Afisi ya Habari
Wilayah Sudan
| H. 26 Rabi' II 1447 | Na: HTS 1447 / 44 |
| M. Jumamosi, 18 Oktoba 2025 |
Hotuba ya Msemaji Rasmi wa Hizb ut Tahrir / Wilayah Sudan
Katika Mkutano na Waandishi wa Habari mnamo Jumamosi 26 Rabi’ al-Akhir 1447 H sawia na 18/10/2025 M
Anwani: “Mkanganyiko wa Serikali katika Jinsi ya Kudhibiti Miamala ya Dhahabu na Athari Zake kwa Thamani ya Pauni”
(Imetafsiriwa)
Baada ya kujitenga kwa Sudan Kusini mwaka wa 2011, na Sudan kupoteza zaidi ya 75% ya mauzo yake ya nje ya mafuta, dhahabu iliibuka kama njia badali kuu ya kufidia hasara hii na kupata faida kwa fedha za kigeni. Uchimbaji madini ulikuwa umeenea sana nchini Sudan baada ya karibu mwaka wa 2008, na uzalishaji wa dhahabu wa Sudan ukawa mkubwa, na kufikia tani 73.8 mwaka wa 2024, na kushika nafasi ya tano barani Afrika. (AlJazeera.net). Hata hivyo, uzalishaji huu mkubwa haukuinufaisha serikali wala watu; uliporwa na watu binafsi, na makampuni ya kigeni na ya ndani, na hata kile kinachozalishwa kupitia uchimbaji wa jadi hununuliwa na kutolewa kimagendo na baadhi ya makampuni na mashirika. Ili kuthibitisha kile tulichosema kuhusu hili, tunahakiki migodi mikubwa zaidi ya dhahabu nchini Sudan, kwa njia ya mfano na sio kipekee, na jinsi serikali inavyoshughulikia migodi hii!
Mojawapo ya migodi hii ni mgodi wa Jebel Amer, ulioko takriban kilomita 100 kaskazini mwa jiji la Al-Fashir, ukiwa na wastani wa uzalishaji wa takriban tani 50 kwa mwaka, kulingana na Reuters, na kuufanya kuwa mgodi wa tatu kwa ukubwa wa dhahabu barani Afrika. Hata hivyo, serikali haijachukua udhibiti wake; badala yake, iliuacha uporwe na makundi yenye silaha. Mwisho kati ya haya ulikuwa mwaka wa 2017, wakati mgodi huo ulipokuwa mali ya Vikosi vya Msaada wa Haraka na makampuni ya Urusi kama vile Wagner.
Ingawa Kampuni ya Al-Junaid, inayoshirikiana na Vikosi vya Msaada wa Haraka, ilitangaza mwaka wa 2021 kwamba ilikuwa imekabidhi mgodi wa Jebel Amer kwa serikali, kwa kweli mgodi huo ulibaki chini ya udhibiti wake hadi leo.
Mgodi wa Hassal, ulioko kaskazini mashariki mwa Sudan, unamilikiwa kwa 60% na Kampuni ya Sudan ya Ariab, na 40% unamilikiwa na La Mancha Resources, inayomilikiwa na mfanyibiashara wa Misri Naguib Sawiris. Mgodi wa Block 14, ulioko karibu na mpaka wa Misri kaskazini mwa Sudan, unaojulikana kama Mradi wa Meyas Sand, unamilikiwa kwa 70% na kampuni ya Australia Per Sues, 20% na serikali ya Sudan, na 10% na kampuni ya ndani ya Sudan inayoitwa Meyas.
Kulingana na ripoti iliyochapishwa na Al Jazeera Net, dhahabu kutoka mgodi wa Jebel Amer na zaidi ya migodi mengine 10 huko Darfur Kusini husafirishwa kisiri hadi dola ya Chad, ambapo karatasi hutolewa kwa ajili yake kama dhahabu ya Chad, na kisha husafirishwa kwenda Imarati. Usafirishaji wa dhahabu kutoka Sudan unahusisha watu wenye ushawishi mkubwa serikalini tangu enzi ya Serikali ya Wokovu, kwani ilisafirishwa kimagendo kupitia Uwanja wa Ndege wa Khartoum na bandari za Sudan. Pia kuna kampuni zinazohusiana na jeshi na zengine zinahusiana na vyombo vya ujasusi zinazofanya kazi katika utafutaji wa dhahabu, na mapato ya kampuni hizi hayaingii kwenye hazina ya serikali.
Baada ya kuzuka kwa vita kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), vita hivi vilivyoharibu miundombinu mingi ya kiuchumi na mengineyo, na kusimamisha mauzo ya nje ambayo yalikuwa yakilisha hazina kwa kile kinachoitwa sarafu ya kigeni (dolari), sarafu ya ndani, pauni ya Sudan, ilianza kumomonyoka na kuporomoka dhidi ya dolari ya Marekani na sarafu zengine za kigeni. Hii iliakisi maisha ya watu, ambayo tayari yalikuwa hayawezi kuvumilika kwa sababu ya vita; umaskini na uchochole uliongezeka, na magonjwa na njaa vilienea.
Katika jaribio la kukomesha kuzorota huku, Kamati ya Dharura ya Uchumi, iliyoongozwa na Waziri Mkuu Kamil Idris, ilifanya mkutano mnamo Jumatano, tarehe 20 Agosti 2025, na kamati hiyo ilitoa maamuzi ya kudhibiti utendaji wa kiuchumi, kulingana na Shirika la Habari la Sudan. Maamuzi muhimu zaidi kati ya haya yalikuwa:
1. Kuainisha umiliki au uhifadhi wa dhahabu bila hati kama uhalifu wa magendo.
2. Kufuatilia mauzo ya nje ili kuepuka magendo ya dhahabu.
3. Kudhibiti ununuzi na uuzaji wa dhahabu kwa chombo cha serikali.
Licha ya uthibitisho wao kwamba ununuzi na uuzaji wa dhahabu unapaswa kudhibitiwa kwa chombo cha serikali, walikiuka uamuzi huu. Kulikuwa na mkutano ambapo gavana aliyefutwa kazi wa Benki Kuu ya Sudan, Burai Al-Sadiq, alisisitiza kwamba Benki Kuu ya Sudan iwe chombo pekee kinachosafirisha dhahabu nje. Mzozo mkali uliibuka katika mkutano huu rasmi, uliofanyika katika Jengo la Wizara jijini Port Sudan mnamo 12/10/2025, ambapo Gavana Burai alishikamana na uamuzi wa kuufanya usafirishaji nje wa dhahabu kuwa wa Benki Kuu pekee, huku wawakilishi wa kampuni zinazosafirisha dhahabu wakisisitiza haki yao ya kusafirisha moja kwa moja bila wasitwa wa Benki Kuu. Waziri wa Fedha Jibril Ibrahim aliunga mkono msimamo wa kampuni hizo, na gavana akaondoka kwenye mkutano huo kwa hasira. Hiyo ndiyo sababu ya kufutwa kazi kwake siku iliyofuata, wakati Al-Burhan alipotoa uamuzi wa kumwondoa na kumteua Amina Mirghani, mwanamke wa kwanza kuchukua nafasi hii nchini Sudan.
Wakati huo huo, shina la tatizo katika utunzaji wa dhahabu wa serikali linabaki:
a. Kuweka migodi mikubwa ya dhahabu mikononi mwa makampuni na watu binafsi badala ya serikali, na kusababisha nchi kupoteza utajiri wake mwingi kwa mikono michache.
b. Kutoweza kudhibiti dhahabu inayochimbwa na kujua wingi wake.
c. Sera zinazokinzana kuelekea dhahabu inayochimbwa kuhusiana na bei ya ununuzi, chombo cha ununuzi, na ukiritimba, ambazo zilisababisha kuenea kwa magendo ng’ambo na nchi jirani (Misri, Imarati, na Chad).
d. Kutofaidika na uchimbaji wa jadi, ambao unasafirishwa kimagendo, ikizingatiwa kuwa karibu 70% ya kiasi kilichotangazwa cha uzalishaji wa dhahabu kinatokana na uchimbaji wa jadi, na kufichua ukubwa wa magendo yanayotokea katika dhahabu.
Kwa sababu suala la dhahabu linahusiana kwa karibu na sarafu, tatizo la mmomonyoko wa pauni ya Sudan linaweza kufupishwa katika sababu kuu kadhaa:
1. Pauni ya Sudan inategemea dolari badala ya dhahabu na fedha.
2. Uchapishaji noti bila kuziegemeza na dhahabu au bidhaa, ambao huongeza viwango vya mfumko wa bei na kusababisha mmomonyoko wa pauni.
3. Usafirishaji nje dhaifu kutokana na magendo na ukosefu wa utulivu wa kisiasa, licha ya utajiri mkubwa wa kilimo, wanyama, na madini nchini Sudan ambao ungeweza kuifanya kuwa miongoni mwa nchi tajiri zaidi duniani.
4. Kutegemea uagizaji bidhaa kutoka nje kwa mahitaji mengi kama vile ngano, dawa, vifaa vya petroli, na nyenginezo, ambazo zinahitaji dolari, ikiongeza mahitaji ya dolari na kudhoofisha pauni. Watu wamepoteza imani na pauni, ambayo imeendelea kumomonyoka kila siku, na kusababisha watu - haswa wafanyibiashara - kupendelea kushikilia dolari au dhahabu kama njia ya kuhifadhi thamani ya akiba zao, ikiongeza bei ya dolari na kupunguza thamani ya sarafu ya ndani.
Huu ndio uhalisia kuhusu jinsi serikali inavyoamiliana na dhahabu na sarafu ya ndani - pauni - na inaonyesha mkanganyiko na ukosefu wa maono katika jinsi ya kushughulikia hilo.
Sisi katika Hizb ut Tahrir / Wilayah Sudan, kwa mtazamo wa jukumu letu kwa Ummah wetu, tunawasilisha suluhisho msingi kuhusu suala hili kwa mujibu wa itikadi ya Kiislamu, na tunasema:
Kwanza: Dhahabu, haswa migodi yenye uzalishaji usiokoma kama ile iliyotajwa hapo awali, inachukuliwa kuwa mali ya umma. Hairuhusiwi kumiliki mali hizo kibinafsi na makampuni au watu binafsi; ni haki ya Ummah mzima. Kazi ya dola ni kusimamia uchimbaji na uuzaji, na mapato yake yanapaswa kwenda kwenye miradi ya umma kwa watu wote au kugawanywa kwao. Dola haina haki ya kuuza mali ya umma kwa kuigawa kwa watu binafsi au makampuni, iwe kwa ruzuku au muunganisho au vyenginevyo. At-Tirmidhi amesimulia kutoka kwa Abyad ibn Hammal:
«أَنَّهُ وَفَدَ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ ﷺ فَاسْتَقْطَعَهُ الْمِلْحَ فَقَطَعَ لَهُ، فَلَمَّا أَنْ وَلَّى قَالَ رَجُلٌ مِنْ الْمَجْلِسِ: أَتَدْرِي مَا قَطَعْتَ لَهُ؟ إِنَّمَا قَطَعْتَ لَهُ الْمَاءَ الْعِدَّ. قَالَ: فَانْتَزَعَهُ مِنْهُ»
“Kwamba alikwenda kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na kumwomba amgawie chumvi, naye akamgawia. Alipogeuka, mtu mmoja kutoka kwenye mjumuiko akasema: Unajua ulichomgawia? Umemgawia maji ya kudumu. Kwa hivyo akayachukua kutoka kwake.”
Maji ya kudumu ni yale ambayo hayaishi, yaani, alikuwa amemgawia madini ambayo hayaishi, kwa sababu chumvi ni madini mithili ya maji ya kudumu.
Kwa hivyo, si haki ya serikali kutoa sehemu yoyote ya dhahabu kwa makampuni. Lazima ifanye makubaliano na makampuni kwa kiasi maalum cha uchimbaji kwa manufaa ya umma, si kwa manufaa ya makampuni. Makampuni hayana haki ya dhahabu iliyochimbwa. Hii inahakikisha kwamba dhahabu yote inabaki mikononi mwa dola ili itumike kwa manufaa ya Umma.
Pili: Msingi wa sarafu ya dola lazima uwe dhahabu na fedha. Mtume (saw) aliidhinisha dinari ya Kirumi na dirham ya Kiajemi kama sarafu ya dola ya Kiislamu kwa uzito unaojulikana hadi dinari ya Kiislamu ilipotengenezwa kwa uzito wa gramu 4.25 na dirham kwa gramu 2.975 za fedha, hadi dolari ilipotawala baada ya uamuzi wa Rais wa Marekani Nixon wa kufuta uhusiano wa dolari na dhahabu. Dolari ikawa sarafu ambayo karibu ulimwengu mzima unategemea. Hizb ut Tahrir imechapisha Rasimu ya Katiba ya Dola ya Khilafah ambapo Kifungu cha 167 kinasema:
“Sarafu ya dola ni dhahabu na fedha, iwe imechongwa au haijachongwa. Dola hairuhusiwi kuwa na sarafu nyengine yoyote isipokuwa hizo. Dola inaweza kutoa kitu chengine badali ya dhahabu na fedha kwa sharti kwamba katika hazina ya dola kuna kile kinacholingana nayo katika dhahabu na fedha. Dola inaweza kutoa shaba, karatasi, au kitu chengine chochote na kuipiga muhuri kwa jina lake kama sarafu yenyewe ikiwa ina kiwango kamili katika dhahabu na fedha.”
Tumebainisha dhahabu na fedha kama msingi kwa sababu Uislamu uliunganisha dhahabu na fedha na hukmu madhubuti zisizobadilika, kama vile pesa za damu (diya), dinari 1000 za dhahabu, na kiasi cha hadd ya wizi kuwa robo ya dinari au zaidi, na hukmu zengine zilizounganishwa na Sharia kwa dhahabu na fedha. Uislamu ulifanya zakat kwa sarafu iliyoegemeza na dhahabu na fedha, na miamala yote ya kifedha katika Uislamu inaegemezwa juu ya dhahabu na fedha.
Tatu: Sudan ni nchi ya dhahabu. Itakapofanya dhahabu kuwa msingi wa sarafu yake, sarafu yake itakuwa yenye nguvu na yenye thamani zaidi kwa sababu ina thamani ya dhati isiyoathiriwa na kitu chengine chochote. Thamani yake inabaki thabiti; inaweza kupungua kidogo au kuongezeka kidogo, lakini haitakuwa kama mmomonyoko wa sasa wa sarafu ya ndani ya Sudan. Hili litapatikana kwa kutekeleza hukmu za Sharia kuhusu dhahabu.
Mtume (saw) alisema: «...وَفِي الرِّكَازِ الْخُمُسُ» “...na katika hazina iliyozikwa (rikaz) ni khumusi moja.”
Dola inachukua migodi yote ya kudumu ambayo haiishi, na ina haki ya kupata khumusi moja ya kile ambacho watu wanazalisha.
Nne: Dola inayotekeleza masuluhisho haya msingi ni dola huru yenye kimfumo, si dola inayofanya kazi kama hali yetu ya sasa, iliyo chini ya mkoloni kafiri anayetafuta kupora rasilimali, kuwafukarisha watu, na kufanya kazi ya kuchana umoja wao ili kuwadhoofisha! Amerika, ambayo ilitenganisha Sudan Kusini ili Sudan isinufaike na mafuta, sasa inatafuta kutenganisha Darfur, yenye dhahabu nyingi na madini ya thamani.
Enyi Watu wa Sudan: Hakuna wokovu kwenu isipokuwa kwa kufanya kazi kwa dhati pamoja na Hizb ut Tahrir ili kusimamisha Khilafah Rashida kwa njia ya Utume, ambayo inamridhisha Mola wenu Mlezi, inaregesha heshima yenu, na kuwawezesha kuishi chini ya kivuli chake kufurahia neema ambazo Mwenyezi Mungu ameipa ardhi yetu.
Wa Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh.
Ibrahim Othman (Abu Khalil)
Msemaji Rasmi wa Hizb ut Tahrir
katika Wilayah Sudan
| Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Wilayah Sudan |
Address & Website Tel: 0912240143- 0912377707 http://www.hizb-sudan.org/ |
E-Mail: Spokman_sd@dbzmail.com |