Jumanne, 22 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/24
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Watoto Watakuwa na Njaa Daima chini ya Nidhamu za Kibepari

(Imetafsiriwa)

Habari:

Mgogoro wa gharama ya maisha unapozidi kuongezeka nchini Uingereza, umakini umegeukia kiwango cha njaa kinachoathiri watoto nchini humo. Vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti kuwa njaa ya watoto ni mojawapo ya changamoto kubwa zinazokabili shule nchini Uingereza. Kulingana na gazeti la ‘The Guardian’, walimu wakuu na mashirika ya misaada ya chakula wamesema kuwa wanajitahidi kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka kutoka kwa familia ambazo haziwezi kumudu chakula. Kumekuwa na ripoti za watoto kula vifutio ili kutuliza njaa au kujifanya kula kwenye masanduku matupu ya chakula cha mchana ili kuficha ukweli kwamba hawana chakula nyumbani. Baadhi ya watoto wanaingia shuleni wakiwa hawajala chochote tangu chakula cha mchana siku iliyotangulia. Kulingana na kundi la ‘Child Poverty Action Group’, kuna watoto 800,000 nchini Uingereza wanaoishi chini ya mstari wa umaskini ambao hupitisha siku ya shule wakiwa na njaa kwa sababu hawafikii vigezo uchungu vya serikali vya kustahiki milo ya bure shuleni. Mfumko wa bei wa juu na gharama kubwa za kawi zinalazimisha familia kuchagua kati ya kununua chakula na kupasha joto nyumba zao, huku wengi wakishindwa kumudu yoyote katika hayo.

Maoni:

Hali hii ya kuvunja moyo inatokea katika nchi ambayo imetajwa kuwa ya 5 tajiri zaidi duniani. Kuna watoto milioni 4.3 wanaoishi katika umaskini nchini Uingereza, na inatabiriwa kuwa wengi zaidi watalazimika kuingia katika umaskini kutokana na mgogoro wa sasa wa gharama ya maisha. Utafiti wa Chuo Kikuu cha Loughborough nchini Uingereza, uliochapishwa Julai hii, ulionyesha kuwa karibu 40% ya watoto na vijana kaskazini-mashariki mwa Uingereza wanaishi chini ya mstari wa umaskini. Inaripotiwa kuwa kuna benki nyingi za chakula cha msaada nchini humu, ambako wale ambao hawawezi kumudu mahitaji ya msingi huenda kutafuta msaada, kuliko maduka ya McDonalds ambayo yapo karibu kila barabara kuu nchini.

Haya yote ni mashtaka ya kulaani mfumo wa kibepari unaotabikishwa nchini humu na ndani ya dola kote duniani - nyingi zao zikiwa zinakabiliwa na viwango sawa na hivi au vibaya zaidi vya umaskini na njaa jumla na watoto. Ni mfumo ambao daima utashindwa kutoa mahitaji msingi ya wananchi. Hata hivyo, hili haliepukiki chini ya mfumo huu mbovu ulioundwa na mwanadamu ambao unazalisha uchumi uliojaa madeni kutokana na mtindo wake wa kiuchumi wa kimada na unaoegemea riba, na unaoliona tatizo la kiuchumi kama la uzalishaji badala ya ugavi wa mali. Serikali ya Uingereza hivi majuzi bila aibu ilitangaza kwamba ilipanga kuondoa kikomo cha mafao ya kilafi ya mabenki, na pia kuwapunguzia ushuru matajiri wakubwa, ikisema kwamba hii ingewezesha ukuaji wa uchumi nchini. Sambamba na hilo, ilikataa kuondoa awamu mpya ya kupunguza matumizi ya umma ambayo ingeathiri raia wa kawaida, ikiwa ni pamoja na kuweka vikwazo vya manufaa kwa maskini. Mfumo wowote unaoegemeza ukuaji wa uchumi kwenye sera zinazozidi kuwafanya wananchi wa kawaida kuwa maskini zaidi, hasa mafukara - kuwalazimisha kuchagua kati ya njaa na kuganda hadi kufa - hakika hauwezi kuwa mfumo mzuri wa kusimamia mambo ya watu. Serikali baadaye ilibatilisha tangazo lake la kupunguza kodi kwa matajiri kufuatia misukosuko kwenye soko, badala ya kuzingatia athari za kutisha za sera zao kwa raia wa kawaida.

Urasilimali ni mfumo ambao siku zote utawanufaisha matajiri juu ya maskini, wafanyibiashara wakubwa juu ya raia wa kawaida, na wenye nguvu juu ya watu walio hatarini na wanyonge wa jamii. Tunaona kwa mfano; jinsi makampuni ya kawi ya mabilioni ya dolari yanavyopewa uhuru ili kupata faida kubwa kupita kiasi kwa gharama ya familia za kipato cha chini ambazo zimeachwa kutetemeka katika nyumba za baridi kutokana na kushindwa kumudu gharama zao za kawi. Mapema mwaka huu, kampuni kubwa ya mafuta ya BP ilisema kuwa ina "fedha nyingi kuliko tunavyojua cha kufanya nazo" baada ya kupata faida ya karibu pauni bilioni 10. Na urasilimali ni mfumo ambao chini yake daima kutakuwa na mtengano kati ya wale wanaotawala na mahangaiko na shida za wale wanaowatawala. Takwimu za ukuaji wa uchumi zinatukuzwa, huku uhalisia unaolemaza wa maisha ya kila siku ya raia wa kawaida ambao wanaohaingaika kujikimu kifedha ukipuuzwa.

Kinyume chake, mfumo wa Uchumi wa Kiislamu unaliona tatizo la kiuchumi kuwa ni lile la ugavi madhubuti wa mali ili kuhakikisha kuwa kila mtu anakidhi mahitaji yake ya kimsingi, kama vile chakula, malazi na mavazi, na pia kuhakikisha uchumi unakuwa mzuri kiasi kwamba watu binafsi wanakuwa na uwezo kuboresha hali zao za kifedha na kiwango cha maisha. Kwa hivyo, unaharamisha riba na ufichaji mali ambayo inalimbikiza mali mikononi mwa wachache. Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

(كَىْ لَا يَكُونَ دُولَةًۢ بَيْنَ ٱلْأَغْنِيَآءِ مِنكُمْ)

“ili yasiwe yakizunguka baina ya matajiri tu miongoni mwenu.” [Al-Hashr 7]. Uislamu pia unakataza ubinafsishaji wa maliasili kama vile mafuta, gesi na maji - kiasi kwamba wote wanufaike na wema na mapato yao. Mtume (saw) amesema:

«الْمُسْلِمُونَ شُرَكَاءُ فِي ثَلاَثٍ فِي الْمَاءِ وَالْكَلإِ وَالنَّارِ»

Waislamu ni washirika katika vitu vitatu: katika maji, malisho na moto”. Zaidi ya hayo, mfumo wa kiuchumi wa Kiislamu huitoza kodi mali ya ziada ambayo ni zaidi ya ile inayohitajika ili kupata mahitaji ya kimsingi, na hutoza kodi uwezo wa uzalishaji wa ardhi (Kharaj). Hii inapunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa kodi kwa watu binafsi na vile vile kushajiisha biashara, uwekezaji na uzalishaji mali ambao huongeza fursa za ajira. Fauka ya hayo, mfumo wa Kiislamu unaamini uwekezaji mkubwa katika maendeleo ya kilimo na viwanda, na una sera mahususi na yenye tija kubwa ya kilimo ambayo inamwezesha mtu yeyote anayelima ardhi iliyokufa kupata umiliki wa ardhi hiyo. Pia inawaamuru wamiliki wa ardhi kutumia ardhi ya kilimo, ambayo imetolewa na serikali, na kuamuru kwamba ardhi yoyote iliyoachwa bila kutumika kwa zaidi ya miaka 3 itachukuliwa na kugawanywa kwa wale ambao watailima. Haya yote huongeza uzalishaji na usalama wa chakula. Kwa hiyo haishangazi kwamba chini ya utawala wa mfumo wa kisiasa wa Kiislamu - Dola ya Khilafah kwa njia ya Utume - umasikini na njaa viliondolewa katika ardhi. Imepokewa na Yahya bin Said, ambaye alikuwa gavana wakati huo wakati wa utawala wa Khalifa Umar bin Abdul Aziz (ra), kwamba alisema: “Nilitumwa na Umar bin Abdul Aziz kuchukua zaka kutoka Afrika. Baada ya kuikusanya, nilikusudia kuwapa watu maskini. Hata hivyo, sikupata yeyote wa kumpa. Umar bin Abdul Aziz aliwatajirisha watu wote wakati wa zama hizo”.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Dkt. Nazreen Nawaz
Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu