Jumatano, 22 Rajab 1446 | 2025/01/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali

Mzozo Kati ya Azerbaijan na Armenia
(Imetafsiriwa)

Swali:

"Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev alisema katika hotuba iliyopeperushwa kwenye runinga ya serikali jioni ya Jumapili tarehe 4/10/2020 kwamba Armenia lazima iweke ratiba ya kujiondoa kutoka katika eneo la Nagorno-Karabakh kabla ya kusitisha makabiliano yaliyofanyika huko takriban wiki moja iliyopita ... Aliyev alichukulia kuwa kuudhibiti mji wa Gabriel jana, Jumapili, ni funzo kwa Armenia na wafuasi wake, na inapaswa kuzingatia kutokana na hilo, kama alivyosema." (Al-Jazeera, 5/10/2020).

Mapigano makali yalizuka kati ya Azerbaijan na Armenia asubuhi ya tarehe 27/9/2020 kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea tangu kuanza kwa usitishaji mapigano kati ya pande hizo mbili mnamo 1994, ingawa walirudia mara kwa mara katika mapigano madogo na makubwa wakati mwingine, kama ilivyofanyika mnamo 2016. Uturuki haikuisaida kijeshi Azerbaijan katika mapigano haya yote ya awali. Lakini wakati huu, pindi Uturuki ilipotangaza usaidizi wake kwa Azerbaijan, inaonekana kana kwamba ina malengo fulani!

Malengo haya ni yapi? Na kwa nini Uturuki iliingilia kati sana? Je! Ni upi msimamo wa kikundi cha Minsk, haswa viongozi wake watatu: (Amerika, Urusi na Ufaransa)? Shukran zote za dhati kwenu.

Jibu:

Ili kujua uhalisia wa yanayojiri, tutahakiki mambo yafuatayo:

1- Azerbaijan ilitangaza kuwa Armenia imeanzisha mashambulizi makubwa kwa ardhi yake asubuhi ya tarehe 27/9/2020; Wizara ya Ulinzi ya Azerbaijan ilisema katika taarifa kwamba ("Moto wa Armenia umesababisha vifo vya raia, pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa kwa miundombinu ya raia katika vijiji kadhaa ambavyo vilifanywa kwa risasi nzito za Armenia." Imesema kuwa, " Vikosi vyake vilikumbwa na shambulizi la mabomu." Ilisema kuwa, "Majeshi yake yalijibu mashambulizi hayo na kufanikiwa kuharibu idadi kubwa ya zana za kijeshi za Armenia na magari kwa kina cha mstari wa mbele, ikiwemo mifumo 12 ya makombora ya kupambana na ndege za kivita ya Urusi (OSA) ... ” Al-Jazeera 27/9 / 2020).

Bunge la Azerbaijan liliidhinisha kutangaza hali ya vita katika miji na maeneo kadhaa na kuweka sheria za kijeshi katika maeneo ya mapigano. Kwa upande mwingine, Armenia ilitangaza hali ya vita, na hata kwenye ukurasa wake rasmi picha ya mtawa aliyebeba bunduki ya mashine na msalaba ukining'inia shingoni mwake, ishara ya Shirk (ushirikina), ikionyesha kwamba wanapigana vita dhidi ya Waislamu. Waziri Mkuu wa Armenia, Nikol Pashinyan, alitangaza msimamo wa nchi yake katika hotuba: ("Azerbaijan imetangaza vita dhidi ya watu wake, na kwamba haiondoi uwezekano kwamba kuongezeka kwa vita kunazidi mipaka ya eneo hilo na kunatishia usalama wa kimataifa. Suluki ya Uturuki imejaa matokeo mabaya kwa Caucasus ya kusini na inaisihi jamii ya kimataifa kuhakikisha kwamba Uturuki haiingilii mzozo kati ya Baku na Yerevan juu ya eneo la Karabakh tangu 1991 ...” chanzo cha awali).

2- Azerbaijan imeonyesha kuwa vita wakati huu ni vikali na vita ni havina shaka. Mnamo tarehe 30/9/2020, Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev, alisema: "Mazungumzo juu ya Karabakh hayakuwezekana na hakuna haja ya wito mpya wa mazungumzo, akielezea azimio la Azerbaijan la kurudisha uadilifu wake wa kieneo na kwamba jeshi la Azerbaijan liliweza kufikia mafanikio uwanjani, wakati wa shughuli zake za hivi karibuni katika eneo linalozozaniwa. Hakuna mtu anayeweza kuyalazimisha majeshi ya Azerbaijan kujiondoa kwenye maeneo waliyoyadhibiti. Kuondolewa kwa vikosi vya Armenia ndio sharti pekee lililopendekezwa na Azerbaijan na endapo Yerevan atalitekeleza, mapigano yatasimama." Na akasema, "Tuna sharti moja: : kuondolewa kikamilifu, bila ya masharti na bila kuchelewesha kwa vikosi vya  Armenia kutoka eneo letu. Ikiwa serikali ya Armenia itakubali ... vita vitasimama na umwagikaji wa damu utasimama ... "

(Al-Jazeera; Russia Today, 30/9/2020) Inaonekana kwamba ana imani na msaada wa Kituruki, akidhani kuwa msaada huu ni wa kweli na kwamba itaikomboa ardhi hiyo kwa ajili yake.

3- Mapigano yalizuka tena upya mwaka huu mnamo 12/7/2020 na yalidumu kwa siku tatu, na kusitisha kupotea kwa maisha baina ya ya pande hizo mbili. Halafu, kwa mara ya kwanza, Uturuki ilituma vikosi vya ardhini na angani hadi Azerbaijan kushiriki katika harakati kubwa za kijeshi kati ya nchi hizo mbili zilizoanza tarehe 29/7/2020 na zilidumu kama wiki mbili. Uturuki ilianza kuonyesha kwamba imelitabanni suala la Azerbaijan na ardhi zake zilizochukuliwa na Waarmenia. Hakuna kitu kama hicho hakikutokea hapo awali ingawaje mapigano ya hapa na pale yametokea kati ya pande hizo mbili mara kwa mara tangu kutangazwa kwa kusitisha mapigano mnamo 1994. Mapigano ya mwisho yalizingatiwa kuwa makali kutoka tarehe hiyo, tangu mwanzo wa Aprili hadi Aprili 26, 2016, lakini Uturuki hakuingilia kati pamoja na Azerbaijan; walipokea tu rambirambi za Rais Erdogan kwa kupotea kwa maisha katika mapigano hayo na kuwa tayari kwake kuiunga mkono Azerbaijan bila kutoa chochote! Dhurufu hizo zilihitaji maelewano ya Uturuki pamoja na Urusi na sio makabiliano, kwani Amerika ilipanga ili nchi hizo mbili zisimame pamoja kupandikiza serikali kibaraka wa Amerika ya Syria, ili kuwapiga watu wa Syria wanaoasi dhidi ya serikali hii na kuzuia kurudi kwa Uislamu mamlakani, haswa tangu uasi wa Armenia dhidi ya Azerbaijan ulipoanza mnamo Februari 1988 na uungwaji mkono na Urusi, na kutangaza udhibiti wao juu ya eneo lenye milima la Karabakh mnamo 1991, na kutangaza jamhuri huru kwao na vita vikaendelea hadi 1994. Azerbaijan kwa hivyo ilipoteza zaidi ya asilimia 20 hadi 24 ya ardhi yake, ambayo ni pamoja na eneo la Karabakh, ambalo lina majimbo 5, pamoja na mikoa mengine 5 magharibi mwa nchi hiyo, pamoja na sehemu kubwa za majimbo ya Aghdam na Fuzuli. Karibu wakaazi milioni moja walihama makazi yao kutoka maeneo haya yenye Waislamu wengi. Jeshi la Urusi liliingilia moja kwa moja, na Urusi ingali nyuma ya Armenia, huku nchi hiyo ndogo, idadi ya watu, mamlaka na uwezo zikilinganishwa na Azerbaijan.

4- Uturuki inacheza na kadhia ya Azerbaijan kwa mujibu wa harakati zake ndani ya duara la Amerika na utekelezaji wa maagizo yake. Uturuki ilitia saini makubaliano mapana ya amani na Armenia huko Zurich, Uswizi mnamo 10/10/2009, ambayo yanaitambua mipaka ya sasa kati ya nchi hizi mbili, kufunguliwa kwa mipaka hii, kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia, kubadilishana mabalozi, kufunguliwa kwa mabalozi na kuimarisha mahusiano katika maeneo yote, ushirikiano wa kikanda na kimataifa, kusuluhisha mizozo ya kikanda na kimataifa kwa njia za amani kulingana na kanuni na sheria za kimataifa, kupambana na ugaidi, kuendeleza demokrasia katika mkoa huo, kuunda na kukuza mazungumzo kwa uchunguzi wa kisayansi wa hati na vyanzo vya kihistoria, kuhusiana na kutatua shida ya madai ya mauaji ya halaiki ya Armenia, akibainisha kwamba Erdogan hapo awali alikuwa amekataa "uelewa" na Armenia kabla ya kuyaondoa majeshi yake kutoka kwa ardhi zinazokaliwa za Azerbaijan katika Karabakh na pambizoni mwake.

Hitimisho la makubaliano haya lilitokana na ombi la moja kwa moja kutoka kwa Rais wa zamani wa Amerika Obama, ambaye alitaka ziara yake nchini Uturuki mnamo 6/4/2009 kutatua mzozo kati ya Uturuki na Armenia na kuanzisha amani kati yao, baada ya uhusiano kati ya pande hizo mbili kukatwa na mipaka kufungwa mnamo 1993. Erdogan alitii na kutia saini makubaliano mapana ya amani na Armenia bila ya kushughulikia Azerbaijan na uvamizi wa Armenia kwa ardhi za Azerbaijan, wala suala la Waislamu milioni moja waliohamishwa kutoka kwa watu wa Azerbaijan. Wizara ya Mambo ya Nje ya Amerika ilitangaza kuwa kutiwa saini huko ni tukio la kihistoria na kwamba imeshiriki ndani yake!

5- Wakati huo, Azerbaijan ilikashifu utiaji saini wa makubaliano hayo kabla ya kuondolewa kwa Waarmenia kutoka kwa ardhi zilizokaliwa za Azerbaijan kutimizwa, na Azerbaijan iliitaka Uturuki ifuate ahadi zake za hapo awali za kutofungua mipaka na kuanzisha uhusiano na Armenia kabla ya kujitoa kwa Armenia kutoka kwa ardhi zake zinazokaliwa. Tovuti ya Elaph ilichapishwa mnamo 10/10/2009: [ZURICH: Mawaziri wa Mambo ya nje wa Uturuki na Armenia walitia saini Jumamosi jioni jijini Zurich (Uswizi) makubaliano ya pande mbili ambayo yalilenga kusawazisha mahusiano

kati ya pande hizo mbili. Mawaziri hao wawili, Edward Nalbandyan na Ahmet Davutoglu, walipeana mikono kwa muda mrefu baada ya kutiwa saini ... Phil Gordon, Waziri Msaidizi wa Mambo ya Nje anayehusika na Maswala ya Ulaya na Eurasia alisema, "Jioni ya leo (Jumamosi) tumeshiriki katika hafla ya kihistoria" ... Gordon alikuwa ameandamana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Amerika Hillary Clinton, ambaye aliwasili Jumamosi jioni jijini London kama sehemu ya ziara ya siku tano katika miji sita ya Ulaya. Kabla ya kuwasili London, Clinton alishiriki huko Zurich, Uswizi, katika hafla ya kutiwa saini kwa makubaliano ya Uturuki na Armenia. Kwa upande wake, afisa mmoja mkuu wa Amerika alisema kwamba Obama "ana shauku" juu ya makubaliano hayo na anachukulia kuwa ni "hatua kubwa mbele".

Kwa upande wake, Azerbaijan mnamo Jumapili ililaani makubaliano hayo ya kusawazisha mahusiano kati ya Armenia na Uturuki, na kuonya wakati huo huo kwamba kufunguliwa kwa mipaka ya Armenia na Uturuki kunaweza kusababisha kutokuwa na utulivu Kusini mwa Caucasus. Wizara ya Mambo ya nje ya Azerbaijan ilisema katika taarifa yake, "Kusawazisha mahusiano kati ya Uturuki na Armenia kabla ya kuondolewa kwa majeshi ya Armenia kutoka eneo linalokaliwa la Azerbaijan kunapingana moja kwa moja na maslahi ya Azerbaijan na kunaziba uhusiano wa kindugu kati ya Azerbaijan na Uturuki, ambao ni unatokana na mizizi ya kihistoria. ” (Elaph, Jumamosi, Oktoba 10, 2009) Mwisho.

6- Lakini Erdogan wa Uturuki alijaribu kuidanganya Azerbaijan kwa maneno mazuri bila vitendo. Haikuweka masharti yoyote katika makubaliano ya kuondolewa kwa Armenia kutoka Karabakh, bali ilikubaliana nayo kama yalivyo! Lakini miaka tisa baadaye, Mnamo Machi 2018, chini ya shinikizo la Urusi, Armenia ilifutilia mbali rasmi makubaliano hayo kutokana na kujisalimisha kwa ushawishi wa Urusi. Kwa hivyo, Amerika ilikosa nafasi ya kuichukua Armenia kutoka Urusi kupitia makubaliano haya na Uturuki. Badala yake, Urusi iliimarisha ushawishi wake huko Armenia na kuimarisha silaha zake za makombora katika kambi yake, kambi ya Kiarmenia ya Gyumri, na kisha ikatia saini makubaliano ya pamoja ya ulinzi wa anga mnamo Desemba 2015 na Armenia na kupeleka kikosi cha ndege za MiG-29, na maelfu ya wanajeshi, silaha, mifumo ya ulinzi wa anga na makombora ya masafa marefu ya S-300, na vile vile mfumo ulinzi wa anga wa kati na kati wa SE-6. Urusi ilizindua katika soko lake, Muungano wa Kiuchumi wa Eurasia, ambao ulianza kufanya kazi rasmi mnamo tarehe 01/01/2015, pamoja na Belarusi, Kazakhstan na Kyrgyzstan. Nchi hizi, pamoja na Armenia, zimekuwa soko la utupaji wa bidhaa za Urusi chini ya jina la matembezi huru ya bidhaa na huduma katika nyanja zote. Pato la taifa la soko hili ni zaidi ya dolari trilioni 5 za Amerika, na nyingi zake ni kwa manufaa ya Urusi.

7- Baada ya yote hayo, Amerika ilitafuta njia zingine za kuimarisha ushawishi wake huko Azerbaijan na kudhoofisha ushawishi wa Urusi ndani yake, na kisha kuingia Armenia. Iliiagiza Uturuki kuimarisha uhusiano wake wa kijeshi pamoja na uhusiano wa kiuchumi na kisiasa na Azerbaijan ili kuongeza ushawishi wa Amerika na kuishinikiza Armenia kufungua milango ya ushawishi wa Amerika, hadi mapigano ya mwisho yalipotokea Julai iliyopita kana kwamba ni kitendo cha makusudi hivyo kwamba Uturuki inaweza kuyatumia kama kisingizio cha kuingilia kijeshi, na kutuma vikosi kwa mafunzo na harakati za pamoja, na kisha mapigano ya ghasia ya hivi karibuni yalizuka na hali ya kivita kwa pande zote mbili ikatangazwa.

Mara tu baada ya mapigano haya, Rais wa Uturuki Erdogan aliandika mnamo tarehe 27/9/2020 kwenye akaunti yake ya Twitter kufeli kwa jamii ya kimataifa kujibu mashambulio ya Armenia inaonyesha unafiki wake. "Kwa kushikilia msimamo wake wa kizembe kwa karibu miaka 30, kikundi cha (OSCE) Minsk, kwa bahati mbaya, kiko mbali na kutenda kwa njia ambayo imejikita katika kutafuta suluhisho la mzozo," Erdogan alisema .. Alisema, "Uwekaji amani katika eneo hilo utakuwa kupitia kuondoka kwa majeshi ya Armenia kutoka katika ardhi zinazokaliwa za Azerbaijan tangu 1992. Uturuki itaendelea kusimama na Azerbaijan ya kirafiki na ya kindugu ... ”(Shirika la Habari la Uturuki, 28/9/2020), lakini alidhani kuwa watu wamesahau! Kwa hivyo, alisahau kwamba alikuwa amepuuza hayo yote na akayafumbia macho wakati alipotia saini makubaliano hayo, makubaliano ya amani na Armenia mnamo 2009 kuitumikia Amerika bila kudai kuondolewa kwa majeshi ya Armenia kutoka katika ardhi za Azerbaijan, na hilo halikutajwa, hata kwa neno moja!

8- Na pindi Armenia ilipofuta makubaliano haya, miaka tisa baada ya kutiwa saini, na Amerika kushindwa kuingia Armenia, Erdogan kwa mara nyingine alidai kuondolewa kwa vikosi vya Armenia kutoka katika ardhi hizi zilizokaliwa. Alimkashifu rafiki yake mpendwa, Putin, kama alivyomsifia, na pia alimkashifu Macron na kusema ("Nilizungumza juu ya jambo hili na Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, lakini bila matokeo." Shirika la Habari la Uturuki 1/10 / 2020), na hakumkashifu rafiki yake na mshirika wake, Trump, kama pia alivyomsifia. Anawezaje kumkashifu wakati yeye ndiye injini nyuma ya pazia, bali hata mbele yake?! Hata kama Amerika ilitumia njia za kidiplomasia, imefichuka kwa kila mtu mwenye macho na busara. Na hilo linajumuisha tangazo la Rais Trump wa Amerika katika mkutano na waandishi wa habari jioni ya tarehe 27/9/2020 kwamba ("Amerika itatafuta kukomesha vurugu zilizotokea kati ya Armenia na Azerbaijan." Lakini akasema: "Amerika ina mahusiano mengi mazuri katika eneo hilo. Tutaona ikiwa tunaweza kuzizuia. ”Al-Jazeera 27/9/2020), yaani, atazikomesha wakati atakapoona ni muhimu kuzikomesha, na hakusema kwamba atatia shinikizo na kuweka uzito wote wa Amerika kuweka shinikizo kwa pande zote mbili kupata suluhisho. Badala yake, aliepuka hilo kwa kusema "ikiwa tunaweza kuzizuia," na ni ilhali ni dola ambayo ikiwa inataka kutekeleza kitu, inaweka uzito na shinikizo lake lote juu yake! Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Amerika ilisema kwamba "Amerika inalaani vikali kuongezeka kwa vurugu. Naibu Waziri wa Mambo ya nje, Stephen Pigeon, alimsihi Waziri wa Mambo ya nje wa Azerbaijan na mwenzake wa Armenia kusitisha uhasama kutoka pande zote mbili, na kushirikiana na wenyeviti wenza wa Kikundi cha Minsk kwa lengo la kurudi kwenye mazungumzo muhimu haraka iwezekanavyo na ilithibitisha kujitolea kwa Washington kusaidia pande zote mbili kufanikisha utatuzi wa amani na endelevu wa mzozo huo ... "(Qatari, Al-Jazeera na Al-Alam ya Irani, 27/9/2020). Ililinganisha katika ya upande wa Azerbaijan na Armenia katika kudai kusitishwa kwa uhasama, kwa sababu msimamo wa Amerika unazilenga nchi hizo mbili kuongeza ushawishi ndani yake na kudhoofisha au kuondoa ushawishi wa Urusi kutoka kwao. Haya yote yanaonyesha kuwa Amerika kisiri imeridhika kabisa na hatua za Uturuki na kwamba amehamia upande wa Azerbaijan kwa maagizo ya Amerika. Vyenginevyo, kwanini msemaji wa rais wa Uturuki, Ibrahim Kalin, mnamo tarehe 29/9/2020 aliwasiliana na Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Amerika, Robert O'Brien, kama ilivyoripotiwa na Shirika la Anadolu juu ya mzozo kati ya Azerbaijan na Armenia ikiwa Amerika haikuwa nyuma ya hatua hizi?

9- Kwa kuongezea, Erdogan na uthibitisho wa maafisa wake kwamba walijadili utekelezaji wa maazimio yasiyo ya haki ya Baraza la Usalama na maamuzi ya Kikundi cha Minsk kilichoibuka kutoka Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya mnamo 1992 na viongozi wake ni Amerika, Urusi na Ufaransa, ingawa maamuzi haya ni kwa neema ya Armenia na kupata usitishaji mapigano kwa niaba yake. Yote haya yanathibitisha kuwa kuna hatua ya kukusudia kukoleza hali hiyo, ili kufungua njia ya hatua za kisiasa na kidiplomasia na kutia shinikizo ambalo Amerika inalitaka.

Vita aghlabu hutumiwa kama njia ya kusukuma hatua za kisiasa na kidiplomasia, ambazo zinafungamanishwa na maagizo ya Amerika. Wito umeanza kutoka kwa pande zote kujadili na kupata suluhisho la kisiasa kwa suala hilo na kutekeleza maazimio ya Baraza la Usalama.

Maafisa wa Uturuki wamewahi kutoa matamshi kuunga mkono Azerbaijan kwa msingi wa kutatua suala hilo kulingana na maazimio ya Baraza la Usalama. Wakati wa ziara yake kwa ubalozi wa Azerbaijan huko Ankara, Waziri wa Mambo ya nje, Cavusoglu, alisema ("Maamuzi ya Umoja wa Mataifa, Baraza la Ulaya na Shirika la Ulaya la Usalama na Ushirikiano kuhusiana na hadhi ya ardhi ya Azerbaijan ni dhahiri, na ikiwa Armenia haitajiondoa, kadhia hii halitatatuliwa." Al-Jazeera, 29/9/2020). Akijua fika kwamba maamuzi haya kamwe hayakugusia milima ya Karabakh, badala yake yaligusia ardhi nyenginezo, ambapo inaonyesha ushirikiano dhidi ya suala la Azerbaijan.

10- Urusi inasimama nyuma ya Armenia, nchi iliyo na eneo dogo, idadi ya watu, nguvu na uwezo ikilinganishwa na Azerbaijan. Urusi ndio inayoifadhili na kuisaidia Armenia kwa silaha na vifaa na kila kilicho muhimu kwa uhai wake. Armenia ni mwanachama wa shirika la usalama la pamoja linaloongozwa na Urusi na ina uwepo mkubwa wa kijeshi huko, kwa hivyo ni vigumu kuiacha; vyenginevyo, mgongo wake kutoka upande huu utafichuliwa na kutoa mwanya kwa Caucasus Kaskazini, ambayo ni sehemu ya Shirikisho la Urusi. Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi, Sergey Lavrov, wakati wa mazungumzo ya simu na mwenzake wa Armenia, Zohrab Mnatsakyanyan, alielezea "wasiwasi wake juu ya uhasama huko Karabakh, akisisitiza haja ya kusitisha mapigano" (Sputnik, 27/9/2020), ambayo inaonyesha msaada wa Urusi kwa Armenia dhidi ya Azerbaijan. Huku Uturuki ikilaani Armenia, ni lazima imlaani msaidizi mkuu, Urusi, ambayo inafichua ushawishi wake huko na kuilinda Armenia. Armenia inathubutu kufanya uchokozi tu kwa msaada wa Urusi. Anayemuunga mkono adui yeye pia ni adui. Lakini, Erdogan wa Uturuki alianzisha uhusiano bora kabisa na adui Urusi na ambaye ni mshirika wake nchini Syria dhidi ya watu wake Waislamu wanaoasi dhidi ya serikali ya kihalifu inayoongozwa na Bashar Assad.

Wakati huo huo, ni chombo cha Amerika cha kuihadaa Urusi na kuitumia kufikia maslahi ya Amerika. Lakini si rahisi kwa Urusi kufanya maafikiano katika eneo lake muhimu, kama ilivyotokea kwa Ukraine na Georgia. Kwa hivyo, mzozo huu hautatatuliwa katika vita hivi, na hatua za kisiasa na kidiplomasia zitauteka, kwani zinafaa zaidi katika kuihadaa Urusi.

11- Ama kuhusu uwepo wa Ufaransa huko, ni tofauti. Haina ushawishi wowote huko, na inajaribu kujionyesha kama nchi kubwa. Inataka kudumisha ushirika wake katika Kikundi cha Minsk ambacho kiliundwa mnamo 1992 kulingana na uamuzi wa Baraza la Usalama na Ushirikiano la Ulaya kusuluhisha suala la mzozo wa Azeri na Armenia na kuhakikisha kusitishwa kwa mapigano kwa njia ya kudumu.

Inasimama katika njia ya Uturuki, ambayo inazuia ushawishi wa Ulaya na Ufaransa, kwa sababu Uturuki imo ndani ya duara la Amerika. Macron alisema katika mkutano na waandishi wa habari huko Latvia mnamo 30/9/2020: "Nimepata habari kuhusu matangazo ya Uturuki "yanayounga mkono Azerbaijan", ambayo nadhani ni ya kizembe na hatari. Ufaransa bado ina wasiwasi sana juu ya jumbe za kivita zilizotumwa na Uturuki katika masaa yaliyopita, ambazo zinaondoa vizuizi vyovyote mbele ya Azerbaijan kuvamia tena Nagorno-Karabakh, na hatutakubali hili." (Reuters, 30/9/2020). Waziri wa Mambo ya nje wa Uturuki, Cavusoglu, alijibu mnamo tarehe 30/9/2020, akisema, "mshikamano wa Ufaransa na Armenia unajumuisha uungaji mkono uvamizi wa Armenia nchini Azerbaijan." (Anadolu, 30/9/2020).

Ufaransa inajaribu kuonekana kama mpatanishi 'mwaminifu' katika msimamo unaokinzana, wakati ndio nchi ambayo haina weledi wa ujanja wa kisiasa, msimamo wake daima hufichuka, na endapo itajaribu kuuficha, ukinzani hujitokeza. Katika taarifa iliyotolewa baada ya mapigano hayo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya Ufaransa Von Der Muhll alisema:

"Ufaransa ina wasiwasi sana juu ya mapigano makubwa huko Karabakh na ripoti za majeruhi, haswa miongoni mwa raia, na inataka kusitishwa mara moja kwa uhasama na kuanza mazungumzo." Na akasema, "Ufaransa, kama mwenyekiti mwenza wa Minsk, inathibitisha na washirika wake wa Urusi na Amerika kujitolea kwake kufikia suluhisho la mazungumzo ya mzozo ndani ya mfumo wa sheria za kimataifa" (Sputnik, 27/9/2020). Wakati huo huo, inaongozwa na chuki dhahiri dhidi ya Uislamu na Waislamu kila wakati, iwe ni ndani, kama inavyodai kuwa mtekelezaji wa uhuru, na huku inazuia uhuru wa Waislamu katika msimamo wazi wa kukinzana, au iwe ni nje, kama inavyoyatabanni maswala ya Waarmenia na Wakristo wengine kuwatumia ili kuasisi ushawishi wake, kama ilivyo wadanganya wakati wa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu na kuwachochea dhidi ya Dola ya Uthmani, ambayo ilisimamia mambo yao kwa karne nyingi. Ufaransa iliwaahidi nchi ya makazi huko Anatolia, kwa hivyo waliisaliti Dola ya Uthmani na kuwaua Waislamu wengi kwa uchochezi wa Ufaransa. Na ingelikuwa ni kwa maslahi yao lau kama wangebaki kama watu wa Dhimma (Ahl al-Dhimma), salama chini ya dola ya Kiislamu, inayowafanyia uadilifu na haiwanyanyashi kama Ufaransa na nchi nyingine za kikoloni.

12- Kuhusu maazimio ya Baraza la Usalama ambayo yanataka nchi zitekeleze, pamoja na Uturuki yenyewe, hayakulizungumzia jimbo la Karabakh, ambalo linadhibitiwa na Waarmenia ambao walilitangaza kuwa jamhuri kwao. Azimio la kwanza lilitolewa mnamo Aprili 30, 1993 chini ya nambari 822 likidai kumaliza mara moja mapigano na uhasama, na kudai kusitishwa kwa mapigano ya kudumu. liliwataka wanajeshi vamizi wa Armenia kujiondoa kutoka katika jimbo la Zhangilan, mji wa Horadiz Kurdlar na maeneo mengine ya Azerbaijan, lakini halikushughulikia eneo linalokaliwa la Karabakh. Kuna maamuzi mengine yaliyotolewa mwaka huo huo yakithibitisha uamuzi huu, kwa hivyo Azimio Nambari 853 lilitolewa mnamo Julai 29, 1993. Uamuzi wa awali ulithibitisha na kulaani kuchukuliwa kwa Mkoa wa Aghdam na maeneo mingine ya Azerbaijan, ukiwataka Waarmenia kujiondoa kikamilifu kutoka kwa maeneo haya na kuitaka serikali ya Armenia iweke shinikizo juu ya jimbo la Karabakh kutii Azimio la 822. Mwaka huo huo, Oktoba 14, Azimio Nambari 874 lilitolewa, likirudia kuunga mkono mchakato wa amani kati ya pande hizo mbili na kutaka kukubalika kwa ratiba iliyopitiwa upya kwa hatua za haraka. Azerbaijan ililikataa kwa sababu liliunganisha kuondolewa kwa vikosi vya Armenia huko Karabakh kutoka katika ardhi zilizochukuliwa za Azerbaijan na kuondoa kizuizi kilichowekwa kwa Armenia. Kwa hivyo, serikali ya Azerbaijan ililalamika juu ya matibabu yake kama upande ulioshindwa. Ratiba iliyorekebishwa ilijumuisha mapendekezo yanayohusiana na uondoaji wa wanajeshi kutoka wilaya mpya zilizochukuliwa na kuondoa vizuizi vyote kwa mawasiliano na uchukuzi na kwamba maswala mengine yote ambayo hayakushughulikiwa kulingana na baraza lazima yatatuliwe kwa mazungumzo ya amani. Na mnamo Novemba 12 ya mwaka huo huo, Azimio Nambari 884 la 1993 lilitolewa, likithibitisha maamuzi ya hapo awali na kulaani ukiukaji wa usitishaji vita kati ya pande hizo mbili, haswa huko Zangilan na Horadiz. Iiliwataka wanajeshi wa Armenia wajiondoe kutoka Zangilan na Horadiz, na vikosi vya uvamizi kujiondoa katika ardhi walizochukua kutoka Azerbaijan. Sio maazimio yote ya Baraza la Usalama yaliyotaja kujiondoa kwa Karabakh. Uamuzi huo uliundwa kwa njia ya kufikiria, ukizingatia ardhi za Kiazerbaijani zilizo nje ya jimbo la Karabakh, na kulizingatia kisiri kwa jimbo hili sio kama ardhi ya Azerbaijan. Hii inamaanisha kuwa ikiwa mazungumzo na kisha makubaliano yatawezekana, jimbo hili, jimbo la Karabakh haswa, lingesalia chini ya udhibiti wa Waarmenia kwa badali ya kujiondoa kwao katika ardhi za Azerbaijan. Uturuki inataka utekelezwaji wa maamuzi haya, ambayo hayataki kuondolewa kwa Waarmenia kutoka eneo la Karabakh, na pia kutaka utekelezwaji wa maazimio ya Baraza la Usalama nchini Syria ambayo hayaathiri serikali hiyo bali yanathibitisha kubakia hai kwake na uhifadhi wa kitambulisho chake cha kisekula. Pia inataka utekelezwaji wa suluhisho la dola mbili nchini Palestina, ambalo linaruhusu kukaliwa kwa asilimia 80 ya ardhi za Palestina na Mayahudi. Kwa hivyo, kadhia ya Karabakh ilikwama, na usitishaji wa vita ulikuwa ushindi kwa Waarmenia. Kikundi cha Minsk hakijatangaza suluhisho ambalo lingekuwa nini na nini kinajadiliwa isipokuwa maazimio hayo ya Baraza la Usalama, lakini inaeleweka kutoka kwa muktadha na mazingira na mabishano ambayo wanataka kuchukua kutambuliwa kutoka Azerbaijan kwa uvamizi wa Armenia wa mikoa mitano ya jimbo la Karabakh, ambayo Waislamu walitolewa humo kabisa na nafasi yao kuchukuliwa na makafiri Wakristo wa Armenia, hadi Armenia ijiondoe kutoka mikoa mingine mitano na maeneo yanayokaliwa ya Aghdam na mikoa ya Fuzuli, na kesi hiyo iwe imesuluhishwa. Ni kama ilivyotokea nchini Palestina ambapo Mayahudi na wale walio nyuma yao, Amerika, walichukua kutambuliwa na PLO na serikali zilizopo katika nchi za Kiarabu na Kiislamu za unyakuzi wa karibu asilimia 80 ya Palestina na Mayahudi, na karibu asilimia 20 ya ardhi iliyokaliwa kimabavu na Mayahudi tangu 1967 zilikuwa zikijadiliwa, lakini ambazo walipewa na watawala wasaliti, walipokubali usitishaji wa mapigano na kukubali Maazimio 242 na 243 yaliyotolewa na Baraza la Usalama, ambayo yanaeleza tu kujiondoa kwa umbile la Kiyahudi kutoka kwa ardhi iliyokaliwa, lakini kisha ilikabidhiwa ardhi hiyo mnamo Juni 5 ya mwaka huo.

 

13- Hamu hii ya Uturuki haiko vizuri, kwa hivyo wakati wowote Erdogan wa Uturuki anapoliingilia suala, itakuwa kwa gharama ya watu wake na kwa maslahi ya Amerika, kama vile ilivyotokea nchini Syria; Uturuki ilitia shinikizo kwa vikundi vya kisilaha kukubali kupunguza kasi vita na makubaliano ya kusitisha mapigano, ambayo hayakuzingatiwa na serikali ya Syria na wale waliounga mkono moja kwa moja kutoka kwa serikali ya Iran na wafuasi wake na Urusi, hadi wakati vikundi hivi vilipofukuzwa kutoka kwao maeneo hayo na kukabidhiwa kwa serikali. Vivyo hivyo, kile kilichotokea nchini Libya wakati Uturuki ilitoa msaada kwa serikali ya Sarraj, na wakati vikosi vya Sarraj viliposonga kuelekea Sirte na Jufra, Uturuki ilisitisha uungwaji mkono wake na kumtaka Sarraj atekeleze usitishaji vita wa kudumu na kujadiliana na upande wa pili, chama cha Haftar, ambacho Uturuki inakizingatia kuwa haramu! Haijaamuliwa kwamba msaada wa Uturuki ni kuishinikiza Azerbaijan kulainisha msimamo wake, na hivi ndivyo inavyoonyeshwa na matamshi ya maafisa wa Uturuki, kwani kukwama kwa mazungumzo yaliyoongozwa na Kikundi cha Minsk, haswa Amerika, hayajavunjika. Hii ni hadi Azerbaijan itoe makubaliano juu ya suala la Karabakh, wakati inasisitiza ahadi yake ya kuirudisha Karabakh kwa nguvu kutoka kwa wavamizi. Amerika, Urusi na Ufaransa zinaichukulia Karabakh kuwa ni eneo la Kiarmenia kutokana na sauti ya mazungumzo yao na vyombo vyao vya habari ambavyo daima vinaunga mkono Waarmenia na maazimio ya Baraza la Usalama yaliyotolewa na nchi hizi tatu na kupitishwa na nchi zingine kwenye Baraza. Jamhuri iundwe katika eneo hilo, kana kwamba ni huru kutoka Armenia, ikizidi kutatiza majadaliano, na eneo hili halitatoa umbile lake huru! Na ili Armenia isiwajibike moja kwa moja na kukwepa shinikizo ikiwa litaletwa dhidi yake. Msimamo wa Erdogan wa Uturuki hauaminiki katika suala hili na kwengineko, kwani hajatoa msaada tangu vita vilipotokea kati ya vyama viwili miaka thelathini iliyopita, na Azerbaijan ilibaki imesimama peke yake, na Uturuki haikuiunga mkono, na ndio sababu inahofia kwamba msaada wa mwisho ni sawa na kuweka udhibiti juu ya uamuzi wa Azerbaijan na kisha kufanya makubaliano!

14- Azerbaijan ni nchi ya Kiisilamu na watu wake wengi ni Waislamu, lakini serikali yake ni ya kisekula, na ni mwendelezo wa utawala wa zamani wa kikomunisti katika kuibakisha dini imetenganishwa na dola na jamii. Nchi hii ilifunguliwa pamoja na Armenia wakati wa utawala wa Khalifa wa tatu mwongofu Uthman bin Affan, Mwenyezi Mungu amuwie radhi. Hatuwezi kuitegemea Uturuki au Iran kuziokoa na kuzikomboa nchi za Kiislamu kutoka kwa mshiko wa Amerika au Urusi, lakini badala yake wanashirikiana nao. Hakuna wokovu kwa Waislamu isipokuwa kwa kurudi kwa Khilafah Rashida wa Pili kwa njia ya Utume ambayo ni bishara njema ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):

«إِنَّكُمْ فِي النُّبُوَّةِ مَا شَاءَ اللَّهُ أَنْ تَكُونَ، ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا، ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةٌ عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ، فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللَّهُ أَنْ تَكُونَ، ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا، ثُمَّ تَكُونُ مُلْكاً عَاضّاً، فَيَكُونُ مَا شَاءَ اللَّهُ أَنْ يَكُونَ، ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا، ثُمَّ تَكُونُ جَبْرِيَّةً، فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللَّهُ أَنْ تَكُونَ، ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا، ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةٌ عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ»

“Utume utakuwepo kwenu kwa muda atakao Mwenyezi Mungu kuwepo, kisha atauondoa anapotaka kuuondoa, kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume, na itakuwepo kwa muda atakao Mwenyezi Mungu kuwepo, kisha ataiondoa anapotaka kuuondoa, kisha utakuwepo utawala wa kifalme, na utakuwepo kwa muda atakao Mwenyezi Mungu kuwepo, kisha atauondoa anapotaka kuuondoa, kisha utakuwepo utawala wa kimabavu, utakuwepo kwa muda atakao Mwenyezi Mungu kuwepo, kisha atauondoa anapotaka kuuondoa,kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume". Kisha akanyamaza. Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ni mkweli.

18 Safar 1442 H

5/10/2020 M

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu