Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Umoja wa Ummah wa Kiislamu Si Rasmi au wa Kinadharia Tu, Khilafah Ni Umbo Lake la Kivitendo

(Imetafsiriwa)

Waislamu ni Ummah mmoja, tofauti na watu wengine; Mola wao Mlezi ni Mmoja, Dini yao ni moja, Mtume wao ni mmoja, Kibla chao ni kimoja, na Kitabu chao ni kimoja. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[إِنَّ هَذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ]

“Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi.” [Al-Anbiya: 92].

Amesema Mtume (saw): «بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ، هَذَا كِتَابٌ مِنْ مُحَمَّدٍ النَّبِيِّ ﷺ بَيْنَ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُؤْمِنِينَ مِنْ قُرَيْشٍ وَيَثْرِبَ وَمَنْ تَبِعَهُمْ فَلَحِقَ بِهِمْ وَجَاهَدَ مَعَهُمْ أَنَّهُمْ أُمَّةٌ وَاحِدَةٌ دُونَ النَّاسِ»Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu. Huu ni waraka kutoka kwa Muhammad Mtume (saw), kati ya Waislamu na waumini kutoka Quraysh na Yathrib na wale waliowafuata na kujiunga nao na kupigana nao, kwamba wao ni Ummah mmoja kando na watu wengine” (imesimuliwa na Al-Bayhaqi katika Al-Sunan Al-Kubra). Pia (saw) amesema: «الْمُسْلِمُونَ تَتَكَافَأُ دِمَاؤُهُمْ، وَيَسْعَى بِذِمَّتِهِمْ أَدْنَاهُمْ، وَيُجِيرُ عَلَيْهِمْ أَقْصَاهُمْ، وَهُمْ يَدٌ عَلَى مَنْ سِوَاهُمْ، يَرُدُّ مُشِدُّهُمْ عَلَى مُضْعِفِهِمْ، وَمُتَسَرِّيهِمْ عَلَى قَاعِدِهِمْ، أَلَا لَا يُقْتَلُ مُسْلِمٌ بِكَافِرٍ، وَلَا ذُو عَهْدٍ فِي عَهْدِهِ» Waislamu ni sawa kwa upande wa damu. Wale walio chini kabisa kati yao wana haki ya kutoa ulinzi kwa niaba yao, na yule anayeishi mbali anaweza kutoa ulinzi kwa niaba yao. Wao ni kama mkono mmoja dhidi ya wale wote walio nje ya jamii yao. Wale walio na farasi wa haraka wanapaswa kurudi kwa wale walio na farasi wa polepole, na wale waliotoka pamoja na kikosi (wanapaswa kurudi) kwa wale waliobaki nyuma. Muumini hatauawa kwa ajili ya kafiri, wala mtu aliye chini ya agano hatauawa akiwa chini ya agano lake” (imesimuliwa na Abu Dawud, Ibn Majah, na Ahmad).

Umoja wa Ummah wa Kiislamu si umoja rasmi au wa kinadharia, bali ni umoja wa kivitendo unaotokana na itikadi yao, ambayo inawafanya kuwa ndugu. [إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ] “Hakika Waumini ni ndugu” [Al-Hujurat: 10]. Umoja huu lazima uonekane wazi katika nyanja zote za maisha yao; katika ibada zao na matendo yao ya ibada, hasa yale yanayofanywa kwa pamoja katika wakati au mahali maalum, kama vile kufunga wakati wa Ramadhan, Hajj, na Idd al-Fitr na Idd al-Adha; na katika hisia zao, ili Muislamu afurahie kila jambo jema linalompata Muislamu mwengine, na kuhuzunika na kuteseka kwa kila baya au madhara yanayompata Muislamu mwengine katika sehemu yoyote ya dunia. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amewafananisha Waislamu na mwili mmoja, kama alivyosema (saw): «مَثَلُ الْـمُؤْمِنِينَ فِي تَوَادِّهِمْ وَتَرَاحُمِهِمْ وَتَعَاطُفِهِمْ مَثَلُ الْجَسَدِ، إِذَا اشْتَكَى مِنْهُ عُضْوٌ تَدَاعَى لَهُ سَائِرُ الْجَسَدِ بِالسَّهَرِ وَالْحُمَّى» “Mfano wa Waumini katika mapenzi yao wenyewe kwa wenyewe, kuhurumiana kwao, na kuoneana upole kwao, ni kama kiungo cha mwili mmoja, pindi kinaposhitakia maumivu, mwili mzima huitikia kwa kukosa usingizi na homa” (Bukhari na Muslim). Hili pia lazima lidhihirike kwa upande wa kifikra kwa kuifanya itikadi ya Kiislamu kuwa msingi wa fikra na tabia, kukataa fikra au rai yoyote isiyoegemezwa au isiyotokana na itikadi hiyo, na kujisalimisha kwa amri ya Mwenyezi Mungu (swt) na kuiweka juu ya matamanio na maslahi ya kibinafsi. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللهُ وَرَسُولُهُ أَمْراً أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ]

“Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapo kata shauri katika jambo lao.” [Al-Ahzab: 36]. Kutoka kwa Abdullah bin Amr bin Al-Aas, kutoka kwa Mtume (saw), yeye (saw) alisema: «لا يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى يَكُونَ هَوَاهُ تَبَعاً لِمَا جِئْتُ بِهِ» “Hawi na imani ya kweli mmoja wenu mpaka matamanio yake yaendane na niliyoyaleta.”

Ukweli kwamba Waislamu ni taifa tofauti na watu wengine unamaanisha kwamba hili linapaswa kuonekana katika umoja wao wa kisiasa, ili ardhi za Waislamu ziwe kiungo kimoja cha kisiasa na kijiografia kinachotawaliwa na mtawala mmoja anayetumia katiba moja inayotokana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu (swt) na Sunnah ya Mtume Wake (saw). Hiki ndicho kilichokuwa kimejumuishwa katika dola ya Khilafah tangu wakati Mtume (saw) alipoisimamisha Madina hadi ilipovunjwa na Makafiri wa Magharibi mikononi mwa Mustafa Kemal mnamo tarehe ishirini na nane ya Rajab, 1342 H, sambamba na tarehe tatu ya Machi, 1924 M. Kukosekana kwake ndiko kulikosababisha umoja wa Ummah kujeruhiwa vibaya, na kusababisha Ummah kuishi katika hali ya kugawanyika na kutengana kwa zaidi ya karne moja, na kusababisha nchi zetu kugawanyika vipande vipande na kuwa dola za kikatuni zinazotawaliwa na watawala wasaliti. Hakika, imeenda mbali zaidi katika kugawanya kile ambacho tayari kilikuwa kimegawanyika vipande vipande, kama ilivyotokea nchini Sudan.

Khilafah ni dola inayosimamia moja kwa moja hifadhi ya madhihirisho na sifa za umoja wa Ummah wa Kiislamu. Inawakilisha tafsiri ya kivitendo ya umoja wake wa kifikra na kihisia. Kwa kukosekana kwake, fikra za Kimagharibi zimetuvamia, na wakoloni na zana zao miongoni mwa watawala wamefanya kazi ya kubadilisha itikadi ya Kiislamu kwa fikra za kibepari za kisekula kama msingi wa fikra na tabia. Katika kiwango cha umoja wa kihisia, tunajiona tukiwa na uchungu na kuungua kwa uchungu kwa yaliyowapata ndugu zetu huko Gaza, Sudan, Myanmar, Turkestan Mashariki, na nchi zengine za Kiislamu. Hata hivyo, mipaka bandia na watawala wahalifu hutuzuia kuchukua hatua ya kuwasaidia ndugu zetu waliokandamizwa. Hata matendo yetu ya ibada na matambiko ambazo kwazo tunajikurubisha kwa Mola wetu Mlezi na ambazo kwazo umoja wetu unadhihirika, kwa kukosekana kwa Khilafah, watawala wameyahadaa na kuyaharibu kwetu na wamefanya kazi kwa bidii kutuzuia kuwa wamoja katika kuyatekeleza. Labda ushahidi dhahiri zaidi wa hili ni kwamba tunaanza kufunga Ramadhan katika siku tofauti na kufungua saumu yetu na kutekeleza swala ya Idd katika siku tofauti. Hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliye Juu Zaidi.

Ni muhimu kusisitiza kwamba ingawa Umma wa Kiislamu umekumbwa na udhaifu na mfarakano, hii ni hali ya muda tu ambayo haikanushi kuwepo kwake au kuzuia umoja wake na kuregea kwa ufanisi wake. Umma bado unamiliki vipengee vyake muhimu: itikadi inayounganisha, na mifumo ya maisha inayotokana na itikadi hii. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[قَدْ جَاءكُم مِّنَ اللّهِ نُورٌ وَكِتَابٌ مُّبِينٌ * يَهْدِي بِهِ اللّهُ مَنِ اتَّبَعَ رِضْوَانَهُ سُبُلَ السَّلاَمِ]

“Bila shaka imekujieni kutoka kwa Mwenyezi Mungu nuru na Kitabu kinacho bainisha * Mwenyezi Mungu huwaongoa wenye kufuata radhi yake katika njia za salama” [Al-Ma’idah: 15-16]. Mtume (saw) amesema: «تَرَكْتُ فِيكُمْ أَمْرَيْنِ لَنْ تَضِلُّوا مَا تَمَسَّكْتُمْ بِهِمَا: كِتَابَ اللهِ وَسُنَّةَ نَبِيِّهِ ﷺ» “Nimekuachieni mambo mawili kamwe hamtapotea pindi mtakaposhikamana nayo: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake (saw).” Hayako au hayajakamilika, na ni wajibu wa Waislamu leo ​​kufanya kazi katika kuregesha ufanisi na umoja wake, na kufanya kazi kwa umakini pamoja na watendaji kazi wenye ikhlasi kuhuisha Ummah na kusimamisha Khilafah Rashida ya pili kwa njia ya Utume ambayo Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alitoa bishara yake njema. Hawapaswi kuregeshwa nyuma na madai ya kuvunja moyo na kukata tamaa, wala ujanja wa Magharibi na zana zake. Badala yake, wanapaswa kujitahidi katika kazi yao na ulinganizi wao, wakimtegemea Mwenyezi Mungu na ushindi Wake kwa waja Wake waumini, na kujiamini wenyewe na Ummah wao na katika kile ulicho nacho cha vipengele na sifa zinazouwezesha kuchukua kiti cha izza kwa mara nyengine tena, Mwenyezi Mungu akipenda.

[وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْناً يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئاً وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ]

“Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na watao kufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu.” [An-Nur: 55]

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Bara’a Manasrah

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.