Ijumaa, 16 Muharram 1447 | 2025/07/11
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Njama Endelevu, Iliyoimarishwa ya Kimataifa ya Kuzuia Mapinduzi ya ash-Sham yasifikie Malengo na Misingi yake

(Imetafsiriwa)

Gazeti la Al-Rayah – Toleo 555 – 09/07/2025

Na: Ustadh Shadi Al-Abboud

Mwenyezi Mungu (swt) alipowapa watu wa ash-Sham baraka za kumwangusha dhalimu mhalifu wa Syria, asubuhi ya tarehe 8 Disemba 2024, licha ya mipango na njama kubwa zilizopangwa na ulimwengu wote wa Magharibi, ukiongozwa na Marekani, ili kuyabatilisha mapinduzi na kuyazuia yasifikie lengo lake, ulikuwa ni utashi, azma, na Iman ya watu ash-Sham, kwa zana zao hafifu na za kawaida, ambapo hatimaye walishinda dhidi ya jumuiya ya kimataifa.

Baada ya ushindi huu mkubwa, vita havikuisha. Badala yake, vilihama kutoka nyanja za kijeshi kwenda kwenye uwanja wa kisiasa. Watu wa ash-Sham waliibuka washindi katika mapambano yao dhidi ya utawala wa kihalifu, na hili linaonekana kwa Wamagharibi makafiri kuwa ni tatizo kubwa. Ndio maana tunaona dola za Magharibi zikijitahidi kuwadhibiti watu wa ash-Sham, ili kuwaibia ushindi huu kutoka mikononi mwao, na kuwanyima kuvuna matunda yake ya kwanza kabisa, yaani, utabikishaji wa Shariah ya Mola wao Mlezi (swt). Wanatumia udhaifu wa utawala mpya unaoongoza Syria kukita mfumo wa kisekula, wakiishinikiza kuiweka Syria kwa mara nyingine tena chini ya mkono wa kimataifa na taasisi zake za kihalifu.

Yeyote anayefuata sera za Magharibi nchini Syria anaweza kuona wazi juhudi za makusudi za kufunga mustakabali wa Syria kwa Magharibi na kuimarisha udhibiti wa Magharibi juu ya nchi hii. Kauli ya hivi majuzi ya Mjumbe Maalum wa Marekani kwa Syria, Tom Barrack, ni mfano mmoja tu wa hili, aliposema Marekani ina "imani kamili na serikali ya Syria na jeshi la serikali mpya ya Syria." Kuondoa vikwazo ili kuhimiza mabadiliko kulifanya kazi vizuri zaidi kuliko kuvibakisha hadi Syria itakapotimiza matakwa maalum, Barrack aliongeza. Vile vile, Rais wa Uturuki Erdogan alithibitisha mnamo Jumatano, Juni 25, kwamba nchi yake itaendelea kuunga mkono utulivu wa Syria kwa kuhifadhi uadilifu wa eneo lake na umoja wa kisiasa.

Kwa hivyo, juhudi za dola hizo, kusaidia utawala mpya kusimama kwa miguu yake, ziko wazi. Hata hivyo, juhudi hizi ziko katika njia ambayo wahalifu wa Magharibi wanataka, sio kwa jinsi Mwenyezi Mungu (swt) anavyotaka, anavyoridhishwa navyo, na vile watu wa al-Sham wanavyotaka.

Kuchunguza kwa karibu sera ya utawala mpya kunaonyesha udhaifu wa wazi katika kushughulikia masuala muhimu zaidi ambayo unakabiliana nayo. Hakuna uchukuaji maamuzi au uimara. Badala yake kuna upole kupita kiasi na kuridhika kunakofedhehesha. Hii, kwa upande wake, italeta maafa na kuwa na matokeo ya hatari ambayo yanafungua njia kwa matokeo mabaya. Kwa ajili hiyo, vizuizi na vikwazo vitawekwa katika njia ya watu wa ash-Sham, na kutoa fursa kwa dola zinazoinyemelea kuingilia Syria, kwa kutumia zana mbalimbali, ya kwanza kabisa miongoni mwao ikiwa ni umbile nyakuzi la Kiyahudi.

Utayari wa utawala huo kujivua kitambulisho chochote cha Kiislamu, na kujificha nyuma ya fikra za utaifa, na mradi wa kisekula, ni kilele cha udhaifu na kushindwa, ukifikiri kwamba kwa kufanya hivyo utapata idhini ya Magharibi, ambayo ingeweza kulinda kiti chake cha utawala. Bali Mwenyezi Mungu (swt) alilizungumzia jambo hili kwa uwazi na akafunga mlango kwa yeyote anayetaka kuzua au kufanya majaribio kwa njia isiyo sahihi, akisema,

[وَلَنْ تَرْضَى عَنْكَ الْيَهُودُ وَلَا النَّصَارَى حَتَّى تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ]

“Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao.” [Surah Al-Baqarah: 120].

Fauka ya hayo, uhalisia umethibitisha bila shaka yoyote kwamba dola hizi zinafanya kazi kwa msingi wa maslahi pekee. Pindi yule waliyemkamata mikononi mwao anapokuwa hana maana tena, humtupa kando ya njia, baada ya kuchuma ghadhabu ya Mwenyezi Mungu (swt), Mtume wake (saw) na Ummah. Bashar mhalifu aliyetupwa, na watawala wasaliti waliotupwa mbele yake, ndio mifano iliyo wazi zaidi.

Kutelekezwa kwa kitambulisho cha Kiislamu, na kuiendea fikra mbovu ya utaifa, kumeshajiisha kila mpatilizaji fursa kughushi historia safi ya mapinduzi ya ash-Sham. Siku chache tu zilizopita, kauli zilitolewa na Msemaji wa Kamati Kuu ya Uchaguzi, Nawar Najmeh, ambazo ziliwashtua watu wa ash-Sham kwa ujasiri wa kupotosha ukweli. Lilikuwa ni jaribio la kufuta maumbile ya Kiislamu ya mapinduzi hayo, historia ambayo ni kubwa mno na adhimu kuweza kudanganywa na mdanganyifu.

Kwa muda wa miaka kumi na nne, watu wa ash-Sham wamewatoa watoto wao wapenzi zaidi, na kujitolea mhanga kile ambacho ni cha thamani zaidi kwao, ili kupindua utawala wa kihalifu na kuanzisha mfumo wa uadilifu unaoegemezwa juu ya itikadi (Aqidah) yao, aqida ile ile ambayo kwayo walipigana na utawala wa kihalifu, na wanamgambo wake wa kimadhehebu na wa ubaguzi wa rangi. Hakuna hata mtu mmoja aliyewahi kuinuka kutoa damu yake, mali yake, na maisha yake ili kuzalisha tena utawala wa kihalifu kwa sura mpya, au kushiriki katika serikali ya kisekula ambayo inaleta Ghadhabu ya Mwenyezi Mungu (swt) na kuchochea hasira yake. Kafara hizi zilizolipwa sana na wana wa mapinduzi hayo, zilifanywa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (swt) na Radhi zake pekee.

Watu wa ash-Sham walikusanyika kuzunguka malengo hayo, wakitaka yatimizwe, wakaandamana katika mapinduzi yao, wanaume kwa wanawake, wazee kwa watoto, wakitoka misikiti kwa sauti wazi zenye matakwa na nyimbo zinazoakisi roho ya Mapinduzi ya Kiislamu, هي لله هي لله ولتحكيم شرع الله  “Mapinduzi ni ya Mwenyezi Mungu, Mapinduzi ni ya Mwenyezi Mungu, na kwa ajili ya kuhukumu kwa Shariah ya Mwenyezi Mungu (swt),” لن نركع إلا لله “Hatumuinamii yeyote ila Mwenyezi Mungu (swt),” na قائدنا للأبد سيدنا محمد “Kiongozi wetu milele ni Bwana wetu Muhammad (saw).” Walitafuta Radhi za Mwenyezi Mungu (swt) pekee na si mwengine, na hivyo wakakumbatia kafara, kufa shahidi, na kutoa kilicho chenye thamani zaidi katika walichokuwa nacho, wakiwa na hakika kabisa kwamba walikuwa kwenye njia inayoelekea kwenye mojawapo ya matokeo mawili matukufu, ushindi au kifo cha kishahidi. Hii ilikuwa kweli hasa wakati ulimwengu wote ulipowaacha na kula njama dhidi yao, lakini mapinduzi yalisonga mbele, kwa uwazi na kwa ukaidi, yakitafuta Radhi za Mwenyezi Mungu na kujitahidi kuinua Neno Lake.

Zaidi ya miezi sita imepita tangu kuanguka kwa dhalimu, na watu wa ash-Sham bado wanasubiri utawala mpya utimize madai na malengo yao, yale yale waliyojitolea kwa ajili yake. Malengo haya matukufu ni utabikishwaji wa Uislamu, kukatwa ushawishi wa kigeni ndani ya nchi yao, kufunguliwa mashtaka kwa wahalifu kutoka kwa utawala uliotoroka wa Bashar na wale wote ambao mikono yao imetapakaa damu, kusimamisha uadilifu wa Kiislamu, na kunufaika kwa utajiri wa nchi, ambao uliibiwa na magenge ya wahalifu na mamluki wa utawala huo.

Katika hatua hii, maswali yalianza kuibuka katika akili za wengi, walipoona matukio na vitendo kutoka kwa utawala mpya ambavyo viliwaacha wakipigwa na butwaa na kushangaa. Msemo ulianza kusambaa kwa mshangao mkubwa kwenye ndimi za watu, “Nendeni zenu, kwa kuwa muko huru,” ukielekezwa kwa mabaki ya serikali na wahalifu wake waliokimbia. Watu wanauliza, vipi kunaweza kuwa na msamaha kwa wale majambazi waliowasababishia madhara makubwa wanamapinduzi? Baya zaidi, wanawezaje kukirimiwa na kujumuishwa ndani ya dola mpya, na hata kupewa nyadhifa za juu na nyeti?

Kwa mfano, baadhi wameandikishwa katika Idara Kuu ya Usalama, na wahalifu kama vile Fadi Saqr wameteuliwa kama maafisa katika "Kamati ya Amani ya Raia," hadi kufikia hatua ambapo sasa anaingilia kati kwa niaba ya majambazi waliofungwa wa utawala wa zamani, na kupanga kuachiliwa huru kwao kwa makundi mara kwa mara. Vile vile, mhalifu Ahmad Al-Omar, mwenye uhusiano wa karibu na Asma Al-Assad, mke wa Bashar aliyekimbia, ameteuliwa kuwa mshauri wa Kamati ya Uchaguzi ya Bunge la Wananchi.

Hili lilidhihirika zaidi wakati wa Kongamano la Amani ya Kiraia lililofanyika mnamo Jumanne, Juni 10, 2025, lililoongozwa na Hassan Soufan, mjumbe wa Kamati ya Amani ya Kiraia, pamoja na ushiriki wa Nureddin Al-Baba, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani katika utawala mpya. Kongamano hilo halikuwa chochote zaidi ya sindano za kuua maumivu zilizokwisha muda wake. Majadiliano hayo yalitoa tu visingizio na uhalali wa kuwaachilia huru majambazi na maafisa wahalifu, yote hayo yakiwa katika jina la kulinda amani ya raia, hadi pale serikali ya Damascus itakapotekeleza "haki ya mpito." Wanaonekana kuamini kuwa hii itatuliza hasira za wale ambao wamepoteza wapendwa wao, na kujitolea sana, baada ya kuvumilia uhalifu wa serikali kwa miaka mingi.

Leo, waumini wa al-Sham wanajaribiwa na Mwenyezi Mungu (swt), baada ya kuwapa ushindi na kuwatukuza nao. Sasa wanakabiliwa na chaguo. Ima wanaweza kuendelea na njia yao na kuonyesha shukrani kwa Mwenyezi Mungu (swt.) kwa Neema Yake kwa kutabikisha Shariah Yake duniani, kusimamisha uadilifu wa Kiislamu baina ya watu, na kuwaadhibu wahalifu, mabaki maovu ya utawala unaokimbia na hivyo kutimiza Maneno Yake,

[لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ]

“Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.” [Surah Ibrahim: 7]. Au, wanaweza, Mwenyezi Mungu (swt) aepushilie mbali, wakufuru Neema ya Mwenyezi Mungu na ushindi, na kukaa kimya mbele ya uovu mkubwa wanaoushuhudia. Hii ni sawa na upotoshaji wa ukweli wa mapinduzi na wizi wa matunda yake kutoka mikononi mwao. Katika hali hiyo, watakabiliana na kutimia kwa Maneno Yake,

[وَإِنْ تَتَوَلَّوْا يَسْتَبْدِلْ قَوْماً غَيْرَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُونُوا أَمْثَالَكُمْ]

“Na mkigeuka atawaleta watu wengine badala yenu, nao hawatakuwa kama nyinyi.” [Surah Muhammad: 38].

Na tunawaambia watu wetu wa ash-Sham: kuweni kama Ummah wenu ulivyo kuwa ukikujueni, kama Waislamu kila mahali wanavyokujueni. Endeleeni kusonga mbele, mkiweka imani yenu kwa Mwenyezi Mungu (swt). Tangazeni kwa sauti na kwa uwazi, mkiyagonga masikio ya wanafiki na wahalifu wakuu: Ndio, kwenye kusimamisha Khilafah Rashida na kwenye utabikishaji wa Shariah ya Mwenyezi Mungu pekee. Mwenyezi Mungu (swt) yuko pamoja nanyi na hataruhusu vitendo vyenu vipotee bure.

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu