Alhamisi, 06 Ramadan 1446 | 2025/03/06
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

Afisi ya Habari
Wilayah Sudan

H.  16 Sha'aban 1446 Na: HTS 1446 / 50
M.  Jumamosi, 15 Februari 2025

Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Hotuba ya Msemaji Rasmi wa Hizb ut Tahrir katika Wilaya ya Sudan katika Mkutano na Waandishi wa Habari yenye kichwa:
“Usomaji wa Awali wa Hotuba ya Al-Burhan”
(Imetafsiriwa)

Sifa njema zote anastahiki Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote, na rehma na amani zimshukie mtukufu zaidi wa Mitume, Bwana wetu Muhammad, na jamaa zake, na maswahaba zake, na walio mfuata.

Ndugu Mlio Kongamana,

Assalamu Alaikum wa Rahmatu Allah wa Barakatahu,

Wakati wa hotuba yake katika hitimisho la mashauriano ya kile kinachoitwa nguvu za kisiasa za kitaifa na kijamii, juu ya ramani ya utendakazi ya mazungumzo ya Sudan na kuanzisha amani, Luteni Jenerali Al-Burhan alielezea sifa za utawala katika kipindi kijacho, na alianza hotuba yake iliyoboreshwa kwa kusema: "Shukrani na sifa ni miongoni mwa mahitaji ya kutolewa. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba tumebaki katika hali nzuri zaidi kuliko miaka iliyopita.”

Je, kumshukuru Mwenyezi Mungu ni kitendo kwa mujibu wa Shariah ya Mwenyezi Mungu au ni kitendo kwa mujibu wa sheria ya makafiri wakoloni wa Magharibi, ambacho kimetufikisha kwenye shimo hili? Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:

[اعْمَلُوا آلَ دَاوُودَ شُكْراً وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ]

“Enyi watu wa Daudi! Fanyeni kazi kwa kushukuru. Ni wachache katika waja wangu wanao shukuru.” [Saba’:13].

Hotuba ya Al-Burhan pia ilijumuisha: “Tunajali kumridhisha Yule ambaye lazima aridhishwe; Mola wetu.” Hapana shaka kwamba kumridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu ndilo lengo la kila Muislamu katika maisha yake, na hilo linahitaji Muislamu anayekaa kwenye kiti cha utawala atumie mifumo na sheria za Uislamu, na sio mifumo ya makafiri wa Magharibi, kama vile usekula, demokrasia na mengineyo. Na wale wanaoomba mifumo na masuluhisho, na kuyatafuta kwenye ubongo wa wanadamu kupitia warsha na makongamano, hawapaswi kukaa katika kiti cha serikali, maana yeye hastahili hilo!

Ingawa Al-Burhan aliviona vita hivi kuwa ni nukta ya mabadiliko katika historia ya Sudan, na watu wa Sudan lazima wajifunze kutokana navyo na kusahihisha njia yao, kama alivyosema katika hotuba yake: “Kama hatutajifunza kutokana na vita hivi na kuanza kujenga au kuanzisha dola ambayo ni tofauti na ilivyokuwa hapo awali, hatutakuwa tumenufaika navyo hata kidogo, na tutakuwa tumeangamiza vijana wetu na uwezo wetu, na kuharibu uwezo wa dola ambao haufai kitu.” Kwa hivyo ni mfumo gani uliokuwa hapo awali, ambao lazima tuondokane nao?! Bila shaka ni usekula, demokrasia, mfumo wa jamhuri, ubwana kwa watu, na mifumo ya maisha chanya. Hivi kweli tuko makini na hilo?!

Hotuba ya Al-Burhan ilijumuisha nia yake ya kuunda serikali mpya kusimamia kipindi cha mpito, ambayo inaweza kuitwa serikali ya muda, ambayo itaundwa na uwezo huru wa kitaifa. Al-Burhan pia aliashiria kuwa waziri mkuu atachaguliwa baada ya kuidhinishwa kwa hati ya kikatiba, na kwamba atakuwa na jukumu la kusimamia vyombo vya utendaji vya serikali, bila kuingiliwa, na kwamba marekebisho ya hati ya katiba yanaifanya kuwa tofauti na ilivyokuwa kwa washirika wa zamani ambao wamekuwa maadui leo, na kwamba ikiwa Bunge la Kitaifa linataka kutawala, lazima lishindane katika siku zijazo na nguvu zengine za kisiasa. Ramani utendakazi iliyopitishwa na Al-Burhan, na kuwasilishwa kwake na nguvu za kisiasa, ilijumuisha awamu mbili za baada ya vita; ya kwanza ni ya msingi na itadumu kwa mwaka mmoja kukamilisha kazi za kijeshi na kuregesha utulivu na amani, na nyingine ni ya mpito ya kujiandaa kwa uchaguzi na itadumu kwa takriban miaka minne, huku Al-Burhan akiwa mtawala katika kipindi chote hiki. Ramani hiyo pia ilipendekeza kudumisha baraza huru, huku Burhan akimtaja waziri mkuu wa kiraia aliyepewa jukumu la kuunda serikali yenye uwezo huru ambapo vikosi vya kiraia havishiriki, pamoja na kuunda baraza la kutunga sheria linalojumuisha wanachama 250 ambalo linajumuisha wawakilishi wa nguvu za kisiasa na kijamii, wanawake na vyama vya wafanyikazi. Al-Burhan alisisitiza wakati wa hotuba yake kwamba mapendekezo ya nguvu za kisiasa yatapata umakini na wigo wa utekelezaji.

Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِمَ تَقُولُونَ مَا لَا تَفْعَلُونَ * كَبُرَ مَقْتاً عِندَ اللهِ أَن تَقُولُوا مَا لَا تَفْعَلُونَ]

“Enyi mlio amini! Kwa nini mnasema msiyo yatenda? Yanachukiza vikubwa mno kwa Mwenyezi Mungu kuwa mnasema msiyo yatenda.” [As-Saff: 2-3]. Mwenyezi Mungu (swt) pia asema:

[وَلَوْ أَرَادُوا الْخُرُوجَ لَأَعَدُّوا لَهُ عُدَّةً وَلَكِن كَرِهَ اللهُ انبِعَاثَهُمْ فَثَبَّطَهُمْ وَقِيلَ اقْعُدُوا مَعَ الْقَاعِدِينَ]

“Na ingeli kuwa kweli walitaka kutoka bila ya shaka wangeli jiandalia maandalio, lakini Mwenyezi Mungu kachukia kutoka kwao, na kwa hivyo akawazuia na ikasemwa: Kaeni pamoja na wanao kaa!” [At-Tawba:46].

Ni wazi kutokana na hotuba ya Al-Burhan kwamba anazalisha tena utawala ule ule uliopita na miundo yake; hati ya kikatiba, Baraza la Enzi Kuu, Baraza la Mawaziri (wataalamu), na Baraza la Kutunga Sheria. Yaani, hatukutoka kwenye sanduku la mkoloni kafiri aliyeamini kutenganisha dini na maisha, na kwa kuzingatia hilo akaweka mifumo yake ya maisha; kisiasa, kiuchumi, kijamii na mengineyo. Kwa msingi wa imani hii, mifumo yao ya kidemokrasia ya serikali iliasisiwa, kisha wakaisafirisha hadi Sudan kwa kuingia kwa vikosi vya jeshi la Uingereza lililoongozwa na Kitchener mnamo 1899 M. Tangu zama hizo, mifumo ya utawala katika nchi yetu imekuwa kinyume na Uislamu, kwa shina na matagaa, na zile zinazoitwa serikali za kitaifa zimerithiana madarakani, baadhi zikiwa za kiraia na nyingine za kijeshi, lakini hazikutoka katika mifumo ya mkoloni kafiri kwa lolote, kwa hivyo Mwenyezi Mungu akatutia katika vita hivi ili turudi kwenye utawala wa Uislamu katika maisha yetu yote; kwa upande wa ibada, siasa, utawala na muamala, ili tuishi maisha ya Kiislamu, ambayo Mwenyezi Mungu ameturidhia. Kisha watawala wetu, wa kijeshi na kiraia, wanasisitiza kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na kabla Mwenyezi Mungu hajatuondolea balaa hii, wanazungumza juu ya kutekeleza mifumo ya makafiri, wakoloni wa Magharibi, ambayo imetudhalilisha na kutuonjesha fedheha na udhalilifu!

Ni lazima turudi kwenye njia ya Mwenyezi Mungu na kuitumia ili tuweze kuishi maisha yanayomridhisha Mola wa walimwengu wote.

Kwa kujibu aliyoyasema Al-Burhan katika hotuba yake: “Tuna matatizo mawili; madaraka na mali, hizi ndizo sababu za matatizo yote ya Sudan... Tutaiongozaje nchi hii na mali iliyoko ndani yake tutaigawanya vipi?”

Tunamwambia yeye na nguvu za kisiasa walio mahabusu kwa mfumo tawala wa kirasilimali wa Kimagharibi: Mfumo wa utawala katika Uislamu ni Khilafah Rashida kwa njia ya Utume, kama alivyoeleza Mtume, rehma na amani ziwe juu yake katika Hadith iliyopokewa na Muslim katika Sahih yake: «كَانَتْ بَنُو إِسْرَائِيلَ تَسُوسُهُمْ الْأَنْبِيَاءُ كُلَّمَا هَلَكَ نَبِيٌّ خَلَفَهُ نَبِيٌّ وَإِنَّهُ لَا نَبِيَّ بَعْدِي وَسَتَكُونُ خُلَفَاءُ تَكْثُرُ...» “Bani Israil wanasiasa wao walikuwa ni manabii. Kila nabii alipokufa, nabii mwengine alimrithi. Na hakika yake hakutakuwa na nabii baada yangu, na kutakuwepo na makhalifa wengi...” Ni mfumo wa kipekee, mfumo maalum kwa dola spesheli maalum, tofauti na mifumo yote ya serikali iliyopo duniani, ima katika msingi ambao mifumo hii imeegemezwa, au katika fikra, fahamu, na vipimo ambavyo mambo yanatawaliwa kwayo, au katika maumbo ambayo yanawakilishwa nayo, au katika  katiba na sheria zinazotekelezwa nayo.

Dola ya Kiislamu imeegemezwa kwenye Aqidah (itikadi) ya Kiislamu, na hili linahitaji kwamba katiba yake na sheria zake zote zichukuliwe kutoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah za Mtume Wake (saw). Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:

[فَلاَ وَرَبِّكَ لاَ يُؤْمِنُونَ حَتَّىَ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ]

“La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayo khitalifiana” [An-Nisa:65]. Mwenyezi Mungu (swt) vilevile asema:

[وَأَنِ احْكُم بَيْنَهُم بِمَآ أَنزَلَ اللهُ]

“Na wahukumu baina yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu” [Al-Maidah:49].

Watu katika dola ya Kiislamu hawawezi kuweka kanuni za kudhibiti mahusiano yao, au kutunga katiba au sheria. Hakuna nafasi kwa mtawala kuwalazimisha watu au kuwapa chaguo la kufuata sheria zilizowekwa na wanadamu ili kudhibiti mahusiano yao. Bali, kuna kujitolea kamili kwa yale ambayo Uislamu umeamua. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

[وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللهُ وَرَسُولُهُ أَمْراً أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ]

“Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapo kata shauri katika jambo lao.” [Al-Ahzab:36].

Mtume (saw), aliisimamisha dola ya Kiislamu mjini Madina kwa msingi wake, kanuni zake, nguzo zake, vyombo vyake, jeshi, na mahusiano yake ya ndani na nje. Yeye (saw) alikuwa mkuu wa dola, na alikuwa na wasaidizi, magavana, mahakimu, jeshi, wakurugenzi, na baraza ambalo angeweza kuliregelea kwa mashauriano... Muundo huu wa dola ulitajwa katika nususi za Sharia, kwa hiyo ukadhihirika na kujulikana kwa Maswahaba, Mwenyezi Mungu awawie radhi, wakafuata njia yake (saw) wakishikamana na muundo wa dola alioufafanua yeye (saw), washikamana na kauli ya Mwenyezi Mungu (saw):

[لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ]

“Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu” [Al-Ahzab:21]. Na kauli Yake (swt):

[وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا]

“Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho.” [Al-Hashr:7]. Kwa hiyo Ijmaa ya Maswahaba ni kwamba baada ya Mtume kutakuwa na mkuu wa dola ambaye atakuwa mrithi wa Mtume katika kiti cha Urais wa dola pekee, si katika ujumbe au utume, kwa sababu utume ulishatamatika.

Ni wazi kutokana na sura ya dola, misingi yake, na kanuni zake katika Uislamu kwamba ni tofauti kabisa na mifumo ya serikali duniani. Utawala katika Uislamu sio wa kifalme ambao watoto wanarithi utawala kutoka kwa baba zao. Bali, utawala unachukuliwa na Khalifa kupitia bayah ya Ummah (kiapo cha utiifu) kwake kwa ridhaa na chaguo, kwa sababu moja ya kanuni za mfumo wa serikali ni kwamba mamlaka ni ya Ummah, kumaanisha kwamba Ummah ndio una haki ya kuchagua mtawala. Mfumo wa utawala katika Uislamu sio mfumo wa kijamhuri unaoegemezwa kwenye demokrasia, ambamo ubwana ni wa watu, ambao hutunga sheria na kumteua mtawala kama mwajiriwa kutekeleza kile wanachokitunga. Ubwana katika mfumo wa serikali katika Uislamu ni wa Shariah. Umma wala khalifa hana haki ya kutunga sheria. Mtunzi wa sheria ni Mwenyezi Mungu Mtukufu Peke Yake, na Khalifa anayo haki ya kutabanni hukmu kutoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume Wake, rehma na amani zimshukie. Khalifa si mwajiriwa wa Ummah, bali yeye ni mwakilishi wake katika kutekeleza Sheria ya Mwenyezi Mungu ardhini. Kwa hiyo, mamlaka ni ya Ummah kwani Ummah ndio unaomchagua mtawala anayekidhi masharti ya kustahiki kuuwakilisha katika utawala na mamlaka. Hana upendeleo wowote maalum, haki, au kinga kama katika mifumo iliyoundwa na mwanadamu. Kwa hiyo, hakuna jamhuri ya Kiislamu. Huu ni udanganyifu na upotoshaji, bali ni ulaghai na utumiaji dini vibaya. Hakuna shaka kwamba maelezo ya kina ya hukmu za Kiislamu kuhusiana na mamlaka, yanapowekwa katika vitendo na utekelezaji, yanaweza kushughulikia na kutatua mgogoro wa utawala nchini Sudan.

Ama kuhusu suala la mali na ugawanyaji wake baina ya watu, hakuna mfumo unaozusha katika hili kwa masuluhisho yenye hekima na tajriba isipokuwa mfumo wa Kiislamu, na tunayo maelezo juu ya hilo. Miongoni mwa hukmu za kisheria ni kwamba umiliki katika Uislamu ni wa aina tatu: umiliki wa mtu binafsi, umiliki wa dola, na umiliki wa umma. Hili la mwisho pekee linatosha kutibu matatizo ya kiuchumi ya watu wakati meno ya makampuni ya kikoloni ya makafiri yanayovuka mabara na kupora mali yanazuiliwa. Je, watu wanawezaje kutafuta tiba ya matatizo yao katika mifumo kando na Uislamu, ambao umeifanya dola kuwa mlinzi wa mambo kama baba mlezi wa watoto wake? Ni mdhamini wa kushibisha mahitaji ya kimsingi ya chakula, mavazi, na makaazi kwa kila mtu binafsi ndani ya dola. Ni chombo kikuu kinachoangalia utoshelevu wa mahitaji ya watu katika masuala ya elimu, matibabu, na usalama. Pindi dola inaposhughulikia mambo ya watu wake, mfumo wa umoja inaoutekeleza humfanya Khalifa kuchukua kutoka katika ardhi zenye utajiri mkubwa wa rasilimali, kuboresha utunzaji wa mambo ya watu katika maeneo maskini, ili watu wote wa dola waishi katika kiwango cha heshima na maisha ya staha. Mfumo wa uchumi wa Kiislamu utakapotekelezwa kikamilifu chini ya Khilafah ya Waislamu, utaugeuza kuwa kitovu cha matajiri wanaowekeza katika uchumi halisi unaozalisha bidhaa na huduma.

Kwa kumalizia, Hizb ut Tahrir imetayarisha rasimu ya katiba ya Dola ya Khilafah, yenye vifungu 191 vinavyotokana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah za Mtume Wake (saw) na yale waliyoyaongoza kutoka katika Ijmaa’ (Makubaliano ya Maswahaba) na Qiyas (ukisiaji) kwa ijtihad sahihi. Zaidi ya hayo, imeeleza sababu za katiba hii na msingi uliojengewa dalili zake, na njia ya hoja, katika vitabu viwili tofauti. Sisi katika Hizb ut Tahrir / Wilayah Sudan tunawasilisha rasimu hii ya katiba kwa vikosi vyote vya kisiasa, kijeshi na kiraia, kwa kuzingatia kwamba kila mtu ni Muislamu ambaye ameamrishwa kuhukumu na Uislamu, ili kuisoma na kuitekeleza uwanjani, ili Mwenyezi Mungu (swt) apate kuwa radhi nasi na kutuondolea ugumu wa maisha.

Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكاً وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَى]

“Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu.” [Ta-Ha:124].

Wa Alaikum Assalam wa Rahmatu Allah wa Barakatahu,

Ibrahim Othman (Abu Khalil)
Msemaji Rasmi wa Hizb ut Tahrir
katika Wilayah Sudan

Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari
Wilayah Sudan
Address & Website
Tel: 0912240143- 0912377707
http://www.hizb-sudan.org/
E-Mail: Spokman_sd@dbzmail.com

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu