Jumatano, 22 Rajab 1446 | 2025/01/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali
Mapinduzi ya Kijeshi Nchini Mali
(Imetafsiriwa)

Swali:

Baraza la Kijeshi nchini Mali lilitangaza mnamo Alhamisi jioni 27/8/2020 kuachiliwa huru kwa Raisi Ibrahim Boubacar Keita, kwa mujibu wa kile kilicho ripotiwa na shirika la Anadolu. Na jioni ya tarehe 18/8/2020, ikatangazwa kuwa mapinduzi ya kijeshi yamefanyika nchini Mali dhidi ya Raisi Ibrahim Boubacar Keita, na kwamba yeye na waziri wake mkuu, Bobo Cisse, wamekamatwa. Ni nani aliye nyuma ya mapinduzi haya? Je, yanahusiana na mzozo wa Amerika na Ulaya?

Jibu:

Ili kupata picha wazi tutahakiki mambo yafuatayo:

1- Tutalinganisha yale yaliyojiri leo na yale yaliyojiri nyuma, miaka minane iliyopita, kwa kuwa mapinduzi sawa na haya yalifanyika mnamo 22/3/2012 M, wakati kundi moja la maafisa wa ngazi za chini liliandaa mapinduzi dhidi ya Raisi Amadou (Ahmadu) Toumani Toure, ambaye wakati huo alikuwa amebakisha mwezi mmoja kumaliza muhula wake wa pili. Tulifafanua kwamba Amerika ilikuwa nyuma ya mapinduzi hayo, hivyo tukasema katika "Jibu la Swali" tulilolitoa mnamo 24/3/2012 M: [Yote yale tuliyoyataja yanaashiria kuwa Amerika ilikuwa nyuma ya mapinduzi yaliyofanyika nchini Mali ili kuingia ndani ya nchi hii ya Kiislamu na kupanua ushawishi wake juu yake na kumbadilisha mkoloni wake mkongwe wa Kifaransa, ambayo ingali inapanua ushawishi wake juu yake. Amerika ilitaka kuuvuruga uchaguzi unaokuja nchini Mali, kwa sababu kitovu hicho cha kisiasa kina nasibishwa na Ufaransa. Kupitia mapinduzi haya, meza ziligeuzwa kwa wachezaji ambao ni vibaraka wa Ufaransa, ambao walikubaliana na mchezo huo kwa mujibu wa sera ya Kifaransa. Ili, Mali ifungamanishwe na Amerika ambayo itadhibiti harakati za "jeshi"]. Leo, maafisa wa vyeo vidogo, cha juu zaidi kikiwa ni kanali, walianzisha mapinduzi dhidi ya Raisi Boubacar Keita, ambaye alichaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo 15/8/2013, na kuchaguliwa tena kwa muhula wa 12/8/2018. Wanajeshi hao walianzia kutoka kambi ya "Kati", ambayo iko umbali wa 15 km kutoka mji mkuu, na ni kambi iyo hiyo ambayo kwayo mapinduzi yalianzishwa mnamo 2012.

Baada ya mapinduzi ya Machi 2012, Ufaransa iliweza kuyapata maazimio ya Baraza la Usalama la UN ya kuingilia kaskazini mwa Mali, azimio 2071 la mnamo 23/9/2012 M na azimio jengine, 2085 la mnamo 20/12/2012 M ili kulinda ukoloni wake chini ya kisingizio cha kupigana na Al Qaeda na makundi yenye misimamo mikali! Majeshi 15,000 ya kimataifa yaliundwa, hususan kutoka Ufaransa na Ulaya, na majeshi ya Kiafrika, ambayo kwayo Ufaransa iliunda majeshi ya muungano ya Afrika yaliyoitwa Majeshi ya Sahel ya G5, ambayo ni kutoka Mauritania, Mali, Niger, Burkina Faso na Chad, ambako ushawishi wa Ufaransa una nguvu; iliweza kuregesha ushawishi wake chini ya mwaka mmoja na nusu baada ya mapinduzi ya 2012. Hii ilikuwa kwa kupitia uchaguzi wa Boubacar Keita mnamo 15/8/2013. Alichaguliwa tena kwa mara ya pili mnamo 12/8/2018! Ingawa Amerika haiko imara katika maduara maarufu kama Ufaransa, inao mwanya katika jeshi unaoiwezesha kufanya mapinduzi ya sasa kuwa imara zaidi kuliko mapinduzi yake ya awali mnamo 2012! Baada ya mapinduzi yake ya awali kufeli, ambayo yalimalizika chini ya mwaka mmoja na nusu kabla ya kufanyika, ilianza kufanya kazi kujishindia vibaraka katika kitovu hicho cha kisiasa na mashirika ya kijamii, sio tu jeshi pekee, katika jaribio la kuwa na kitovu maarufu ili kuyasaidia mapinduzi yake ya sasa.

2- Mnamo 19/8/2020, kiongozi mpya wa mapinduzi, Kanali Qasimi Quetta, alijiwasilisha kama kinara wa lile aliloliita "Baraza la Kitaifa la Ukombozi wa Watu" nchini Mali. Alionekana kwenye Runinga mnamo Jumanne jioni 18/8/2020 pamoja na kundi la maafisa waliotekeleza mapinduzi hayo. Walimchukua Keita, Waziri Mkuu Cisse, mawaziri wengine na maafisa ambao jumla ya idadi yao ni 17 hadi gerezani. Kisha wanajeshi hao wakamleta Keita katika runinga kutangaza kusalimisha utawala kwa jeshi. Alisema katika hotuba yake: "Hataki damu imwagwe ili abakie mamlakani." (Reuters 19/8/2020). Kanali Ismail Waghi, msemaji wa kundi la mapinduzi, alisema ("… nchi yetu inatumbukia katika ghasia, machafuko na utovu wa usalama, na hili sehemu kubwa ni kutokana na makosa ya watu ambao wanahusika na hatma yake." 

"Tutaunda baraza la mpito pamoja na raisi wa mpito, ambaye ima atakuwa mwanajeshi au raia. Tuko katika mawasiliano na mashirika ya kijamii, vyama vya upinzani, walio wengi na kila mmoja, ili kujaribu kupangilia mpito. Kamati ya Kitaifa ya Uokozi wa Watu – ambayo imeundwa leo na viongozi wa mapinduzi – iliongeza kuwa Baraza la Mpito lijumuishe wanajeshi 6 na raia 18, na kuendelea kuwa litacheza dori ya asasi mpito ya utunzi wa sheria, maadamu raisi wa baraza hili atachaguliwa na wanachama wake." (Al-Jazeera 21/8/2020).

Hapa, inaonekana kwamba wanajeshi walipanga mapinduzi hayo pamoja na wanasiasa na makundi ya upinzani, ikiwemo yale yanayoitwa mashirika ya kijamii kama jumuiya na vyama, ambapo walianza kutekeleza vitendo vya kisiasa huku nchi za kikoloni zikiwafadhili na kuwahonga. Inaonekana kuwa Amerika iliweza kujishindia wengine wao hadi Keita akaanguka kabla ya kumaliza muhula wake wa pili katika jaribio la Amerika la kuhakikisha mafanikio ya vibaraka wake katika mustakbali huku angazo lake likiwa katika jeshi na kujishindia vibaraka kutoka kwa maafisa wake.

3- Inaonekana kana kwamba Amerika wakati huu imejaribu kuwa na nguzo maarufu kwa ajili ya mapinduzi yake, hivyo ikayatolea njia yake tangu mwanzoni mwa Juni iliyopita, wakati maandamano yalizuka ambapo maelfu ya waandamanaji waliandamana katika barabara za Bamako, mji mkuu wa Mali, wakitoa wito wa kujiuzulu kwa Raisi Keita na kumkashifu yeye na serikali yake kwa ufisadi, mapendeleo na huduma duni za umma na ulaghai katika uchaguzi, kutokuwa na uwezo katika uongozi, na kupigana na kile wanachokiita misimamo mikali na ugaidi. Vyama fulani viliunda muungano unaojulikana kama muungano wa Juni 5 au M5. Nohom Tojo, kinara wa muungano wa Juni 5 aliye yaongoza maandamano hayo, alisema: "Anafanya kazi na jeshi lililochukua mamlaka," akivitaja vikwazo vya kundi la ECOWAS kama "majibu ya kupitiliza yaliyosababishwa na hofu za baadhi ya viongozi wake kuwa mapinduzi haya yatapelekea ghasia za kisiasa nchini mwao" na akayapongeza mapinduzi hayo ya kijeshi, na kuyasifu kama "yamekuja kukamilisha harakati za watu wa Mali na matamanio yao ya dola ya kisekula ya kiraia ya kidemokrasia." (Al-Jazeera 21/8/2020). Inaonekana kana kwamba maandamano hayo nchini Mali hayakuzuka ghafla, bali yaliongozwa na vibaraka wanaobeba fikra za mkoloni za demokrasia, uraia na usekula. Walishirikiana na jeshi na kuunga mkono mapinduzi. Amerika inalenga kuifanya Mali kuwa nukta kianzilishi ya angazo la maambukizi ya mapinduzi katika eneo hilo ili kuzing'oa serikali zinazojinasibisha na Ufaransa na Uingereza katika Afrika Magharibi na Kati.

4- Kisha balozi wa Amerika eneo la Sahel, J Peter Pham, aliandika katika akaunti yake ya Twitter baada ya mapinduzi hayo ya Mali: ("Amerika inapinga mabadiliko yote ya serikali kinyume na katiba" na akasema, "Amerika imeakhirisha vipengee vyote vya ushirikiano na jeshi la Mali hadi hali ya kisiasa iwe shwari punde tu baada ya maafisa hao kumng'oa Raisi Ibrahim Keita. Alisema: "Uamuzi wa ima kuyaita rasmi yale yaliyotokea hivi majuzi mapinduzi ni lazima utolewe baada ya uhakiki wa kisheria." (Reuters 22/8/2020), hivyo inaonekana kwamba Amerika haiyashutumu mapinduzi hayo wala kundi lililoyatekeleza. Maneno yaliyotolewa na balozi wake kuhusu upinzani wake kwa mabadiliko kinyume na katiba ni

maneno jumla ambayo hayana uhusiano wowote na mapinduzi. Bali iliyaunga mkono mapinduzi yaliyofanywa na Sisi nchini Misri na mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan, na haikuyachukulia kama mapinduzi kwa sababu ndiyo iliyoyaunda. Hii ndio hali katika mapinduzi ya Mali, kama ilivyosema kupitia balozi wake kwamba itafanya uhakiki wa kisheria ili kuchunguza ikiwa yale yaliyotokea ni mapinduzi au la!! Ambapo inaashiria kwamba ilikuwa nyuma ya mapinduzi hayo.

Hili linaungwa mkono na ripoti ya wavuti wa shirika la habari la Qatar la Al-Jazeera mnamo 21/8/2020: ("Amerika inatoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wanajeshi wa Mali, wakiwemo baadhi ya maafisa walioongoza mapinduzi dhidi ya Keita.") Wale walioongoza mapinduzi hayo walikuwa ni wale waliopewa mafunzo na Amerika na ambao Amerika ilijishindia kama vibaraka wake. Jambo lilo hilo lilitokea katika mapinduzi ya mnamo 2012, na tulitaja hili katika "Jibu la Swali" tulilotoa kuhusiana na hili mnamo 24/3/2012: ("Mnamo 24/3/2012, wavuti wa Al-Asr ulinukuu duru za kuaminika za Kiamerika kwamba balozi mmoja wa Kiamerika aliyeomba asitambulishwe kwa vyombo vya habari alieleza: "Kiongozi wa mapinduzi, Kapteni Amadou "Ahmadu" Hay Sanogo, alichaguliwa kutoka miongoni mwa kipote cha maafisa mahiri na ubalozi wa Amerika ili kupokea mafunzo ya kijeshi nchini Amerika, ili kupambana na ugaidi, na akaongeza kwamba "Sanjo alisafiri mara kadhaa hadi Amerika kwa misheni maalumu…"). Amerika inachukua hatua iyo hiyo iliyochukua mnamo 2012, kupitia mapinduzi, ili kuwafurushwa Wazungu na kuchukua nafasi yao, kuikoloni nchi hii kipekeyake. Lakini wakati huu, angazo lake huenda likawa zaidi kushinda nyuma, kwani imeanza kutafuta kitovu cha kisiasa kwa vyama vya kisiasa na mashirika ya kijamii ili kusimama mahali pa kitovu cha kisiasa kinachoegemea Ufaransa.

5- Ufaransa ndiyo nguvu ya ushawishi huko, majibu haya (mapinduzi) yalipingwa vikali. Ilighadhabishwa, na afisi ya raisi wa Ufaransa ilisema, ("Raisi wa Dola hii Macron anafuatilia kwa karibu hali na kushutumu jaribio la uasi linaloendelea sasa…" (AFP 18/8/2020) Waziri wa Kigeni wa Ufaransa Le Drian alisema: ("Ufaransa inashutumu vikali mno tukio hili hatari"… (Al-Hurra 19/8/2020 M) Wakati wa mkutano wake pamoja na Chansela wa Ujerumani Merkel ili kujadili yanayojiri nchini Mali, Macron alisema mnamo 20/8/2020 M: ("Ufaransa na Ujerumani zinashutumu mapinduzi nchini Mali na zinataka nchi hiyo irudi katika utawala wa raia haraka iwezekanavyo. Hakuna kinachopaswa kubabaisha umakini wa kupambana na vitendo vya ghasia vinavyotekelezwa na wanamgambo wa Kiislamu katika eneo la Sahel". Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Florence Parly alisema, "Ufaransa itaendelea na operesheni zake za kijeshi nchini Mali dhidi ya wanamgambo licha ya kung'olewa raisi wa nchi hiyo huko siku mbili zilizopita katika mapinduzi ya kijeshi." (Reuters 20/8/2020).  

Taarifa hizi zinaashiria kiwango cha kukasirishwa kwa Ufaransa na mapinduzi hayo, ambapo inathibitisha kuwa mapinduzi haya yalikuwa yanalenga ushawishi wake huko kwani imefuja utajiri wa Mali na nchi jirani, kwani ni tajiri kwa rasilimali nyingi za madini yaliyo adimu, na imeichukua kama eneo muhimu la kistratejia ili kulinda ushawishi wake eneo la Afrika Magharibi, kwa pamoja na nchi za Sahel zinaunda eneo moja. Endapo Mali itachukuliwa kutoka kwa Ufaransa, "maambukizi" hayo huenda yakaenezwa hadi nchi nyenginezo. Ufaransa inafanya kazi kusaidia uwepo wake wa kijeshi, ambao ni takriban wanajeshi 5100, pamoja na majeshi ya Ulaya, na inatafuta usaidizi kutoka Ujerumani, ambapo Ujerumani, pamoja na Ufaransa, wana kikosi shirika cha wanajeshi takriban 1100 chini ya ile inayoitwa operesheni ya Barkhane. Imeamua kuzifuata nchi za Ghuba, ikiwemo Imarati, ili kufadhili muungano wa majeshi ya Afrika. Uingereza inashiriki kwa takriban wanajeshi 250 na helikopta tatu. Muungano wa Ulaya unashiriki kwa takriban wanajeshi 620. Na Amerika inakataa kulisaidia jeshi la Barkhane kwa pesa na zana, na kusema kwamba inachangia kupitia ujasusi na uchunguzi kwa sababu ya droni zake.

6- Muungano wa Afrika na ECOWAS zimeshutumu mapinduzi hayo, hivyo Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, alisema katika Twitter: "Nalaani vikali kukamatwa kwa Raisi Ibrahim Keita, Waziri Mkuu na wanachama wengine wa serikali ya Mali na kutoa wito wa kuachiliwa huru kwao mara moja." Jumuiya ya Kiuchumi ya Dola za Afrika Magharibi (ECOWAS), nazo ni nchi 15, zilikubaliana kufunga mipaka yao kwa Mali, kuakhirisha uingiaji wote wa pesa nchini humo, na kuifukuza Mali kutoka katika asasi zote za utoaji maamuzi katika jumuiko hilo. Mnamo 22/8/2020, ujumbe kutoka jumuiko hili ulizuru Mali na kukutana na viongozi wa mapinduzi. Mkutano huo ulitarajiwa kuchukua saa moja na nusu, lakini ukachukua dakika 20 pekee, ambapo inaashiria kufeli kwa misheni ya kundi hili ambalo lilikuja kuwashawishi viongozi hao wa mapinduzi kumrudisha Keita na serikali yake mamlakani kama mashirika ya habari yalivyo ripoti. Lakini viongozi wa mapinduzi walikataa hili na kusisitiza juu ya mapinduzi yao, na kusema kwamba majadiliano na ujumbe wa jumuiko hilo yangeweza kufanyika wakati wa kipindi cha mpito. Tambua kwamba Muungano wa Ulaya na ECOWAS aghlabu yao ni vibaraka wa Ulaya, hususan eneo la Afrika Magharibi.

7- Kwa kuhitimisha, Amerika inashindana na Ulaya, hususan Ufaransa na Uingereza, barani Afrika, na hususan katika nchi za Kiislamu, ikiwemo Mali, kwani ni nchi ya Kiislamu ambayo kwayo wakoloni wanaipigania ili kupanua ushawishi wao ili waweze kufuja utajiri wake. Ufaransa kwa sasa inamiliki hisa kubwa ya utajiri huo, na wakoloni pia wanaipigania kwa ajili ya eneo lake la kistratejia katika Afrika Magharibi, ambayo pamoja na nchi za Sahel zinaunda eneo moja, na watu wake Waislamu wameachwa kuteseka na umasikini, uchochole na maradhi, na watawala vibaraka wanalinda kile ambacho wakoloni wanakitaka ili kupata kiti kibovu cha utawala huku wakidhalilishwa. Mali ni nchi dhaifu iliyo na tishio la ukoloni, kwani hakuna jeshi la Waislamu linaloweza kuilinda kutokana na uvamizi wa wakoloni, huku wakitoa uamuzi wa uingiliaji wa moja kwa moja wa kijeshi chini ya visingizio vya kipuuzi. Na hakuna jeshi la Kiislamu kama la dola inayosubiri ya Khilafah Rashida, apendapo Mwenyezi Mungu, ili kupambana na uvamizi wao na kuwapa funzo ambalo hawatalisahau. Hivyo basi, kazi ya kusimamisha dola hii ni mojawapo ya majukumu muhimu zaidi, na katika hilo kuna utukufu, ushindi, na ulinzi dhidi ya makafiri wote wenye kiburi. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«وَإِنَّمَا الإِمَامُ جُنَّةٌ يُقَاتَلُ مِنْ وَرَائِهِ وَيُتَّقَى بِهِ»

“Hakika Imam ni ngao watu hupigana nyuma yake na kujilinda kwayo” [Muslim]

 13 Muharram Al- Haram 1442 H

1/9/2020 M

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu