- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Mazungumzo ya Usaliti Kati ya Lebanon na Umbile la Kiyahudi
(Imetafsiriwa)
Swali:
Jijini Washington, mazungumzo yalifanyika kati ya mabalozi wa Lebanon na umbile la Kiyahudi. Hii ilionekana kama mazungumzo ya kiwango cha juu cha amani, pamoja na makubaliano ya kusitisha mapigano ya siku kumi ambayo baadaye yaliongezwa hadi miezi mitatu mnamo Aprili 24, 2026. Hata hivyo, umbile la Kiyahudi linaendelea kuzidisha uchokozi wake, “jeshi la uvamizi lilitangaza kwamba lilifanya mfululizo wa mashambulizi usiku kucha likilenga zaidi ya maeneo hamsini kusini mwa Lebanon...” (Al-Jumhur, Mei 2, 2026). Je, nia, kama Trump alivyosema, ni amani kupitia nguvu? Basi watawala wa Lebanon wanawezaje kukubali mazungumzo haya ya usaliti ambayo waziwazi, na si kwa siri, yanamaanisha kupanda treni ya uhalalishaji mahusiano? Tafadhali tujibu, na tunakushukuru na kukuthamini.
Jibu:
Ili kujibu maswali haya, tutahakiki yafuatayo:
1- Kwa kuregea kwa utawala wa Trump serikalini kwa muhula mpya mnamo 2025, ilileta mradi wake wa zamani, Makubaliano ya Abraham, pamoja na ahadi zake za “uhalalishaji mahusiano,” na ahadi mpya za kuliwezesha umbile la Kiyahudi kutawala eneo hilo na kulikabidhi kwa kusimamia sehemu kubwa ya maslahi ya Amerika huko. Kuzinduliwa kwa mazungumzo kati ya vibaraka wa Amerika nchini Lebanon na umbile la Kiyahudi mnamo tarehe 14 Aprili 2026, jijini Washington, kulikuwa kubwa na pana zaidi kuliko makubaliano ya usalama ambayo serikali inakuza kama jaribio la kusimamisha mauaji na uharibifu na kukomboa kusini. Badala yake, ilikuwa ni juhudi kamili ya kupata kiti kwenye treni ya uhalalishaji mahusiano ya Trump. Ingawa mkutano huu wa “kwanza” ulikuwa katika ngazi ya ubalozi, Rais wa Marekani Trump, katika jaribio la kuzalisha kasi, alitangaza kwamba Rais wa Lebanon Aoun na Waziri Mkuu wa Kiyahudi Netanyahu wangefanya mazungumzo ya simu, ikionyesha kwamba mawasiliano kama hayo hayakuwa yametokea kwa miongo kadhaa. (i24, 16 Aprili 2026). Wakati simu hiyo haikutokea, Trump alisisitiza kudumisha kasi hiyo. Waziri wake wa Mambo ya Nje aliwasiliana na Rais wa Lebanon, na kisha Trump mwenyewe akampigia simu—hatua ambayo ilisifiwa sana na vibaraka wa Amerika nchini Lebanon. Kisha Trump akatangaza hatua ya kidiplomasia ambayo haijawahi kutokea: nia yake ya kuwakaribisha Waziri Mkuu wa “Israel,” Benjamin Netanyahu, na Rais wa Lebanon Joseph Aoun katika Ikulu ya White House. (Saudi News, 16 Aprili 2026). Licha ya kukataa kioga kwa Lebanon, kujiunga kwa Lebanon katika treni ya uhalalishaji mahusiano sasa kumekaribia!
2- Kisha ikaja msururu wa kauli kutoka kwa Aoun na Waziri Mkuu wake kuhusu hili:
a- Katika hotuba iliyoelekezwa kwa watu wa Lebanon, Aoun alifafanua, “Acha niwaambie kwa uwazi na kwa ujasiri: mazungumzo haya si ishara ya udhaifu, kurudi nyuma, au makubaliano. Badala yake, ni uamuzi uliotokana na nguvu ya imani yetu katika haki zetu, kujali kwetu watu wetu, na jukumu letu la kulinda nchi yetu kwa njia zote, haswa kukataa kwetu kufa kwa ajili ya mtu mwingine yeyote isipokuwa Lebanon. Mazungumzo hayamaanishi, na hayatamaanisha kamwe, kuacha haki yoyote, kuacha kanuni yoyote, au kuhatarisha uhuru wa taifa hili. Tumepoteza maelfu ya Walebanoni; hawa ni wana na binti zetu, na hatutawasahau kamwe. Sitamruhusu Mlebanoni mwingine afe, wala sitaruhusu umwagaji damu unaoendelea miongoni mwa watu wangu, kwa ajili ya maslahi na ushawishi wa wengine au hesabu za kambi za nguvu, karibu au mbali.” (Independent Arabia, Aprili 18, 2026)
b- Kuhusu Waziri Mkuu Nawaf Salam, alisema katika mkutano na waandishi wa habari na Rais wa Ufaransa Macron, ““Atahitaji msaada wa washirika wote wa Lebanon huku mazungumzo ya moja kwa moja yakiendelea katika ngazi ya ubalozi baadaye wiki hii huko Washington, akiongeza, “Tunaendelea katika njia hii kwa kuzingatia imani yetu kwamba diplomasia si ishara ya udhaifu, bali ni kitendo cha uwajibikaji cha kuacha njia yoyote bila kuchunguzwa ili kuregesha uhuru wa nchi yangu na kuwalinda watu wake.”” (Independent Arabia, Aprili 21, 2026).
c- Kisha Aoun akategemea juu ya dori ya uungaji mkono ya Saudia, kama ilivyoripotiwa katika Gazeti la Al-Riyadh, “Joseph Aoun alisifu dori ya Saudia, akithamini juhudi za Mtukufu Mwana Mfalme Mohammed bin Salman, Mrithi wa Taji na Waziri Mkuu, na kusisitiza kwamba hatua hizi zilionyeshwa kwa hekima na usawa... na juhudi za Saudia zilitegemea misimamo imara inayowaunga mkono watu wa Lebanon, haswa kutokana na hali ngumu zilizosababishwa na kupamba moto kijeshi hivi karibuni. Kujitolea kwa Ufalme huo kuunga mkono mipango yote inayolenga kusitisha mapigano kulikuwa dhahiri, pamoja na kufanya kazi ya kuamsha suluhu endelevu za kidiplomasia zinazohakikisha kupatikana kwa amani na uhifadhi wa utulivu wa Lebanon.” (Gazeti la Al-Riyadh, 19 Aprili, 2026)
3- Kisha, licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano na Iran, umbile la Kiyahudi lilikataa kukomesha vita na Hizb ya Iran nchini Lebanon, baada ya makubaliano ya wiki mbili ya kusitisha mapigano na Iran. Waziri mkuu wa umbile hilo la Kiyahudi alitangaza kwamba Lebanon haikujumuishwa katika makubaliano hayo, na ili kuthibitisha hili, ndege yake ililipua mabomu mengi Beirut na Lebanon kwa ujumla siku ya kwanza makubaliano hayo na Iran yalipoanza kutumika. “Israel ilifanya mashambulizi yake makali zaidi dhidi ya Lebanon tangu mzozo na Hezbollah ulipoanza mwezi uliopita, hata wakati kundi hilo linaloungwa mkono na Iran lilipositisha mashambulizi chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya wiki mbili kati ya Marekani na Iran. Axios iliripoti, ikimnukuu msemaji wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt mnamo Jumatano, kwamba Lebanon si sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran.” (France 24, 4 Aprili 2026).
4- Kwa kuzingatia msimamo huu wa Marekani, matamshi ya vibaraka wa Amerika nchini Lebanon dhidi ya Hezbollah yanaongezeka, na kuashiria hatari ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kwa mfano, “Waziri Mkuu wa Lebanon Nawaf Salam alisema mnamo Jumanne kwamba serikali haitafuti mapambano na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, lakini haitaruhusu kutishwa wakati inaendelea na mazungumzo ya moja kwa moja na Israel ili kukomesha vita. (Independent Arabia, 21 Aprili, 2026).” Hii inaashiria kwamba umbile la Kiyahudi pamoja na serikali ya Lebanon zinafanya kazi, ingawa tofauti, ili kuipokonya silaha Hizb ya Iran nchini Lebanon.
5- Hata hivyo, huku Iran ikiendelea kushinikiza makubaliano ya kusitisha mapigano yaijumuishe Lebanon, Marekani ilikubali kusitisha mapigano nchini Lebanon baada ya kukataa mwanzoni. “Rais wa Marekani alitangaza kusitisha mapigano kwa siku kumi nchini Lebanon” (RT, 16 Aprili, 2026). Marekani inaona kusitisha mapigano huku kama njia ya kusukuma Lebanon kuelekea uhalalishaji mahusiano. Rais Trump alisema, “Nimekuwa na mazungumzo mazuri tu na Rais Anayeheshimika Sana Joseph Aoun, wa Lebanon, na Waziri Mkuu Bibi Netanyahu, wa “Israel”, akiongeza kwamba “Viongozi hawa wawili wamekubaliana kwamba ili kufikia AMANI kati ya Nchi zao, wataanza rasmi Mkataba wa Siku 10 wa KUSITISHA VITA saa 5:00 PM EST.” Alibainisha kuwa “Mnamo Jumanne, nchi hizo mbili zilikutana kwa mara ya kwanza katika miaka 34 hapa Washington, D.C., na Waziri wetu Mtukufu wa Mambo ya Nje, Marco Rubio.” Trump alithibitisha kwamba, “Nimemwelekeza Makamu wa Rais JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje Rubio, pamoja na Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi, Dan Razin' Caine, kufanya kazi na “Israel” na Lebanon ili kufikia AMANI ya Kudumu.” Alihitimisha chapisho lake kwa kusema, “Imekuwa heshima kwangu kutatua Vita 9 kote Duniani, na hivi vitakuwa vyangu vya 10, kwa hivyo, hebu na TULIFANYE HILI!” (Truth Social, 16 Aprili 2026).
6- Kisha Trump alitangaza kuongezwa muda kwa makubaliano ya usitishaji vita kati ya umbile la Kiyahudi na Lebanon kwa wiki tatu, “Rais wa Marekani Donald Trump alisema mnamo Alhamisi kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya “Israel” na Lebanon yataongezwa kwa wiki tatu. Trump aliongeza katika chapisho kwenye akaunti yake ya Truth Social kwamba uamuzi huo ulikuja baada ya mkutano uliofanyika Alhamisi katika Afisi ya Oval, uliohudhuriwa na Rais wa Marekani, Makamu wa Rais Jay D. Vance, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, Balozi wa Marekani kwa “Israel” Mike Huckabee, na Balozi wa Marekani nchini Lebanon Michel Issa.” (Sky News Arabia, 24 Aprili 2026). Hata hivyo, licha ya haya, mashambulizi yanaendelea! ““Israel” inaendelea na mashambulizi yake kusini mwa Lebanon...” (RT Arabic, 30 Aprili 2026). “Pia, jeshi la “Israel” lilifanya mfululizo wa mashambulizi makubwa katika siku mbili zilizopita, na kusababisha vifo vingi. Mamlaka ya Lebanon iliripoti kwamba takriban watu 29 waliuawa na kadhaa kujeruhiwa katika mashambulizi 84 tofauti ya “Israel”, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya anga, mashambulizi ya mizinga, na mabomu ya majengo ya makaazi.” (Al Jazeera, Mei 1, 2026). Na leo, “jeshi la uvamizi lilitangaza kwamba lilifanya mfululizo wa mashambulizi jana usiku likilenga zaidi ya maeneo 50 kusini mwa Lebanon...” (Al-Jumhur, 2 Mei 2026). Amerika inataka mazungumzo yaendelee kulingana na maono yake ya kiburi ya amani kupitia nguvu! Kwa lengo hilo, umbile la Kiyahudi linaanzisha kambi mpya za kijeshi katika vijiji vya Lebanon ambavyo limevimiliki, likivitangaza kuwa maeneo ya ulinzi dhidi ya vitisho vya Hezb ya Iran—marudio ya mandhari ya Gaza na Hamas na Mstari wa Manjano!
7- Hivyo, watawala wa Lebanon na watawala wengine wa nchi za Kiislamu, badala ya kuikomboa Palestina na kuliondoa umbile la Kiyahudi, wanajitahidi kuhalalisha mahusiano nalo. Wanashirikiana na Amerika na umbile la Kiyahudi ili kuhakikisha usalama wake. Watawala hawa hawatambui hatari ya kushirikiana na makafiri, kwamba ni fedheha hapa duniani na kesho Akhera ni adhabu kali,
[الَّذِينَ يَتَّخِذُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِنْ دُونِ الْمُؤْمِنِينَ أَيَبْتَغُونَ عِنْدَهُمُ الْعِزَّةَ فَإِنَّ الْعِزَّةَ لِلَّهِ جَمِيعاً]
“Wale ambao huwafanya makafiri kuwa ndio marafiki badala ya Waumini. Je! Wanataka wapate kwao utukufu? Basi hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu.” [Surah An-Nisaa: 139]. Hawatambui kwamba dola za kikafiri zinajali zaidi maslahi yao wenyewe na zina uadui dhidi ya Uislamu na Waislamu mchana na usiku. Ikiwa zitaonyesha kuridhika na dola inayozunguka ndani ya duara lao la sera za kigeni, au hata na vibaraka wao, haziwatakii kheri. Badala yake, zinaficha na kutangaza waziwazi nia zao ovu, hata kama watawala hawa, wowote watakaokuwa, ni washirika wa kweli wa umbile la Kiyahudi. Iwe wanazunguka Amerika, au walikuwa vibaraka wake, ikiwa wangeelewa kwamba Amerika haiwathamini pindi maslahi yake yanahitaji waangamie, wangejifunza kutokana na mafunzo ya historia. Je, ni washirika wangapi ambao Amerika imewatupa, baada ya kutimiza kusudi lao? Kama watawala hawa wangekuwa na akili yoyote, wangewakataa makafiri moja kwa moja, lakini ni viziwi, mabubu, na vipofu, na hawatarudi. Utiifu wao kwa wakoloni makafiri umefikia hatua ambayo wakati moja ya nchi zao inashambuliwa, zengine haziendi kuisaidia. Bora kati yao ni wale wanaohesabu tu waliokufa na waliojeruhiwa! Kanuni msingi kwa Waislamu ni kwamba wao ni Ummah mmoja; Amani yao ni moja, na vita vyao ni vimoja. Shambulizi dhidi ya sehemu yoyote ya Ummah ni shambulizi dhidi yake yote. Ingawa ni faradhi ya Sharia ya kila sehemu inayoshambuliwa kumzuia mvamizi, hii haisuluhishi tatizo. Walinzi wa Mapinduzi nchini Iran wanazuia, na Hezb wa Iran nchini Lebanon wanazuia, lakini haya yote hayatasuluhisha tatizo isipokuwa Khilafah isimamishwe, kumnusuru Mwenyezi Mungu (swt) kupitia utiifu na kutabikisha Shariah zake, ili iweze kupata ushindi, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (swt) ikiangaza ulimwengu kwa uadilifu na Jihad, ili Mwenyezi Mungu (swt) aikirimu kwa ushindi (nasr) wake.
8- Hili pekee ndilo litakalouokoa Ummah, kuregesha izza yake, kuimarisha nguvu zake, na kuwafanya maadui zake wafikiri mara elfu moja kabla ya kuushambulia. Hili linawezekana tu kwa kurudi kwa Khilafah ili dunia ing'ae kwa kheri na uadilifu wake. Kama vile Khilafah ilivyomaliza kiburi cha Makaisari wa Kirumi na watawala wa Fursi, ndivyo pia itamaliza kiburi cha wafuasi wao, kama vile dhalimu Trump na wenzake miongoni mwa wakoloni makafiri. Ama kuhusu umbile la Kiyahudi, ni dogo sana kupewa uzito wowote. Ni kama Mwenyezi Mungu (swt) alivyosema, [لَنْ يَضُرُّوكُمْ إِلَّا أَذًى وَإِنْ يُقَاتِلُوكُمْ يُوَلُّوكُمُ الْأَدْبَارَ ثُمَّ لَا يُنْصَرُونَ] “Maadui hawatakudhuruni ila ni maudhi tu. Na wakipigana nanyi watakupeni mgongo, na tena hawatanusuriwa.” [Surah Aali-Imran: 111]. Halina uwezo wa kusimama lenyewe. Halina uwezo wa kupigana ila kwa msaada wa watu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu, [ضُرِبَتْ عَلَيْهِمُ الذِّلَّةُ أَيْنَ مَا ثُقِفُوا إِلَّا بِحَبْلٍ مِنَ اللهِ وَحَبْلٍ مِنَ النَّاسِ] “Wamepigwa na udhalili popote wanapo kutikana, isipo kuwa wakishika kamba ya Mwenyezi Mungu na kamba ya watu.” [Surah Aali Imran: 112]. Wameikata Kamba ya Mwenyezi Mungu (swt) na wamebakiwa tu na kamba ya watu kutoka Amerika na Ulaya, na vibaraka wao kutoka miongoni mwa watawala wasaliti katika ardhi za Waislamu, ambao hawanyanyui kidole mbele ya uchokozi wa kikatili wa Mayahudi. Tatizo liko katika dola zilizopo katika nchi za Waislamu siku hizi, kwani watawala wao ni watiifu kwa wakoloni makafiri, maadui wa Uislamu na Waislamu. Hivyo, msiba wa Waislamu uko kwa watawala wao, na utiifu wao kwa wakoloni makafiri. Watawala hutii amri zao na kujiepusha na wanachokataza, badala ya utiifu wao kuwa kwa Mwenyezi Mungu (swt) wakisimamisha Shariah zake na kupigana Jihad katika Njia ya Mwenyezi Mungu (swt) na kumfuata Mtume Wake (saw) ili Uislamu na Waislamu wapate kuheshimiwa na ukafiri na makafiri wadhalilike.
[وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بنَصْرِ اللَّهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ]
“Na siku hiyo Waumini watafurahi * Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.” [Surah Ar-Rum: 4-5].
15 Dhul Qi’dah 1447 H
2 Mei 2026 M



