Jumamosi, 12 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/14
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 UCHUMI MUOVU WA KIBEPARI NDIO CHANZO CHA MSOTO ULIMWENGUNI

Ni wazi kuwa uchumi ndio uti wa mgongo wa maisha ya wanadamu na hupelekea udharura wa kuweko utaratibu wa kuendesha ukuzaji na usambazaji wa rasilimali (utajiri) katika jamii. Mfumo wa kiuchumi leo ni ubepari/urasilimali uliotungwa na msomi wa kimagharibi Adam Smith anayetambulika ‘Baba wa mfumo wa Kirasilimali’. Ubepari humaanisha kwamba biashara, viwanda na vitegauchumi vyote vinamilikiwa na watu binafsi waliojaa uchu na tamaa ya kujirundikizia mali pasina na kujali thamani ya utu. Matokeo yake, utajiri hubakia na kumilikiwa na kipote cha mabepari huku jumla ya watu wakisota kila siku.

Urasilimali ndio chanzo halisi cha msoto wa kiuchumi duniani kote, hii inarudia falsafa yake katika kuainisha tatizo msingi la kiuchumi na katika kulisuluhisha kwake; nayo ni kudai kwamba kuna uhaba wa bidhaa na huduma katika kukimu mahitaji ya wanadamu. Kukabiliana na tatizo hili, wakoloni wa kirasilimali hudai ni kupitia uzalishaji wa bidhaa na huduma! Kwa msingi huu, Ubepari ukafanya uzalishaji wa bidhaa na huduma ndio kipaumbele huku ukipuuza usambazaji wake. Natija yake ikawa utajiri wa nchi ndio mizani ya ukuaji wa kiuchumi hata kama jumla ya wananchi wa kawaida wapo kwenye lindi la umasikini.

Mabwenyenye wa kirasilimali wamepagawa na uchu wa kupata faida ya kupindukia na hawatukuzi lolote ila maslahi ya kiuchumi kwao. Sifa hii ndio yenye kuathiri pia utendakazi wa serikali, sera za kiuchumi na hata siasa. Utekelezwaji wa mfumo huu wa utumwa mambo leo katika shingo za watu, umewazalishia maafa mengi ya kiuchumi kama inavyodhihirika kwenye suala la ajira. Kwa haya ndio, wafanyikazi wanaendelea kuhudumikia maslahi ya mabwenyenye huku wakiambulia patupu na hata mishahara huishia kuwa kijungumwiko.

Makucha ya urasilimali huingia ndani ya mfuko wa wanjiku kwa kumlimbikizia zigo la ushuru katika kila bidhaa na huduma msingi. Kwa kuwa kila mwanadamu huhitaji bidhaa na huduma kwenye maisha ya kila siku, utozwaji wa ushuru moja kwa moja huzidisha dhiki ya maisha ya raia. Tunasema kuwa ushuru ni zigo kwa mlalahoi wala si kwa matajiri kwa sababu hautozwi kwa mali za matajiri bali ni kwa bidhaa na huduma. Na hata zile ziitwazo kodi za makampuni bado hazigusi utajiri wa wamiliki wa kampuni bali mara nyingi matajiri huweka hesabu ghushi. Hivyo inabainika kwamba katika mfumo wa kirasilimali utajiri huzunguka kwa watu wachache huku wengi wakibakia kuwa watumwa wasomudu kukimu hata mahitaji msingi. Utumwa huu wa Kirasilimali ni katili zaidi hata kuliko ule wa mabwenyenye wa kiquraishi kwani watumwa wa zama hizo walikuwa wakifadhiliwa malazi na chakula.

Uislamu kwa upande wake nao ni mfumo kamili wa kimaisha unaojumuisha utaratibu wa kiuchumi/nidhamu. Uchumi wa Kiislamu huangazia vipengele vitatu; njia za kumiliki mali, matumizi na ugavi. Tatizo la kiuchumi katika mfumo wa Kiislamu linalopaswa kutatuliwa sio uhaba wa bidhaa na huduma bali ni usambazaji. Kwa maana hii, suluhisho la tatizo la kiuchumi ni usambazaji wa mali wala sio kupitia uzalishaji wa mali. Mfano hai ni kuwa Kenya kiuhalisia ni yenye utajiri mkubwa, lakini kwa sera mbovu za usambazaji, watu hufa njaa maeneo mengi ya nchi huku baadhi ya maeneo vyakula vinatupwa! Kwa uhalisia huu, umasikini wa watu hautokamani na uwezo wa uzalishaji wa mali bali ni usambazaji wake kukidhi mahitaji msingi ya wanadamu. Katika kutilia mkazo Uislamu ukaharamisha urundikizaji wa mali na ukiritimba. Mwenyezi Mungu (Swt) anasema,

وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيم

"Na wale wanaokusanya dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njiya ya Mwenyezi Mungu wape habari za adhabu inayoumiza." [At-Twabah 9:34]

Ama suala la ajira, Uislamu umefafanua kwa kina suala hili, awali ya yote ni kulifungamanisha kwake na ibada. Kazi yoyote ile haiangaliwi kwa msingi wa manufaa ni kwa kuzingatia uhalali na uharamu kwani ndio vipimo katika matendo ya wanadamu. Kiislamu, mishahara au malipo ya juhudi ya mfanyikazi haifungamanishwi na manufaa ya mwajiri bali ni kwa kulingana na manufaa yanayozalishwa na yule mfanyikazi. Kwa maana hii inabainika kuwa ajira katika Uislamu ni njia ya kujikwamua kikweli na msoto wa kiuchumi wala sio utumwa mambo leo kama ilivyo ndani ya urasilimali. Fauka ya haya, mapato ya kuendesha serikali kwa mujibu wa Uislamu sio utozwaji ushuru bali ni kuegemea mali/utajiri ulioko kwa mazingatio ya usambazaji. Kwa mfano pato la zaka ya mali, huchukuliwa asilimia 2.5 kwa mali iliyofikia kiwango maalum kwa muda maalum.

Enyi Waislamu na Wasokuwa Waislamu, kwa hakika msoto wa kiuchumi unaoshuhudiwa ni dalili tosha ya kufeli kwa mfumo wa kiuchumi wa Kibepari. Wakati ni sasa wa kuitikia mwito wa mabadiliko msingi yatakayowapelekea kupata mafanikio ya hapa duniani na kesho akhera. Mabadiliko  haya ni  kuulingania Uislamu kuwa mfumo pekee ulio na nidhamu ya kikweli ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ili uongoze watu katika nyanja zote maishani kupitia kusimamishwa tena kwa Khilafah katika mojawapo ya nchi katika ulimwengu wa Kiislamu.

يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱسْتَجِيبُواْ لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ ۖ

"Enyi Mlioamini Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume wake anapokuiteni katika yale yatakayokupeni uhai mzuri (wa duniani na Akhera)" [Al-Anfaal 8:24]

H. 26 Dhu al-Hijjah 1442
M. : Ijumaa, 06 Agosti 2021

Hizb-ut-Tahrir
Kenya

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu