Afisi ya Habari
Wilayah Sudan
H. 19 Jumada II 1446 | Na: HTS 1446 / 36 |
M. Jumamosi, 21 Disemba 2024 |
Hotuba ya Msemaji Rasmi wa Hizb ut Tahrir katika Wilaya ya Sudan katika mkutano na waandishi wa habari yenye kichwa:
“Sarafu Kati ya Kiwango cha Dhahabu na Fedha na Mshtuko wa Nixon”
(Imetafsiriwa)
Sarafu inafafanuliwa kuwa ni njia iliyokubaliwa na watu kutumika kama bei ya bidhaa, mishahara kwa juhudi, na malipo ya huduma, iwe ni ya chuma au isiyo ya chuma. Ni kipimo cha bidhaa, juhudi na huduma zote.
Kabla ya kuanzishwa kwa sarafu, watu walitumia ubadilishanaji wa bidhaa kwa huduma. Kwa kuwa dhahabu na fedha zimezingatiwa kuwa madini ya thamani yenye kima cha asili kwa binadamu tangu nyakati za zamani, zilitabanniwa kama pesa, huku sarafu zikichongwa kwazo ili kurahisisha ubadilishanaji. Dhahabu, hasa, inajulikana kwa kuhimili kwake kuharibika kwa muda mrefu.
Himaya ya Rumi na maeneo yake ilitabanni dhahabu kama msingi wa sarafu yao, ikichonga dinari za Heraclean kwa maumbo na uzani maalum. Vilevile, Himaya ya Fursi na maeneo yake yalitegemea fedha zao kwa kutengeneza dirham kwa maumbo na uzani maalum.
Kabla ya Uislamu, Waarabu, haswa Maquraishi, walifanya biashara na nchi jirani, wakileta dinari za dhahabu za Byzantini kutoka ash-Sham na dirham za fedha za Sassania kutoka Iraq.
Uislamu ulipowasili, Mtume Muhammad (saw) aliidhinisha matumizi ya dinari na dirham hizi kama sarafu, bila kujali mamlaka zilikotolewa, kwa kuwa zilikuwa na thamani ya dhati iliyo huru na Himaya ya Kirumi au ya Kifursi. Mtume (saw) vile vile amethibitisha uzani waliokuwa wakiutumia Maquraishi kwa sarafu hizi, akasema: «الْوَزْنُ وَزْنُ أَهْلِ مَكَّةَ، وَالْمِكْيَالُ مِكْيَالُ أَهْلِ الْمَدِينَةِ» “Uzani ni uzani wa watu wa Makka, na kipimo ni kipimo cha watu wa Madina.” (Imepokewa na Abu Daawuud na Al-Nasa’i).
Utendaji huu uliendelea hadi utawala wa Khilafah (Khalifa) Abdul Malik bin Marwan. Katika mwaka wa 75 au 76 H, Abdul Malik alitengeneza dirham kwa miundo maalum ya Kiislamu iliyo na maandishi ya Kiislamu. Mnamo mwaka wa 77 H, alitengeneza dinari za Kiislamu, kuashiria kuhama kwa Waislamu kwenye mfumo wao wa sarafu. Sarafu hii ilishikamana na uzito maalum uliowekwa na Mtume (saw), ambao pia ulitumika kama msingi wa hukmu mbalimbali za kisheria, kama vile zaka, diya (fidia ya umwagaji damu), na adhabu ya wizi.
Uzito wa dinari uliwekwa kuwa gramu 4.25 za dhahabu, na uzito wa dirham ulikuwa gramu 2.975 za fedha. Uzani huu uliidhinishwa na Mtume (saw) na kufungamanishwa na hukmu za Kiislamu kama sarafu. Kwa mfano:
1. Uharamu wa kulimbikiza dhahabu na fedha: Mwenyezi Mungu (swt) anasema:
[وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنْفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللهِ فَبَشِّرْهُمْ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ * يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنْفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنْتُمْ تَكْنِزُونَ]
“Na wanao kusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu. (34) Siku zitapo tiwa moto katika Moto wa Jahannamu, na kwazo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, wakaambiwa: Haya ndiyo mlio jilimbikia nafsi zenu, basi onjeni mliyo kuwa mkilimbika.” [At-Tawba:34-35]. Uharamu huu ni maalum kwa sarafu, sio mali.
2. Zaka ikawekwa juu yazo kama sarafu, bei ya bidhaa, na ujira wa juhudi, na nisab (kiwango) maalum iliwekwa kwa ajili yake kutokana na dinar za dhahabu na dirham za fedha: فِي كُلِّ عِشْرِينَ دِينَاراً نِصْفُ دِينَارٍ... وَفِي كُلِّ مِائَتَيْ دِرْهَمٍ خَمْسَةُ دَرَاهِمَ “Kwa kila dinari ishirini nusu dinari... na kwa kila dirham mia mbili dirham tano.” Diya ilipoagizwa, ilifanywa kulipwa kwazo. Imepokewa kutoka kwa Al-Nasa'i kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) aliwaandikia watu wa Yemen, na katika barua yake, iliandikwa: «وَأَنَّ فِي النَّفْسِ الدِّيَةَ مِائَةً مِنْ الْإِبِلِ ... وَعَلَى أَهْلِ الذَّهَبِ أَلْفُ دِينَارٍ» “Kwa nafsi, diya ni ngamia mia moja... na kwa wale wanaofanya biashara kwa dhahabu, dinari elfu moja,” ikimaanisha kwamba diya, kwa mujibu wa Shariah, ni kilo 4 na gramu 250 za dhahabu.
Hii inaashiria kwamba sarafu katika Uislamu inachukuliwa kuwa dhahabu na fedha, kwani hukmu zote zinazohusiana na fedha zinafungamana na dhahabu na fedha. Vyuma hivi hutumika kama kiwango cha thamani ya bidhaa na huduma na kama sarafu ya kubadilishana, iwe ni sarafu zilizotengenezwa au zenyewe asili (zisizochongwa). Kihistoria, ulimwengu ulitabanni dhahabu na fedha kama sarafu hadi kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia, wakati matumizi yake yaliposimamishwa. Baada ya vita, kulikuwa na kurudi nusu kwa matumizi dhahabu na fedha kama sarafu, ambayo iliendelea hadi Kongamano la Bretton Woods mwaka wa 1944. Kongamano hilo lililenga kupanga mifumo ya fedha, hasa mfumo wa kiwango cha ubadilishanaji cha dhahabu. Katika kongamano hilo, dolari ya Marekani ilipata hadhi maalum kwa sababu Amerika ilishikilia hifadhi kubwa zaidi ya dhahabu duniani. Pauni ya Uingereza ilifuata kwa umuhimu. Dolari hiyo iliegemezewa dhahabu, huku Amerika ikiweka kiwango rasmi cha $35 kwa pauni moja ya dhahabu. Taasisi ya kimataifa ilihitajika kudhibiti viwango vya ubadilishaji na kuanzisha mfumo thabiti wa miamala ya mali na fedha. Jukumu hili lilikabidhiwa kwa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF). Kwa kuwa Amerika inamiliki takriban theluthi mbili ya akiba ya dhahabu duniani, sarafu za dunia zilifungamanishwa na dolari, kwani iliegemezwa kwa dhahabu. Hii ilifuatiwa na Mpango wa Marshall (1947-1952) wa kujenga upya Ulaya, ambao ulijaza benki za Ulaya dolari za Marekani.
3. Mfumo huu uliendelea hadi machafuko ya fedha yalipoanza kujitokeza mwaka 1960, wakati mahitaji ya dhahabu yalipoongezeka kutokana na imani iliyotingishika kwa dolari, ambayo mitambo yake ya uchapishaji ilifanya kazi usiku na mchana. Hii ilisababisha kupungua kwa akiba ya dhahabu ya Amerika na kutokuwa na uwezo wa kudumisha kiwango cha ubadilishaji wa dhahabu. Marekani haikuweza tena kutimiza ahadi zake za kubadilisha dolari kwa kiwango rasmi kilichoanzishwa na Kongamano la Bretton Woods. Kwa sababu hiyo, mnamo Agosti 15, 1971, Rais wa Marekani Nixon alikomesha mfumo wa ubadilishanaji sarafu wa dolari kwa dhahabu, tukio lililojulikana kama “Mshtuko wa Nixon.” Kwa kufanya hivyo, Marekani ilihusisha dunia nzima kuifanya sarafu ya akiba kuwa dola katika benki kuu zao ambazo, baada ya uamuzi wa Nixon, zikawa karatasi tu isiyo na thamani ya dhati, iliyotumika kupora utajiri na juhudi za dunia, hasa katika nchi za Kiislamu zilizo na utajiri wa rasilimali.
Sudan ni sehemu ya mfumo huu wa kimataifa, unaounganisha sarafu yake na dolari, ambayo haina thamani zaidi ya thamani ya karatasi na wino iliyochapishiwa! Wakati huo huo, serikali za Sudan mara kwa mara hubadilisha sarafu na kuishusha thamani yake dhidi ya dolari, na kupora mali za watu kwa dhulma. Ikiwa tutachunguza sarafu ya kwanza ya Sudan iliyotolewa baada ya kile kinachoitwa uhuru - na nasema “kile kinachoitwa” kwa sababu bado hatujajikomboa kutoka kwa ukoloni ili kudai uhuru na ubwana - ilikuwa ni pauni ya Sudan, ambayo ilikuwa na thamani zaidi ya dolari tatu. Leo, baada ya zaidi ya miongo sita, pauni ya Sudan imeshuka thamani dhidi ya dolari hadi kufikia hatua ambapo dolari moja ni sawa na karibu pauni milioni tatu za Sudan!
4. Sarafu ya kwanza ya Sudan ilitolewa mnamo Septemba 15, 1956, na iliitwa pauni ya Sudan, iliyofunganishwa na dolari, ambapo pauni moja ilikuwa na thamani ya zaidi ya dolari tatu.
Kati ya 1960 na 1969, sarafu hiyo ilichapishwa mara tatu, na wakati wa kipindi hicho hicho, uanzishwaji uchongaji kwa ajili ya uzalishaji wa sarafu ulikamilishwa.
Mnamo Machi 1970, chini ya utawala wa Nimeiri, sarafu ya karatasi na chuma ilibadilishwa.
Mnamo Januari 1981, sarafu ilibadilishwa na kujumuisha picha ya Rais Nimeiri.
Mnamo Juni 1985, sarafu iliyokuwa na picha ya Nimeiri iliondolewa baada ya kuondolewa madarakani.
Mnamo 1990, noti ya kwanza ya pauni 100 ilitolewa.
Mnamo Machi 1992, sarafu ilibadilishwa kutoka pauni hadi dinari, kwa kuondolewa sifuri, na kuifanya dinari moja kuwa sawa na pauni 10.
Baada ya kutiwa saini kwa Mkataba maarufu wa Naivasha, sarafu ilibadilishwa Januari 2007 kutoka dinari kurudi kwa pauni, na pauni mpya ikiwa sawa na dinari 100. Hii ilimaanisha kuwa sarafu ya Sudan ilipoteza sifuri tatu katika thamani, na kupunguza pauni mwaka 2007 hadi 0.001 tu ya thamani yake mwaka 1992.
Mnamo Juni 2022, Benki Kuu ya Sudan ilitangaza kutoa noti ya pauni 1,000.
Mnamo Agosti 2023, uchapishaji wa pili wa noti za pauni 1,000 na pauni 500 ulifanywa.
Hatimaye, mnamo Novemba 2024, noti ya pauni 1,000 ilibadilishwa.
Malengo yaliyotajwa na Waziri wa Fedha ni pamoja na kulazimisha watu kufungua akaunti benki, kuweka kikomo cha utoaji pesa kila siku, kuondoa fedha bandia na kubaini vyanzo vya fedha nyingi. Malengo haya yote yaliyotajwa yanakinzana na hukmu za Kiislamu. Watu wana mamlaka kamili juu ya mali zao, na hakuna yeyote, hata Khilafah ya Waislamu, mwenye haki ya kuwata watu kuweka pesa zao, hata kwenye hazina ya Waislamu, achilia mbali katika benki zenye riba. Fauka ya hayo, kuweka kikomo cha utoaji pesa kunaifunga mali ya watu, ambayo inajuzu tu kwa anayeonekana kuwa safihi, kama Mwenyezi Mungu (swt) anavyosema:
[وَلَا تُؤْتُوا السُّفَهَاءَ أَمْوَالَكُمُ الَّتِي جَعَلَ اللهُ لَكُمْ قِيَاماً]
“Wala msiwape wasio na akili mali yenu ambayo Mwenyezi Mungu ameyajaalia yawe ni kiamu yenu.” [An-Nisa:5].
Kwa kufanya hivi, serikali kimsingi inawachukulia watu wote kama masafihi, wanaohitaji kuzuiwa mali zao! Ama kuhusu kuondosha pesa ghushi, kuchapisha pesa bila ya kuziegemeza kwa dhahabu au fedha, kama ilivyo leo, yenyewe ni aina ya ulaji mali ya watu pasi na haki.
Ama kubainisha vyanzo vya mali, ni tuhuma dhidi ya watu bila ushahidi. Kanuni ya msingi katika Uislamu ni dhana ya kutokuwa na hatia. Mtume (saw) amesema: «الْبَيِّنَةُ عَلَى مَنِ ادَّعَى وَالْيَمِينُ عَلَى مَنْ أَنْكَرَ» “ushahidi upo juu ya mwenye kudai na kiapo lazima kichukuliwe na yule anayekataa madai hayo.”
Kwa hivyo, malengo yaliyotajwa ya kubadilisha sarafu ni batili. Suluhisho pekee linalowezekana ni kuiegemeza sarafu kwenye dhahabu na fedha, hatua ambayo dola binafsi za kitaifa, ikiwemo Sudan - nchi ya dhahabu - haiwezi kufikia. Hili linaweza tu kutekelezwa na dola ya kimfumo, yaani, Khilafah Rashida ya pili kwa njia ya Utume, ambayo Ummah wote lazima uifanyie kazi kuisimamisha. Kupitia hilo, dunia nzima, sio Waislamu pekee, itafurahia amani na maisha salama.
Ibrahim Othman (Abu Khalil)
Msemaji Rasmi wa Hizb ut Tahrir
katika Wilayah Sudan
Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Wilayah Sudan |
Address & Website Tel: 0912240143- 0912377707 http://www.hizb-sudan.org/ |
E-Mail: Spokman_sd@dbzmail.com |