- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Mapya Yanayojiri Nchini Libya
(Imetafsiriwa)
Swali:
Baada ya kusimama kwa muda kwa ghasia baina ya Haftar, kibaraka wa Marekani, na majeshi yanayo husishwa na al-Sarraj, kibaraka wa Ulaya, majeshi ya Haftar yameregelea mashambulizi yao ya mji mkuu, Tripoli. Je, Haftar, na nyuma yake Marekani, wanaona kuwa udhibiti wa Tripoli sasa unawezekana? Na ni kipi kilicho tokea kupelekea ghasia hizo kuzuka kwa nguvu kiasi hicho? Kisha ni upi ukweli kuhusu usaidizi wa Uturuki kwa serikali ya Fayez al-Sarraj jijini Tripoli? Je, uingiliaji kati wa Urusi nchini Libya ni wa kihakika, huwa hivi ni vitisho tu? Ni yapi yanayo tarajiwa kutokana na Kongamano la Berlin lililoitishwa na Ujerumani juu ya mgogoro wa Libya?
Jibu:
Ili kufafanua jibu la maswali hayo ya juu, tutatathmini yafuatayo:
Kwanza: Baada ya Marekani kufaulu kumpandikiza kibaraka wake Haftar kama nukta imara katika uwanja wa mzozo wa kijeshi nchini Libya, Libya sasa imegawanyika baina ya shawishi mbili, ushawishi wa kibaraka wa Marekani katika maeneo anayoyadhibiti, na ushawishi wa vibaraka wa Uingereza na Ulaya katika maeneo ya Libya yaliyosalia. Na huku Marekani ikiongeza kasi ya usaidizi wa kijeshi inaoutoa kwa kibaraka wake Haftar, hususan kupitia Misri, ushawishi wake umechukua umbo la kupamba moto nchini Libya, na hili limejitokeza katika shambulizi la Haftar kusini mwa Libya. Ushawishi wa Ulaya ukadidimia, hususan kwa shambulizi lililo anzishwa na Haftar kwa Tripoli mapema mnamo Aprili 2019. Haftar, na nyuma yake Marekani, alitaka kuongeza shinikizo juu ya serikali ya al-Sarraj, kibaraka wa Ulaya jijini Tripoli, na kuichukua hii kama njia ya kujishindia hisa katika windo la simba katika majadiliano ya kisiasa. Hivyo, shambulizi la Haftar juu ya Tripoli mwanzoni mwa Aprili 2019, baada ya udhibiti wake wa nyuma wa kusini akipatiliza fursa ya kujishughulisha kwa Algeria, liliwakilisha uzito wa nguvu ya Haftar, na Marekani ikajaribu kujitoa ndani ya kikaango cha serikali inayotambulika kihalali jijini Tripoli kupitia kuwasiliana hadharani na Haftar kwa njia mithili ya kuwasiliana na afisa rasmi wa serikali "Raisi wa Marekani alimpigia simu Haftar…" (Sky News Arabia, 19/04/2019).
Pili: Ulaya haikuweza kupata cha kukabiliana na hili isipokuwa kuiendesha kadhia ya Libya kisiasa, na hivyo mradi na ualishi wa chansela wa Ujerumani Merkel kwa kongamano la kimataifa jijini Berlin ili kutatua mgogoro wa Libya. Na ingawa mradi huu haukuweka tarehe maalumu. "Hakuna tarehe maalumu ya kongamano linalotarajiwa kufanywa katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin …" (Deutsche Welle 12/12/2019), kuna habari za vyombo vya habari ambazo hazijathibitisha kuwa mkutano wake huenda ukawa mwishoni mwa mwezi huu. Katika hali yoyote ile, ni utekelezaji wa lile Ulaya inalolitaka na kulipanga tangu mkutano wa G-7, "Kundi la G-7 liliitisha kongamano la kimataifa juu ya mzozo wa Libya. Kundi hilo lilitamatisha mwishoni mwa kongamano lake katika mji wa Ufaransa wa Biarritz mnamo Jumatatu kuwa pande zote husika na dola za kieneo zinapaswa kushiriki katika kongamano hili) (Al-Quds Al-Arabi 26/8/2019). Nchi za Ulaya zinaona kutokana na kongamano la Berlin matumaini ya kuhifadhi vibaraka nchini Libya na hivyo kudumisha ushawishi wao, "al-Sarraj leo amempokea, jijini Tripoli, Waziri wa Kigeni wa Italia Luigi Di Maio, ambaye alifikisha usaidizi wa Italia kwa juhudi zake za kupata usalama na utulivu nchini humo. Di Maio alikariri kuwa hakuna suluhisho la kijeshi kwa mgogoro wa Libya, na kwamba nchi yake inaunga mkono juhudi za Salame za kufufua mchakato wa kisiasa, akionyesha matumaini yake kuwa kongamano la Berlin kutapatikana makubaliano baina ya nchi zote zilizo na hamu na mambo ya Libya" (Arabic Independent 17/12/2019).
Tatu: inaonekana kuwa Marekani inajaribu kwa bidii kuziba njia ya Ulaya katika kuandaa Kongamano la Berlin, hususan kwa hali ambazo balozi wa kimataifa wa Marekani nchini Libya anaziweka kabla ya Kongamano la Berlin. "Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Ghassan Salame, alifichua kuwa aliweka masharti matatu wakati wa matayarisho ya Kongamano la Berlin". Akisisitiza kuwa "ukingo wa harakati yake ya kutatua mgogoro huo umekuwa mgumu sana kutokana na mfarakano katika Baraza la Usalama …" (Bawabat Al Wasat, 11/13/2019). Ulegevu huu kutoka kwa mjumbe huyo wa kimataifa unafichua ulegevu wa Marekani kwa Kongamano la Berlin na ni kana kwamba ndio sababu ya kuwepo ugumu wa kuamua tarehe ya kufanyika kwake! Lakini, Marekani haikutosheka na hilo, badala yake ikaziingiza Urusi na Uturuki ndani ya uwanja wa Libya, hivyo basi ikazigeuza karata za kieneo na kimataifa kuhusiana na Libya zilizo zikanganya juhudi za Ulaya na hivyo kulishawishi kongamano hilo kabla halijafanywa kupitia kuiingiza Urusi na Uturuki ndani ya uwanja wa Libya, ili Ulaya isiwe nukta muhimu katika suluhisho pamoja na Marekani, bali izozane na au iongozwe na Urusi na Uturuki na hivyo kuidhoofisha dori ya Ulaya. Hivyo basi, inatarajiwa kuwa matokeo ya kongamano hilo hayatakuwa yale ambayo Ulaya ingeyatarajia endapo kongamano hilo lingefanyika! Ulaya inajaribu kuushawishi msimamo wa Marekani ili kuliunga mkono kongamano hilo na uhudhuriaji wake kwa kila njia na mbinu, hivyo maafisa wa Ulaya wanajaribu kuifedhehesha Marekani kupitia kutangaza kwa niaba ya Marekani kuwa ina hamu na kongamano hilo! "Maas – Waziri wa Kigeni wa Ujerumani – alieleza wakati wa mkutano mmoja kwa waandishi wa habari pamoja na mwenzake wa Italia, Luigi de Maio, kuwa Marekani ina hamu sana na Kongamano la Berlin, na kwamba itashinikiza ushawishi wake ili kulifaulisha kongamano hilo. (Ean Libya, 10/11/2019) yaani Marekani sio inayotangaza! Ama Marekani, jicho lake liko uwanjani nchini Libya. Baada ya mkutano wa matayarisho ya kongamano hilo jijini Berlin, mnamo 17/9/2019, balozi wa Marekani nchini Libya, Richard Norland, alisafiri hadi Algeria, japokuwa hakualikwa kuhudhuria kongamano la Berlin na kukutana na Waziri wa Kigeni wa Algeria Bougadom (Al-Quds Al-Arabi, 11/2/2019) jambo linalo ashiria kuwa jicho la Marekani haliondoki Algeria na inahofia uingiliaji wake dhidi ya Haftar nchini Libya .
Nne: Ama kuhusu ni vipi Marekani ilivyo geuza karata kupitia kuziingiza Urusi na Uturuki ndani ya uwanja wa Libya ili kudhoofisha msimamo wa Ulaya na kisha ule wa al-Sarraj, ni kama ifuatavyo:
A- Marekani imeipa Urusi idhini yake ya kuingilia kati na kumsaidia kibaraka wake Haftar, na kampuni ya usalama ya Urusi, Wagner Group, ilijitokeza nchini Libya, na kampuni hii ni mwenza wa kampuni ya uhalifu ya Marekani ya Blackwater ambayo imezuka nchini Iraq. Inaonekana kana kwamba Marekani imeipa ari Urusi kuiingiza Wagner nchini Libya ili kumsaidia Haftar, kampuni iliyo jihami kwa silaha za kisasa za kijeshi za Kirusi, kama vile mifumo ya upiganaji kwa halaiki, ikiifanya kuwa nukta muhimu katika kulipa uzani jeshi la Haftar dhidi ya wapinzani wake nchini Libya, na ina uhusiano wa karibu sana na Rais Putin, na inafanya kazi kupata pesa kupitia mikataba ya kijeshi. Rais wa Urusi Putin amekiri kuitikia mwito wa matakwa ya Marekani na kusema: "Urusi ina mawasiliano na Haftar na pamoja na serikali ya al-Sarraj …" (Russia Today, 12/19/2019) Wakati huo huo, Marekani pia inamsaidia Haftar: "Ikulu ya White House ilisema wakati ambapo Trump aliifagilia dori muhimu ya Mpiganaji Haftar katika kupambana na ugaidi na kuhakikisha usalama wa rasilimali za mafuta za Libya …" (Deutsche Welle, 24/11/2019). Marekani inataka kuionyesha Libya kama uwanja wa vita kati yake na Urusi, na shirika la habari la Ujerumani, Deutsche Welle, lilichapisha taarifa mnamo 24/11/2019 iliyo tolewa na taasisi za serikali ya Marekani "zinazounga mkono ubwana wa Libya na heshima kwa mipaka yake katika kukabiliana na majaribio ya Urusi ya kupatiliza fursa ya mzozo dhidi ya matakwa ya watu wa Libya."
B- Ama Uturuki, dori yake katika mgogoro wa Libya imekuwa dhahiri kabisa "kupitia kutia saini Rais wa Uturuki Erdogan na Waziri Mkuu wa Libya Fayez al-Sarraj mkataba wa maelewano mnamo 27/11/2019 kwa ajili ya usalama na ushirikiano wa kijeshi kati ya Ankara na Tripoli, na kuyatambua maeneo ya uhalali baharini. Erdogan alisema katika maoni yake kwa maripota: "Misri inafanya nini nchini Libya? Serikali ya Abu Dhabi inafanya nini nchini Libya?". Kuhusiana na dori ya Urusi, Erdogan alisema, "Kupitia kampuni inayoitwa Wagner, ni wazi wanafanya kazi kama mamluki wa Haftar nchini Libya. Munajua ni nani anaye walipa". Aliongeza, "Hiyo ndio hali, na haitakuwa sawa kwetu kubakia kimya dhidi ya yote haya. Mpaka sasa tumefanya kila tuwezalo, na tutaendelea kufanya hivyo …" (Al-Jazeera Net, 20/12/2019). Kutokana na haya, bunge la Uturuki liliidhinisha mradi wa Erdogan, "Bunge la Uturuki liliidhinisha mswada kwa kura 325 dhidi ya 184 unaoidhinisha upelekaji vikosi nchini Libya ili kuisaidia serikali ya Tripoli inayo ongozwa na al-Sarraj inayo tambuliwa na Umoja wa Mataifa. Amri hii inairuhusu Ankara kutuma vikosi visivyo vya kivita kama washauri na wakufunzi kwa majeshi ya serikali hiyo inayo tambuliwa katika vita vyake dhidi ya majeshi ya Khalifa Haftar jijini Tripoli" … (BBC Arabic, 2/1/2020).
Tano: Ama malengo ya Marekani ya kuilazimisha dori ya Uturuki nchini Libya, sio kwa ajili ya kumsaidia al-Sarraj kama anavyo eleza Erdogan; bali, ni kutafiti kile kinacho endelea huku uchunguzi na mazingatio ya kina yakionyesha kuwa malengo yake ni ya kindani, kieneo na kimataifa, na aghalabu ni kama yafuatayo:
1- Kindani, kuna makundi mengi ya kijeshi yaliyo chini ya bendera ya serikali ya al-Sarraj yanayo kadiriwa kuwa "Waislamu poa" na Uturuki ina mawasiliano nao kabla ya uingiliaji kati huu, na ni rahisi kwa Uturuki kuyasukuma makundi hayo hadi katika kifo chao kama ilivyo fanya nchini Syria pindi ilipo yasukuma makundi tiifu kwake kuyasalimisha maeneo hayo kwa mhalifu Bashar. Hivyo basi, Uturuki nchini Libya inapigana vita ili kujishindia utiifu na kuidhoofisha serikali ya al-Sarraj mbele ya Haftar. Na al-Sarraj ni lazima anatambua kuwa Erdogan anatembea ndani ya duara la Marekani na kwamba hakuingilia kati kumsaidia yeye bali kumhadaa ili kuipa uzito mizani ya Haftar kupitia kuyadhoofisha makundi hayo kwa kuyaondoa maeneo tete kama alivyo fanya kwa makundi nchini Syria. Lakini, al-Sarraj kwa matayarisho na Ulaya anataka kuifedhehesha Marekani kupitia ukaribu wake na Uturuki na kuifanya Uturuki ya Erdogan ilazimike kuiunga mkono serikali yake, kama serikali inayo tambulika kimataifa inayostahiki kutafuta msaada kutoka kwa nchi yoyote, na kisha Ulaya kuibua kilio cha kimataifa juu ya uingiliaji kati wa Uturuki na nyuma yake Marekani na Misri. al-Sarraj, na nyuma yake Ulaya, anatarajia kuwa fedheha hii na kelele hizi zitaifanya Marekani kuhafifisha shinikizo la Haftar na Misri juu ya al-Sarraj.
2- Kieneo, chini ya visingizio vya usaidizi wa kijeshi wa Kituruki, Misri inaweza kuongeza pakubwa usaidizi wake kwa Haftar katika wakati ambapo ni vigumu kwa Algeria kutoa usaidizi kwa serikali ya al-Sarraj kwa sababu ya dhurufu zilizoko kwa sasa. Misri huenda ikatuma majeshi yake moja kwa moja kupigana nchini Libya, ilhali usaidizi wa Uturuki kwa serikali ya al-Sarraj utakuwa wa kinadharia tu usio wa kihakika, kama vile usaidizi wa Uturuki kwa makundi ya Syria tiifu kwake. Kwani Uturuki tayari iko mbali na Libya, bila ya kutaja kuwa malengo yake yamefungika tu na usanii na gumzo la usaidizi litapeana kichache tu kwa lengo la kuyaingiza majeshi ya Libya ndani ya mtego wa usaidizi wa Uturuki, ambapo watakachoona ni mangati tu kama ilivyokuwa nchini Syria.
3- Kimataifa, uingiliaji kati wa Uturuki unaufanya uwanja wa Libya kuwa uwanja wa taharuki na kivutio baina yake na Urusi, na ndiyo yanayojiri kwa sasa. Erdogan anashambulia uwepo wa majeshi ya Urusi nchini Libya, na Urusi inatangaza kutoridhishwa kwake na uingiliaji kati wa Uturuki, kisha taarifa hizi zinafuatia taarifa nyinginezo kuhusu makubaliano kati ya Uturuki na Urusi juu ya Libya! Ni sawia na njama za Uturuki pamoja na Urusi juu ya matukio nchini Syria.
4- Ama kuhusu yale ambayo Erdogan anajaribu kuwahadaa watu kwayo, kupitia makubaliano yake pamoja na al-Sarraj ili kuyapatiliza katika utafutaji wa gesi na mafuta, "Waziri wa Kawi wa Uturuki Fatih Donmez alisema kuwa pindi mkataba wa baharini kati ya Ankara na serikali ya Libya iliyo na makao yake jijini Tripoli utakapo idhinishwa na kusajiliwa na Umoja wa Mataifa, Uturuki itaanza kufanya kazi ya kutoa leseni ya utafiti na uzalishaji mafuta na gesi eneo hilo", na akasema "Nadhani tutaanza mchakato huu katika miezi ya mwanzo ya 2020" (Reuters 18/12/2019). Inaonekana kuwa Erdogan ameiona hii kuwa fursa ya kuhadaa kana kwamba ameingia kwa ajili ya kutafuta gesi na mafuta na hivyo kutia saini makubaliano haya, kama hatua zake za kutafuta gesi katika eneo la Mediterranean, lililo na umbali wa kilomita 100 kutoka jimbo la Antalya tangu Oktoba 2018 haikuwa makini vile, mithili ya kuponda maji ndani ya kinu. Na Waziri huyo wa Kawi alikiri kuwa Uturuki bado haijaanza kuchimba mafuta na gesi, licha ya kutuma meli kwa ajili ya lengo hili, na sasa anataka kuwahadaa watu kuwa atafanya utafiti wa mafuta na gesi na kwamba ameingia nchini Libya ili kutafuta maslahi ya Uturuki huku akicheza dori hii hadaifu nchini Libya kwa ajili ya Marekani.
Sita: Ama kuhusu kutatua vita vya Tripoli, kuna mambo ambayo yameibuka katika miezi ya hivi karibuni yanayoupiku upande wa Haftar:
1- Mbele ya mandhari yaliyo kanganyika ya Ulaya yaliyo buniwa na Marekani kupitia kuiingiza Urusi na Uturuki ndani ya uwanja wa Libya na kupamba moto kwa uwezo wa dori ya Misri kama tulivyo onyesha juu, Haftar alishajiishwa kukoleza amali za kijeshi jijini Tripoli "Kamanda wa lile linalojulikana kama Jeshi la Kitaifa la Libya, Khalifa Haftar, ametangaza mnamo Alhamisi jioni, Disemba 12, kuanza kwa vita muhimu mno na kusonga mbele kuelekea Tripoli, na kuamuru vitengo vinavyo songa mbele kujifunga na kanuni za makabiliano". Huku akiwa amevalia sare za kijeshi Haftar alitangaza, katika hotuba iliyo peperushwa katika runinga, "Saa Sifuri" kwa vitengo vyote vya kijeshi jijini Tripoli, akisema: "Leo, tunatangaza vita muhimu mno na kusonga mbele kuelekea kitovu cha mji mkuu …" (Deutsche Welle German, 12/12/2019), na kupamba moto kwa amali ya kijeshi kunaendelea.
2- Uingiliaji kati wa Urusi, hususan kampuni ya Wagner Group sambamba na Haftar, ambapo Marekani iliipa Urusi idhini yake ya kuingilia kati na kumsaidia kibaraka wake Haftar. Ni kampuni iliyojihami kwa zana za kisasa za kijeshi za Kirusi kama vile mifumo ya upiganaji kwa halaiki, ikiifanya kuwa nukta muhimu katika kulipa uzito jeshi la Haftar dhidi ya wapinzani wake nchini Libya. Rais wa Urusi Putin amekiri kuitikia mwito wa matakwa ya Marekani, akisema, "Urusi ina mawasiliano na Haftar pamoja na serikali ya al-Sarraj …" (Russia Today, 19/12/2019).
3- Uingiliaji kati wa Uturuki katika uwanja wa Libya, kuna makundi mengi ya kijeshi yaliyo chini ya bendera ya serikali ya al-Sarraj yanayo kadiriwa kuwa "Waislamu poa" na Uturuki ina mawasiliano nao kabla ya kuingia kwake huku, na ni rahisi kwa Uturuki kuyasukuma makundi hayo hadi kifo chao kama ilivyo fanya nchini Syria pindi ilipo yasukuma makundi tiifu kwake kuyasalimisha maeneo kwa mhalifu Bashar. Hivyo basi, Uturuki inapigana vita nchini Libya ili kuchukua utiifu na kuidhoofisha serikali ya al-Sarraj mbele ya Haftar. Hii ni upande mmoja, upande mwengine, tangazo la Uturuki kuwa inaingilia kati nchini Libya ili kumsaidia al-Sarraj ni utangulizi kwa Misri kutangaza uingiliaji kati wake nchini Libya badala ya kuiweka iwe siri!
4- Uhadaifu baina ya Uturuki na Urusi, huku Uturuki ikionyesha kuwa uingiliaji kati wake ili kumsaidia al-Sarraj, na Erdogan kuishambulia Urusi kwa sababu inamsaidia Haftar, kutangaza kuwa "Kupitia kampuni kwa jina Wagner, waziwazi wao wanafanya kazi kama mamluki wa Haftar nchini Libya. anaye walipa munamjua ni nani". Akaongeza, "Hiyo ndio hali, na haitakuwa sawa kwetu kubakia kimya dhidi ya yote haya. Mpaka sasa tumefanya kila tuwezalo, na tutaendelea kufanya hivyo …" (Al-Jazeera Net, 20/12/2019). Kisha siku mbili baadaye, anatangaza kukutana na Putin! "Yeye na Raisi Putin wameunda ujumbe miwili ili kujadili maendeleo nchini Libya na kwamba maafisa wa nchi mbili hizi watakutana hivi karibuni …" (Turkish NTV, 18/12/2019). Kama alivyo kutana na Urusi na kushirikiana nayo huku ikiwabwagia mabomu watu wa Syria mchana na usiku huku wakati huo huo akionyesha unafiki kuwa aliingia Syria ili kuyasaidia makundi na watu wa Syria! Ni kana kwamba pande zote mbili zinacheza mchezo wanaodhani kuwa umefichika machoni ilhali uko parwanja! Mtandao wa Al-Jazeera.Net mnamo 20/12/2019 uliripoti kutoka kwa mtandao wa Kiitaliani wa Corriere Della Sera: "Kuwa mandhari ya Libya inashuhudia mchezo kati Uturuki na Urusi, na kwamba kuna makubaliano ambayo yameanza kuchukua umbile katika Bahari Nyeusi kati ya pande hizo mbili kwa kuwa wako tayari kuurudia ujuzi wa amani ya Syria nchini Libya", na kufichuka kwa uhadaifu kati ya Uturuki na Urusi kunaharakisha na kutia motisha kazi ya Haftar.
Mambo haya manne yanausaidia na kuutia motisha msimamo wa Haftar wa kukoleza mapigano jijini Tripoli na yanamshajiisha kufanya hivyo. Bila shaka, mambo haya yanasimamiwa na kupangiliwa na Marekani. Hii ni kwa upande wa Haftar. Ama upande wa al-Sarraj, hakuna shaka kuwa Ulaya inamsaidia, ikiwemo Uingereza, Ufaransa, na Italia. Hii ni ikiongezewa na ukakamavu wa makundi ya upiganaji, hususan wapiganaji wa Misurata, lakini kuendelea kwa uingiliaji kati kama ilivyo ashiriwa juu na ongezeko la shinikizo la kijeshi juu ya Tripoli na kupatikana utiifu kwa Uturuki ndani ya kambi ya al-Sarraj yamaanisha kuwa ushawishi wa Ulaya nchini Libya unayumba. Vilevile ni vigumu kwa mazingira makubwa ya kisiasa ya Uingereza na Ulaya nchini Libya kuuokoa ushawishi huo hususan baada ya Marekani kubadilisha karata kupitia kuziingiza Urusi na Uturuki ndani ya uwanja wa Libya. Ikiwa na maana kuwa ni vigumu kwa ushawishi wa Ulaya nchini Libya kurudi kama ulivyo kuwa kwa mujibu wa matukio na uhalisia ulioko. Lakini, si rahisi kumaliza mgogoro huu kijeshi katika mustakbali wa karibu, na hivyo basi wanatarajiwa kutumia suluhisho la kisiasa katika njia yao kama warasilimali katika kukubali maridhiano endapo itakuwa ni vigumu kwa upande wowote ule kuutatua kijeshi ukizingatia wingi wa mapato ya kisiasa kwa mujibu wa uzito wa kijeshi ambao kwa sasa uko upande wa Haftar, yaani upande wa Marekani.
Saba: Katika kutamatisha, inatia uchungu kwa biladi za Waislamu kuwa uwanja wa vita ambao wakoloni makafiri wanashindana kupitia vifaa kutoka kwetu ili kutumikia maslahi ya ukafiri na watu wake, kutokana na utiifu wa watawala katika biladi za Waislamu kwa makafiri ili kuwabakisha katika viti vyao vibovu! Watawala hawa hawajui kuwa matokeo mazuri ni kwa watu wema, kwa Uislamu na watu wake, na kisha watajuta, lakini wakati huo hautakuwa ni wakati wa majuto,
﴾فَتَرَى الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ مَرَضٌ يُسَارِعُونَ فِيهِمْ يَقُولُونَ نَخْشَى أَنْ تُصِيبَنَا دَائِرَةٌ فَعَسَى اللَّهُ أَنْ يَأْتِيَ بِالْفَتْحِ أَوْ أَمْرٍ مِنْ عِنْدِهِ فَيُصْبِحُوا عَلَى مَا أَسَرُّوا فِي أَنْفُسِهِمْ نَادِمِينَ ﴿
“Utawaona wale wenye maradhi nyoyoni mwao wanakimbilia kwao wakisema: Tunakhofu yasitusibu mabadiliko. Huenda Mwenyezi Mungu akaleta ushindi au jambo jingine litokalo kwake wakawa wenye kujuta kwa waliyo yaficha katika nafsi zao.” [Al-Maidah: 52].
11 Jumada I 1441 H
Jumatatu, 06/01/2020 M