Alhamisi, 19 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/21
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Mapinduzi ya Kijeshi Nchini Zimbabwe Ni Mbinu Tu ya Kikoloni ya Kufanyia Ukarabati Nidhamu Mbovu ya Demokrasia Iliyovunda

Mwanzoni ikitambulika kama ghala la chakula la Afrika, mnamo Jumatano iliyopita 15 Novemba 2017; Zimbabwe ilitiwa taharuki ya kisiasa baada ya viongozi wake wa kijeshi kuchukua mamlaka ya nchi hiyo kwa njia ya mapinduzi, wakieneza vifaru ndani ya jiji kuu la Harare na kumueka raisi Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 93 chini ya kifungo cha nyumbani. Katika hotuba iliyo peperushwa katika runinga, msemaji wa jeshi la nchi hiyo Meja Jenerali Sibosiso Moyo, alisema kuichukua nchi hiyo ilikuwa ni kwa lengo la "kuleta utulivu kutokana na kuzorota kwa hali ya kijamii na kiuchumi", pamoja na kuwalenga wahalifu wanaomzunguka Mugabe.

Hisia kali zimeibuka kutoka kwa vyama vya kieneo na kimataifa kuhusiana na mgogoro huu, huku Muungano wa Afrika (AU) ukiuita mgogoro huu "unaonekana kama ambaye ni mapinduzi" ukilisihi jeshi kusitisha matendo yake na kuregesha hali ya utulivu wa kikatiba. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito kwa pande zote nchini Zimbabwe kuonyesha "kujizuia" na kurai kudumishwa kwa amani na kukomeshwa kwa ghasia. Waziri wa Kigeni wa Uingereza Boris Johnson alitoa taarifa kwa bunge la Uingereza almaarufu 'House of Commons' kuhusu mgogoro unao endelea akisema, "Hatuwezi kuelezea jinsi gani matukio nchini Zimbabwe yatakavyo kuwa siku za mbeleni na hatujui kama huu ndio mwanzo wa kuanguka kwa Mugabe au la, na tunatoa wito wa utulivu na kujizuia." Akaongeza kuwa kitu pekee ambacho daima Uingereza imekuwa ikitamani kupatikana kwake ni uhuru wa watu wa Zimbabwe wa kujiamulia mambo yao wenyewe, ambapo Mugabe alikuwa ameigandamiza demokrasia na kuudhuru uchumi wa nchi hiyo. Aliongezea kusema zaidi: "Kamwe hatutasahau mafungamano thabiti ya kihistoria na ya kirafiki na nchi hiyo nzuri; inayotambulikana barabara kama kito cha thamani cha Afrika." Alitoa wito wa kufanywa kwa uchaguzi huru na wa haki uliopangwa kufanyika mwaka ujao na kusema kuwa Uingereza itafanya kazi kuhakikisha inawapatia Wazimbabwe "fursa muwafaka… ya kujiamulia mustakbali wao"

Mnamo Ijumaa iliyopita tarehe 17 Novemba 2017, Wazimbabwe waliamkia hali ya wasiwasi baada ya raisi Mugabe kukataa kujiuzulu. Mambo kadhaa yamepelekea kuwepo kwa tandabelua hili la kisiasa:

Hali inayozidi kuzorota ya kiuchumi kutokana na kupungua kwa uzalishaji jumla wa nchi kwa asilimia 40%, mazao ya ukulima kushuka kwa asilimia 51% na uzalishaji wa viwanda kushuka kwa asilimia 47%. Serikali ya Mugabe imeshutumiwa kwa hali hii.

Taharuki ndani ya chama tawala cha ZANU-PF baina ya aliyekuwa makamu wa raisi Emerson Mnangagwa (aliye ungwa mkono na jeshi) na mkewe raisi Grace Mugabe (aliye ungwa mkono na kundi la kisiasa la vijana la G40) juu ya ni nani atakaye mrithi mkongwe Mugabe. Kufutwa kazi kwa Bwana Mnangagwa mapema Novemba kunaaminika na wengi kuwa ndio sababu ya hali iliyoko sasa. Alituhumiwa kwa njama ya kumpindua raisi Mugabe. Chama tawala cha ZANU-PF mnamo 14 Novemba kilimtuhumu mkuu wa jeshi la nchi hiyo kwa "tabia ya uhaini" baada ya kumshutumu Mugabe dhidi ya kumfuta kazi Mnangagwa. Kitendo hiki kilisababisha kuenea kwa hali ya kutoridhika miongoni mwa wafuasi wa Mnangagwa na kufichua mgawanyiko mkubwa baina ya makundi ndani ya uongozi wa chama cha ZANU-PF.   

Kumekuwepo na vita vya muda mrefu kati ya wapiganaji maarufu wa kivita – wanasiasa wakongwe wa miaka ya sabiini na thamanini na kizazi kipya cha wanasiasa walioko chini ya ubavu wa Grace Mugabe. Katika miaka ya hivi karibuni, Robert Mugabe amedumu kuwaondoa mashujaa wakongwe wa vita vya ukombozi kutoka katika vyeo vya chama. Wakongwe hawa wa kivita wakavunja mafungamano yao na Mugabe mnamo 2016 na wakaapa kuunda vuguvugu pana pamoja na upinzani kupambana na utawala wake. Chris Mutsvangwa, kiongozi wa kundi la wapiganaji hao wakongwe, wiki jana aliwaambia waandishi habari jijini Johannesburg kuwa Grace Mugabe ni "mwanamke mwenda wazimu" aliye jishindia mamlaka kupitia "mapinduzi… kwa cheti cha ndoa"      

Inavyo onekana ni kuwa mapinduzi haya ya kijeshi hayadhamirii kuweka uongozi wa kijeshi nchini humo badala yake yanadhamiria kutia shinikizo kwa Mugabe anaye ugua kung'atuka mamlakani. Kama baadhi ya vyombo vya habari vinavyo ripoti, kuna uwezekano mkubwa wa kuundwa kwa serikali ya mpito kama natija ya mapinduzi haya.   

Inavyo onekana ni kuwa siku za Mugabe mamlakani ziko ukingoni kama taarifa na juhudi za kuingilia kati hali hii zinavyo ashiria. Kwa kuwa Uingereza ndio inayo dhibiti pote la wanasiasa pamoja na jeshi kwa sasa inataka kumng'oa kibaraka wake Mugabe ambaye wakati mmoja ilimnyanyua daraja kuwa mwanamapinduzi na kumleta kibaraka mwengine kupitia 'uchaguzi wa kidemokrasia'. Uingereza inatumia vibaraka wake na taasisi zake za eneo kama raisi Zuma wa Afrika Kusini, Jumuia ya Maendeleo ya Afrika Kusini (SADC) na Muungano wa Afrika (AU) kujaribu angaa kumueka "mtu anayestahili" katika usimamizi. Tayari raisi Zuma ametuma wajumbe maalum waliokutana na raisi Robert Mugabe na jeshi la Zimbabwe.    

Cha maana zaidi ni kuwa mapinduzi haya mpaka kufikia sasa yameteka nyara hamasa za watu walio na kiu ya mabadiliko nchini mwao. Inaumiza kuona wazimbabwe kutoka katika nyanja zote za kimaisha wamefanywa kuamini kuwa mustakbali wa nchi hiyo ni angavu na kuondolewa kwa dikteta mkongwe kutawaokoa! Watu wa Zimbabwe hawana budi kutambua kuwa mapinduzi ya sasa ya kijeshi ni mbinu tu ya kikoloni ya kufanyia ukarabati mfumo wao mbovu wa kirasilimali uliovunda pamoja na kujaribu kuipa uhai nidhamu fisidifu ya kisiasa ya demokrasia. Barani Afrika, wakoloni hutumia mapinduzi ya kijeshi kuwatupa mkono vibaraka wao wenyewe ambao mwanzoni waliwanyanyua daraja na kisha kuleta vibaraka wapya. Ni wazi kuwa mabadiliko ya uongozi kwa mpangilio ule ule wa kiuchumi wa kirasilimali kamwe hautaleta mabadiliko yoyote msingi.

Imeandikwa na Shaban Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Hizb ut Tahrir Kenya

Kwa Ajili ya Gazeti la Ar-Rayah – Toleo la 157

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumamosi, 18 Aprili 2020 15:51

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu