Jumatano, 11 Rabi' al-awwal 1447 | 2025/09/03
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Mpango wa Mipaka ya Damu na Uhalifu wa Kujitenga kwa Darfur
(Imetafsiriwa)
Gazeti la Al-Rayah - Toleo 562 - 27/08/2025 M
Na Ustadh Muhammad Jami (Abu Ayman) *

Baada ya kuanguka kwa kutia shaka kwa miji mikubwa ya Darfur, na kuondolewa kwa jeshi kutoka kwao, mbele ya utekaji nyara wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), pamoja na kuzingirwa kwa nguvu na vikosi hivi katika jimbo la mwisho lililosalia, Darfur Kaskazini na mji mkuu wake, Al-Fashir, wakati jeshi likishindwa kuwafukuza, ghafula yanakuja mazungumzo ya serikali sambamba yakiongozwa nao huko Nyala, mji mkuu wa Darfur Kusini, ambao wanaudhibiti, kwa ushiriki wa vibaraka wa Amerika kama vile Al-Hilu, na uungaji mkono wake kwa serikali hii, hata kuwa naibu ndani yake ...

Haya yote yameibua katika akili za watu kile ambacho Hizb ut Tahrir imekuwa ikikariri mara kwa mara: kwamba kuna mpango wazi na kamili wa kukabidhi Darfur kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), chini ya ufadhili na ulinzi wa Marekani, kama sehemu ya mpango wake wa kuichana Sudan kupitia vibaraka wake miongoni mwa viongozi wa jeshi na RSF, kama ilivyofanya hapo awali kujitenga kwa Kusini kupitia vibaraka wake wawili,  Al-Bashir na John Garang.

Mpango wa Mipaka ya Damu uliibuka na ripoti iliyopewa jina la “Mpango wa Mipaka ya Damu”, iliyotayarishwa na Luteni Kanali Mstaafu wa Marekani Ralph Peters pamoja na ramani mpya ya Mashariki ya Kati. Ilichapishwa katika jarida la kijeshi la Marekani, Jarida la Jeshi, mwaka 2006, ambapo jenerali huyu aliligawa eneo hilo katika dola ya Sunni, Shia, na Wakurdi, pamoja na kile alichokiita “Dola Takatifu ya Kiislamu” inayojumuisha Harramayn (Makka na Madina) huru kutoka Saudi Arabia, pamoja na kile alichokiita Jordan Kubwa na dola zengine ndogo. Kulingana na madai yake, kugawanya eneo hilo kwa misingi ya kimadhehebu na kikabila, ili kila dhehebu au kabila liishi kivyake katika nchi yake huru ya kisiasa, kungekomesha ghasia katika eneo hili.

Hata hivyo, inaweza kusemwa kwamba mpango wa dola za kikoloni za kuzigawanya ardhi za Waislamu ni wa zamani, zikiongozwa na Uingereza na Ufaransa, kama ilivyo katika makubaliano kati ya wajumbe wa utumishi wa kigeni wa Uingereza na Ufaransa, Mark Sykes na Georges Picot, wa kuchonga ardhi za Kiislamu, baada ya kuvunjwa kwa Khilafah, katika kile kilichojulikana kama makubaliana ya Sykes-Picot ya 1916. Baadaye, Amerika iliingia katika mbio hizi za kikoloni ili kuwadhoofisha Waislamu, na kupora rasilimali zao, kwa kutekeleza kanuni ya gawanya na utawale. Lengo hili limefuatiliwa kwa njia ya mgawanyiko na usambaratishaji kwa visingizio vya kujitawala wenyewe, uhuru, shirikisho, na dhana zinazofanana, na vile vile kwa kutumia suala la makabila madogo na madhehebu madogo. Miongoni mwa njama mashuhuri zaidi za hivi karibuni ni mpango wa Bernard Lewis, mwanafikra wa Kizayuni na mshauri wa utawala wa Rais George H. W. Bush wa Marekani, Bush mwandamizi, uliolenga kuzigawanya nchi zote za Kiislamu katika miaka ya 1980. Mpango wake ulijumuisha kuigawanya Sudan katika sehemu nne: Dola ya Nubian na Aswan kama mji mkuu wake, Dola ya Sudan katikati, Dola ya Darfur, na Dola ya Sudan Kusini. Eneo pekee ambalo mpango huu ulifanikiwa ni Sudan kupitia kujitenga kwa Kusini yake.

Marekani ilifungua njia ya kujitenga kwa Darfur wakati wa utawala wa kibaraka wake Al-Bashir kupitia Mkataba wa Doha, unaoitwa “Hati ya Doha ya Amani huko Darfur,” ambao ulitiwa saini na serikali ya Sudan na Vuguvugu la Ukombozi na Haki mnamo 14 Julai 2011. Jambo la hatari zaidi ndani yake lilikuwa kile kilichoitwa kugawanya mali, pamoja na Khartoum na serikali ya Darfur hadhi ya kiutawala ya eneo hilo, ambapo iliamuliwa kuelekea kwenye kura ya maoni ili kubainisha kitambulisho cha Darfur ikiwa itakuwa jimbo moja au dola kadhaa. Kulingana na Mkataba wa Doha, mamlaka ya kikanda yalianzishwa huko Darfur, ambayo ilimaanisha kuiweka Darfur katika hadhi maalum tofauti na Sudan iliyo bakia. Hili ndilo hasa lililotokea na Kusini hapo awali, kabla ya kujitenga kwake.

Miongoni mwa uthibitisho mkubwa wa kutekelezwa kwa mpango wa kuisambaratisha Sudan ni kauli za rais aliyepinduliwa Al-Bashir na maafisa wa utawala wake wenyewe. Mnamo tarehe 25 Novemba 2017, Tovuti ya Urusi Sputnik ilichapisha mahojiano na Rais Al-Bashir wakati wa ziara yake nchini Urusi, ambapo alisema, “Shinikizo na njama za Marekani dhidi ya Sudan ni kubwa... Chini ya shinikizo la Marekani, Sudan Kusini ilijitenga, ikimaanisha kuwa Sudan iligawanyika. Mgawanyiko huo ulitokana na shinikizo na njama za Marekani, na mpango wa Marekani ni kuiangamiza Sudan na kuigawanya katika dola tano.”

Vile vile, Shirika la Anadolu liliripoti mnamo tarehe 13 Aprili 2017 kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Ibrahim Ghandour, alisema, “Kutenganishwa kwa Kusini ilikuwa njama, lakini tulikubali.” Alisema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege, akimjibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov. Lavrov alisema siku iliyotangulia, wakati wa mkutano na waandishi wa habari na mwenzake wa Marekani Rex Tillerson, kwamba, “Utawala wa Obama uliiomba serikali ya Omar Al-Bashir kukubali kugawanywa kwa Sudan katika sehemu mbili kama suluhisho la matatizo yake, kwa badali ya kutompeleka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.”

Lavrov aliongeza kuwa utawala wa Obama hata uliiomba serikali ya Urusi wakati huo kupata kibali cha Al-Bashir kujitenga, licha ya hamu yao kutaka kumwona akihukumiwa katika mahakama ya ICC. Alihitimisha, “Kujitenga kwa Kusini ulikuwa mradi wa Amerika ulioanzishwa na utawala wa Obama.”

Mnamo tarehe 21 Novemba 2018, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Al-Dirdiri Mohamed Ahmed, katika mahojiano na France 24, alisema kuwa nchi yake “imeisaidia Amerika katika kutatua mtanziko mkubwa katika eneo hilo, ambayo ni Sudan Kusini.”

Kwa hivyo, vita vilivyoanza mnamo 15 Aprili 2023, vilizuka kwa kutiliwa shaka kati ya vikosi viwili ambavyo, kimsingi, viliundwa kutoka chanzo kimoja, na viongozi wao wakifuatana chini ya ushawishi wa Amerika. Matukio kisha yaliongezeka kwa kujiondoa kwa jeshi mbele ya Vikosi vya Msaada wa Haraka, bila sababu za kuridhisha, hadi mambo yakafikia kukaliwa kwa miji yote mikubwa ya Darfur, na sasa wa mwisho umezingirwa. Hii ilifuatiwa na kuasisiwa kwa serikali iliyojitenga na nchi yote iliyosalia, ambayo ni ushahidi wa wazi wa dhamira iliyopangwa nyuma ya mpango huu muovu.

Ishara na ushahidi wote unathibitisha kwamba vibaraka wa Amerika nchini Sudan wanafanya kazi kwa nguvu kutekeleza mpango wa kuisambaratisha Sudan, kutumia vita hivi vibaya, na watu kutofahamu njama hii chafu.

Kwa hiyo ni wajibu kwa watu wa Sudan, hasa wale wenye nguvu za kijeshi na ushawishi miongoni mwao, kama vile maafisa wa jeshi, viongozi wa Ummah, na watu wake wenye ushawishi kusimama kama kizuizi imara dhidi ya mpango huu. Hili linaweza kufikiwa tu kwa kupitishwa kwa mradi wa kimfumo ambao unafichua njama hii na kulinda maslahi ya Ummah. Na mradi huo unaweza tu kuwa mradi mtukufu wa Uislamu na dola yake, Khilafah Rashida kwa Njia ya Utume. Kwani hiyo  pekee ndiyo iliyo na suluhisho, tiba na njia ya kutokea.

Aliyenyimwa ni yule ambaye anajishughulisha na kitu chengine chochote, na akafa bila ya bay’ah ya Kisharia (kiapo cha utiifu) kwa Khalifa Rashid (Khalifa Mwongofu) ambaye anaisimamisha Dini na kutabikisha Shariah.

Mtume (saw) amesema, «وَمَنْ مَاتَ وَلَيْسَ فِي عُنُقِهِ بَيْعَةٌ مَاتَ مِيتَةً جَاهِلِيَّةً» “Mwenye kufa bila ya kiapo cha utiifu juu ya shingo yake amekufa kifo cha Kijahiliya.” (Imepokewa na Muslim).

* Msaidizi wa Msemaji wa Hizb ut Tahrir katika Wilayah Sudan

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu