Jumatano, 22 Rajab 1446 | 2025/01/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Fuliza M-Pesa, Riba Inayofululiza

Habari:

Wakenya walikopa kutoka  kwa mfumo wa FULIZA wa Safaricom shilingi bilioni 1.32 kila siku hii ikiwa ni kati ya mwezi Aprili na Septemba mwaka huu jambo linaloonesha wazi hali ya wakenya kutegemea mikopo kwa matumizi yao ya nyumbani. Hili lilidokezwa na shirika la Safaricom siku ya Jumatano tarehe 10 Novemba mwaka huu ambapo faida ya shilingi bilioni 37.055 iliandikishwa na Safaricom kwa nusu ya mwaka hadi mwezi wa Septemba iliongezwa zaidi na mapato ya M-Pesa. Ripoti ya matokeo ya kifedha ya shirika la Safaricom yanaonesha kwamba katika kipindi cha siku 183 pekee shirika hili liliweza kusambaza shilingi bilioni 242.6 ambayo hii ni asilimia 62.4 nyongeza ya kipindi sawa na hicho mwaka jana pale ilipotoa mkopo wa kitita cha shilingi bilioni 149.4 kupitia FULIZA.

Maoni:

Wazo la kuweka mfumo wa kuwezesha wakenya masikini na hata wenye pato la kadri, kupata mikopo kwa haraka nchini Kenya liliundiwa neno rahisi kulitamka la Kiswahili linalofahamika kama FULIZA kutoka kwa kitenzi cha kufululiza. Kampuni ya Safaricom inayomilikiwa na Kampuni kubwa ya mawasiliano ya Uingereza Vodafone, ilizindua rasmi mpango wa Fuliza mwaka 2019 unaomilikiwa na mashirika ya kifedha matatu Safaricom yenyewe na benki ya KCB ikimiliki kiwango sawa cha asilimia 40 huku benki ya CBA ikimiliki asilimia 20. Mpango huu huruhusu wateja wa Mpesa kufanikisha miamala yao ya kifedha endapo wanakabiliwa na uhaba wa fedha kwenye akaunti zao za Mpesa.

Fuliza ni mpango wa huduma ya kifedha kwenye akaunti yako ya MPESA inayokuwezesha kununua au kupata mkopo kupitia kwa Mpesa hata kama una uhaba wa senti. Ni mfumo maarufu wa Safaricom wa ukopeshaji unaoruhusu wateja kupata mkopo kupitia akaunti zao za Mpesa kufidia mapungufu ya fedha na mkopo huu unaofuata viwango vilivyowekwa. Kwa kiwango cha Riba inayotozwa cha asilimia 1.1 na ada ya huduma ya shilingi 30 kila siku, huduma hii ya Safaricom imevutia wakenya zaidi ya milioni 1.4 wanaokopa kila siku. Kiwango cha mkopo kinachokadiriwa kiasi cha kitita cha shilingi bilioni 1.34, huku Safaricom ikitaja kwamba ilipata nyongeza ya bilioni 1.2 kwa wakopaji ambacho kwa muda wa miezi sita hadi Juni mwaka huu hii ikiashiria upungufu wa mapato kwa wakenya unaowasukuma kutegemea madeni ya gharama ya muda mfupi.

Kwa ushindani wa soko na mabadiliko ya mara kwa mara ya uchumi wa mtaji, mara kwa mara Riba hubadilisha sura yake mbaya.  Miamala ya riba ambayo ni sawa na unyonyaji mkubwa wa jasho la watu na kuhujumu biashara ni yenye kwenda kinyume na Uislamu. Sheria ya Kiislamu imeainisha kwamba aina yoyote ya mapato ya ziada kwenye huduma za mikopo ni Riba. Hali zinazobadilika za riba na bima ya mipangilio mipya ya kifedha ya Kirasilimali na taasisi zake mbovu za kifedha zenye kuwa na mapato yaliyopangwa zinaendelea kuwaweka Waislamu katika hali tata wasijue msimamo halisi wa Kiislamu juu ya miamala hii.

Fuliza inaendana kikamilifu na muamala wa Riba hivyo kulingana na Uislamu aina hii ya muamala haufai kama ilivyoainishwa katika Qur’an Tukufu na Hadith za Mtume (ﷺ). Fuliza inaingia katika aina ya Riba iitwayo Riba Nasiia  ilioshamiri kwa zama za ujahilia ambayo mtu alitakikana kulipa malipo ziada ya ule mkopo aliupokea. Aina hii ya riba inatokana na riba iliyoamuliwa mapema ambayo mkopeshaji hupokea nyongeza ya kiasi cha alichokopesha. Ukopaji wa Fuliza ni aina ya riba inayotozwa mikopo ambayo leo imesheheni kote ulimwenguni.

Riba ambalo ni tamko la Kiarabu na kilugha humaanisha ziada, ongezeko au ukuaji. Kiupande wa kisheria Riba humaanisha kiasi cha ziada cha pesa apatacho anayekopesha. Aidha ziada yoyote aitoayo mkopaji kwa mkopeshaji. Kwa uchumi wa leo, riba huzunguka kama bei ya mkopo uliokopeshwa ili mtu aweze kupata mkopo huo. Katika mfumo wa benki leo kuingia kwa riba ya kinyonyaji kumegeuza pesa kuwa bidhaa ya biashara.

Al Imam Ghazal alisema: “Kufanya biashara ya pesa kwa lengo la kupata riba kunafanya pesa iwe ni bidhaa ya sokoni. Kushiriki aina hii ya biashara ni moja ya njia za unyanyasaji na sisi twajua wazi adhabu kali kwa wanaoamiliana na miamala ya riba. Kula riba ni mojawapo ya madhambi saba makuu yenye kuangamiza na ni sambamba na ushirika, uchawi, kuuwa nafsi iso na hatia, kula mali ya mayatima, kukimbia kwa uwanja wa mapambano (vita) na kumtuhumu kwa zinaa mwanamke mwenye staha.

Hakika ya wanaofanya miamala ya riba huibia watu mali zao kama vile ni miongoni mwa njia mbovu na biashara mbaya wanasubiriwa na adhabu ya moto.

ٱلَّذِينَ يَأْكُلُونَ ٱلرِّبَوٰاْ لَا يَقُومُونَ إِلَّا كَمَا يَقُومُ ٱلَّذِى يَتَخَبَّطُهُ ٱلشَّيْطَٰنُ مِنَ ٱلْمَسِّ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوٓاْ إِنَّمَا ٱلْبَيْعُ مِثْلُ ٱلرِّبَوٰاْ ۗ وَأَحَلَّ ٱللَّهُ ٱلْبَيْعَ وَحَرَّمَ ٱلرِّبَوٰاْ ۚ فَمَن جَآءَهُۥ مَوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّهِۦ فَٱنتَهَىٰ فَلَهُۥ مَا سَلَفَ وَأَمْرُهُۥٓ إِلَى ٱللَّهِ ۖ وَمَنْ عَادَ فَأُوْلَٰٓئِكَ أَصْحَٰبُ ٱلنَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَٰلِدُونَ

"Wale walao riba hawasimami ila kama anavyo simama aliye zugwa na Shet'ani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba. Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba. Basi aliye fikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akajizuia, basi yake ni yaliyo kwisha pita, na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye kurudia basi hao ndio watu wa Motoni, humo watadumu." [Al-Baqara 2: 275]

Ni muhimu kutambua kwamba Ummah unakabiliwa na matatizo ya kiuchumi na mashambulizi mengi ya fikra kutoka kwa hadhara ya Kimagharibi. Hili limeufanya ummah kukumbwa na matatizo ya kiuchumi ya mfumo wa Kirasilimali ambao uchumi wake umekita kwenye mizizi ya riba. Hivyo kazi kuu leo ni kuhuisha Ummah, kwa kuupa fikra sahihi za Kiislamu.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut-Tahrir na

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari Hizb ut-Tahrir Kenya

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu