Jumapili, 06 Ramadan 1442 | 2021/04/18
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Hizb ut Tahrir: Chama Chenye Sifa za Kufikia Mabadiliko ya Kweli Katika Ardhi za Waislamu

[فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَنِ اتَّبَعَ هُدَايَ فَلَا يَضِلُّ وَلَا يَشْقَى * وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَى]
“Na ukikufikieni uongofu kutoka kwangu basi atakayeufuata uwongofu wangu, hatapotea wala hatataabika. Na atakaejiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu” [TaHa: 123-124]

Katika miaka 100 iliopita, ardhi za Waislamu hazikujua chochote isipokuwa kiza, vifo, maangamizi, ufukara na kukata tamaa. Mauwaji, mateso, ukandamizaji, ufidhuli na maafa yamefumwa kwenye msingi wa maisha ya watu katika eneo hili. Yote haya ni matokeo ya kuondoka kwa dola ya Khilafah, Mfumo wa Mwenyezi Mungu (swt), mnamo tarehe 28 Rajab 1342 Hijri, muwafaka na tarehe 3 Machi 1924 M.

Ili kumaliza mzunguko huu wa mateso yasio na huruma, ni lazima kuwepo na chama ambacho kimebeba uoni wa wazi katika kusimamisha tena Khilafah juu ya msingi wa njia ya Utume. Kiwe na sifa zinazohitajika kufikia lengo hili na kuleta mabadiliko ya kweli kwa ajili ya ardhi za Waislamu, na pia kwa dunia, ili kusibakie ndoto tupu kwenye karatasi. Makala hii itaonyesha namna Hizb ut Tahrir ilivyokusanya sifa zilizotajwa kufikia uoni huu, Bi-idhnillah.

Hizb ut Tahrir ni chama cha kisiasa cha Kiislamu, kilichoanzishwa mwaka 1953 Palestina na msomi maarufu na mwanafikra Sheikh Taqiudiin An-Nabhani kwa lengo la kurejesha njia ya maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha tena dola ya Khilafah. Chama hivi sasa kimeenea kwenye zaidi ya makumi ya nchi kikiwa na wanachama wake kwa waume walioenea kote katika ulimwengu wa Kiislamu na usio wa Kiislamu – kutoka Mashariki ya Kati hadi Ulaya, Asia hadi Afrika, bara la Australasia hadi Amerika. Wanachama wake ni kutoka mataifa tofauti, asili, madhehebu ya Kiislamu – ikiwemo Sunni na Shia, na kutoka nyanja zote za jamii – kama wanafunzi, walimu, wasomi, madaktari, vibarua, wake nyumbani, wanasheria, wanasayansi, wanahabari, na maafisa wa kijeshi – wote wakifanya kazi bila kuchoka kupitia harakati za kisiasa za kujitolea ili kufikia lengo tukufu. Zifuatazo ni baadhi ya sifa muhimu zilizojumuishwa na Hizb ut Tahrir kubadilisha uoni wake wa kufikia mageuzi ya kweli na kuwa uhalisia katika ulimwengu wa Kiislamu.

1. CHAMA KINACHOTAKA MABADILIKO YA KWELI LAZIMA KIJENGWE JUU YA MSINGI WA UISLAMU PEKEE

Sifa ya mwanzo na ya muhimu zaidi chama lazima kiwe nayo ili kusimamisha Khilafah na kuweka mustakbali mzuri kwenye ardhi za Waislamu ni kuhakikisha kuwa lengo lake, fikra zake, mikakati yake ya mageuzi, matendo yake katika kila ufafanuzi yawe yamejengwa juu ya Uislamu pekee, kwa kuwa hiki ni kigezo muhimu kwenye mafanikio, kama Mwenyezi Mungu (swt) alivyosema:

 [وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَأُوْلَـئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ]

“Na uwe kutokana na nyinyi ummah unaoligania kheri na unaoamrisha mema na unakataza maovu. Na hao ndio waliofanikiwa” [Al-Imran: 104].

Hizb ut Tahrir imeanzishwa kutokana na amri hii ya Mwenyezi Mungu (swt) yenye kusadikishwa sana kabisa ya kuwa mafanikio katika maisha haya na yajayo huamuliwa na kujifunga moja kwa moja na fikra, hukumu, na sheria za Uislamu na kuwa kisichokuwa hicho ni chenye kupelekea kushindwa – kama tulivyoshuhudia hayo wazi wazi katika miaka 100 iliopita tokea kuvunjwa kwa Khilafah. Muasisi wake, Sheikh Taqiudiin An-Nabhani ni Mujtahid Mutlaq, aliyejulikana miongoni mwa maulamaa wa wakati wake kwa upeo mkubwa wa elimu yake katika sheria za Uislamu. Alianzisha tokea mwanzoni mwa kuundwa chama nukta ambayo aliirejea rejea katika maandishi yake – kuwa Aqida ya Kiislamu ndio kiini, moyo, na siri ya uhai wa kundi na kuwa nguvu ya chama haitegemei wingi wa idadi bali katika usafi na uwazi wa fikra ya Kiislamu na kanuni katika thaqafa yake na katika akili za wanachama wake wabebaji wa da’wah yake – wakishikilia maneno ya Mwenyezi Mungu (swt), aliposema:

[وَمَن يُطِعِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَيَخْشَ اللَّهَ وَيَتَّقْهِ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْفَائِزُونَ]

“Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakamwogopa Mwenyezi Mungu na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu.” [An-Nur: 52].

Mafanikio hayapatikani kwa kulingania baadhi ya misingi michache katika katiba, au kulingania utekelezaji wa Sharia chini ya mwavuli wa mfumo usio wa Kiislamu wa demokrasia. Bali, mafanikio ya kweli yanahitajia chama kikumbatie, kama ifanyavyo Hizb ut Tahrir, mfumo wa kipekee wa kisiasa wa Kiislamu wa Khilafah juu ya msingi wa njia ya Utume, kwani hiki ndicho kigezo cha utawala kilichofafanuliwa na Mwenyezi Mungu (swt) kuwa ni njia pekee inayokubalika ya kutekeleza hukumu za Sharia. Chengine chochote kitaongeza tu maumivu na kutonesha vidonda vya Ummah huu.

2. CHAMA KINACHOLENGA MAFANIKIO LAZIMA KIWE NA UONI WA WAZI KWA AJILI YA MABADILIKO 

Sifa ya pili ambayo chama kinachotaka mafanikio lazima kiwe nayo ni uoni wa wazi wa mfumo mpya inaotaka kuujenga na mchanganuo wa namna utakavyotatua matatizo ya jamii. Haitoshi tu kuwa na kanuni zisizo wazi, sera zilizo na mashaka au malengo jumla kwa kuwa hakuna dola inayoweza kufanya kazi katika misingi dhaifu namna hiyo. Harakati yoyote ya kuleta mafanikio lazima iwe na ufafanuzi madhubuti wa misingi, sera, na sheria za namna itakavyoelezea matatizo kama ukandamizaji, ufisadi, umasikini, ukosefu wa kazi, kodi, jinai, kuongezeka kuporomoka kwa familia, huduma mbovu za Ummah, unyanyasaji wa wanawake, watoto na wazee, muamala mbaya kwa wale walio na dini tofauti, na masuala mengine. Lazima iwe na programu za hatua kwa hatua kwa ajili ya mabadiliko ya jamii na dola. Upungufu wowote utamaanisha kuufanya Ummah usiwe wenye kufikiri.

Uoni kwa ajili ya Khilafah ambao Hizb ut Tahrir inauonyesha hauegemei kwenye misingi isiojifunga, sera za mashaka, au malengo ya ujumla. Bali hukmu zake, nidhamu za kiuchumi, kijamii, elimu, na sheria, pamoja na sera zake za habari na za kigeni zimefafanuliwa kwa kina katika vitabu vyake na thaqafa yake ilio pana, na iliokusanywa katika kielelezo cha katiba kwa ajili ya dola ambayo imeichapa na ambayo iko tayari kwa utekelezaji HIVI SASA! Kila kifungu cha katiba yake kimewekewa dalili za wazi za Kiislamu na haina mshindani katika ufafanuzi wake. Wakati huo huo, thaqafa yake pana inaelezea sio tu asasi za kipekee za Khilafah bali pia namna dola itakavyoweza kutatua matatizo ya sasa yanayousibu Ummah na dunia.

Mfano vitabu kama, Nidhamu ya Hukmu katika Uislamu, na Nguzo za Dola katika Khilafah (Katika Hukmu na Utawala), vinaelezea namna ya kubadilisha muundo wa utawala wa kifisadi na kidikteta, ukiwa nidhamu yake ya utawala imejengwa juu ya usimamizi wa watu na misingi ya Kiislamu ya uwajibikaji, uwazi, utawala wa sheria, kiongozi aliyechaguliwa, na uhuru wa sheria na vyombo vya habari. Kitabu kama, Nidhamu ya Uchumi na Kijitabu, Kuelekea Utulivu wa Dunia Salama Chini ya Kivuli cha Nidhamu ya Uchumi wa Kiislamu kinaelezea suluhisho la Uislamu katika mgogoro wa kiuchumi unaoathiri mataifa ya dunia na namna ya kubadilisha mifumo ya kifedha isiyojimudu inayofukarishwa kwa madeni kuelekea kwenye uchumi wenye ustawi. Vinaelezea muelekeo wa Khilafah wa kupambana na umasikini jumla na ukosefu wa kazi kupitia sheria za Kiislamu kama kuharamisha miamala ya kifedha ya riba na badala yake kuwa na miamala ya mikataba inayoegemea mgawanyo wa hisa wa faida na hasara; kuharamisha ubinafsishaji wa mali asili kama mafuta, gesi, na maji ili kwamba watu wote washirikiane katika manufaa na mapato; nidhamu ya uadilifu ya kodi inayowatoza walio na mali zaidi ya mahitaji yao itumiwe kwa masikini wakati wa janga; na kuachana na nidhamu ya soko la hisa la kasino na badala yake kuwa na uwekezaji mkubwa wa dola katika uchumi halisi wa uundaji, viwanda, na kilimo ambapo mapato yanayopatikana yatatumika kwenye miundo mbinu na majengo ya elimu ya Ummah ya daraja ya juu na mfumo wa huduma za afya – huduma ambazo Uislamu unazichukulia kuwa ni za msingi kwa ustawi wa jamii yoyote na haki za msingi za kila mtu – mwanamume na mwanamke, Muislamu na asiye Muislamu.

3. CHAMA KINACHOEGEMEA JUU YA UAMINIFU BILA MARIDHIANO 

Sifa ya tatu ambayo chama kinahitaji kuwa nayo ili kusimamisha Khilafah ni uaminifu katika njia yake, kwa Ummah huu, na kwa Mwenyezi Mungu (swt), kikikataa kabisa kufanya mapatano juu ya misingi yake au lengo. Hizb ut Tahrir inajulikana duniani kote kuwa ni chama kisichoyumbishwa katika kung'ang'ania kwake misingi ya Kiislamu na ushupavu wake katika kukataa mapatano juu ya maadili yake ya Kiislamu licha ya upinzani inayokumbana nayo kwenye fikra yake, kauli na matendo au matokeo juu ya kazi zake au wanachama wake. Chama hiki, hakiamini katika ahadi za manufaa ya kiuchumi ya muda mfupi kwa watu ili kupata uungaji mkono wao, bali ni kuwalingania Waislamu kuikumbatia itikadi ya Kiislamu na mfumo ambao sio tu utaleta mafanikio katika dunia hii bali pia katika Akhera. Chama hiki, hakiamini katika kusema kile ambacho watu wanataka kukisikia ili kiweze kujijengea mchezo wa umaarufu, bali kuzungumza ukweli na kuuhifadhi Ummah huu na Dini yake muda wote. Hii hujumuisha kuzungumza bila uoga dhidi ya fikra zisizo za Kiislamu zinazotawala na hisia miongoni mwa jamii, au matendo yasio ya Kiislamu na hukumu za viongozi maarufu, licha ya kuwa ni dhidi ya maono ya Ummah au kupata ghadhabu za watawala.

Hii ni kwa sababu Hizb ut Tahrir ni chama ambacho hakihitajii utawala kwa sababu tu ya utawala wenyewe bali kupata mamlaka kwa ajili ya Uislamu. Na kwa kuwa Uislamu haupindi, hauinami au kuvunjika kwa mbinyo wa yeyote – basi pia kwa chama hiki ambacho kimetoa maisha yake kusimamisha na kuihifadhi Dini hii. Tokea kuanzishwa kwake, chama kimekumbana na vitisho, vishawishi, kashfa na vikwazo vyengine vingi katika kubeba da’wah yake. Lakini bado hakijakengeuka kutoka katika lengo lake la Uislamu, misingi yake, njia yake hata kwa kiwango kidogo. Wanachama wetu – wake kwa waume – wamekumbana na changamoto nyingi katika kuibeba Da’wah hii – ikiwemo kufukuzwa kazi, kufukuzwa kutoka vyuo vikuu, na kuzuliwa uongo dhidi yao ili kuwadhibiti waache ulinganizi. Pia wamekuwa wakipitiwa na mateso ya kikatili, yakiwemo kushambuliwa mara kwa mara, kufungwa, kuteswa na kuuliwa na watawala kwa ajili ya fikra zao. Wanachama wetu wamejaza magereza ya Misri, Tunisia, Syria, Iraq, Jordan, Libya, Urusi, Asia ya Kati na duniani kote chini ya udikteta wa kisekula wanaopigana dhidi ya wito kwa ajili ya Uislamu katika ardhi zao. Nchini Libya, wakati chama kilipopingana wazi na Gaddafi kwa kukataa kwake Sunnah – mtawala huyu katili aliwauwa wanachama wetu 13. Baadhi aliwanyonga hadharani katika maeneo ya shule na vyuo mbele ya wanafunzi wao, walimu, familia na watoto. Nchini Pakistan, Bangladesh, na Asia ya Kati idara za usalama zimewafunga makumi ya wanachama wetu – wake kwa waume. Wengi wameteswa vikali ikiwemo kuchomwa, kuunguzwa, kupigwa kwa mijeledi na waya, unyanyasaji wa kijinsia, na hata kuunguzwa ndani ya maji moto hadi kufa.

Lakini licha ya yote hayo, wanachama wetu wameendelea kubeba da’wah hii kwa kujitolea bila kusita. Kwa nini? Kwa sababu hawalikusudii pato la kupita la ulimwengu, wala maslahi binafsi, au utukufu binafsi au bahati – wanafanya bidii katika njia hii kwa ajili tu ya Fii-sabilillah, kutaka sio chengine bali malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt), na kwa sababu kila wanachama katika chama hiki amekula kiapo (Qasam) mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa Mlinzi wa Dini hii na Ummah huu.

4. KILA CHAMA CHA KULENGA MAFANIKIO LAZIMA KIFAHAMU UWANJA WA SIASA ZA KWELI  

Sifa ya nne ambayo chama lazima kiwe nayo ili kisimamishe Khilafah ni ufahamu wa wazi wa maeneo ya siasa. Hizb ut Tahrir imeingia kwenye eneo la siasa za kweli tokea kuanzishwa kwake zaidi ya miongo 6 iliopita: Siasa za Kiislamu – ambazo haziegemei juu ya uongo, kujifikiria binafsi, ukorofi, na tabia ya ufisadi wa siasa za kisekula ambazo zinautaabisha ulimwengu wa Kiislamu na usio wa Kiislamu, lakini ‘siyasa’ zinazoegemea juu ya msingi wa ukweli wa dhati kusimamia mambo ya watu kwa mujibu wa misingi ya Uislamu na sheria.

Kikiwa ni chama cha kisiasa za Kiislamu, siasa imekuwa ni chakula chake cha kila siku na kazi ya chama na wanachama wake tokea mwanzo wake. Kwa miongo kadhaa, wanachama wetu wamekuwa wakiishi sambamba na watu wa ardhi/nchi zao, wakizihisi fikra zao, maono na kukata tamaa, na wakivumilia uonevu, umasikini na matatizo ya raia wenzao. Kwa miongo kadhaa wamelingania kumalizika kwa ukoloni wa Kimagharibi na uingiliaji katika ulimwengu wa Kiislamu, wakiyahami maslahi ya Ummah, na wakiwataka watawala wa Waislamu kuwajibika kwa kupuuza kwao kushughulikia mambo ya watu wao na kwa ushirikiano wao na serikali za kigeni dhidi ya Uislamu. Na kwa miongo kadhaa wanachama wetu wameyachukua masuala ya siasa, uchumi, jamii, elimu, na sheria yanayowagusa Ummah, wakiibua masuluhisho ya uwazi ya Kiislamu, na kuwalingania watawala wa ulimwengu wa Waislamu kutekeleza Dini. Kauli zisizohisabika, matoleo rasmi ya chama, makala, mazungumzo, semina, makongamano na matukio mengine yamefanyika juu ya kadhia hizo katika maeneo tofauti ambayo chama kipo, kikifichua njama na ajenda za serikali za kikoloni dhidi ya Uislamu na ardhi za Waislamu, ikikazia sababu za matatizo yanayoathiri Waislamu na dola, na kuuongoza Ummah katika njia sahihi ya siasa za Kiislamu kushughulikia masuala yao yote.

Hizb ut Tahrir kwa hiyo ni chama kilicho na ufahamu wa kisiasa, fikra za kisiasa, na utambuzi wa kisiasa kuuelezea Ummah kwa ufanisi masuala ya ulimwengu wa Kiislamu.

5. KIWE NA MIKAKATI YA WAZI NA SAHIHI KUFIKIA MABADILIKO HALISI

Na mwisho, chama ambacho kinataka kusimamisha Khilafah lazima kiwe na mikakati ya wazi ya namna ya kufikia lengo hili. Kila uoni wa Kiislamu unahitaji mkakati wa Kiislamu kwa ajili ya mabadiliko. Hizb ut Tahrir kwa hiyo imejipanga katika njia yake kufikia Khilafah ikitegemea Sira ya Mtume (saw), ikifuata njia ya kifikra na kisiasa  iliosimamisha dola ya mwanzo ya Kiislamu Madina. Upande wa kifikra wa njia ya Hizb ut Tahrir wa kusimamisha Khilafah inahusisha kuzikosoa fikra zisizo za Kiislamu za jamii kama Urasilimali, demokrasia, usekula, utaifa, Ujamaa, na fikra ya uhuru kwa kuangazia kasoro zake, hatari na kufeli, na kuulingania Ummah kuzikumbatia fikra, sheria na Mfumo wa Mwenyezi Mungu (swt) badala yake. Mapinduzi yoyote mwanzoni yanahitaji matayarisho msingi ya uungwaji mkono wa Ummah na mchakato wa kubadilisha fikra jumla za watu na hisia zao kuelekea kwenye fikra na hisia juu ya msingi wa Uislamu ambazo zitaleta mabadiliko ya kudumu ya jamii.

Upande wa kisiasa wa njia ya Hizb ut Tahrir ya mabadiliko ni kufichua mipango ya wakoloni dhidi ya Uislamu na kukosoa mifumo isiyo ya Kiislamu ya kidhalimu na hukumu za watawala katika ulimwengu wa Kiislamu na kutoa wito wa kuondolewa. Kwa mujibu wa Sira ya Mtume (saw), njia ya chama ya kusimamisha Khilafah pia inahusisha kutaka Nussra (nguvu za kimada) kutoka kwa wenye nguvu za kijeshi. Hivyo inatoa wito kwa wale walio katika majeshi ya Waislamu kuondosha tawala hizi za kifisadi zisizo na uwezo na kuulinda Mfumo wa Mwenyezi Mungu (swt).

Hizb ut Tahrir inaamini kwa ushupavu kabisa katika mabadiliko ya msingi na yaliokamilika katika kurejesha Khilafah badala ya mabadiliko ya hatua kwa hatua, kwa kuwa hii ndio Sunnah ya Mtume wetu (saw) aliyeukubali uongozi wa dola wakati tu alipokinaika juu ya uwezo wake kutawala kwa Uislamu pekee na sio kugawanya mamlaka pamoja na ukafiri katika namna zote. Zaidi ya hivyo, haiwezekani kujenga nyumba mpya, imara, iliomakinika juu ya msingi uliyooza. Bali, tunahitaji kuyang'oa mabaki yote ya tawala za zamani, kubomoa misingi na nguzo za mifumo ilioundwa na wanaadamu ambayo imeenea kwenye ardhi zetu na kusimamisha msingi wa kipekee, taasisi, na muundo wa Khilafah mahala pake. Kwa kweli, mabadiliko ya hatua kwa hatua si chochote bali ni hadaa zinazozuia mabadiliko ya kweli. Ni mabadiliko yanayobakisha hali ilivyo kama tunavyoyashuhudia kwa miongo kadhaa katika nchi tofauti ambamo harakati zimejaribu kuleta mabadiliko ya Kiislamu kwenye nchi zao kupitia mabadiliko ya hatua kwa hatua na kujiingiza katika nidhamu isio ya Kiislamu ya kidemokrasia, ambayo imejionesha kuwa isioleta matunda yoyote.

Hizi ni baadhi tu ya sifa ilizonazo Hizb ut Tahrir zinazoiwezesha kuuongoza Ummah katika kusimamisha Khilafah kwa Msaada wa Mwenyezi Mungu (swt) na kuleta mabadiliko ya kweli kwenye ardhi za Waislamu. Ni chama kisichowadanganya watu wake, hakitosaliti imani ya Ummah wa Kiislamu na kitawakilisha vyema maslahi na matarajio yao. Kina uwezo wa kweli wa kuzikomboa ardhi za Waislamu na Ummah wote wa Waislamu kutoka katika hali ya sasa ya ukandamizaji kupitia Uislamu. Kwa hivyo wapenzi kina kaka na kina dada! Tunakuiteni katika kujibu Wito wa Mwenyezi Mungu (swt) na kujiunga na kazi yetu tukiwa Hizb ut Tahrir, kusimamisha mfumo huu mkubwa, Khilafah Rashidah ya pili kwa njia ya Utume katika dunia hii – mfumo utakaounganisha ardhi za Waislamu, kuzima ufisadi, uongo, na ukandamizaji na kusimamisha mahala pake mapambazuko mapya ya haki na heshima kwa ajili ya Ummah huu, na naam kwa wanaadamu wote.

 [يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اسْتَجِيبُواْ لِلّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُم لِمَا يُحْيِيكُمْ وَاعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ يَحُولُ بَيْنَ الْمَرْءِ وَقَلْبِهِ وَأَنَّهُ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ]

"Enyi mlioamini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume wake anapokuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele.  Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu  huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye tu mtakusanywa." [Al-Anfal: 24]

#أقيموا_الخلافة

#ReturnTheKhilafah

#YenidenHilafet

#خلافت_کو_قائم_کرو

 Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Dkt. Nazreen Nawaz

Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu