بسم الله الرحمن الرحيم
Zimwi Lililo Lala: Hijja Yatoa Wito wa Umoja
(Imetafsiriwa)
Kila mwaka, zaidi ya Waislamu milioni mbili kutoka kote ulimwenguni hukusanyika katika eneo takatifu la ardhi kufanya moja ya matendo matukufu zaidi ya ibada ya pamoja: Hijja. Mahujaji hufika wakiwa wamevaa mavazi meupe ya aina moja, wakitamka maneno ya pamoja, na kufanya ibada za pamoja - ushuhuda hai wa Dini inayovuka mipaka ya utaifa, lugha, utamaduni, na hadhi ya kijamii - yote yakiwa na kusudi moja: ibada ya Mwenyezi Mungu (swt).
Hijja ni mojawapo ya nguzo kuu za Uislamu; ni kitendo cha ibada - kama vile swala tano za kila siku zinazotumika kutakasa nafsi, kufufua uhusiano wa mtu na Mwenyezi Mungu (swt). Mtume (saw) amesema: «مَنْ حَجَّ لِلَّهِ فَلَمْ يَرْفُثْ وَلَمْ يَفْسُقْ رَجَعَ كَيَوْمِ وَلَدَتْهُ أُمُّهُ»“Yeyote anayefanya Hija kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na hafanyi uchafu wowote (rafath) au kosa (fusooq) atarudi akiwa hana dhambi, kama alivyokuwa siku mama yake alipomzaa.” (Sahih Bukhari) Zaidi ya thawabu hizi kubwa, Hijja hutumika kama ufufuo wa kila mwaka wa maadili msingi ya Kiislamu, Yanayo ongoza zaidi kati ya hayo, umoja na kujitolea.
Umoja: Nguvu ya Ummah
Katika wakati ambapo ulimwengu wa Kiislamu unakabiliwa na ukoloni usiokoma, mauaji ya halaiki, na utaifa ambayo yamegawanya sehemu kubwa ya Ummah wa Kiislamu, Hijja huja kila mwaka kama ukumbusho wa wakati mwafaka kwamba umoja wa Waislamu ni faradhi ya Kisharia na hitaji la lazima la kisiasa. Kuwaona tu mahujaji - hata kwa mbali - huchochea hisia ya mshangao: mamilioni wakitembea kama mwili mmoja, wenye sifa ya nidhamu, kujitolea, na lengo moja la pamoja.
Kwa njia nyingi, mkusanyiko huo unafanana na mkusanyiko mkubwa wa nguvu na usawazishaji - dhihirisho linaloonekana kwamba Waislamu wanapoungana chini ya Talbiya Labbaik Allahumma Labbaik na lengo moja, matokeo yake ni ya kutia moyo.
Mtume (saw) aliwahi kuisifia enzi yetu ya sasa – katika zama ambapo Ummah wa Kiislamu utakuwa mkubwa kwa idadi lakini dhaifu “kama povu la bahari.” Udhaifu mwingi leo unatokana na mgawanyiko wa kisiasa: kwa hakika, ni Ummah ulioenea katika dola 57 za kitaifa kila moja ikiwa na serikali, majeshi, na sera za kigeni tofauti.
Lakini fikiria uwezo wa ulimwengu wa Kiislamu ulioungana:
- Masafa ya Kijiografia: Eneo la pamoja la nchi za Kiislamu lina ukubwa wa takriban maili za mraba milioni 12 na kulifanya liwe karibu mara mbili ya ukubwa wa Urusi, zaidi ya mara tatu ya ukubwa wa Marekani, na kuunda takriban 21% ya eneo lote la ardhi duniani, na hivyo kuwapa uwezo mkubwa wa uzalishaji wa nishati badali.
- Wingi wa Kilimo: Ardhi hii kubwa na yenye utofauti wa ikolojia inawezesha uzalishaji wa mazao mengi makubwa duniani, pamoja na utajiri mkubwa wa mifugo ambao hutumika kama msingi wa usalama wa chakula na uchumi.
- Idadi ya Vijana Wachanga na Wachangamfu: Idadi ya Waislamu inakadiriwa kuwa takriban watu bilioni 2, wakiwakilisha karibu 26% ya idadi ya watu duniani, wakiwa na umri wa wastani wa takriban miaka 24 - wakiunda nguvu kazi kubwa zaidi duniani na moja ya nguvu kazi yake changamfu zaidi.
- Ushawishi wa Kimkakati wa Baharini: Nchi za Kiislamu zinapakana na maeneo matano kati ya saba makubwa ya usafirishaji wa mafuta duniani kama ilivyotambuliwa na Idara ya Habari za Nishati ya Marekani ikijumuisha Mlango wa Hormuz, Bab el-Mandeb, Mkondo wa Suez, Mlango wa Malacca, na Bosporus. Ushawishi juu ya njia hizi muhimu za maji ungetoa faida kubwa za kifedha na kisiasa.
- Udhibiti wa Nishati: Nchi za Kiislamu zina takriban 60-65% ya akiba ya mafuta duniani, pamoja na rasilimali nyingi za asili na madini adimu.
- Uwezo wa Kijeshi: Ummah ulioungana ungeongoza mojawapo ya vikosi vikubwa zaidi vya kijeshi duniani, ukiwa na wastani wa wafanyikazi changamfu na wa akiba wa pamoja wa milioni 20-25.
Kujitolea Muhanga: Kitovu cha Hijja
Kujitolea muhanga ni thamani ya pili kubwa inayoonyeshwa kupitia Hijja - thamani ambayo imesikika katika vizazi vyote.
Mila ya kujitolea muhanga katika Uislamu inaanzia kwa Nabii Ibrahim (as), ambaye alionyesha aina ya juu zaidi ya muhanga na kujitolea: nia ya kumtoa mwanawe mpendwa aliyezaliwa baada ya kusubiri kwa muda mrefu na kwa bidii; kumwacha mkewe Hajar na mtoto wao mchanga katika bonde tasa la jangwa, akiamini kabisa riziki ya Mwenyezi Mungu; na kuacha starehe, familia, na yakini kwa ajili ya utiifu kwa Mola wake Mlezi.
Vivyo hivyo kwa mahujaji; mihanga ya Hijja huanza muda mrefu kabla ya kufika Makka wanapoacha biashara zao, riziki, na familia zao na kubeba mizigo mikubwa ya kifedha.
Pindi wanapofika, mihanga inaendelea. Mahujaji hufanya ibada takatifu chini ya joto kali, wakiongozwa na mapenzi kwa Mwenyezi Mungu (swt) na utiifu wao kwake pekee. Baada ya kukamilika kwa Hijja, mahujaji hutoa sadaka ya mnyama na kunyoa vichwa vyao - matendo ya kinje ambayo yanaashiria upya wa ndani wa utiifu wao kwa Mwenyezi Mungu na kuachana kwao na mengine yote.
Hivyo, Waislamu hawapaswi kamwe kusita kutoa sadaka pindi zinapotolewa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (swt).
Kadri msimu wa Hijja unavyokaribia, tunakumbuka kafara za wale waliotutangulia: tunamkumbuka Mtume (saw) wakati wa kususia na Banu Hashim; Sumayyah (ra) shahidi wa kwanza wa Uislamu, uimara wa Maswahaba wakati wa Vita vya Handaki; na Abu Ayyub al-Ansari (ra) ambaye alizikwa karibu na kuta za Konstantinopoli.
Hii ni mifano michache tu. Hata hivyo, ujumbe wao haukuishia kwa kufariki kwao au kuuawa kwao kishahidi; bali unaendelea nasi, ukithibitisha kwamba utimilifu wa ujumbe huu utahitaji kafara ya kiwango sawa.
Kwa mfano, mfarakano wa kisiasa ambao umeudhoofisha Ummah hautaondolewa bila muhanga. Mipaka bandia iliyochorwa na dola za kikoloni haitaondoka bila muhanga. Watawala madhalimu hawataondolewa bila muhanga. Na kusimamishwa kwa Khilafah - taji la faradhi zote - hakutakuja bila muhanga.
Hijja hutumika kama ukumbusho wa kila mwaka kwamba hatukuumbwa ili tugawanyike bali tuunde Umma mmoja—kuamini katika Mola mmoja, Dini moja, Umma mmoja. Njia ya kurudi kwenye umoja huo iko kupitia kujitolea muhanga.
Njia ya Mwamko
Maswali yanayofaa kutafakariwa ni: Vipi ikiwa Umma wa Kiislamu ungeungana kisiasa, kama unavyofanya kiroho katika Hijja kila mwaka? Je, Umma unao uwezo wa kuwa na umoja na uhuru? Je, tuko tayari kuungana na kujitolea?
Jibu ni dhahiri: Umma una kila rasilimali, kila faida ya idadi ya watu, na kila mali ya kijiografia inayohitajika kujenga dola ya kisasa, huru, na yenye ustawi – dola inayotumia uwezo wake mkubwa kuanzisha mfumo wa utawala unaomridhisha Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume Wake (saw). Chini ya mfumo wa haki uliojikita katika Wahyi wa Kimungu, ukandamizaji haungepata hifadhi, na hakuna ukiukwaji wa utakatifu wa Waislamu – maisha yao, utajiri au heshima – ungeruhusiwa. Hali kama hiyo ingeuwasilisha Uislamu kwa ulimwengu kupitia tofauti isiyopingika kati ya haki na uadilifu wa utawala chini ya Uislamu na ulafi, ukosefu wa usawa, na kuharibika kwa maadili ambapo mfumo uliopo sasa wa kisekula-kibepari umezama ndani yake, kwa upande mwengine.
Njia ya mwamko si tu suala la mageuzi ya kisiasa au maendeleo ya kiuchumi; bali inahusisha kuregeshwa kwa mfumo kamili wa maisha ya Kiislamu, na kusimamishwa kwa hukmu kwa mujibu wa yale yote aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, chini ya utawala kwa njia ya Utume: Khilafah inayounganisha Umma, kuregesha hadhi yake, na kuuweka katika nafasi kama ile ambayo Mwenyezi Mungu (swt) aliutangaza kuwa - umma bora uliotolewa kwa ajili ya wanadamu.
Umma lazima utoe mihanga na kuonyesha ikhlasi katika kutafuta mwamko huu, na katika kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu bila kuyumba. Hakika, ushindi wa dunia hii na malipo ya Mwenyezi Mungu ya Akhera vinawangojea wale watakaoitikia wito huu.
[وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنْكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَى لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُمْ مِنْ بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْناً يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئاً وَمَنْ كَفَرَ بَعْدَ ذَلِكَ فَأُولَئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ]
“Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na watao kufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu.” [An-Nur: 55]
H. 24 Dhu al-Qi'dah 1447
M. : Jumatatu, 11 Mei 2026
Hizb-ut-Tahrir
Amerika