wababiloni, Waashuri, Wasasani (Waajemi), Warumi au Wagiriki na ni pamoja na pesa, sarafu, vito na johari zilizowekwa kwenye makaburi ya wafalme na viongozi wao au hata mabaki ya miji yao ya zamani ambayo imeangamizwa. Vile vile inatumika kwa sarafu zao za dhahabu au fedha zilizowekwa kwenye jagi na vyombo vingine vilivyofichwa ardhini kuanzia siku za kijahiliya au zama za Kiislamu zilizopita. Hizi pia huchukuliwa kuwa hazina zilizofichwa, kama vile vitu vingine vilivyotajwa. Al-Rikaz inatokana na Rakaza, Yarkazu kama Gharaza, Yaghruzu yaani ‘inapofichwa’, hivyo unaweza kusema: ‘Rakaza’ mkuki unapopandwa ardhini. Kutokana na hili imechukuliwa ar-Rikz, ambayo ni sauti iliyofichwa. Amesema Mwenyezi Mungu Ta’ala:

[أَوْ تَسْمَعُ لَهُمْ رِكْزاً]

“...au kusikia hata minong'ono (rikz) kutoka kwao?” [Maryam: 98].

Ama madini (Al-m’adin), ni vile Mwenyezi Mungu (swt) alivyoviumba katika ardhi Siku alipoziumba mbingu na ardhi au dhahabu, fedha, shaba, risasi na vitu vinavyofanana na hivyo. Al-m’adin inatokana na ‘Adana (mahali), Ya’adanu anapokaa humo, na kutoka kwalo neno Bustani ya Eden linatokana na kwa kuwa ni mahali pa kuishi na milele. Madini ni ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu na hayakuzikwa na mwanadamu na kwa hivyo ni tofauti na hazina, ama ya pili imezikwa na mwanadamu.

B- Kanuni (qaidah) kuhusu hazina na madini ni ile iliyopokelewa na Abu Huraira kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: «العجماءُ جرحها جُبار، وفي الركاز الخمس» “Kuhusu mnyama aliyejeruhiwa hakuna fidia wala adhabu (Qisas) na katika hazina yake khumusi inadaiwa.” Pia kile kilichopokewa na Abdullah bin Amr kwamba Mtume aliulizwa mali iliyopatikana katika sehemu ya kale sana iliyoharibika na akasema: «فيه وفي الركاز الخمس» “Humo na katika hazina iliyozikwa ni khumusi.” Na pia kile kilichopokewa kutoka kwa Ali bin Abi Talib kwamba Mtume amesema: ««وفي السيوب الخمس. قال: والسيوب عروق الذهب والفضة التي تحت الأرض» “Na katika Suyyub ni khumusi. Akasema: Suyyub ni mishipa ya dhahabu na fedha iliyozikwa chini ya ardhi.” Haya yametajwa na Ibn Qudamah katika al-Mughni.

C- Kwa hiyo, mali yoyote ya dhahabu, fedha, vito, johari na mfano wa hayo, kuzikwa na kupatikana katika makaburi, magofu, miji ya watu wa kale, ardhi isiyolimwa, magofu ya kale sana, kama walivyoandikiwa watu wa Adi, sawa na hazina za Siku za Ujahiliya au zile za Waislamu katika zama za Kiislamu zilizopita, huwa ni mali ya mtafutaji wake ambaye anatoa khumusi kwa Bait ul-Mal. Kwa hivyo, kiasi kidogo, kisichoendelea (si I'id), cha kiwango kidogo cha madini, dhahabu au fedha iwe kwenye mishipa au kama chuma ghafi kwenye ardhi isiyolimwa isiyo ya mtu yeyote, ni mali ya mpataji ambaye hutoa khumusi yake kwa Bait ul-Mal. Lakini ikiwa ni endelevu (I’id) yaani, mgodi na sio kiasi kidogo cha kuzikwa, inachukua hukmu ya mali ya umma, ambayo ina maelezo mengine.

Khumusi iliyochukuliwa kutoka kwa mpata hazina na madini inachukuliwa kuwa ngawira (Fai’) na inachukua hukmu yake. Inawekwa kwenye Bait ul-Mal katika idara ya Fai’ na Kharaj na inatumika kwa njia sawa na Fai’ na Kharaj. Mas’ala yake yamekabidhiwa kwa Khalifah kuyatumia katika kuchunga mambo ya Ummah na kutimiza maslahi yake kwa mujibu wa mtazamo wake na Ijtihad ya lililo jema na lenye manufaa.

D- Atakayepata hazina au madini katika mali yake, iwe ardhi au majengo, basi anamiliki, sawa sawa iwe amerithi ardhi hii na jengo au kanunua kwa mtu mwingine. Atakayepata hazina au madini katika ardhi au jengo la mtu mwingine, basi hazina au madini yanayopatikana ni ya mwenye ardhi au jengo na si ya mpataji wake.

5 Muharram 1435 H sawia na 11/8/2013 M) Mwisho wa jibu la swali.

2- Kutoka kwa Jibu la Swali 18/9/2014:

(...Imepokewa na Al-Bukhari na Muslim kutoka kwa Ibn Shihab, kutoka kwa Said Ibn Al-Musayyib, kutoka kwa Abi Salamah bin Abdul Rahman, kutoka kwa Abu Hurairah (ra): Kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: «وَفِي الرِّكَازِ الخُمُسُ» “(Chukua) kutoka kwenye Rikaz (hazina iliyozikwa) khumusi (kiasi).”

Rikaz ni hazina za kale zilizozikwa chini ya ardhi au vyombo vya madini ya kiasi kidogo ... ikiwa imegunduliwa na mtu katika mali yake, iwe ardhi au jengo, itakuwa ya mgunduzi, lakini ikiwa Rikaz au chuma kitapatikana katika ardhi au jengo la mtu mwingine, Rikaz au chuma kitakuwa cha mwenye mali na sio mpataji wa Rikaz au chuma... khumusi ya kiasi cha Rikaz inalazimika kulipwa wakati inapogunduliwa kwa Bait ul-Mal na ni haramu kuchelewesha.

Ama iwapo khumusi (ya Rikaz) ni Zaka au Fai' (ngawira) yaani "mali ya dola", jibu ni kuwa sio zaka bali ni Fai', na kutokana na dalili za hili ni kile kilichopokelewa na Abu Ubaid kutoka kwa Mujalid kutoka kwa As-Sha'bi kwamba:

“Mtu mmoja alipata Dinari 1,000 zimezikwa mahali nje ya Madina hivyo akaja nazo kwa Umar bin Al-Khattab ambaye alichukua khumusi, Dinari 200, na akazirudisha zilizobaki kwa mtu huyo.’ Umar akaanza kugawanya zile 200 miongoni mwa Waislamu waliokuwa mbele mpaka zikabaki ziada.’ Umar akasema: ‘Yuko wapi mwenye Dinari?’ Kwa hiyo, alisimama mbele yake na Umar akamwambia: ‘Chukua Dinari hizi. Ni zako.”

Kutokana na Hadith ya As-Sha'bi, ni wazi kwamba kiasi kilichochukuliwa na Umar (ra) kutoka katika Rikaz nzima ni khumusi moja tu, na khumusi nne zilizobaki zilirudishwa kwa mpataji Rikaz; hii khumusi haikuwa Zaka, bali ilizingatiwa kuwa ni Fai', kwa sababu lau ingekuwa Zaka ingelitolewa kwa wale wanaostahiki Zaka, na Umar (ra) asingempa mwenye kuipata Rikaz kwa sababu alikuwa tajiri, na Zaka haitolewi kwa matajiri.

Hii ndiyo sababu kiasi chochote cha Rikaz kitakavyokuwa, khumusi nne yake anapewa mpataji wake na khumusi moja inapewa Bait ul-Mal. Hili halina sharti kwa Nisab kwa sababu si Zaka, sawa iwe kiasi cha Rikaz kimefikia Nisab au la, khumusi yake inalipwa kwa Bait ul-Mal ya Waislamu. Hivi sasa Waislamu hawana Bait ul-Mal, hivyo mwenye kuipata Rikaz anaweza kulipa khumusi hiyo kwa yale ambayo yanawanufaisha Waislamu au masikini miongoni mwao... anafanya anachoona bora zaidi. 23 Dhul Qi’dah 1435 H sawia na 18/9/2014 M). Mwisho wa jibu la swali.

Na katika hayo yatosheleza, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yote na Mwenye hikima.

Ndugu Yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

19 Safar Al-Khair 1444 H

15/9/2022 M

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.