Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali

Sudan Baada ya Vikosi vya Msaada wa Haraka Kuchukua Udhibiti wa El Fasher
(Imetafsiriwa)

Swali:

“Massad Boulos, mshauri mkuu wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu masuala ya Mashariki ya Kati, alithibitisha kwamba jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka wamekubaliana kusitisha mapigano kwa miezi mitatu, kulingana na mpango wa Quartet, unaojumuisha Imarati, Marekani, Saudi Arabia, na Misri, uliotangazwa mnamo Septemba 12.” (Sky News Arabia, 3/11/2025).

Makubaliano haya ya mpango wa Marekani ya pande za Sudan—serikali na Vikosi vya Msaada wa Haraka—yalikuja baada ya Vikosi vya Msaada wa Haraka kunyakua udhibiti wa El Fasher nchini Sudan. Ni nini kilicho nyuma ya makubaliano haya ya mpango wa Marekani? Zaidi ya hayo, ni yapi yaliyotokea kwa jeshi la Sudan yaliyoruhusu Vikosi vya Msaada wa Haraka kunyakua udhibiti wa El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur? Ni mji mkubwa sana na wenye ngome nzito ambao jeshi lilikuwa limeulinda vikali dhidi ya mashambulizi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka kwa muda mrefu. Mji huo ulishindwaje? Na vipimo na athari zake ni vipi?

Jibu:

Ili kufafanua jibu la maswali haya, hebu tuchunguze yafuatayo:

Kwanza: Al Jazeera iliripoti kwenye tovuti yake mnamo 28/10/2025: “Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vilitangaza mnamo Jumapili asubuhi udhibiti wao wa El Fasher, baada ya kuzingirwa kwa zaidi ya mwaka mmoja. Hii ina maana ya kupanua ushawishi wa vikosi hivyo juu ya majimbo yote matano ya Darfur na kugawanya nchi kati ya mashariki inayodhibitiwa na jeshi la Sudan na magharibi chini ya udhibiti wa Vikosi vya Msaada wa Haraka.” Simulizi hii fupi kutoka kwa Al Jazeera inaweka wazi kwamba udhibiti wa Vikosi vya Msaada wa Haraka dhidi ya El Fasher ni zaidi tu ya ushindi katika vita vya kupigania mji; ni utekaji wa ajabu wa eneo lote! RSF ilikuwa imezingira mji huo kwa mwaka mmoja, lakini ilikosa silaha za kisasa zinazohitajika ili kupata ushindi dhidi ya vitengo vya jeshi la Sudan vinavyoulinda. Vikosi hivi vilikuwa vimeulinda mji huo kwa ushujaa kwa mwaka mmoja, lakini ghafla, serikali ya Burhan iliukabidhi kwa muasi anayetaka kujitenga Hamdan Dagalo (Hemedti), kamanda wa Vikosi vya Msaada wa Haraka. Makabidhiano hayo yalikuwa ya wazi na yasiyo na utata:

1- “Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Sudan Abdel Fattah al-Burhan alisema kwamba watu wa Sudan na vikosi vyake vya jeshi watashinda, akisisitiza kwamba tathmini ya uongozi katika El Fasher (mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini) ilikuwa ni kuhamisha watu mji huo kutokana na uharibifu wa kimfumo uliokuwa umeupata.” (Al Jazeera Net, 27/10/2025). Kisha akafuatisha haya kwa maneno matupu: (Katika hotuba iliyopeperushwa kwenye televisheni, al-Burhan aliongeza, “Vikosi vyetu vina uwezo wa kupata ushindi, kugeuza meza, na kurudisha ardhi,” akiongeza, “Tumeazimia kulipiza kisasi kwa mashahidi wetu wote”)

2- “Vyanzo vya kijeshi vya Sudan viliiambia Al Jazeera kwamba jeshi la Sudan lilihamisha makao makuu ya tarafa kutoka mji wa El Fasher “kwa sababu za kimkakati.”” (Al Jazeera Net, 27/10/2025).

Taarifa hizi kutoka kwa Abdel Fattah al-Burhan na vyanzo vyake vya kijeshi zinaonyesha wazi, kwa njia ya moja kwa moja, kwamba jeshi lilihama kutoka El Fasher, na kuiacha ikiporwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka.

Pili, serikali ya Burhan na uongozi wake wa kijeshi walijizuia kutoa msaada wa kijeshi na kilojistiki kutoka maeneo yao ya kati ya udhibiti kwa vikosi vyao huko El Fasher kwa mwaka mmoja. Matokeo yake, vikosi hivi vilibaki vimezingirwa, vikipigana na kurudisha nyuma mashambulizi ya RSF kwa rasilimali yoyote waliyokuwa nayo kutoka ndani ya mji huo. Amri ya kijeshi ya serikali ya Burhan, ambayo ilijivunia kuzisafisha Khartoum, Omdurman, na Bahri kutokana na RSF, hakika ilikuwa na uwezo wa kusaidia vikosi vyake vikubwa huko El Fasher, lakini ilikosa kufanya hivyo kwa mwaka mmoja. Kwa maana nyengine, mpango ulikuwa ni kuviacha vikosi hivyo vianguke.

Tatu: Baada ya uchunguzi wa kina, tunaona kwamba makabidhiano ya vikosi vya Hemedti, mtengaji muasi, yalifanyika sambamba na mazungumzo yaliyofanywa na Amerika, kati ya pande mbili za Sudan nchini Marekani kwa lengo la kusitisha mapigano: (“Baada ya Baraza Kuu la Sudan kukataa kuwepo kwa mazungumzo yoyote ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja na ujumbe kutoka Vikosi vya Msaada wa Haraka jijini Washington, vyanzo vya kidiplomasia vilifichua kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Mohi El-Din Salem, aliwasili nchini Marekani kwa ziara rasmi yenye lengo la kujadili juhudi za kusitisha vita ambavyo vimekuwa vikiendelea nchini Sudan kwa zaidi ya miaka miwili.” (Al-Arabiya, 24/10/2025)).

Hii ina maana moja: Amerika iliwakusanya pamoja jijini Washington wajumbe wa vibaraka wake wawili wa Sudan—Burhan na Hemedti—na kukataa kwa Baraza la Kuu la Sudan kufanya mazungumzo na RSF jijini Washington kunatumika kama uthibitisho. Utekelezaji wa maagizo ya Amerika kwa vibaraka wake wawili ulifanywa waziwazi siku mbili au tatu baadaye huko El Fasher. Kulingana na chanzo hicho hicho kilichotangulia (vyanzo viliiambia Al-Arabiya/Al-Hadath mnamo Ijumaa kwamba waziri huyo wa Sudan atafanya mfululizo wa mikutano jijini Washington na maafisa wa utawala wa Marekani, akiwemo Massad Boulos, mshauri mkuu wa rais wa Marekani kuhusu Masuala ya Mashariki ya Kati na Afrika. Waliongeza kuwa Salem pia atakutana na wenzake kadhaa wa Kiarabu, ikibainisha kuwa ziara hiyo inakuja kwa mwaliko rasmi wa utawala wa Marekani kujadili masuala kadhaa ya maslahi ya pande zote. Afisa mmoja wa Marekani pia aliielezea Al-Arabiya/Al-Hadath kwamba Boulos ataongoza mikutano ya Quartet kuhusu mgogoro wa Sudan).

Ushahidi zaidi wa ukusanyaji wa Marekani wa wajumbe wa vibaraka wake wawili jijini Washington ni huu: [Afisa mmoja wa kidiplomasia alithibitisha jana, Alhamisi, kwamba Nchi nne (Quartet)  (Marekani, Saudi Arabia, Imarati, na Misri) watakutana leo jijini Washington na wawakilishi wa jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka ili kusukuma pande zote mbili kuelekea makubaliano ya kibinadamu ya kusitisha mapigano ya miezi mitatu. Alisema lengo lilikuwa “kutia shinikizo la pamoja ili kuimarisha usitishaji mapigano na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia raia,” Al-Arabiya, 24/10/2025]. Hii ina maana kwamba wakati wa shambulizi la RSF la El Fasher na jeshi la Sudan kuondoka humo, sanjari na mkutano wa Washington, hauachi shaka kwamba uamuzi wa kukabidhi mji huo wa kimkakati kwa RSF ulifanywa jijini Washington na kwamba pande hizo mbili za Sudan zilianza kuutekeleza mara moja uwanjani, yaani, siku mbili baadaye, huku matokeo yakipatikana siku ya tatu.

Nne: Mkutano huu jijini Washington ni hatua ya pili baada ya wa kwanza, wakati Amerika ilipowakusanya vibaraka na wafuasi wake katika eneo hilo katika kile kinachoitwa Quartet (Saudi Arabia, Imarati, na Misri) na kuanza kutekeleza matakwa yake ya kulazimisha kusitisha mapigano nchini Sudan. Al-Arabiya iliripoti mnamo 12/9/2025, taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo: (Taarifa ya pamoja ilisomeka: “Kwa mwaliko wa Marekani, mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani, Misri, Saudi Arabia, na Imarati walifanya mashauriano ya kina kuhusu mzozo wa Sudan, wakikumbuka kwamba umesababisha mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani na unahatarisha amani na usalama wa kikanda. Mawaziri hao walithibitisha kujitolea kwao kwa seti ya kanuni za pamoja za kukomesha mzozo nchini Sudan.”) Nukta ya nne ya taarifa hiyo ilisomeka: “Mustakabali wa utawala nchini Sudan utaamuliwa na watu wa Sudan kupitia mchakato wa mpito kamili na wazi usio chini ya udhibiti wa upande wowote unaopigana.” Pia ilisema katika moja ya nukta zake: “Juhudi zote zitafanywa ili kuunga mkono suluhisho la mzozo lililojadiliwa kwa ushiriki thabiti wa Vikosi vya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka.”

Kwa upande mmoja, Quartet hii ni fomula iliyochaguliwa na Amerika ili suluhisho lake nchini Sudan lionekane kuwa na sura ya kikanda pia, yaani, kwa idhini ya nchi muhimu katika eneo hilo. Hata hivyo, nchi hizi hazisongi hadi Washington izisukume, na hazichukui hatua yoyote bila Amerika. Kwa upande mwingine, maandishi ya taarifa hiyo yanaonyesha kutambuliwa kwa pande mbili za mzozo nchini Sudan sawa kwa sawa na yanawataka kushiriki kwa ufanisi. Hiyo ni kusema, taarifa hiyo haivichukulii Vikosi vya Msaada wa Haraka kama vikosi vya kujitenga na vya waasi, wala haitoi wito kwao kuacha uasi wao, hasa kwa kuwa waliunda serikali ya kujitenga ili kuigawanya Sudan.

Tano: Baada ya Vikosi vya Msaada wa Haraka kuchukua udhibiti wa El Fasher, mji wa kimkakati, udhibiti wao juu yake ulimaanisha kulichukua eneo lote la Darfur, pamoja na majimbo yake matano, ambayo mengi yalikuwa tayari chini ya udhibiti wao wa kweli. Kwa hivyo, kukubali makubaliano ya kusitisha mapigano ya miezi mitatu, au hata kudai, inamaanisha kutambuliwa kwa udhibiti wa RSF na uwepo halali katika eneo la Darfur na katika mji muhimu zaidi wa eneo hilo, El Fasher. Mkataba huu wa amani, ambao Amerika inaupendekeza na kuufanya uonekane kama makubaliano ya “Quartet”, unafuatwa na hatua zaidi za mazungumzo kati ya pande mbili za mzozo nchini Sudan, baada ya mipango ya Amerika kuiwezesha RSF kudhibiti Darfur yote, na baada ya kibaraka wa Amerika, Hamdan Dagalo (Hemedti), kuanzisha serikali ya kujitenga, ambayo aliitangaza mwishoni mwa Februari 2015 jijini Nairobi, mji mkuu wa Kenya, akiwa na yeye mwenyewe kama mkuu wake. Ilikuwa ikiendesha kazi zake kutokea Nyala, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kusini, na sasa njia imeandaliwa kikamilifu kwa serikali ya kujitenga ya Hemedti kuhamia El Fasher.

Sita: Kuhusu msimamo wa Marekani, ulikuwa wazi na haukuonyesha hata kutoridhishwa na udhibiti wa Vikosi vya Msaada wa Haraka dhidi ya El Fasher. Badala yake, iliitaka hatua inayofuata katika mpango wa Marekani kwa Sudan: kusitisha mapigano. Hii ingezuia kabisa njia ya jeshi la Sudan ya kuichukua tena El Fasher na kuhakikisha udhibiti wa Hemedti juu yake umeimarika, bila kuingiliwa na mapigano yoyote:

[Massad Boulos, mshauri wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu masuala ya Afrika, alitoa wito kwa pande zinazopigana nchini Sudan kuzingatia na kuidhinisha mara moja makubaliano ya kusitisha mapigano ya kibinadamu yaliyopendekezwa. Aliongeza kuwa alikuwa amewasilisha pendekezo la makubaliano ya kusitisha mapigano ya kibinadamu la miezi mitatu, ambalo lilikaribishwa na pande zote mbili katika mzozo wa Sudan. Alivihimiza Vikosi vya Msaada wa Haraka kuendelea na makubaliano ya kusitisha mapigano ya kibinadamu na kuacha mapigano. Boulos alikuwa amesema siku iliyopita kwamba ulimwengu ulikuwa ukiangalia kwa wasiwasi mkubwa vitendo vya Vikosi vya Msaada wa Haraka na hali katika El Fasher, akitoa wito wa ulinzi wa raia.] (Al Jazeera Net, 27/10/2025).

Hili lilithibitishwa tena, kama ilivyoripotiwa na Sky News mnamo 3/11/2025: [Massad Boulos, mshauri mkuu wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu masuala ya Mashariki ya Kati, alithibitisha kwamba jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka vimekubaliana kusitisha mapigano kwa miezi mitatu, kulingana na mpango wa Quartet, unaojumuisha Imarati, Marekani, Saudi Arabia, na Misri, uliotangazwa mnamo Septemba 12. Boulos alielezea, katika taarifa alizotoa kutoka Cairo mnamo Jumatatu, kwamba majadiliano ya kiufundi na ya kimkakati yalikuwa yakiendelea kabla ya kusainiwa kwa mwisho kwa usitishaji mapigano, akibainisha kwamba wawakilishi wa pande zote mbili walikuwa Washington kwa muda kujadili maelezo yake. Aliongeza kuwa pendekezo la kusitisha mapigano linawakilisha fursa halisi ya kukomesha mgogoro huo, akisisitiza kwamba jeshi na Vikosi vya Msaada wa Haraka vinashiriki katika kujadili waraka uliowasilishwa na Marekani kwa usaidizi wa Quartet, unaolenga kufikia amani. Alibainisha kuwa mzozo nchini Sudan umekuwa tishio kwa kanda na dunia, hasa kwa usalama wa Bahari Nyekundu.] (Sky News Arabia, 3/11/2025).

Saba: Katikati ya majisifu ya Rais wa Marekani Trump kwamba yeye ni mletaji amani na mwenye kumaliza vita, Amerika inaendelea waziwazi na bila shaka na mpango wake, na kwa kasi ya juu, ya kuigawanya Sudan na kutenganisha eneo la Darfur, kama vile ilivyoitenganisha Sudan Kusini hapo awali. Hili ndilo ambalo tumeonya mara kwa mara dhidi yake. Katika jibu la swali lenye kichwa cha habari “Mashambulizi ya Droni na Maendeleo katika Vita nchini Sudan” tulisema yafuatayo mnamo 21/5/2025:

[(Ni wazi kutokana na haya yote kwamba mashambulizi makubwa mashariki mwa Sudan, hasa kwenye vituo vya kimkakati vya mji wa Port Sudan, yanahusiana na vita vya Darfur. Yanalenga kulazimisha jeshi kuachana na kushambulia El Fasher na kuelekea mashariki kuilinda Port Sudan) tuliongeza: (Nne: Ni uchungu kwamba mkoloni kafiri Amerika inaweza kusimamia mapigano ambayo huvuna uhai nchini Sudan na kuwaunganisha vibaraka wake kuyatekeleza hadharani, si kwa siri, na hadharani, si kwa faragha. Burhan na Hemedti wanapigana na damu ya watu wa Sudan bila sababu nyingine isipokuwa kutumikia maslahi ya Amerika, kwani inataka kurudia mgawanyiko wa Sudan kama ilivyofanya katika kutenganisha kusini na Sudan. Sasa inafanya kila iwezalo kutenganisha Darfur na kile kilichobaki cha Sudan. Kwa hivyo, jeshi linaelekeza umakini wake maeneo mengine ya Sudan, na RSF inaelekeza umakini wake eneo la Darfur. Ikiwa wanyoofu katika jeshi watafanya kazi katika kuregesha udhibiti wa Darfur, RSF itahamisha vita hadi maeneo mengine nchini Sudan ili kuvuruga jeshi, hivyo vikosi vyake vitaondoka Darfur hadi mashariki mwa Sudan, ambapo RSF inazidisha mashambulizi yao kwa kutumia droni. Hii ni kuiwezesha RSF kuchukua udhibiti kamili wa Darfur!

Kabla ya hapo, katika jibu la swali lenye kichwa la “Kuongeza kasi Operesheni za Kijeshi nchini Sudan” la tarehe 6/2/2025, tulionya kwamba uongozi bandia wa kisiasa na kijeshi nchini Sudan, ambao unachukua maagizo yake kutoka kwa utawala wa Trump, unaelekeza jeshi kufungua korido za Vikosi vya Msaada wa Haraka kutoka eneo la kati kuelekea Darfur. Tulisema:

[Sita: Kwa hivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba maendeleo ya uwanjani nchini Sudan yanapangwa na kusimamiwa na Trump na kwamba yanalenga kufikia yafuatayo:

- Kuharakisha mpango wa Marekani wa kuandaa mazingira ya kugawanya nchi kati ya vibaraka wa Amerika kwa msingi wa Darfur chini ya udhibiti wa Vikosi vya Msaada wa Haraka na utawala wa Hemeti, huku jeshi linaloongozwa na Burhan likidhibiti Sudan ya kati na mashariki, hivyo  maumbo mawili yanajitokeza nchini Sudan, na jambo hili lililazimishwa kwa sababu ya udhibiti wa Hemeti juu ya Darfur. Hapo awali tumetaja mpango huu kujibu swali la tarehe 19/12/2023, ambapo tulielezea wakati huo “kwamba Amerika inaandaa mazingira ya mgawanyiko... pindi maslahi ya Amerika yanapohitaji hilo. Hata kama maslahi ya Amerika yanahitaji kutengana kwengine baada ya Sudan Kusini, itafanya utengaji huu huko Darfur... na inaonekana kwamba wakati wa kutengana huku haujafika bado... lakini kuandaa mazingira yake ndio kinachoendelea sasa.” Hili ndilo tulilosema hapo awali, na inaonekana kwamba maslahi ya Amerika yanakaribia kuharakisha utengaji wa Darfur kama ilivyofanya Sudan Kusini... na hili ni hatari sana ikiwa Trump atafanikiwa kulitekeleza... kwa hivyo Ummah lazima usimame dhidi yake na usiwe kimya kama ulivyokuwa kimya wakati Sudan Kusini ilipotenganishwa!]

Nane: Hizb ut Tahrir imekuwa ikionya tangu mwanzo wa mwaka huu, na kwa kweli tangu 2023 wakati Amerika ilipoanzisha vita kati ya vibaraka wake wawili mnamo 2023, kwamba mpango wa Amerika wa kuigawanya Sudan ungetimia. Na sasa, hatua za kuelekea mgawanyiko zinajitokeza mbele ya macho yenu, huku watu wengi wa Sudan wakizongwa  na mauaji haya kati ya vibaraka wa Amerika ili kufikia malengo ya Amerika na kudumisha ushawishi wake nchini Sudan. Leo, mpango wa Amerika uko karibu kufikia kujitenga na kutenganishwa kwa eneo la Darfur na Sudan, na hili linatokea huku mkisimama na kutazama! Je, kuna kiongozi yeyote mwenye busara na nguvu katika jeshi ambaye atakaa chini kwa saa moja na kuamua kuwa mtiifu kwa Mola wake, na kuchukua hatua zinazohitajika kuzuia mpango wa Amerika na kuwaangamiza vibaraka wake ambao wamewaua makumi ya maelfu ya Wasudan na kuwafukuza mamilioni, kwa madhumuni mengine isipokuwa kutekeleza matakwa ya Washington? Je, kuna kiongozi yeyote mwenye busara na nguvu katika jeshi ambaye ataweka mamlaka ya Sudan katika mikono ya dhati, akiipa Nusra (ushindi wa nguvu) Hizb ut Tahrir, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikipiga kelele, ikionya, na kutaka kusimamishwa kwa Uislamu, ili kutoka Sudan, Dola ya Kiislamu, Khilafah ya pili kwa njia ya Utume, iweze kusimamishwa? Na ni mtu huyu mwenye busara na nguvu ni mtukufu alioje anayekutana na Mwenyezi Mungu (swt), ilhali Mwenyezi Mungu amemtumia kutimiza bishara njema ya Mtume Wake Mtukufu (saw) ya kurudi kwa Khilafah Rashida baada ya utawala huu dhalimu tunaoishi:

«...ثُمَّ تَكُونُ مُلْكاً جَبْرِيَّةً فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللَّهُ أَنْ تَكُونَ، ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا، ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ ثُمَّ سَكَت»

...kisha utakuwepo utawala wa kidhalimu, na utakuwepo kwa muda apendao Mwenyezi Mungu uwepo, kisha atauondoa atakapokuuondoa, kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume.” Kisha akanyamaza.” [Imepokewa na Ahmad].

12 Jumada Al-Awwal 1447 H
3/11/2025 M

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.