Afisi ya Habari
Wilayah Sudan
| H. 7 Jumada II 1447 | Na: HTS 1447 / 60 |
| M. Ijumaa, 28 Novemba 2025 |
Jibu kwa Vyombo vya Habari
Sudan ni Milki ya Hadhara Tukufu Zaidi Iliyowahi Kujulikana Katika Historia
(Imetafsiriwa)
Katika makala ya maoni ya Al-Burhan, yaliyochapishwa na jarida la ‘American Wall Street Journal’ mnamo 26 Novemba 2025, aliandika yafuatayo: “Sudan ni nchi yenye kumbukumbu ndefu: Historia yetu inaanzia Ufalme wa Kush wa kibiblia...”
Tunamwambia kwamba Sudan ni nchi ya Kiislamu, inayomilikiwa na hadhara tukufu zaidi unayojulikana katika historia, na watu wake wanajivunia Uislamu, ambao uliwatoa katika giza la ukafiri na upagani na kuwaingiza katika nuru ya Uislamu na Upweke wa Mwenyezi Mungu. Chini ya Uislamu waliibuka viongozi wakuu nchini Sudan, kama vile Sultan Ali Dinar, ambaye alikuwa akiivisha Kaaba Takatifu na kuchimba visima ili kuwapa maji mahujaji, na athari za matendo yake bado ziko na jina lake. Visima vya Abyar Ali barabarani kutoka Al-Madinah Al-Munawarah hadi Makkah Al-Mukaramah vinasimama kama ushahidi bora wa utukufu wa mtu huyo na utukufu wa matendo yake.
Hata hivyo, Al-Burhan alipuuza Uislamu katika makala yake, akiitukuza Amerika, Trump wake, na mlinzi wake umbile la Kiyahudi, katika jaribio la kujikurubisha nao! Kinachothibitisha hili ni kauli yake katika makala hiyo hiyo: “Sudan ilichukua hatua ya kihistoria mwaka wa 2021 kwa kujiunga na Makubaliano ya Abraham.”
Sidhani kama Muislamu yeyote angejivunia mikataba ya fedheha, udhalilifu, na aibu iliyotiwa saini na baadhi ya nchi za Kiarabu, ikihalalisha mahusiano na umbile la Kiyahudi ili kumfurahisha Trump. Ni mikataba ya khiyana, na wale waliotia saini wamemsaliti Mwenyezi Mungu, Mtume Wake, na waumini, badala ya kutimiza wajibu wao wa Sharia wa kuliondoa umbile hili lemavu na kurudisha Msikiti wa Al-Aqsa na Palestina yote kwenye asili yake – ardhi ya Kharaaj ambayo hakuna mtu anayemiliki haki ya kuiacha hata shubiri yake moja. Lakini wao ni ruwaybidha (watawala duni watepetevu), hawafanani na Ummah huu uliotoa viongozi wakubwa walioikomboa Al-Aqsa kutoka kwa Wapiganaji wa Msalaba, kama Salahuddin Al-Ayyubi alivyofanya, na ambao waliihifadhi Palestina kama Sultan Abdul Hamid II licha ya vishawishi vya Mayahudi kwa pesa na dhahabu – wakati ambapo Khilafah ilikuwa inawahitaji sana. Lakini alikataa hata wazo kwamba Mayahudi waishi katika Ardhi Takatifu kwa msingi wa Agano la Umar, achilia mbali kuwaruhusu kuanzisha dola inayonajisi matukufu ya Waislamu, kuwaua watoto na wanawake wao, na kuangamiza mazao na watoto.
Alisema maneno yake maarufu: “Ikiwa Dola ya Khilafah itachanika siku moja, basi wanaweza kuichukua Palestina bila malipo. Lakini maadamu tu niko hai, kisu mwilini mwangu ni sahali kwangu kuliko kuona Palestina ikikatwa kutoka kwenye mwili wa Ummah – na hili halitakuwa. Siwezi kukubali kuipasua miili yetu tukiwa bado hai.”
Kauli hii inakusudia kukataa kwa Sultan Abdul Hamid II kuitoa Palestina, akiichukulia kuwa sehemu isiyoweza kutenganishwa ya Dola ya Khilafah. Alikuwa mkweli — kwani Palestina ilichukuliwa bila malipo baada ya kuanguka kwa Khilafah na kugawanyika kwa ardhi za Waislamu!!
Kama ilivyoandikwa pia katika makala ya Al-Burhan: “Vita vinatishia utulivu wa Bahari Nyekundu upande wa mashariki, na eneo tete la Sahel upande wa magharibi, na vinahatarisha moja kwa moja maslahi ya Marekani.”
Al-Burhan anajali maslahi ya Marekani, ambayo kwa kweli ni maslahi ya kikoloni yanayolenga kudhibiti eneo hili kwa ajili ya rasilimali zake. Ama kuhusu Sudan, maslahi ya Amerika ni kuichana chana Sudan, baada ya kufanikiwa kutenganisha kusini yake, na inatafuta kukamilisha mpango wake wa kihalifu kwa kuitenganisha Darfur. Rais aliyeondolewa madarakani Omar Al-Bashir alikiri kwamba Amerika ilitenganisha kusini na inataka kuigawa Sudan katika dola tano. Alisema katika mahojiano na Shirika la Sputnik la Urusi: “Shinikizo na njama za Marekani dhidi ya Sudan ni kubwa, na chini ya shinikizo la Marekani kusini mwa Sudan ilitenganishwa.” Aliongeza: “Tuna taarifa kwamba Amerika inatafuta kuigawa Sudan katika dola tano.” (Al Jazeera Net, 25/11/2017).
Kwa hivyo ikiwa Al-Burhan anajua mpango huu na bado anajali maslahi ya Marekani, hilo ni janga. Na ikiwa hajui, basi janga hilo ni kubwa zaidi!
Ukweli unaojulikana kwa kila Muislamu ni kwamba makafiri wakoloni ni maadui wa Uislamu na Waislamu, kwa mujibu wa maandiko dhahiri ya Qur'an. Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:
[إِنَّ الْكَافِرِينَ كَانُوا لَكُمْ عَدُوّاً مُبِيناً] “Hakika makafiri ni maadui zenu walio wazi wazi.” [Surah An-Nisa:101] na aya zengine zinazothibitisha uadui wa makafiri kwa Waislamu.
Ibrahim Othman (Abu Khalil)
Msemaji Rasmi wa Hizb Ut Tahrir
katika Wilayah Sudan
| Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Wilayah Sudan |
Address & Website Tel: 0912240143- 0912377707 http://www.hizb-sudan.org/ |
E-Mail: Spokman_sd@dbzmail.com |



