Afisi ya Habari
Tanzania
H. 7 Rajab 1443 | Na: 1443 / 03 |
M. Jumanne, 08 Februari 2022 |
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Tunataka Haki kwa Mahabusu Sio Ahadi za Kilaghai Ambazo Kamwe Hazitekelezwi
Mahakama kwa mara nyingine imewabwaga chini ndugu zetu: Ust Ramadhan Moshi Kakoso (45), Waziri Mkaliaganda (37) na Omar Salum Bumbo (55) wanachama wa Hizb ut Tahrir Tanzania ambao walitekwa, wakabambikiwa kesi ya ‘ugaidi’ na bado wako kizuizini kwa miaka minne na nusu sasa kwa kisingizio cha ‘uchunguzi unaendelea’ huku wakinyimwa haki zao za msingi kama kutembelewa na ndugu zao na kuletewa chakula cha nje ya mahabusu. Tunauliza kwa nini walikamatwa kama upelelezi haujakamilika, ikiwa na maana kuwa hakukuwa na ushahidi wowote?
Kwa bahati mbaya katika kipindi chote walichopo kizuizini kesi yao imekuwa ikitajwa tu kila baada ya wiki mbili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mtwara ambapo waendesha mashtaka wamekuwa wakiwadanganya mahabusu hao mara kadhaa kuwa upelelezi wa kesi yao umeshakamilika na kesi yao itaanza kusikilizwa.
Mnamo tarehe 14 Januari 2022, Mahakama hiyo hiyo ilitoa ahadi ya kuwahadaa na kuwatuliza kuwa ndani ya wiki 3 wangekuwa huru au kesi yao ingepelekwa mahakama kuu yenye mamlaka ili kusikilizwa, kitu ambacho kwa mara nyengine hakijatokea.
Ni jambo lenye mashaka kwa mtu yeyote makini, kwa namna ulivyo uendeshwaji wa kesi za ugaidi nchini Tanzania. Maswali mengi yanaibuka, kama vile: Kwa nini ushahidi hauwasilishwi mbele ya mahakama? Kwa nini watuhumiwa hawapewi haki ya kusikizwa kesi zao kwa wakati muwafaka? Kwa nini watuhumiwa ambao kimsingi bado hawana hatia hawapewi haki ya dhamana? Kwa nini kunadhihirika wazi wazi hali ya vitisho na uonevu katika kesi hizi? Na la msingi zaidi, kwa nini watu wanakamatwa na kushikiliwa mahabusu kwa miaka mingi, huku upande wa waendesha mashtaka unakiri hadharani mahakamani kuwa uchunguzi unaendelea, ikiwa na maana kuwa hawana ushahidi wowote dhidi ya tuhuma hizo hata baada ya kipindi cha miaka minne na nusu?
Hitimisho pekee la hali hiyo ni uwepo wa ajenda ya dhulma kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na pia uwepo wa uvunjifu mkubwa wa haki msingi za utu.
Sisi Hizb ut Tahrir Tanzania kwa mara nyingine tena tunazitaka taasisi zote za usimamizi wa haki Tanzania kushikamana ipasavyo na taratibu za kimahakama, amma kwa kuwaachia huru mara moja bila ya masharti yoyote watu watatu tuliowataja wanaofahamika na kila mtu kwamba wapenda amani, ili waweze kujumuika tena na familia zao zinazowasubiri kwa hamu kubwa, au wapewe dhamana, wakati mchakato polepole wa upelelezi ukiendelea, mpaka pale kinachoitwa ushahidi kitakapokuwa tayari kuwasilishwa mbele ya mahkama ili kusikilizwa kesi yao.
Sasa imetosha, haki lazima itendeke kwa haraka na kwa wote
#KomeshaUkandamizajiWaKisheriaNaUtekaji
#StopOppressiveLawsAndAbduction
Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut Tahrir Tanzania
Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Tanzania |
Address & Website Tel: +255778 870609 |
E-Mail: mediarep@hizb.or.tz |