Ijumaa, 10 Shawwal 1445 | 2024/04/19
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali

Riba ni Riba, Sawa Iwe ni Ndani ya Dar ul-Islam au Dar ul-Kufr.

Kwa: Muhammad Abu Khdhair

(Imetafsiriwa)

Swali:

Assalamu Alaikum. 

Je, mwaweza kutuwekea wazi kuhusu rai ya Abu Hanifah na Sufyan al-Thawri na wengineo, kwamba hapana Riba katika Dar ul-Kufr. wakitolea dalili hadith isemayo: “Hapana Riba katika Dar ul-Kufr”. Na wakitolea dalili ya Al-Abbas kuamiliana na Riba katika Dar ul-Kufr. Pia wakitolea dalili kuwa Abu Bakr aliwekeana rahani na washrikina wa Makkah, na Mtume (saw) akashirikiana naye. Je, yafaa kufuata rai kama hizi? na hasa kwa mtu aliyebanwa na dunia ingawa ikunjufu?. Tafadhali mtumieni hili Amiri na mnitumie mimi binafsi. Shukran.

Jibu:

Kwanza: Kwa hakika, Riba ni haramu katika hali zake zote. Haijalishi ni katika Dar ul-Islam ama Dar ul-Kufr. Kwani zimekuja dalili zake zikiwa jumla bila kukhasisishwa, na zimeachwa wazi bila kufungwa. Na hilo ni kama ilivyo katika nususi za kisheria kwenye kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah za Mtume wake (saw).

- Asema Mwenyezi Mungu (swt):

((الَّذِينَ يَأْكُلُونَ الرِّبَا لَا يَقُومُونَ إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا إِنَّمَا الْبَيْعُ مِثْلُ الرِّبَا وَأَحَلَّ اللَّهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا فَمَنْ جَاءَهُ مَوْعِظَةٌ مِنْ رَبِّهِ فَانْتَهَى فَلَهُ مَا سَلَفَ وَأَمْرُهُ إِلَى اللَّهِ وَمَنْ عَادَ فَأُولَئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ * يَمْحَقُ اللَّهُ الرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ وَاللَّهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ كَفَّارٍ أَثِيمٍ))

"Wale walao riba hawasimami ila kama anavyo simama aliye zugwa na Shet'ani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba. Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba. Basi aliye fikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akajizuia, basi yake ni yaliyo kwisha pita, na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye kurudia basi hao ndio watu wa Motoni, humo watadumu. Mwenyezi Mungu huiondolea baraka riba, na huzibariki sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kukanya na afanyae dhambi." [Al-Baqara: 275 – 276]

((يَاأَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَذَرُوا مَا بَقِيَ مِنَ الرِّبَا إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ * فَإِنْ لَمْ تَفْعَلُوا فَأْذَنُوا بِحَرْبٍ مِنَ اللَّهِ وَرَسُولِهِ وَإِنْ تُبْتُمْ فَلَكُمْ رُءُوسُ أَمْوَالِكُمْ لَا تَظْلِمُونَ وَلَا تُظْلَمُونَ))

"Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba zilizo bakia, ikiwa nyinyi ni Waumini. Basi mkitofanya jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe." [Al-Baqara: 278 – 279]

- Na amesema Mtume (saw) - kama alivyopokea Muslim kutoka kwa Ubadah ibn Swamit, amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):

«الذَّهَبُ بِالذَّهَبِ وَالْفِضَّةُ بِالْفِضَّةِ وَالْبُرُّ بِالْبُرِّ وَالشَّعِيرُ بِالشَّعِيرِ وَالتَّمْرُ بِالتَّمْرِ وَالْمِلْحُ بِالْمِلْحِ مِثْلاً بِمِثْلٍ سَوَاءً بِسَوَاءٍ يَداً بِيَدٍ فَإِذَا اخْتَلَفَتْ هَذِهِ الْأَصْنَافُ فَبِيعُوا كَيْفَ شِئْتُمْ إِذَا كَانَ يَداً بِيَدٍ»

“Dhahabu kwa dhahabu, na fedha kwa fedha, na buru kwa buru, na ngano kwa ngano, na tende kwa tende, na chumvi kwa chumvi, zibadilishanwe sawa kwa sawa, mkono kwa mkono. Na hizi aina zikitafautiana basi uzeni mtakavyo itakapokuwa ni mkono kwa mkono”

Na amepokea tena Muslim kutoka kwa Abu Saidi Al-Khudriy, kwamba Mtume (saw) amesema:

«الذَّهَبُ بِالذَّهَبِ وَالْفِضَّةُ بِالْفِضَّةِ وَالْبُرُّ بِالْبُرِّ وَالشَّعِيرُ بِالشَّعِيرِ وَالتَّمْرُ بِالتَّمْرِ وَالْمِلْحُ بِالْمِلْحِ مِثْلاً بِمِثْلٍ يَداً بِيَدٍ فَمَنْ زَادَ أَوْ اسْتَزَادَ فَقَدْ أَرْبَى الْآخِذُ وَالْمُعْطِي فِيهِ سَوَاءٌ»

 “Dhahabu kwa dhahabu, na fedha kwa fedha, na buru kwa buru, na ngano kwa ngano, na tende kwa tende, na chunvi kwa chunvi, sawa kwa sawa, mkono kwa mkono, hivyo yeyote atakayezidisha au kutaka ziada basi atakua hakika amefanya ribaa: mpokeaji na mtoaji katika hilo wako sawa”.

- Na Amepokea Abu Daud Katika Sunan Yake Kutoka Kwa Ubaada Ibn Swamit Kwamba Mtume (saw) amesema:

»الذَّهَبُ بِالذَّهَبِ تِبْرُهَا وَعَيْنُهَا وَالْفِضَّةُ بِالْفِضَّةِ تِبْرُهَا وَعَيْنُهَا وَالْبُرُّ بِالْبُرِّ مُدْيٌ بِمُدْيٍ وَالشَّعِيرُ بِالشَّعِيرِ مُدْيٌ بِمُدْيٍ وَالتَّمْرُ بِالتَّمْرِ مُدْيٌ بِمُدْيٍ وَالْمِلْحُ بِالْمِلْحِ مُدْيٌ بِمُدْيٍ فَمَنْ زَادَ أَوْ ازْدَادَ فَقَدْ أَرْبَى وَلَا بَأْسَ بِبَيْعِ الذَّهَبِ بِالْفِضَّةِ وَالْفِضَّةُ أَكْثَرُهُمَا يَداً بِيَدٍ وَأَمَّا نَسِيئَةً فَلَا وَلَا بَأْسَ بِبَيْعِ الْبُرِّ بِالشَّعِيرِ وَالشَّعِيرُ أَكْثَرُهُمَا يَداً بِيَدٍ وَأَمَّا نَسِيئَةً فَلَا«

“Dhahabu kwa dhahabu: ambayo haijatengenezwa na ilo tengenezwa (dinar), na fedha kwa fedha: ambayo haijatengenezwa na ilo tengenezwa (dirham), na buru kwa buru: kipimo kwa kipimo (sawa sawa), na ngano kwa ngano: kipimo kwa kipimo (sawa sawa), na tende kwa tende: kipimo kwa kipimo (sawa sawa), na chumvi kwa chumvi: kipimo kwa kipimo (sawa sawa) na yeyote atakayezidisha au kutaka ziada basi atakuwa hakika amefanya riba. na hapana neno kuuza dhahabu kwa fedha na fedha ikawa nyingi zaidi, iwe ni mkono kwa mkono. ama kwa kuchelewesha: hapana, na hapana neno kuuza buru kwa mawele na mawele yakawa mengi zaidi, iwe ni mkono kwa mkono. ama kwa kuchelewesha: hapana”

Na yameandikwa katika vitabu vyetu yanayotosheleza kuhusiana na riba. Imekuja katika kitabu cha Nidhamu ya Kiuchumi, [ukurasa 250-254 nakala ya Kiarabu / ukurasa 244 nakala ya Kiingereza]: [Riba na Ubadilishanaji wa Sarafu (Swarf)] – "Riba: ni kuchukua mali kubadilishana na mali nyengine kutokana na jinsi moja, hali ya kuwa zimezidiana. Na ubadilishanaji wa sarafu: ni kuchukua mali kubadilishana na mali kutokana na dhahabu, kutokana na jinsi moja za kufanana, au kutokana na jinsi mbili tofauti, za kiwango sawa au kuzidiana. Na swarf haiwi ila katika mauzo. Ama riba, haiwi ila katika mauzo, au mkopo, au salam…”.

Na Riba haipatikani ila kwenye mauzo na salam (yoyote) isipokuwa katika vitu sita peke yake: kwenye tende, ngano, na mawele, chumvi, na dhahabu na fedha. Na mkopo hupatikana katika kila kitu, hivyo basi si halali kukopesha kitu chochote ili urudishiwe kichache zaidi au kingi zaidi, wala kitu cha aina yoyote kabisa. Badili yake ni (urudishiwe) mfano wa ulichokopesha: aina na kiwango hicho hicho. Na tafauti kati ya mauzo na salam na mkopo: ni kwamba, mauzo na salam huwa kwa (kubadilishana) aina (ya kitu) kwa aina (nyengine) au (kubadilishana) aina moja. Lakini mkopo hapana budi kuwa aina kwa aina hiyo hiyo. Ama riba kuwa katika hivyo vitu aina sita peke yake: ni kwa sababu ya Ijmaa (makubaliano) ya Maswahaba imepatikana juu ya hivyo vitu sita tu. Na kwa sababu pia kwamba Mtume (saw) amesema:

«الذَّهَبُ بِالذَّهَبِ وَالْفِضَّةُ بِالْفِضَّةِ وَالْبُرُّ بِالْبُرِّ وَالشَّعِيرُ بِالشَّعِيرِ وَالتَّمْرُ بِالتَّمْرِ وَالْمِلْحُ بِالْمِلْحِ مِثْلاً بِمِثْلٍ سَوَاءً بِسَوَاءٍ يَداً بِيَدٍ فَإِذَا اخْتَلَفَتْ هَذِهِ الْأَصْنَافُ فَبِيعُوا كَيْفَ شِئْتُمْ إِذَا كَانَ يَداً بِيَدٍ»

“Dhahabu kwa dhahabu, na fedha kwa fedha, na buru kwa buru, na ngano kwa ngano, na tende kwa tende, na chunvi kwa chunvi, zibadilishanwe sawa kwa sawa, mkono kwa mkono. na hizi aina zikitafautiana basi uzeni mtakavyo itakapokua ni mkono kwa mkono”. (Imepokewa na Muslim kutoka kwa ubadah ibn swamit).

Kwa hiyo, Ijmaa na hadith zimekuwa zimetaja juu ya vitu maalumu ambavyo huwa na riba na haithubutu riba ila katika vitu hivi, wala haikuja dalili ya kuharamisha vitu vyengine mbali na hivi vitu aina sita, kwa hiyo, riba haiwi katika vitu vyengine. Na itaingia kwenye vitu hivyo kitu chochote ambacho ni jinsi ya vilivyotajwa na vyenye sifa zake. Ama vyenginevyo havitaingia humo.

Ama kutolea sababu ya kisheria (illah) uharamu wa hivi vitu, haikutajwa katika andiko, kwa hiyo havitatolewa illah. kwa sababu, illah ni iwe ya kisheria, sio ya kiakili. hivyo kama illah haikufahamika kutokana na andiko basi haitozingatiwa.

Ama kukisia illah, haitokubalika hapa kwa sababu, ili kukisia illah yasharutiwa kiwe kile kitu kinachozingatiwa kuwa illah kiwe ni sifa yenye kufahamisha, ili iwe sahihi kufanyiwa Qiyas. Na endapo hicho kitu hakitakuwa na sifa yenye kufahamisha: (kama vile ikiwa ni jina lililoganda, au ikawa ni sifa isiyo fahamisha) basi haitofaa kuwa illah, na wala haitokisiwa kitu chengine…” mwisho wa nukuu kutoka kwenye kitabu cha Nidhamu ya Kiuchumi… na hayo yamefafanuliwa zaidi katika mlango huo huo, waweza kurudia huko.

Na yote hayo yanajulisha kuwa, riba ni haram popote itakapokuwa. Hakuna tofauti ikiwa ni katika Dar ul-Islam ama Dar ul-Harbi. Na hilo ni kwa sababu, nususi za kuharamisha ni za jumla wala hazikukhasisishwa, na hazikufungwa. Na wanachuoni wengi wa fiqh wanasema hivyo.

Pili: Ama yaliyonukuliwa kutoka kwa Mahanafi kwamba yaruhusiwa (riba) katika Dar ul-harbi: hiyo ni Madh-hab ya Abu Hanifah na mwanafunzi wake Muhammad ibn ul-Hasan (na Abu Yusuf ametafautiana nao)…

Ama dalili ulizotaja katika swali lako kwamba wao wanatoa kutoka kwa Abbas na Abubakr: hizo dalili zinahitaji kutizamwa:

1- Kuhusu suala la Al-Abbas (r.a): anasema Abu Jaafar Al-Twahawi, aliyekufa mwaka 321H katika kitabu chake “Bayan Mushkilil Aathaar” chini ya anwani: (Mlango wa Kubainisha Mushkil wa Kilichopokewa kutoka kwa Mtume (saw), ambacho kilitumiwa na Muhammad ibn ul-Hasan kama dalili ya Abu Hanifah kuruhusu riba kati ya Waislamu na washirikina wakiwa Dar ul-Harbi…) kwenye mlango huu asema Twahawi:

“… Kwa hiyo, ikawa katika hizi athaar kwamba riba ilikuwa haramu katika Dar ul-Islam, haramu baina ya Waislamu, kisha tukapata kwamba Mtume (saw) alisema kwenye khutba yake katika Hijja ya kuaga maneno tuliyohadithiwa na Rabii al-Muraadi akisema (kutoka kwa Jaabir r.a kwamba Mtume (saw) alisema katika khutba yake siku ya Arafa katika Hijja ya kuaga:

«وَرِبَا الْجَاهِلِيَّةِ مَوْضُوعٌ وَأَوَّلُ رِباً أَضَعُهُ رِبَا العَبَّاسِ بْنِ عَبْدِ الْمُطَّلِبِ فَإِنَّهُ مَوْضُوعٌ كُلُّهُ»

“Riba za jahiliya zimepomoshwa. Na riba ya mwanzo ninayoondoa ni riba ya Al-Abbas bin Abdil Mutwalib, kwa hakika imeondoshwa yote”… na anaongeza… “kutoka kwa Amr bin Ahwasw asema: nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema:

«أَلَا إِنَّ كُلَّ رِباً مِنْ رِبَا الْجَاهِلِيَّةِ مَوْضُوعٌ، لَكُمْ رُءُوسُ أَمْوَالِكُمْ لَا تَظْلِمُونَ وَلَا تُظْلَمُونَ»

"Jueni na mtambue, hakika kila riba katika riba za jahiliya zimeondoshwa, zenu ni rasilimali, msidhulumu, na hamtofhulumiwa”. Kwa hiyo, katika hayo kukawa na yanayojulisha kwamba riba ilikuwepo Makkah wakati ilipokuwa ni Dar ul-Harb hadi pale ilipokombolewa. Kwa sababu, kuondoka ujahiliya huwa ni kwa kukombolewa kwake. Na katika maneno yake Mtume (saw) kusema “Riba ya mwanzo ninayoondosha: ni riba yetu, riba ya Al-Abbas bin Abdil Mutwalib” kuna dalili hapo kwamba riba ya Al-Abbas ilikuwepo hadi wakati Mtume akiondoa, kwa sababu yeye Mtume haondoi ila kile kilichokuwa kikiendelea, wala sio kuondoa kilichokuwa kimeshaanguka kabla ya yeye kuondoa…”

Hivyo basi, katika hayo kuna dalili kwamba Al-Abbas alikuwa na riba mpaka pale Makkah ilipokombolewa. Na kwa hakika alikuwa Muislamu hata kabla ya hapo. Kwa hiyo, hapo yajulisha kuwa riba ilikuwa halali baina ya Waislamu na washirikina wakati Makkah ilipokuwa Dar ul-Harbi, lakini wakati huo huo ilikuwa haramu baina ya Waislamu katika Dar ul-Islam…

Kama anavyosema Abu Hanifa na Al-Thawriy…”

Na Jibu Lenye Nguvu Kuhusu Hilo:

i) Sio sahihi kutolea dalili kwamba Al-Abas alikuwa akiamiliana na watu wa Makkah kwa riba kwa kuwa ni Dar ul-Harbi. Kwa sababu, Makkah imekuwa Dar ul-Islam kuanzia ilipokombolewa, na ukombozi ulikuwa kabla ya hii hadith kusemwa “na riba ya mwanzo ninayoondoa ni riba ya Al-Abbas bin Abdil Mutwalib…” kwa zaidi ya miaka miwili. Na lau Mtume (saw) ingekuwa ametamka hili wakati wa kukomboa Makkah basi kungekuwa na hoja. Ama kwa kuwa hadith imekuja baada ya miaka miaka miwili basi njia ya kutolea dalili itakuwa sio sawa.

ii) Kisha, riba kutegemezwa kwa jahiliya kwenye hiyo hadith «أَلَا إِنَّ كُلَّ رِباً مِنْ رِبَا الْجَاهِلِيَّةِ مَوْضُوعٌ» “Jueni na mtambue, hakika kila riba katika riba za jahiliya zimeondoshwa” huenda ikajulisha kwamba, hii riba ilikuwa kabla ya Al-Abbas kusilimu. Kwa sababu, ujahiliya ni kabla ya Uislamu. kwa hiyo, lenye nguvu kuhusu maana ya hadith: ni kwamba, Al-Abbas alikuwa akiamiliana kwa riba kabla ya kusilimu, na faida zake za riba zilikuwa kwa waliochukua deni, hivyo Mtume (saw) akamkataza kuzichukua: (فإن تبتم فلكم رءوس أموالكم) na akaelezea kwamba hii riba imeondoshwa.

2- Ama wao kutolea dalili pale waliposema: (na kwa kuwa Abubakr r.a alicheza kamari na washirikina wa Makkah kabla ya Hijra, Mwenyezi Mungu (swt) alipoteremsha (الم -غلبت الروم...) washirikina wakamwambia: je mwadhani Rum watakuja kushinda?! Nikamueleza Mtume (saw) akasema: Ndio. wakasema: uko tayari kuingia kamari na sisi? Abubakr akasema: ndio, akaingia nao kamari. Halafu akamueleza Mtume (saw) na Mtume akasema: nenda uongeze kiasi cha kamari, naye akafanya hivyo. Na kisha Rum wakawashinda Fursi, na Abubakr akachukua alichoshinda, na akamruhusu”. Na hiyo ndio kamari yenyewe kati ya Abubakr na washirikina wa Makkah, na hapo Makkah ilikuwa Dar ul-Shirki…) na neno خاطر maana yake ni: kucheza kamari.

Na jibu kuhusu hilo ni kwa njia mbili:

Njia ya kwanza: wanazuoni wengi wanaonelea kuwa hili lilifutwa. Kwa hiyo, hilo tukio lilikuwa kabla ya kuteremka uharamu wa kamari… Njia ya pili: baadhi ya wanazuoni wanaonelea kwamba, aina hii ya rahan yafaa, na haijafutwa. Kwa sababu, lengo lake ilikuwa ni kuunusuru Uislamu. Na hii ndio kauli aliyochagua Shaikh ul-Islam ibnu Taimiyah na ibn ul-Qayim. Na katika hizo njia mbili zote, kuzitolea hoja ya kufaa riba katika Dar ul-Harbi, ni kauli dhaifu.

3- Kutokana na hayo, basi kauli iliyo na nguvu katika hili suala, ni kwamba, riba ni haramu kati ya Muislamu na Muislamu mwengine, na pia kati ya kafiri na kafiri katika Dar ul-Islam au Dar ul-Kufri/Harbi… na huu ndio msimamo wa wanazuoni wengi wa Madh-ahb ya Malik, Shaafi, na Hanbali. Na kwa ajili ya kujua zaidi… yafuatayo ni maneno ya baadhi ya wanazuoni wa fiqhi kuhusu suala hili:

A. Asema Ibn Qudama Al-Maqdisiy Mwenyezi Mungu amrahamu, katika kitabu cha Al-Mughniy: “na riba ni haramu katika Dar ul-Harbi kama ilivyo haramu katika Dar ul-Islam. Na hiyo ndio kauli ya Malik, Al-Awzaai, Abu Yusuf, Shaafii, na Is-haq. Kwa neno lake Mwenyezi Mungu (swt) aliposema: (وَحَرَّمَ الرِّبَا) na neno lake: (الَّذِينَ يَأْكُلُونَ الرِّبَا لَا يَقُومُونَ إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ) na amesema tena Mwenyezi Mungu (swt): (يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَذَرُوا مَا بَقِيَ مِنَ الرِّبَا) na hadith jumla zinapelekea uharamu wa kuzidiana. na neno lake Mtume (saw): «فمَن زادَ أوِ اسْتَزادَ فقَدْ أرْبَى» “Na yeyote atakayezidisha au kutaka ziada basi atakuwa hakika amefanya riba” ni tamko la jumla. Vilevile hadith zilizobaki, na kwa sababu, kilicho haramu katika Dar ul-Islam pia hua haram katika Dar ul-Harbi, kama vile riba baina ya Waislamu”. Na amesema tena: “ama uharamu wa riba katika Dar ul-Harbi: tumeshataja kwenye mlango wa riba, pamoja na kusema kwake Mwenyezi Mungu (swt): “وَحَرَّمَ الرِّبَا)) na aya nyenginezo, pamoja na hadith zinazo julisha uharamu wa riba: zote ni za jumla zikiihusu riba kila mahali na zama zote” mwisho wa nukuu.

B. Na amesema Nawawiy Mwenyezi Mungu amrahamu katika kitabu cha Al-Majmuu Sharhil Muhadhab: “(riba hukmu yake kwenye Dar ul-Harbi ni sambamba na hukmu yake kwenye Dar ul-Islam. Na huo ndio msimamo wa Malik, Ahmad, na Abu Yusuf. Na dalili yetu: ni dalili jumla zinazo haramisha riba, na kwa sababu, chochote kilicho haramu katika Dar ul-Islam huwa haramu pia katika Dar ul-Shirki, sawa tu na machafu mengine na maasi. na kwa kuwa (hiyo riba) ni mkataba fisidifu hivyo basi hautohalalisha kilicho fungiwa mkataba, kama ilivyo kwa ndoa) ”…

C. Na amesema Imam Shaafii Mwenyezi Mungu amrahamu: (pindi watu miongoni mwa Waislamu watakapoingia miji ya vita kwa amani, basi maadui wawe na amani nao hadi watakapoondoka au wamalize mda wa amani yao. Na haifai kwao (hao Waislamu) kuwadhulumu wala kuwafanyia khiyana”. Mwisho wa nukuu kutoka kwenye kitabu cha Al-Umm (4/263). Na amesema tena katika hicho kitabu (4/284): “na lau mtu ataingia Dar ul-Harbi kwa amani… na akaweza kupata mali zao, basi haitokuwa halali kwake kuchukua kitu chochote, kichache au kingi. Kwa sababu, ikiwa yeye ameaminika nao basi wao pia wapate amani kutoka kwake. Na kwa sababu, si halali kwake - kutokana na amani yao - ila kilicho halali kwake katika mali za Waislamu na watu wa dhimma. Kwa sababu, mali huzuiliwa kwa sababu kadhaa:  kwanza, kwa mwenye mali ni Muislamu, pili: kwa kuwa ni mali ya mwenye dhima, na tatu: kwa kuwa ni mali ya mtu aliye na amani hadi mda wake kuisha”. Mwisho.

Na mwisho: mimi nakuombea kwa Mwenyezi Mungu (swt) akukunjulie riziki safi na halali, akuneemeshe kwa maisha mazuri, ambayo utayamaliza katika kumtii Mwenyezi Mungu, ili ufanikiwe duniani na akhera. Na hayo ndio mafanikio makubwa.

Ndugu Yenu

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

 

8/ Muharram 1443 H

16/8/2021 M

Link ya jibu hili katika ukurasa wa Amiri wa Facebook

 

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu