Jumapili, 22 Muharram 1446 | 2024/07/28
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Utawala wa Marekani: Sura Mpya lakini zenye Njama Zilezile

Habari:

Waziri wa Mambo ya Nje wa Amerika Antony Blinken ataizuru Kenya, Nigeria na Senegal kuanzia Novemba 15-20, akisisitiza umuhimu wa mahusiano yao na washirika wa barani Afrika. (The Star, 12/11/2021).

Maoni:

Kwa mara nyingine tena utawala wa Marekani umemtuma mwanadiplomasia wake mkuu barani Afrika kibinafsi baada ya kuzuru Kenya na Nigeria kimtandao mnamo Aprili 2021. Hata hivyo, mara hii Senegal imejumuishwa katika ziara. Ni muhimu kuweza kuzishughulisha akili zetu kwa kujiuliza maswali yafuatayo: 1 –nini kilichonyuma ya ziara hii? 2 – kwa nini kuyazuru mataifa hayo matatu maalumu? 3 – nani anatarajiwa kunufaika zaidi katika ziara hii? 4 – mataifa hayo matatu na Amerika ni washirika katika nini? Maswali hayo manne yatajibika kimakosa lau tutazizingatia taarifa zilizotumwa kwa ummah kupitia vyombo vikuu vya habari ambavyo hupokea malipo ili kupigia debe propaganda za serikali.

Kwa hakika, ziara hii sio chochote bali ni kampeni ya kidiplomasia ya ukoloni mamboleo inayolenga kukazanisha vitanzi katika shingo za watawala vibaraka barani Afrika, ili waendelee kujifunga na mchoro unaoongozwa na mkaazi mpya wa Ikulu ya White House. Mchoro ambao unajumuisha kuyatia pingu mataifa ili kushikamana na mungu aliyefeli wa demokrasia, nidhamu huria ya kijamii, nidhamu ya kiuchumi iliyojikita katika riba na ukandamizaji miongoni mwa maovu mengine yanayo endelea kusababisha majanga yasiyohesabika kwa wanadamu duniani kote. Kwa kuongezea, utawala wa Marekani unakwenda mbio kuzipiku hatua zilizopigwa na utawala wa Uchina barani Afrika.

Mataifa hayo matatu yanacheza dori muhimu katika maeneo yao na barani Afrika kwa ujumla. Kenya ndio kituo cha uchumi wa eneo la Afrika Mashariki na Kati ikiwa haina mshindani. Nigeria ndio yenye uchumi mkubwa na idadi kubwa ya watu barani Afrika. Rais wa Senegal anatarajiwa kuingia katika cheo cha juu katika uongozi wa Muungano wa Afrika (AU). Fauka ya hayo, mataifa hayo matatu yamebakia kuwa watiifu kwa mabwana zao wakoloni ambao ni Uingereza na Ufaransa. Kwa hiyo, Amerika inatambua umuhimu wa mataifa haya na imewekeza juhudi zake ili kuzitoa kutoka kwa washindani wenza wa kikoloni.

Utawala wa Marekani kwa kuwa ndio wenye usemi duniani inatarajiwa kunufaika zaidi kutokana na ziara hiyo. Hata hivyo, mataifa watumwa yatanufaika kutokamana na makombo machache watakayopewa na bwana mkoloni. Amerika itanufaika kupitia utekelezaji wa mikataba mingi itakayotiwa saini nyuma ya pazia na ambayo itayafadhilisha makampuni ya Marekani pasina kuzingatia viwanda vya nchini. Na wakati huo yakitoa mwanya zaidi kwa taasisi za kifedha za Marekani mfano Benki ya Dunia na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa kuendelea kufanya uharibifu kwa uchumi wa mataifa yaliyosalimu amri. 

Amerika na mataifa hayo matatu ni washirika katika kusababisha ufisadi duniani. Kilele cha kiwango cha ufisadi ni wao kuupiga vita Uislamu na Waislamu. Kwa pamoja wameubandikiza Uislamu kuwa ni itikadi kali na Waislamu ni wenye misimamo mikali na magaidi. Hivyo basi, wameamua kuwakandamiza na kuwaua Waislamu kupitia kutunga na kutekeleza sheria na sera dhidi ya ugaidi na misimamo mikali! Kwa pamoja wanaukashifu Uislamu na kuuona kuwa ni wa kikatili na wa kizamani usioweza kutatua changamoto za karne hizi! Alas! Changamoto zilezile ambazo zimetokamana na kutekeleza mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali na mataifa yayo hayo!

Kwa kutamatisha, ziara hii haileti matumaini wala ustawi kwa Afrika. Badala yake ni ziara nyingine inayotekelezwa na sura mpya lakini zenye njama zilezile ambayo ni ziara ya kikoloni kuja kutathmini mashamba ya kikoloni yanayomilikiwa na washindani wa Marekani. Lau kutapatikana fursa, basi wajaribu kuwavutia wasimamizi wa shamba la kikoloni kwa vijipesa kwa jina la msaada wa kifedha miongoni mwa vivutio vingine ili kuuhamisha utiifu wao wa kikoloni. Lau hakuna fursa, basi angalau kutafuta japo uungwaji mkono katika kutekeleza ajenda ya Amerika iliyo na sumu ndani ya mataifa yao husika na ng’ambo. Sehemu ya ajenda ikijumuisha kupigana vita vya kiwakala vya Amerika.

Afrika itaendelea kutaabika chini ya mikono ya wakoloni Wamagharibi ambao wanatawala mataifa ya Afrika kupitia watawala vibaraka wa kikoloni. Watawala waovu ambao wanaiba mali za watu binafsi na za ummah na kisha kuzituma ng’ambo ilhali raia wamebakia wanateseka kwa umasikini wa kudumu. Kwa kuongezea, wanakula njama na yale yanayojiita ni mashirika ya Magharibi ambayo hudai kuwasaidia raia; lakini yapo kwa ajili ya kulinda hali iliyoko na kuwahadaa watu. Afrika imezama ndani ya dhiki. Kuchipuza kwa nidhamu mbadala ya uongozi ndio pekee itakayo dhamini kuondoka shidani. Nidhamu mbadala inayochipuza kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt) ni Khilafah kwa njia Utume. Khilafah italeta matumaini na ustawi wa kikweli sio tu kwa Afrika bali kwa dunia jumla. Itakuwa na uwezo wa kuyafanya hayo kupitia utekelezaji wake wa nidhamu tofauti za Kiislamu.

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu