Jumapili, 22 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/24
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Familia ya Kiislamu … Na Hatari za Kuvunjika
(Imetafsiriwa)

Familia ya Kiislamu imepigwa na hatari kubwa sana inayoitishia kutoweka, kuvunjika misingi yake na kutahadharisha maangamivu yake na kukata mafungamano ya jamaa zake. Kiungo cha familia, kilicho tawaliwa na mapenzi, mshikamano na utulivu, kiinje inaonekana kuwepo na umoja, lakini kindani imegawanyika, imeunganishwa tu na kuta za nyumba au meza ya chakula; nyumba ambamo mtu anaishi kama ambaye hajulikani miongoni mwa wengine na hawashirikishi katika hofu na matatizo yake binafsi! Kuvunjika huku kumewakumba wanafamilia na kuwapasua na kuwafanya waishi kibinafsi binafsi, wakiteseka kutokana na natija ya mfarakano, upweke, huzuni na kupoteza.  

Kiungo cha familia – taasisi ya kwanza kuu yenye kumlea mtoto na kumjenga fahamu ili kuzitekeleza maishani mwake na kuunda shakhsiyya (utambulisho) yake – iliathiriwa na mambo mengi yanayo lihujumu umbile lake. Hivyo basi, dori za familia zilidunishwa na matatizo mengi yakaibuka; ilitawaliwa na ukavu na mafungamano ya mapenzi yakavunjika na kila mwanafamilia akawa na ulimwengu wake kivyake. Watoto hawawazingatii wazazi wao au ushauri wao: utundu na uchoyo umetawala; hawaoni kupuuza haki za wazazi kama dhambi au kosa. Wazazi pia wanashiriki katika lawama hii ya hali ya watoto wao kwa sababu ya kutofanya kazi yao ya kuwalea watoto kwa umakinifu. 

Maradhi mabaya yanayoisibu familia ya Kiislamu yanayoitwa “kuvunjika kwa familia” ndio tatizo kuu sawia na matatizo mengi yanayoukumba Ummah wa Kiislamu. Ni nini iliyo yasababisha? Je, yatatibiwa vipi?

Kuvunjika kwa familia ni kuyeyuka kwa mafungamano ya familia na kudhoofika na kutoweka kwa mapenzi miongoni mwa wanafamilia huku uhusiano wao unapo kauka; mapenzi sio sehemu yake tena, na nyumba hugeuka kuwa “bweni” ambamo wanafamilia huishi tu na kula humo. Mwanya mkubwa uliundwa kati ya wanafamilia na kila mmoja wao anaishi kama mgeni kwa mwengine.  Ni hatari sana huku kuyeyuka kwa mvunjiko wa familia ni mvunjiko kwa mujtamaa na Ummah wa Kiislamu ulioipatia familia umuhimu mkubwa kama Dini yake ilivyo fundisha hili, na kufafanua kuwa hali nzuri na amani katika mujtamaa imefungamanishwa na kiungo cha familia.

Allah (swt) amesema:

﴿وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم موَدَّةً وَرَحْمَةً

"Na katika alama zake ni kule kukuumbieni kutokana na nafsi zenu wake ili mupate utulivu ndani yao; na akajaaliya baina yenu mapenzi na huruma. Hakika katika hilo zimo dalili kwa watu wenye kutafakari" [Ar-Rum: 21].

Nyumba ni mahali pa utulivu na ustawi. Huwafungamanisha wanachama wake kwa mapenzi na huruma, na huunganishwa kwa elimu na hukmu za Uislamu; hushindana katika matendo mema ili kupata ujira wake. Baba huchunga familia yake na mama humtii mumewe na kumridhisha na kuwalea watoto wake na kuwazunguka kwa mapenzi na upole. Kila mmoja wao anajua haki za mwenzake na kutafuta jinsi ya kuzitimiza ili kupata radhi za Allah. Uislamu hukuza fahamu kuu zinazotilia nguvu mafungamano ya familia na kuyafanya kuwa ya kipekee. Uislamu ulizitambulisha dori na kumpa kila mwanafamilia kazi ya kusaidiana wenyewe kwa wenyewe ili meli hiyo (kiungo cha familia) isafiri pasi na misukosuko ya upepo au dhoruba, ikiongozwa na nahodha anaye saidiwa na wasaidizi. Kila mmoja wao anatekeleza dori aliyopewa ili kufika salama: radhi za Allah na kuingia katika Pepo Yake. 

Uhusiano kati ya wanaume na wanawake ni uhusiano wa amani, utangamano na utulivu. Sio uhusiano wa vita ambapo uhasama, mizozo na uadui umetawala. Kila upande unajua kazi yake na wanasaidiana wenyewe kwa wenyewe. Katika Malalamishi yake kwa Mtume (saw) kuhusu mumewe, Khawla alisema, “Ewe Mtume wa Allah, nikiwatelekeza watoto wangu watapotea na ikiwa nitawaangalia watakabiliwa na njaa…” Utambuzi na ufahamu huu wa dori unafafanuliwa waziwazi na Khawla Allah awe radhi naye. Anajua kwa yakini kuwa jukumu lake ni kuwalea watoto wake na jukumu la baba ni kuwaangalia kimasurufu; wote wanasaidiana na kuwalea watoto kisahihi pasi na ukatili au kuwadekeza zaidi ili mtoto asikulie kwa chuki na ukosefu wa fadhila au dhaifu na mwepesi wa kukosa heshima kwa wazazi au kutowaangalia.

Mtume (saw) asema: «كفى بالمرء إثماً أن يضيّع من يقوت»"Yatosheleza kuwa ni dhambi kubwa kwa mtu kupuuza kutoa (Nafaqa) kwa wale ambao ni jukumu lake (mke, watoto, watumishi, nk)."

Wazazi wengi wametupa nyumba zao na watoto. Hakuna hisia za kiikhlasi na hakuna mapenzi wala upole!! Jukumu kubwa la wazazi limekuwa ni kutoa chakula na mavazi na vyombo za kisasa katika ulimwengu wa elektroniki katika tarakilishi, tablet na simu za rununu. Wako kwa ajili ya kuwapa watoto starehe lakini hawako maishani mwao; hawaonyeshi mapenzi, upole na hamu kwao; hawana muda wa kuzungumza nao na kukaa na kuwasikiza; kila mmoja yu mbioni akimbizana na wakati kufanya kazi nyingi isipokuwa kufikiria na kufanya kazi kwa bidii ili kuhifadhi umoja wa familia!!

Sababu nyingi zimepelekea kupasuka na kuvunjika kwa familia. Manung’uniko ya mara kwa mara yanayo endelea kati ya wazazi kutokana na mashindano ya kuendesha mambo ya familia na kugeuza dori za kimaumbile ambazo Allah ameziumba kwao husababisha mazingira ya msongo wa mawazo na hili huleta taharuki na kuteseka kwa watoto ndani ya nyumba, ikiigeuza nyumba kuwa mahali pa kuogofya na kutisha palipo tawaliwa na chuki na uchoyo baada ya kuwa ni “chimbuko la utulivu, usalama, mapenzi na upole,” na mahusiano yamebadilika na kuwa tofauti nyingi ambazo wakati mwengine hupelekea talaka na kutengana kwa wazazi. Dkt. Seth Meyers, mwanasaikolojia wa Kiamerika na mtafiti katika mahusiano ya kijamii, anabeba mtazamo kuwa familia zinazo pitia taharuki na ugumu katika ulezi wa watoto aghlabu hukosa usaidizi wa kihisia na kijamii utotoni mwao, ima kwa kupuuzwa na wazazi wao au kutokana na kulelewa katika mazingira ya kifamilia yaliyojaa matatizo na ghadhabu, huku baadhi ya wazazi wakikabiliwa na tatizo kubwa na changamoto katika kumlea mtoto mtundu. Hii ndiyo siri ya uchungu wanaokabiliana nao. (Nahi As-Sarraf: malezi ya watoto … Hisia kimya ya uchungu na hofu ya kufeli: Waarabu)

Tunapaza sauti za ving’ora juu ya viwango vya talaka katika familia za Kiislamu, ambazo zimeongezeka maradufu na kukua zikionya kuporomoka kwa kiungo hiki muhimu katika mujtamaa. Kwa mujibu wa tovuti ya “Aswat Magharibiya”, kesi za talaka katika eneo la Maghreb zimeongezeka katika kipindi cha miaka 8 iliyopita, na takwimu kunakili kuwa katika kila saa moja kesi 10 za talaka zinatokea, yaani kesi elfu 90 kwa mwaka, nchini Tunisia, kesi 41 za talaka zilinakiliwa kila siku, zaidi ya kesi 3 kwa saa moja, kwa mujibu wa “Habari za Al-Sabah” kutoka katika Wizara ya Haki. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kituo cha Kiarabu cha Usajili na Takwimu, kesi sita za talaka husajiliwa kila saa moja nchini Algeria, iliyo wapelekea wachunguzi na wanaharakati wengi nchini Algeria kuonya kuenea kwa kadhia ya talaka nchini humo (euronews). Hali hii ni sawa na nchini Misri, ambayo ni ya kwanza duniani katika kiwango cha talaka; cha kesi 250 kwa siku … wanandoa hutengana baada ya masaa tu ya kuoana … wanawake milioni nne waliotalikiwa na watoto milioni 9 ni waathiriwa wa kutengana. (Al-Youm As-Sabi’: 05/09/2017).

Morocco imeorodheshwa ya tano katika ulimwengu wa Kiarabu katika kiwango cha talaka … kesi 5 za talaka hunakiliwa kila saa moja. Chini ya anwani: “Talaka nchini Libya, Kiwango cha Kutisha, na Nambari Zisizokuweko,” idhaa ya 218 ilisema kuwa makundi ya haki za kibinadamu yanasema kuwa kiwango cha talaka kimeongezeka pakubwa kwa zaidi ya miaka michache iliyopita. Ukadiriaji usiokuwa rasmi unadokeza kuwa kiwango cha talaka katika miaka ya hivi karibuni kimeongezeka hadi karibu asilimia 30, ambayo katika lugha ya nambari yamaanisha kuwa katika kila ndoa 100, kesi 30 zinafikia “mwisho wa furaha”.

N Post imethibitisha kuwa Kuwait imechukua usukani katika ongezeko la idadi ya talaka. Kwa mujibu wa takwimu, asilimia 60 ya mahusiano ya ndoa yalimalizika kwa kutengana katika sehemu ya kwanza ya 2017. Sheria ya Kuwait inawapa wanawake waliotalikiwa wa Kuwait idadi ya manufaa, ikiwemo mshahara wa kila mwezi, nyumba, gari na msaidizi.  Hili ndilo linalo wapelekea baadhi ya wanawake kukimbilia kutafuta talaka ili kupata huduma hizi (kwa mujibu wa Wizara ya Haki nchini Kuwait, kwa mujibu wa tovuti ya Arab Times Online Website). Mnamo 2016, idadi ya mikataba ya ndoa nchini Saudi Arabia ilifikia 157,000. Kinyume chake, kesi 46,000 za talaka zilitokea, yaani asilimia 30 ya uhusiano wa wanandoa humalizikia kwa kutengana. Nchini Uturuki, Idara Jumla ya Takwimu za Rekodi za Mahakama ilitangaza kuwa kesi za talaka katika kipindi cha miaka 10 iliyopita zilikuwa ni asilimia 82. Kesi za talaka jijini Istanbul zilikuwa ni asilimia 62.3 ya faili zote za kesi za kijamii mnamo 2016. (Al Ain News). Pakistan pia imesibiwa na maradhi haya ya kuvunjika na mauwaji ya heshima kuenea pakubwa. Tume moja ya Haki za Kibinadamu imenakili mauwaji 280 chini ya kisingizio cha heshima kuanzia 2016 mpaka Juni 2017.  

Ama kuhusu sababu zake, ni kutokana na haswa na uhuru wa kujitegemea kimada kwa wanawake na kuegemea fahamu za uhuru kutokana na mamlaka ya wanaume na uwezekano wa kuachana naye, hususan ikiwa mwanamke hana furaha na mumewe au ikiwa kuna dosari ya awali katika uhusiano inayopelekea matatizo ya kimada yanayo chochea mfadhaiko wa kisaikolojia baina ya wanandoa, inayopelekea taharuki katika uhusiano wa kihisia kutokana na kushinda kuyamudu mahitaji ya kimada ya familia.

Na viwango hivi vya juu vya kuogofya sio vyote bali ni mifano tu; nchi nyingi nyenginezo zinaugua kutokana na kadhia hii inayo enea na kuenea katika familia za Kiislamu kwa sababu ziko mbali na fahamu sahihi za Kiislamu za ndoa ambayo ni mkataba mzito ulio waunganisha wanandoa, na talaka zinatokea kwa sababu ndogo ndogo … Matatizo mengi makubwa mara nyingi hupelekea talaka na kuporomoka kwa familia na hali nguvu kwa watoto.  

Kama natija ya kuvunjika huku na kufarakana, wanafamilia huhisi kupotea na kuishi pasi na usalama; ni wanyonge na kushindwa kutatua matatizo inayo wapelekea kutafuta njia rahisi zaidi na za karibu, hata kama si za halali na kuwaletea hasara.

Kwa kuwa wanajua umuhimu mkubwa wa familia ya Kiislamu ni kujenga watoto na kuwatayarisha kuwa wanaume wa mustakbali, Wamagharibi wametumia mbinu na njia zote kueneza sumu yao ili kuivunja na kuimaliza. Wametulizia makini juhudi zao kwa wanawake, walio na jukumu la ulezi wa vizazi, na kuamua kuchafua na kufisidi fahamu zake sahihi kwa fahamu zao fisidifu zinazomfanya kutupa dori yake muhimu zaidi ambayo Allah alimchagulia yaani, ulezi wa watoto na kuwajenga. “Mama ni shule, ukimuandaa, unawaandaa watu wenye suluki nzuri.” Wamagharibi wamebuni majukwaa na kufanya makongamano na warsha ili kueneza fikra huru za uharibifu. Catherine Forth, Profesa wa Kiamerika, alisema, “Makongamano na makubaliano ya kimataifa yanayohusu wanawake, familia na watu … kwa sasa yanaundwa ndani ya mashirika na kamati zinazo tawaliwa na mambo matatu: utetezi mkali wa wanawake, kupambana na ongezeko la uzazi na watu, mahusiano ya kimapenzi baina ya jinsia moja kwa wanawake na wanaume. Kamati ya wanawake katika Umoja wa Mataifa ilianzishwa na mwanamke wa Kiskandinavia anaye amini ndoa ya wazi, kupinga familia, akikadiria kuwa ndoa ni kizingiti na kuamini kuwa uhuru wa kibinafsi ni lazima uwe wa kikamilifu … Fahamu hii ya uhuru imeangaziwa katika kanuni zilizotolewa na kamati hii. Kutiwa saini kwa makubaliano ya CEDAW kunafanya kupinga ushoga – hata kwa kuchora vinyago – kitendo kinachompelekea mtendaji wake kuhisabiwa na sheria kutokana na kuwa “kinapinga haki za kibinadamu”.

Hivi ndivyo Wamagharibi, ambao wataridhika pekee pindi Ummah wa Kiislamu unapofuata mfumo wao wa kimaisha, wanavyo taka. Wanapanga njama mchana na usiku kuhujumu hadhara yake na kuung’oa Ummah kutoka katika mizizi yake ya Kiislamu. Izza iko kwa Allah (swt). Atawashinda Wamagharibi hawa na kumaliza vitendo vyao na mipango yao, na Yeye (swt) atauregesha Ummah huu katika uongofu na kuupa ilhamu ya kurudi katika utawala wa baraka kwa sheria za Allah na kuasisi mujtamaa unaoongozwa kwa fahamu safi na za ikhlasi ambazo ndio msingi wa malezi ya watoto. Watakuwa ndio wale watakaolelewa kisahihi kwa mizani na kuwafanya taifa bora lililotolewa kwa watu.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Zaina As-Samit

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 12 Aprili 2020 07:19

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu