Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali

Matokeo ya vita vya Urusi nchini Ukraine

(Imetafsiriwa)

Swali:

France 24 iliripoti mnamo Oktoba mosi 2022 kwamba: (Msemaji wa jeshi la Ukraine alitangaza kuingia kwa majeshi yake katika mji wa Lyman mashariki mwa nchi hiyo. (eneo la Donetsk) baada ya kuhusuru vikosi vya Urusi...). Raisi wa Urusi Putin alikuwa ameamuru Jumatatu “uhamasisho wa kwanza katika nchi yake” tangu vita vya pili vya ulimwengu, baada ya pingamizi katika uwanja wa vita Ukraine... (Euronews 21/9/2022). Haya yalikuja baada ya jibu la pigo wakati Ukraine ilimiliki tena maeneo ambayo Urusi ilikuwa imeyachukua: (Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine alisema mnamo siku ya jumapili katika kauli kwa  Idhaa ya Al-Hurra kwamba Ukraine ilimiliki tena kilomita elfu kumi mraba ambazo Urusi ilikuwa imechukua mashariki mwa Ukraine... alielezea kwamba Kiev ilipokea msaada mkubwa kwa nchi za Kimagharibi na walifaulu kurudisha pigo katika mashariki...(Al Balad, Jumapili 18/9/2022).

Swali ni: je, Urusi ni dhaifu kijeshi? Ama msaada wa kivita kutoka Magharibi umekuwa maradufu? Je, uhamasisho nusu wa wanajeshi wa akiba utabadilisha mambo? Na nini umuhimu wa utekaji na uambatisho wa Urusi wa maeneo manne ya Ukraine, hata kama Ukraine ilimiliki tena Lyman siku iliyofuata, ambayo ni sehemu yake? Je, Urusi yaweza jitoa katika mpango wake wa utekaji?

Jibu:

Ili kufahamu haya matukio mapya na kujua undani wake na matokeo, ni lazima isisitizwe kwamba vita vikuu ndio njia ya haraka na yenye dhamana ya kubadilisha usawa wa sasa wa nguvu, kama ilivyokuwa katika historia, na kwa kufuatilia kukua kwa vita nchini Ukraine inakuwa dhahiri kwamba:

1- Urusi haikuanza vita nchini Ukraine ili kulinda watu wanaozungumza kirusi katika eneo la Donbas, hata kama ilisingiziwa hivyo, lakini pia iliwasha moto vita hivyo ili kuimarisha nafasi ya Urusi kimataifa. Ilipokaribia kuanza vita, Urusi ilitaka dhamana za kiusalama kutoka Ulaya, Marekani na NATO, na dhamana hizo zilihusisha kutojiunga kwa Ukraine katika NATO. Haya malengo ya Urusi yaliyotokea baada ya kile Warusi wanakichukulia kuwa ni dhulma za Kimagharibi dhidi ya Urusi na maonevu katika nafasi yake ya kimataifa kama dola ya kinyuklia ya daraja la kwanza yalidhihirika katika kauli zake zilizotolewa na Moscow kabla ya vita. Haya yamehakikishwa na msisitizo wa Moscow katika hizo dhamana na kwamba Marekani na Magharibi walizitoa kimaandishi. Kwa hivyo, na haya ni muhimu sana, Marekani, ikifuatwa na Ulaya, zimechukulia vita ya Urusi kuwa ni uasi dhidi ya mfumo wa kilimwengu na sio madai ya ardhi pekee kutoka Ukraine ama katika ulinzi wa Warusi katika mashariki mwa Ukraine. Nafasi ya Marekani na Magharibi ilikuwa ni tofauti sana katika nafasi sawa na ya 2014 wakati Urusi iliiunganisha Crimea, yaani, ilikuwa katika kiwango cha kuamiliana na nchi kuu iliyo asi mfumo wa kimataifa wa Kimagharibi, unaoongozwa na Marekani pekee.

2- Kwa hivyo, jibu la Marekani na Ulaya lilikuwa kali dhidi ya Urusi, na Urusi haikutarajia hivyo... kwa hivyo Mrekani na Ulaya zikaiwekea Urusi vikwazo vizito katika historia, na kudhibiti mali ya Urusi ugenini, na nchi hizo zikakata uhusiano na Urusi licha ya hitajio kubwa la Ulaya la mafuta na gesi ya Urusi. Ulaya, hasa Ujerumani, ilianza kujiandaa kivita tena na Marekani na Ulaya zikaanza kutoa msaada mkubwa wa kijeshi kuelekea Ukraine.  Na kwa kutokea kwa vita vya Urusi, Marekani ilionyesha uongozi wake kwa Magharibi kwa uwazi na dhahiri baada ya kutiliwa shaka wakati wa raisi aliyeondoka Trump. Marekani ilijaza nafasi katika mahusiano yake na wendani wake. Kwa sababu ya uhalisia wa nguvu za Urusi ambazo ziliisukuma Moscow mbele zilikuwa sio za wazi mwanzoni mwa vita kama zilivyo wazi leo, zaidi ya nusu ya mwaka baada ya kuingia kwake Ukraine, Marekani ilianza kutoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine polepole na ikawa inatazama athari yake kwa Moscow, na muda ulivyopita, mistari mekundu ya Urusi ikaanza kuanguka na Marekani na wendani wake wakavunja mistari mekundu ya Urusi. Kisha ikaivuka kwa zaidi bila ya Urusi kuweza kuzuia, na kuvunja hii mistari ilikuwa ni kutoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine na kuuongeza kwa idadi na ubora, kutoka kujilinda na kwenda kuhujumu... ndivyo, baada ya Marekani kutohamasisha Ukraine kuhujumu Urusi katika Crimea, ikaanza kuihamasisha.

3- Na kwa ujinga wake wa kimkakati, Urusi ilikimbia kiholela kuteka ardhi ya Ukraine, na kwa sababu ya kuhisi kuwa na nguvu kuliko Ukraine, ilikimbilia ndani kuelekea mji mkuu, Kiev, na ikafeli kuuteka na kurudi Donbas. Lakini huku kurudi nyuma kulionyesha udhaifu mkubwa wa jeshi la Urusi. Urusi haikutumia ndege zake na haikudhibiti njia za hewa za Ukraine, na haikutoa msaada wa kimpangilio kwa wanajeshi wake, na kustaajabishwa na ukubwa wa upinzani wa Ukraine, kinyume na upelelezi wake ulivyokuwa unatarajia. Kwa hivyo, udhaifu mkubwa wa jeshi la Urusi ulionekana na kuunda matumaini makubwa Washington kwa kushindwa kwake nchini Ukraine. Ilionekana kuwa kauli za raisi wa Urusi Putin kuhusu nguvu za Urusi hazikuendana na matokea mabaya katika uwanja wa jeshi lake. Kwa sababu ya athari ya udhaifu uliofichuka uwanjani, balozi za ugenini zilirudi Kiev baada ya kuwa zimefungwa, na maafisa wa Kimagharibi wakaingia kwa wingi katika mji mkuu wa Ukraine mmoja baada ya mwengine.

4- Marekani ilianza kutangaza malengo ya msaada wa kivita kwa Ukraine, na tangazo hili la malengo ya Marekani likawa na kishindo kikuu kwa Moscow. Marekani ilikusanya habari za kipelelezi za Uwanjani kupitia setilaiti kwa Ukraine na kuipatia Ukraine nasaha za kijeshi. Hata mnadhimu mkuu wa jeshi la Marekani alisema kwamba anampigia mwenzake wa Ukraine mara saba kwa wiki (Al-Jazeera, Septemba 2022), na kwa vyovyote vile Marekani inachukulia vita vya Ukraine kuwa ni vita vyake, bila ya kujihusisha moja kwa moja. Kweli, Marekani ilitangaza kwamba kwa wiki inatoa msaada zaidi kwa Ukraine kwa mabilioni ya dolari. Ikimaanisha kwamba Amerika imedhamiria kuishinda Urusi huko Ukraine na kuiondoa kwenye orodha ya nchi kuu, na hili ndilo ambalo Urusi inatambua sasa, lakini imechelewa!

5- Miongoni mwa viashiria vya udhaifu wa kimikakati wa Urusi vilivyofichuliwa ni kwamba iliendelea kusambaza mafuta na gesi barani Ulaya katika kipindi cha miezi sita ya vita hivyo, ingawa Ulaya ilitangaza wazi kuwa iko njiani kuachana na uagizaji wa mafuta na gesi kutoka Urusi. Ikimaanisha kuwa haikuanzisha kukata mafuta na gesi kutoka kwa nchi zinazotangaza uadui wao kwake asubuhi na usiku. Hii inaashiria uzito wa uhitaji wa pesa wa Moscow, licha ya kujigamba kuwa uchumi wake haukuathiriwa na vikwazo vya Magharibi na kwamba ruble ni thabiti mbele ya vikwazo! Na ikiwa Urusi ilikuwa imekata kabisa laini ya usambazaji wa gesi ya Nord Stream 1 mapema Septemba 2022 kabla ya milipuko, lakini hilo lilikuja kwa kuchelewa sana, na imekuwa ikitangaza kuwa ni muuzaji wa kutegemewa wa nishati, kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine, njia zingine za usambazaji wa gesi kwenda Ulaya, kama vile njia ya mapito ya Yamal inayopitia Poland, Progress na Soyuz zinazovuka Ukraine, na bomba la Turk Stream linalopitia Uturuki bado zinafanya kazi na kulisha Ulaya kwa gesi, isipokuwa matawi ambayo yalikatwa na Poland na Ukraine na sio Urusi. Uhitaji wa pesa wa Urusi umeifanya kupoteza heshima yake katika medani ya kimataifa. Hii inapingana na juhudi zake kabla ya vita ili kuimarisha msimamo wake wa kimataifa!

6- Zaidi ya hayo, Urusi ilishangazwa na misimamo ya hivi karibuni ya China iliyojitokeza wakati wa Mkutano wa Samarkand wa viongozi wa Shirika la Shanghai, ambao ulifanyika katikati ya Septemba 2022 yaani, muda mfupi baada ya kushindwa kwa Urusi huko Kharkov. Misimamo hiyo ambayo rais wa Urusi mwenyewe alifichua alipoeleza uelewa wake wa "hofu na wasiwasi wa China." Kutokana na vita vya Ukraine, na (Putin alisema - katika mkutano wake wa kwanza na mwenzake wa China tangu kuanza kwa vita vya Urusi huko Ukraine - kwamba Urusi inathamini msimamo wa "usawa" wa China juu ya mgogoro wa Ukraine. (Al Jazeera Net, 15/9/2022). Kwa hivyo, ikawa wazi kwa Urusi kwamba msimamo wa China, ambayo ilitia pamoja saini ya makubaliano ya ushirikiano "kwa kiwango kamili" kabla ya vita huko Ukraine, umekuwa "usawa", ambayo ni, haiko pamoja na Urusi wala Ukraine na Magharibi. Kwa hakika, China ilijiepusha hata kutaja jina la "Ukraine" katika taarifa zake za pamoja na Urusi kwenye Mkutano wa Shanghai na katika taarifa za rais wake lakini ilidokeza tu hilo. Hakuna shaka yoyote kwamba Marekani inaionyesha China hatari ya msaada wowote kwa Urusi katika vita vyake huko Ukraine, ambayo bila shaka ni jambo ambalo China ilijibu, ikihofia biashara yake ya kimataifa ... Kwa hivyo, haikuunga mkono Urusi dhidi ya azimio la Baraza la Usalama ambalo lilishutumu kutekwa kwa maeneo manne nchini Ukraine. Mnamo tarehe 1/10/2022, France 24 ilichapisha yafuatayo: (Mnamo Ijumaa, Urusi ilitumia kura yake ya turufu kuzuia kupitishwa kwa rasimu ya azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inayo laani unyakuzi wake wa maeneo manne ya Ukraine... Rasimu ya azimio iliyoandaliwa na Marekani na Albania iliungwa mkono na nchi wanachama kumi tofauti na nchi nne zilizojizuia: China, India, Brazil, Gabon...)

7- Kwa kuzingatia yote yaliyotajwa, shambulizi la Urusi dhidi ya Ukraine, ambalo halikufanikiwa kwa Ukraine kusalimu amri kwa masharti ya Urusi, linafichua udhaifu mkubwa wa kijeshi wa Urusi, na kufichua uungwaji mkono wa hali ya juu na mkubwa wa kijeshi kutoka Marekani na Magharibi hadi Ukraine, baadhi yake ni dhahiri na mwengine umefichwa, na kwa sababu Urusi imeona mambo haya mapya ambayo haikutarajia kabla ya vita, Lavrov alikumbusha mnamo tarehe 12/9/2022 kwamba Urusi haikatai mazungumzo na Ukraine (Al-Jazeera, 12/ 9/2022), lakini anatambua kuwa masharti ya kujisalimisha kwa Warusi ambayo yaliwekwa kwenye meza ya Ukraine katika siku za kwanza za vita yameyeyuka. Hakuna matumaini ya kurejesha hali hizo za Urusi isipokuwa kwa matumizi ya Urusi ya silaha za nyuklia, ambayo labda ni kadi ya mwisho ya Urusi, lakini pia inajua kwamba matumizi ya silaha za nyuklia yataipeleka Marekani vitani kwa njia moja au nyingine, na  inashindwa kupata ushindi katika vita vyake na jeshi la Ukraine, ambalo hupokea misaada ya Marekani, kwa hivyo inawezaje kufanikiwa ikiwa jeshi la Marekani litashiriki katika vita. Hii ndio sababu Urusi baada ya shambulizi la Ukraine iko katika hali ngumu.

8- Urusi ilitambua hatari hizi zote, na rais wake alionyesha kukataa kushindwa (Rais wa Urusi Vladimir Putin alitangaza uhamasishaji wa sehemu ya jeshi, akimaanisha hatari  ya nchi yake kwa vitisho vya nyuklia. (Al Jazeera Net, 21/9/2022), kama na vile vile (wawakilishi wa mikoa ya Lugansk, Donetsk, Kherson na Zaporizhzhia inayoungwa mkono na Urusi, wametangaza nia yao ya kuandaa kura ya maoni ya kujiunga na Urusi kuanzia Septemba 23 hadi 27. (Shirika la Anadolu la Uturuki, 21/9/2022). Hakika, kura ya maoni ilifanyika na uunganishaji ukatokea. Al Jazeera Net ilichapisha mnamo tarehe 30/9/2022 yafuatayo: (Rais wa Urusi Putin alitangaza kwamba mikoa ya Ukraine ya Lugansk, Donetsk, Zaporizhzhia na Kherson imekuwa ya Urusi. Pia amelaani katika hotuba yake ndefu kile alichokiita udhibiti wa nchi za Magharibi juu ya mfumo wa dunia, wakati Rais wa Ukraine Zelensky alipothibitisha kuwa nchi yake imechukua "hatua madhubuti" kujibu hatua ya Urusi). Licha ya hayo, jeshi la Ukraine liliendelea na harakati zake za kijeshi ndani ya maeneo haya manne... Imesemwa katika tovuti ya France 24 mnamo tarehe 01/10/2022: (Msemaji wa jeshi la Ukraine alitangaza kuingia kwa vikosi vyake katika mji wa mashariki wa Lyman baada ya kuzingira vikosi vya Urusi karibu na ngome muhimu sana ya Moscow. Huku Urusi ikithibitisha kuwa maelfu ya watu walijiondoa katika mji huo huku kukiwa na muendelezo wa mapigano. Huu ni wakati ambapo Moscow inaendelea kuimarika kisiasa baada ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kuidhinisha mnamo Ijumaa kutwaliwa kwa mikoa minne ya Ukraine... Wizara ya Ulinzi ya Ukraine iliandika kwenye Twitter (vikosi vya mashambulizi ya anga vya Ukraine vinaingia Lyman katika mkoa wa Donetsk). Muda mfupi kabla ya hapo, jeshi la Ukraine lilisema kuwa lilikuwa likizingira maelfu ya wanajeshi wa Urusi katika mji huu ulioko katika mkoa wa Donetsk, ambao ulitwaliwa na Urusi mnamo Ijumaa).

9-Uchunguzi wa karibu wa misimamo hii ya Urusi, baada ya yote yaliyotokea, unaonyesha yafuatayo:

a- Kama vile mawazo ya Warusi katika historia yote, Urusi inaangalia faida za ardhi na inataka kuzihifadhi kwa gharama yoyote. Kwa hivyo, inaendesha kura za maoni katika maeneo ambayo iliyadhibiti kwa ujumla au kwa sehemu ili kuyaambatanisha na Urusi, na kufanya hili kuwa sawa. Kwa maana kwamba Urusi inataka kusema kwamba maeneo haya mapya (Lugansk, Donetsk, Zaporizhzhia na Kherson) yamekuwa maeneo ya Urusi na kwamba shambulizi dhidi yao ni shambulizi kwa Urusi, na kwamba hii inaweza kuhitaji ulinzi wao kwa kutumia silaha za nyuklia kulingana na mahitaji ya kile Urusi inachokiita "kanuni yake ya kijeshi-nyuklia", yaani, inataka kuitisha Amerika na nchi za Ulaya na kuzionya hatari ya kuunga mkono jeshi la Ukraine kushambulia ardhi za Urusi na kutishia jeshi lenyewe la Ukraine. Haya yote yanaashiria udhaifu wa jeshi la Urusi na kwamba linakimbilia vitisho vya kutumia silaha za nyuklia baada ya kutokuwa na uwezo wa kushinda nchini Ukraine, licha ya kile kinachoonekana kama makubaliano ya kimataifa ya kupiga marufuku matumizi yao katika vita.

b- Tangazo la uhamasishaji wa jumla wa kuandikisha wanajeshi 300,000 kutoka kwa hifadhi, na idadi kubwa zaidi inaweza kuajiriwa, ambayo yote yanaonyesha kwa njia isiyo ya moja kwa moja udhaifu wa jeshi la Urusi na kwamba haliwezi kufikia malengo ya Urusi huko Ukraine, na kwamba hasara kubwa za kibinadamu zilizopatikana ziliifanya kuhitaji akiba. Hata hivyo Urusi bado inajigamba kuwa haipigani vita bali ni operesheni maalum ya kijeshi.

10- Uwezekano mkubwa zaidi wa vita nchini Ukraine vimeingia katika hatua inayozidi kuzungukwa na hatari kubwa. Ikiwa Urusi inataka kuregesha heshima yake, itachoma kila kitu nchini Ukraine katika siku zijazo, ikiwa ina uwezo na nia ya kufanya hivyo, viashiria vingi vinaonyesha kupungua kwa uwezo wake na kwamba  kudura yake imepungua. Urusi imechelewa kutambua kwamba kwa namna moja au nyingine inaikabili Amerika na nchi za Ulaya katika uwanja wa Ukraine, ingawa nchi za Ulaya zinafungua mlango mdogo kwa Urusi, tofauti na Amerika ambayo iliipa mgongo Urusi. Ulaya inapanga kuachana na mafuta ya Urusi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, na baada ya hapo gesi yake, yote haya yanazifanya nchi za Ulaya kuwa na fujo zaidi katika kukabiliana na Urusi, na hii inaonekana kutokana na kukithiri kwa matamshi ya Wajerumani dhidi ya Urusi na kuzidi kuimarika kwa silaha za Ujerumani. Urusi ilitaka kura za maoni za mikoa ya Ukraine zijiunge na Urusi ili kufanya mafanikio ya Urusi katika maeneo haya kuwa jambo lililofanywa na kuhitimishwa kwa kila mtu, na kuweka utata wa matumizi ya silaha za nyuklia kulinda maeneo haya, lakini nchi za Magharibi zilikataa kura hizi za maoni na kutangaza kuwa zingeendelea kuunga mkono Ukraine kijeshi, na hata kutoa mifumo ya ulinzi ambayo ni ya juu zaidi ya jeshi la anga kwa Ukraine, na hapa hali ya Urusi ilizidi kuwa ngumu zaidi.

11- Kuhusu suala la kutangaza uhamasishaji, kwa mujibu wa wataalamu wa kijeshi, suala la kuhamasisha na kuleta askari wa akiba ambao hawajapata mafunzo halitanufaisha sana jeshi la Urusi. Suala la udhaifu wa jeshi la Urusi ni kubwa zaidi kuliko kusaidiwa na kuongezeka kwa idadi. Ni shida ya uongozi na shida ya vifaa ambavyo havipatikani leo huko Urusi, ingawa Urusi inaendesha viwanda vyake vya kijeshi na vya uzalishaji wa aina mbili kwa jeshi lenye uwezo wa juu kana kwamba iko kwenye vita vya ulimwengu, lakini hii haitakuwa na uwezo wa uamuzi kwa sababu Amerika na nchi za Ulaya zinaipatia Ukraine kile ambacho jeshi lake linahitaji pia, na ikiwa hasara kubwa ya jeshi la Urusi itaendelea huko Ukraine, shinikizo kubwa litawekwa kwa Kremlin kutoka ndani ya Urusi kusimamisha vita. Shinikizo hili litaongezwa na milipuko ya laini za mkondo wa Nord wa Urusi katika Bahari ya Baltiki na usumbufu unaosababishwa na matumaini ya Ulaya ya gesi asilia ya bei nafuu ya Urusi. Na haya yote yanaifanya Urusi kukabili uhasama mkubwa zaidi wa Ulaya, ambao ni ongezeko la uungaji mkono kwa jeshi la Ukraine na kudhoofika kwa sauti za Ulaya zinazotaka maridhiano na Urusi ili kupata gesi ya bei rahisi. Hii ni pamoja na kushuka kwa misimamo ya Wachina, na hivyo hisia za Urusi kuwa iko peke yake katika uwanja wa makabiliano na Amerika na Magharibi kuongezeka, ikimaanisha kuwa China imeiacha kwa kiasi kikubwa. Haya yote yanaibua ukosoaji mkubwa wa ndani wa viongozi wa Kremlin kwamba hesabu zao hazikuwa sawa, ambayo ni kwamba, watalaumiwa kwa hali ngumu mpya ya Urusi.

12- Kuhusu vitisho vya nyuklia vya Urusi, kwanza vinakosa utashi halisi, kwani ujasusi wa Magharibi haukugundua harakati zozote mpya za vikosi vya nyuklia vya Urusi, ambayo huongeza imani ya Wamagharibi kwamba vitisho hivi vya Putin viko karibu na vitisho kuliko matumizi halisi ya silaha za nyuklia. Na kwa sababu Amerika na nchi za Ulaya hazikuonyesha kuogopa silaha za nyuklia za Urusi, ingawa walisema kwamba wanachukulia vitisho hivi kwa uzito, haswa kwa vile kinachomaanishwa mara nyingi ni uwanja wa Ukraine na sio Magharibi yenyewe, na ingawa Amerika ilitangaza kwamba itajibu matumizi yoyote ya Urusi ya silaha za nyuklia nchini Ukraine, hata kama italipiza kisasi kwa silaha za kawaida ili kuzuia vita vya nyuklia kati ya Urusi na Amerika, yote haya yanaweza kusababisha Urusi kupoteza nguvu ya kuzuia silaha ya mwisho inayomiliki, na silaha yake yenye nguvu yaweza kusababisha majanga haya katika masuluhisho ya baada ya vita.

13- Kuhusu kujiondoa kwa Urusi kutoka kwa uambatanishaji, kama ilivyo onyeshwa katika swali, inamaanisha kuiondoa Urusi kutoka kwa msimamo wa kimataifa na kumaliza ushawishi wake juu yake, na hili ni jambo zito kwa uongozi wa Urusi. Kwa hiyo, inatarajiwa kwamba Urusi itasimama kwenye mikoa hii minne, yaani, kwenye mipaka ya mikoa ambayo ilifanya kura za maoni za ujumuishaji, na labda itaongeza kidogo zaidi ya hayo, kwa kujaribu kuregesha maeneo ambayo ilipoteza huko Kharkov. Hii itamfanya rais wa Urusi aonekane "mwenye nguvu" mbele ya watu wake na ameleta faida mpya kwa Urusi baada ya kurudisha Crimea mnamo 2014, na ikiwa hili litafikiwa, ni lengo dogo kwa nchi ambayo ilikuwa ikionekana kama dola kubwa ambayo inatishia kuimeza Ukraine kikamilifu ndani ya muda mfupi. Lakini kwa upande mwingine, Amerika na nchi za Magharibi zinaihimiza Ukraine na kuunga mkono jeshi lake kukomboa maeneo haya yanayokaliwa na Urusi, na kati ya kuongeza msaada wa kijeshi wa Magharibi kwa Ukraine na uhamasishaji wa Urusi wa askari wa akiba, eneo la vita huko Ukraine litashuhudia hali ya vita vikali, na kwamba itadumu kwa muda mrefu zaidi. Huku ikidhoofisha dhamana ya Urusi ya kushinda vita isipokuwa kwa kutumia silaha za nyuklia. Vita vya Ukraine bado viko wazi kwa hatari zaidi za kimataifa… Na ikiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Lavrov atakumbusha kwamba

Urusi haikatai mazungumzo, Amerika na Uingereza haswa zinaonyesha azimio lao la kuifanya Ukraine kuwa uwanja ambao Urusi imeondolewa kwenye orodha ya nchi kubwa. Na kati ya mzozo huu wa utashi, uwanja wa Ukraine umesalia na mshangao tele ambao unaweza kubadilisha mambo juu chini.

14- Hatimaye, nchi kuu katika ulimwengu wa leo hupambana na kila mmoja kufikia malengo yao ya kikatili bila kuzingatia maadili yoyote ya kibinadamu au maadili. Udhalimu hugeuka kuwa uadilifu ukiwa unafanikisha wanachotaka, hata ukiwa unadhuru kwa wengine, hata ukiwa ni uovu wote. Nchi hizi zimezidisha ufisadi duniani, na dunia haitarekebika isipokuwa kwa kuangamia kwao, kisha Khilafah itaregea kwa njia ya Utume kwa kazi ya wafanyao kazi na nusra ya Mola Mlezi wa walimwengu wote.

[وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللَّهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ]

“Na siku hiyo Waumini watafurahi. Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.” [Ar-Rum: 4-5]

6 Rabii’ Al-Awwal 1444 H

2/10/2022 M

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.