Jumanne, 03 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/05
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Haki na Ulinzi kwa Waislamu Yatapatikana Pekee Chini ya Khilafah

Vidonda vya Waislamu Vitapona Pekee kwa Kurudi Khilafah

(Imetafsiriwa)

Kwa kuvunjwa Dola ya Uislamu mnamo 1924 na kwa kukosekana mtawala wa Kiislamu anaye wahami na kuukata kila mkono unaonyoshewa mwanamume au mwanamke Muislamu kwa njia mbaya, mishale inaelekezewa Ummah wa Kiislamu kutoka pande zote. Vidonda vyake vimeongezeka, maumivu na majanga yake yamezidi, na maadui wake wamekazanisha mashiko yao katika ardhi na utajiri wake, na kupanga njama dhidi yake pamoja na watawala waliowapandikiza juu yake ili kutumikia maslahi yao na kutabikisha maagizo na amri zao.

Waislamu katika sehemu nyingi ulimwenguni wanapitia mateso na wanapewa vibandiko vya ugaidi. Damu na heshima zao zimekiukwa kwa sababu zisizo na msingi na chini ya anwani za kirongo, ikiwemo "kupambana na ugaidi". Kibandiko hiki kipana kimewapa maadui wa Uislamu uhalali wa kutapika sumu zao na chuki yao na kutangaza vita vyao juu ya wote wale wanaonusuru dini hii.

Watu wa batili wanafanya kazi, mchana na usiku, ili kuufanya mfumo wao wa Kimagharibi wa kirasilimali na hadhara yao daima zitawale, na uwe ndio kiongozi mkuu anayeuongoza ulimwengu. Wanapanga njama ili mambo yasiwaponyoke mikononi mwao na kuingia mikononi mwa wale wanaowakilisha hadhara ya Uislamu au wanaotafuta kurudi kwake. Wanaichukulia kuwa hatari halisi inayotishia hadhara yao na itaiangamiza – endapo itaregea – kuwa vumbi linalo peperushwa na upepo. Hakika, hadhara ya Uislamu itauangamiza mfumo wao wa kirasilimali na maslahi yao, na itayaongoza maisha kwa mujibu wa sheria adilifu na ya kiwahyi ambayo haitaruhusu ujinga wa wenye nguvu na matajiri, wala udhalimu kwa wanyonge, na itaeneza rehma, kheri, usalama, na utulivu … Hivyo basi, watu wa batili hawatashindwa kutumia silaha zao zote ili kuizuia isirudi maishani.

Katika sehemu nyingi za dunia, Waislamu wanateseka kutokana na aina nyingi za dhulma na mateso. Hakuna jibu kwa maombi ya wanawake na hakuna anaye jibu miito na vilio vya watoto. Ulimwengu unatazama mauwaji na uhalifu kimya kimya, na kubwa ambalo mashirika ya kimataifa yanayo dai kuhami haki za kibinadamu yanalofanya ni kushutumu na kutoa takwimu za idadi ya majeruhi na viwango vya hasara! Ripoti zimethibitisha kuwa ziko kamili katika uhalifu uliotekelezwa dhidi ya Waislamu, na kwamba ni natija ya nidhamu hii ya kimataifa isiyojali kuhusu maisha ya watu wasio na hatia na haijali kuhusu kuteseka kwao wala maumivu yao, kwani wanalojali tu ni kuhakikisha kubakia hai kwake na udhibiti wake juu ya ulimwengu.

Chini na nidhamu hii ya kiulimwengu ya kirasilimali, Waislamu wanateseka:

Katika eneo la Turkestan Mashariki, viungo vya miili ya Waislamu waliohai vinauzwa kwa Wachina, wanaume wanauwawa, wanawake wanabakwa, ufungaji kizazi kwa nguvu unalazimishwa, nywele zao zinanyolewa na kuuzwa kwa kiwango cha pesa nyingi  - na idara ya Forodha ya Amerika imekamata zaidi ya tani 13 za nywele bandia zinazotoka China na inashukiwa kizitengeza kwa kukata nywele za wanawake wa Kiislamu wa Uyghur katika Mkoa wa China wa Xinjiang (Chanzo: Le Monde, 3/7/2020). Kina mama pia wanalazimishwa kupeana watoto wao kwa familia za Kichina ili kusababisha kizazi kilicho tenganishwa na Uislamu.

Na nchini Afrika ya Kati – na kwa miaka mingi – wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka wamekuwa wakiwatesa, kuwauwa na kuwanyanyasa Waislamu, na mauwaji haya ya halaiki yanafanyika chini ya ufadhili wa serikali iliyo pandikizwa na Ufaransa, na mauwaji mapya yalitekelezwa mnamo 4/7/2020 dhidi ya Waislamu ambapo wahanga wengi walikuwa ni wanawake. (Chanzo: Gazeti la Kielektroniki la Al-Omah).

Eneo la Kashmir, Waislamu wanateseka kutokana na unyanyasaji, kukamatwa, na matumizi ya ghasia dhidi yao, na Waziri wa Kigeni wa Pakistan Shah Mahmood Qureshi aliashiria hili, akitaja kuwa New Delhi "inawachukulia Waislamu wa Kashmir, ambao wanapambana kuamua hatma yao, kama magaidi…"

Burma pia imeanzisha kampeni ya kijeshi dhidi ya Waislamu wa Rohingya na kuwauwa kwa halaiki, iliyowalazimu zaidi ya Rohingya 700,000 kutoka Jimbo la Myanmar la Rakhine kukimbilia Bangladesh.

Uhalifu wa kinyama umetekelezwa… mauwaji ya uchungu yamefanywa… maelfu ya Waislamu wameuwawa bila ya ulimwengu kunyosha hata kidole…

Ama harufu ya vifo nchini Bosnia na Herzegovina, imepenya kila mahali kwa kipindi cha miaka 25, na hadi leo Waislamu wangali wanatafuta maiti za familia zao waliouwawa katika mauwaji ya Srebrenica yaliyochukua maisha ya Waislamu 8000; ndio mauwaji ya kuogofya zaidi na janga kubwa zaidi kuwahi kujulikana na Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Waislamu nchini Bosnia na Herzegovina wangali wanaiamsha kumbukumbu hii uchungu na wanajaribu kutafuta maiti za watoto wao (takriban ni waathiriwa elfu tatu wa mauwaji haya ambao maiti zao hazijapatikana hadi leo). 

Katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa hafla ya ukumbusho kwa maiti 33 za waathiriwa wa mauwaji haya katika makaburi ya ukumbusho katika mji wa Potočari, Savik Javierovich (mwanachama wa Baraza la Uraisi nchini Bosnia na Herzegovina) alithibitisha kuwa "waathiriwa wa mauwaji ya Srebrenica waliuwawa kwa sababu tu walikuwa ni Waislamu na Wabosnia pekee" na akaendelea: "Srebrenica itabaki kuwa ni doa la fedheha katika bapa la uso wa kila mmoja aliyekuwa na uwezo wa kuyazuia mauwaji hayo na hakufanya lolote".

Mnamo Juni 28, 2020 Waislamu nchini Bosnia na Herzegovina walisherehekea kumbukumbu ya miaka 510 ya kuingia kwao katika Uislamu: sherehe zilizo onyesha hisia ya fahari na utukufu katika mshikamano huu na kutamani yale waliyokuwa ndani yake chini ya kivuli cha dini hii ambayo Magharibi iliyaondoa maishani mwao na katika maisha kwa jumla, na kulazimisha nidhamu yake ovu ya kirasilimali juu ya Uislamu na Waislamu wanaoteseka na kupitia aina zote za mateso, ikiwasababisha kutamani dola ambayo iliwalinda na kuwaruhusu kuishi kwa usalama na utulivu, ambapo shingo zao zimeinuka zikisubiri kurudi kwake.

Chini ya mfumo huu wa kiulimwengu unaotawala kwa sasa: Waislamu haswa, na wanadamu kwa jumla, wanateseka.

Magharibi imepandikiza vibaraka ambao wamejitolea kutumikia maslahi yao, wanaowatawala Waislamu na kujitolea kuwanyanyasa na kuwasababishia majanga: umasikini, njaa, vita, nk… hadi wakawa kama mayatima mezani mwa matapeli. Ardhi zao zikagawanywa, utajiri wao ukafujwa, na wakatawalia na serikali vikaragosi zinazo kandamiza harakati zao, wakati mwengine kwa vikwazo na wakati mwengine kwa uhadaifu.

Aina za mateso katika nchi za Waislamu ni nyingi, zinazotokana na firauni wanaotawala watu na kuwakandamiza kwa nguvu na kueneza mauaji, maangamivu na vita na kupanda mbegu ya hofu na vitisho nyoyoni mwa watoto wao; Syria: zaidi ya watu laki nne wameuwawa nchini Syria tangu 2011 (Chanzo: shirika la Human Rights Watch: Al-Jazeera Net, 13/3/2020). Mateso pia yanaonekana katika mabaa ya njaa na umasikini. Yemen: UNICEF mnamo 26 Juni 2020 ilionya kuwa idadi ya watoto wanaokosa lishe bora nchini Yemen itapanda hadi milioni 2.4 kufikia mwisho wa mwaka huu kutokana na uhaba mkubwa wa ufadhili wa misaada ya kibinadamu. Pia inaonyesha udhibiti wa dola kuu juu ya hatma za watu na ulazimishaji wao wa miradi na sheria zinazo dhoofisha na kupiga vita vifungu vya Sharia na kuwasukuma Waislamu kuishi kwa migawanyiko na kutengana na dini yao na vifungu vyake. 

Ingawa aina za mateso ya Waislamu zinatofautiana, sababu ni moja, nayo ni kukosekana kwa nidhamu ya dini yao katika maisha yao na utawala wa nidhamu fisidifu ya kisekula juu ya shingo zao na kote ulimwenguni. Nidhamu iliyoundwa na mwanadamu inayo eneza dhulma na kiza, iliyo shindwa kuwaokoa wanadamu kutokana na majanga mtawalia na iliyo shindwa kutatua matatizo yake yenyewe. Nidhamu inayotoa uvundo wa vifo na kuwatupa watu ndani ya shimo na kiza, na kuzifanya shingo zilizoinuka zikisubiri kwa hamu mwokozi atakaye watoa kutoka katika duara hili lililofungika lenye kukosesha pumzi.

Haki na uadilifu ambao Waislamu waliushuhudia chini ya dola yao iliyo wajumuisha wale wote waliokuwa chini ya kivuli chake na utawala wake, na historia inatoa ushahidi wa hilo, kinyume na mateso na mauaji yaliyokuwa yakifanyika barani Ulaya… Waislamu walieneza dini yao ya Uislamu kama rehma kwa Walimwengu na watawala waliitekeleza kwa uchaMungu na utiifu Kwake. Licha ya upotoshaji na uongo wa Wamagharibi, historia imethibitisha kuwa dola ya Kiislamu ilikuwa ni mfano mkubwa wa uchungaji mambo ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu walioishi chini ya kivuli chake. Amir Shakib Arslan anataja sifa za dola ya Uthmani katika kitabu chake, The Modern Islamic World, akiashiria kwamba "kuheshimu mikataba, na kutenda kwa mujibu wa ahadi ya mtu ni miongoni mwa mambo mazuri ya Wauthmani, ambayo kwayo historia yote ya Wauthmani inazunguka".

Wakati Waislamu walipokuwa na dola, wengi wa watawala wao – katika miamala yao na raia wao – walimuiga Mtume wao kipenzi (saw) aliyemcha Mwenyezi Mungu katika viumbe vyake vyote, na alikuwa ni rehma kwa Waislamu na wengineo; akiwapa uangalizi na ulinzi, hivyo waliishi kwa usalama na kuridhika…

Ibn Saad ametaja katika "Al-Tabaqat" yake andiko la barua ya Mtume kwa Wakristo wa Najran: "Mtume (saw) alimwandikia Askofu wa Bani Harith bin Kaab na maaskofu wa Najran, makasisi wao, watawa na wafuasi kwamba "watamiliki kila kilicho mikononi mwao ima kikubwa au kidogo, ikiwemo mali yao, ibada, au watawa, na ulinzi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume Wake. Hakuna Askofu atakaye lazimishwa kuachana na uaskofu wake wala hakuna mtawa atakaye ambiwa aachane na utawa wake wala mtu wa dini atakaye ambiwa aachane na imani yake. Hakuna haki yao itakayo geuzwa, wala mamlaka yao au chochote katika tamaduni zao za nyuma, maadamu watu watatekeleza majukumu yao kisawasawa, hakuna atakaye kosewa, wala yeyote atakaye ruhusiwa kuwakosea wengine".

Na pindi Damascus ilipofunguliwa, Khalid bin Al-Walid aliwaandikia wenyeji wake: "Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehma, Mwenye Kurehemu. Hii inatoka kwa Khalid bin Al-Walid kwenda kwa watu wa Damascus. Waislamu wanapoingia, wao (watu) watakuwa na usalama kwao wao, mali yao, mahekalu yao na kuta za mji wao, ambapo hakuna chochote kitakacho haribiwa. Wanayo dhamana hii kwa niaba ya Mwenyezi Mungu, Mtume wa Mwenyezi Mungu, Khalifah na Waislamu, ambao kutoka kwao hawatapokea chochote ila kheri maadamu watalipa Jizya".

Sultan Muhammad al-Fateh aliandika uamuzi ambao unasomeka: "Wakristo wa Bosnia wa dhehebu la Francisca waliopewa na uamuzi huu wa Kisultan (ferman) wako chini ya ulinzi wangu. Na naamuru kwamba: Watu hawa na makanisa yao wasisumbuliwe wala wasidhuriwe na yeyote! Wataishi kwa amani ndani ya dola yangu. Watu hawa ambao wamekuwa wahamiaji, watakuwa na usalama na uhuru."

Makhalifah waliwachunga watu wao wenyewe na kuangalia hali zao kwa kuhofia kwamba Mwenyezi Mungu atawahesabu kwa uzembe wao au kuwalaumu kwa lawama kutoka kwa mmoja wa raia wao. Bali, uchungaji wao unajumuisha wanyama na ndege. "Endapo nyumbu atateleza nchini Iraq, Mwenyezi Mungu (swt) atanihesabu kwa kutomtolea njia". (Umar bin Al-Khattab). "Mwageni ngano juu ya milima ili isisemwe kwamba ndege mmoja amekaa njaa katika ardhi za Waislamu" (Omar bin Abdul Aziz) ... Na waliweka mifano bora kabisa katika siasa za watu na uchungaji wa mambo yao.

Hizi ndizo sera za dola ya Khilafah pamoja na raia wake Waislamu na wasiokuwa Waislamu; zenye kuwahami, kuwalinda na kuwapa maisha mazuri na yenye amani, kinyume na mfumo huu wa kiulimwengu wa kirasilimali ambao kanuni na sheria zake hazitoi chochote ila harufu ya kifo, umasikini na njaa… Hivyo, kuna tofauti kubwa baina ya sheria ya wahyi, adilifu na rehemevu inayoleta kheri na uhai kwa Waislamu na watu wote na kudhamini kubakia hai kwao, na sheria ya kibinadamu iliyo sheheni harufu ya kifo… yenye kuuharakisha ulimwengu katika maangamivu.

Kuna tofauti kubwa kati ya dola inayo tawala kwa yale yote yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu na kuujaza ulimwengu kwa rehma na utulivu, na serikali ya kibinadamu inayotafuta kupata maslahi ya kikundi cha warasilimali wanaoeneza sumu, chuki na ubinafsi wao, hivyo kuujaza ulimwengu huu kwa uoga, huzuni na hofu…

Kuna tofauti kubwa kati ya dola ya Kiislamu pamoja na raia wake; Waislamu na wasiokuwa Waislamu, na nidhamu ya kirasilimali inayo tawala ulimwengu leo na majanga inayo waletea Waislamu na wengine…

Kuna tofauti kubwa kati ya nidhamu ya mwanadamu iliyo shindwa kutatua matatizo yaliyozaliwa na sheria zake iliyozipitisha na kuwaacha wanadamu kutapatapa katika bahari ya majanga kwa sababu imeshindwa kuyamaliza na kuamua kugeukia mashirika yake ya kimataifa na mbinu zake nyingi ili kurefusha muda wake ambao unakaribia kumalizika, na kati ya nidhamu ya kiwahyi inayo kabiliana na matatizo yote ya maisha. Viumbe na hukmu zote ni za Mwenyezi Mungu, Mjuzi Zaidi na Mtambuzi zaidi…

Ulimwengu kwa jumla na hususan Waislamu wanahitaji mno nidhamu ya Uislamu ili kuwatoa katika kiza cha dhulma ya mfumo wa kirasilimali na kuwapeleka katika nuru na uadilifu wa Uislamu. Kurudi kwa Khilafah sio tu ni jambo la kisheria (ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt), na bishara njema kutoka kwa Mtume Wake (saw) pekee, bali ni hitajio halisi ninalolazimishwa na uhalisia. Ukweli, hususan baada ya Mapinduzi ya Kiarabu, umethibitisha hamu ya watu kutaka mfumo mpya wa kiulimwengu utakaobadilisha dhurufu na hali zao, na kuuondoa mfumo wa urasilimali maishani mwao baada ya kuwathibitikia kushindwa kwake kutatua matatizo yao na ufisadi wake… 

Matarajio ya Waislamu kwa mfumo wa dini yao, ambao utabadilisha maisha yao, yamebadili sura ya ulimwengu, kuangusha mizani na kuuregesha Ummah wa Kiislamu mahali pake pa kimaumbile (kuongoza ulimwengu na kuuendesha kwa nidhamu adilifu ya Muumba), hii ndio hali ya kimaumbile ya Ummah wa Uislamu, na haukuwa udhaifu wake, na ndio ilivyo, ila ni jambo lisilo la kawaida. Hivyo basi, kushona na kutibu vidonda vya Ummah kutapatikana pekee kwa kurudi dola ya Uislamu, ambapo kidonda cha kina – kukosekana kwa mfumo wa Kiislamu katika maisha – kitapona – na vidonda vyote vyengine vitapona.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Zeinah As-Samit

#Srebrenica25YearsOn   #Srebrenitsa25Yıl  #SrebrenicaMiaka25Baadaye  سربرنيتشا_جرح_لم_يندمل#

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumatatu, 27 Julai 2020 22:09

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu