Afisi ya Habari
Ardhi ya Baraka-Palestina
| H. 16 Jumada II 1447 | Na: BN/S 1447 / 11 |
| M. Jumapili, 07 Disemba 2025 |
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Mamlaka ya Kihalifu ya Palestina, ikiwemo Wizara ya Masuala ya Wanawake, Yakimbilia Kutekeleza Miradi ya Maadui wa Uislamu ya Kuharibu Familia, Kuvunja Jamii, na Kumponda Mwanamke wa Kiislamu Anayezaa Mashujaa
(Imetafsiriwa)
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Masuala ya Wanawake ilifichua kwamba Wizara hiyo ilifanya warsha pamoja na Kamati ya Mpito ya Kuandika Katiba ili kujadili sifa za kuzifanyia kazi kwenye rasimu ya katiba na kuingiza masuala ya wanawake katika vifungu vyake. Kulingana na taarifa hiyo: “Kwa ushiriki mpana kutoka kwa taasisi rasmi na za kiserikali, taasisi za wanawake na haki za binadamu, na mashirika ya kiraia, na kwa uhudhuriaji mkubwa kutoka kwa viongozi wanawake wa Kipalestina walioko ughaibuni nchini Syria, Jordan, Lebanon, Misri, na Ulaya, Wizara ya Masuala ya Wanawake ilifanya warsha pana ya kitaifa kwa ushirikiano na Kamati ya Mpito ya Kuandika Katiba ya Palestina, kama sehemu ya kuimarisha mazungumzo ya kitaifa kuhusu kuandika katiba inayoakisi matarajio ya watu wa Palestina na kuhakikisha uwepo changamfu wa masuala ya wanawake katika maudhui yake.”
Warsha hii ilikuja baada ya amri ya sheria iliyoanzisha kamati ya katiba, ambayo ilieleza kwamba wajumbe wa kamati hiyo watajumuisha wawakilishi wa asasi za kiraia na kijinsia.
Leo, Mamlaka ya Palestina imevuka mipaka na kuzidi kiwango cha mchemko cha watu wa Palestina ambao walipinga sheria zinazoegemea juu ya CEDAW. Imechukua kalamu nyeusi kufuta Sheria ya Maisha ya Kibinafsi pamoja na mabaki yaliyobaki ya hukmu za Kiislamu ndani yake na kuibadilisha kwa katiba iliyoandikwa na wanaharakati wa haki za wanawake na mashirika yenye tashwishi yanayofadhiliwa na kafiri ili kuangamiza kila kipengee cha Uislamu kuhusiana na uhusiano kati ya wanaume na wanawake na matokeo yake kwa familia.
[أَفَحُكْمَ الْجَاهِلِيَّةِ يَبْغُونَ وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّهِ حُكْماً لِقَوْمٍ يُوقِنُونَ]
“Je, wao wanataka hukumu za Kijahiliya? Na nani aliye mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu kwa watu wenye yakini?” [Surah Al-Ma'idah: 50].
Jambo hilo limedhihirika bila utata wowote. Taarifa hiyo ilibainisha kuwa Waziri wa Masuala ya Wanawake alithibitisha “umuhimu wa kujumuisha kanuni zilizo wazi zinazohakikisha usawa kamili kati ya wanawake na wanaume na kujitolea kwa mikataba ya kimataifa.”
Kifungu hiki kina fikra mbili ambazo zinagongana kabisa na hukmu za Uislamu. Usawa kamili kati ya wanaume na wanawake unamaanisha usawa katika ulezi, urithi, talaka, ndoa, ndoa ya wake wengi, na majukumu ya wanaume na wanawake. Usawa huu unakinzana na maandiko mahususi ya Qur’an:
[الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّهُ بَعْضَهُمْ عَلَى بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ]
“Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Mwenyezi Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayo yatoa.” [Surah An-Nisa: 34]
[يُوصِيكُمُ اللَّهُ فِي أَوْلَادِكُمْ لِلذَّكَرِ مِثْلُ حَظِّ الْأُنثَيَيْنِ]
“Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili.” [Surah An-Nisa: 11]
[فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ]
“basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wanne.” [Surah An-Nisa: 3]. Hili pia linagongana na maandiko ya Mtume (saw) ambayo yalimpa baba au sawa naye usimamizi. Mtume (saw) amesema: «أَيُّمَا امْرَأَةٍ نُكِحَتْ بِغَيْرِ إِذْنِ وَلِيِّهَا فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ، فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ، فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ، فَإِنْ أَصَابَهَا فَلَهَا مَهْرُهَا بِمَا أَصَابَهَا، وَإِنْ تَشَاجَرُوا فَالسُّلْطَانُ وَلِيُّ مَنْ لَا وَلِيَّ لَهُ» “Mwanamke yeyote anayeolewa bila idhini ya msimamizi (walii) wake, ndoa yake ni batili, ndoa yake ni batili, ndoa yake ni batili. Akimuoa, basi ana haki ya mahari kwa sababu amemuoa. Na wakigombana, basi mtawala ndiye walii wa yule ambaye hana walii.” (Sunan Abu Dawood / Mustadrak al-Hakim)
Kujitolea kwa mikataba hii ni kuhukumu kwa Taghut na uasi dhidi ya hukmu za Uislamu:
[أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُوا بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَنْ يَتَحَاكَمُوا إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُوا أَنْ يَكْفُرُوا بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَنْ يُضِلَّهُمْ ضَلَالًا بَعِيدًا * وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا إِلَى مَا أَنْزَلَ اللَّهُ وَإِلَى الرَّسُولِ رَأَيْتَ الْمُنَافِقِينَ يَصُدُّونَ عَنكَ صُدُودًا]
“Huwaoni wale wanao dai kwamba wameamini yale yaliyo teremshwa kwako na yaliyo teremshwa kabla yako? Wanataka wakahukumiwe kwa njia ya upotofu, na hali wameamrishwa wakatae hayo! Na Shet'ani anataka kuwapotezelea mbali. Na wanapo ambiwa: Njooni kwenye yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, na njooni kwa Mtume; utawaona wanaafiki wanakukwepa kwa upinzani.” [Surah An-Nisa: 60–61].
Mikataba hii — ikiwemo CEDAW — imefanya uzinzi kuwa haki kwa wanaume na wanawake, kuhalalisha ushoga, kuruhusu utoaji mimba, na kuharamisha usimamizi wa wanaume juu ya wanawake. Taarifa hiyo pia inataja hatua za kivitendo: “Kila mtu alikubali kwamba katiba lazima ihakikishe waziwazi masuala ya wanawake, watoto, na familia.” Huu ni utekelezaji wa kivitendo wa Sheria ya Ulinzi wa Mtoto na Sheria ya Ulinzi wa Familia ambayo Mamlaka ya kihalifu ya Palestina imekuwa ikiifanyia kazi kwa miaka mingi, ili kuzifanya sheria hizi kuwa sehemu ya katiba na msingi wa Sheria ya Maisha ya Kibinafsi.
Warsha na makongamano haya ikiwemo kongamano la Chuo Kikuu cha Al-Quds, ambalo waandaaji waliligeuza (kwa ushiriki wa vyuo vikuu na taasisi zengine) kuwa pango la njama za Magharibi dhidi ya Uislamu, familia, na staha yote yanaelekea upande mmoja: kubomoa Sheria ya Maisha ya Kibinafsi, kuharibu maadili na staha ya Kiislamu, kubomoa familia, kukuuza uzinzi na upotovu, na kulazimisha muundo wa Kimagharibi wa maisha ya uovu na maangamivu.
Warsha hizi zinazoandaa rasimu ya katiba ya mpito kwa ajili ya kinachoitwa Dola ya Palestina ambayo haina uhai halisi uwanjani si kitu chengine ila ni zana za kubomoa elimu, familia, wanawake, na watoto, uharibifu ambao si mdogo kuliko mauaji ya nafsi za watu nchini Palestina, bali ni mkali zaidi:
[وَالْفِتْنَةُ أَكْبَرُ مِنَ الْقَتْلِ]
“Na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa.” [Surah Al-Baqarah: 217]
[وَالْفِتْنَةُ أَشَدُّ مِنَ الْقَتْلِ]
“fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa.” [Surah Al-Baqarah: 191].
Watu wa Palestina lazima waamke na kusimama pamoja dhidi ya njama hizi zinazofuatana, kwani hatari hii haitasaza nyumba yoyote, wala haitatofautisha kati ya mwanamume na mwanamke. Ni moto wa sheria za ukafiri uliounguza jamii zao, na Magharibi imeelekeza miale yake kwa Waislamu kupitia serikali, watawala, na mashirika yenye tashwishi.
Na moto huu hauko tu kwa watu wa Palestina pekee, unawaka katika nchi zote za Kiislamu. Kama vile ilivyo faradhi kwa Ummah kuwakomboa watu wa Palestina kutoka kwa makucha ya Mayahudi, pia ni faradhi kuwakomboa wao na wenyewe kutokana na tawala zinazowasukuma kwenye mitego ya makafiri na kupotea kwa dunia hii na Akhera.
[وَاللَّهُ يُرِيدُ أَنْ يَتُوبَ عَلَيْكُمْ وَيُرِيدُ الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الشَّهَوَاتِ أَنْ تَمِيلُوا مَيْلاً عَظِيمًا]
“Na Mwenyezi Mungu anataka kukurejezeni kwenye ut'iifu wake, na wanao taka kufuata matamanio wanataka mkengeuke makengeuko makubwa.” [Surah An-Nisa: 27].
Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir
katika Ardhi Iliyobarikiwa – Palestina
| Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Ardhi ya Baraka-Palestina |
Address & Website Tel: 0598819100 www.pal-tahrir.info |
E-Mail: info@pal-tahrir.info |



