Jumapili, 20 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Kitabu cha “Dola Isiyomkinika”

Uwongo, Ghilba, na Dhana Zisizomkinika

(Imetafsiriwa)

Katika kipindi cha “mahojiano”, mnamo Disemba 12 na 19, 2021, Al-Jazeera ilipeperusha mahojiano na Dkt. Wael Hallaq yakiwa katika mfululizo wa matukio mawili kuhusu kitabu chake, Dola Isiyomkinika: Uislamu, Siasa, na Mashaka ya Kimaadili ya Kisasa. Kitabu hiki kilichapishwa na Dkt. Hallaq kwa Kiingereza mnamo 2021. Kilitafsiriwa na Dkt. Amr Othman kwa Kiarabu na kisha kutolewa na Kituo cha Kiarabu cha Utafiti na Uchunguzi wa Sera mnamo 2014, na kituo hiki kimeshirikishwa na Qatar na kinaongozwa na Azmi Bishara. Kitabu kilitangazwa wakati wa kuzinduliwa kwake, na mengi yaliandikwa kukihusu kama katika Al-Jazeera na sehemu nyengine. Semina zilifanyika za kukijadili ambapo maprofesa wa falsafa na fikra za kisiasa walishiriki. Kitabu kilisifiwa na wengi; kuna wale walioshangazwa nacho na kuvutiwa sana, kama Sheikh Abu Qatada al-Filistini, na wengine waliokizingatia kuwa chenye utatanishi na cha kipuuzi, kama Dkt. Muhammad Mukhtar al-Shanqiti. Hii ilichangia umaarufu wa mwandishi wa kitabu na kukikuza kitabu chake na vitabu vyake vyengine. Kisha mazungumzo kumhusu yeye yalisita kwa miaka michache hadi Al-Jazeera iliponyanyua jina lake tena katika mfululizo wa matukio mawili yaliotajwa awali.

Ndio, kuna ukuzaji imara na uliotengenezwa kwa umakini kwa kitabu hiki. Kitabu hiki ni vita dhidi ya Uislamu, hasa dhidi ya muelekeo wa kisiasa wa Kiislamu unaozunguka juu ya usimamishaji wa dola ya Kiislamu. Hata hivyo, wengi wa wanaofanya kazi katika eneo la Kiislamu walidanganyika na baadhi ya kauli zake, ambazo hawakutambua dhumuni lake. Na baadhi hawakutambua upotofu katika kitabu hiki kwa sababu ya sifa zake za kiini cha maadili katika sheria za Kiislamu na utumiaji wa historia. Ukosefu huu wa utambuzi uliongezeka kutokana na mashambulizi ya kitabu dhidi ya dola ya kisasa; juu ya Wamagharibi na hali iliyopo ndani yake kwa sababu ni tupu katika maadili na yenye ukosefu wa kuyadhibiti.

Watu wengi wamedanganyika kwa kitabu hiki, juu ya kuwa lengo la kitabu kwa anwani Dola Isiyomkinika inalenga Dola ya Kiislamu. Na hawakutanabahi juu ya utegemezi wa kifikra kwa Wamagharibi, japokuwa sentensi yake ya mwanzo inasema: “Wazo la kitabu hiki ni jepesi: “Dhana ya “Dola ya Kiislamu” haiwezekani kupatikana na inahusisha upinzani wa ndani, kwa mujibu wa tafsiri yoyote iliyopo ya kile kinachowakilisha dola ya kisasa.”. Licha ya sumu iliyojificha inayorejewa katika kitabu hiki, na fundisho lenye ujinga wa wazi ndani yake, hoja zake za kijumla jumla hadi kufikia kutokuwa wazi, pamoja na kutangazwa kwake kwa kiasi kikubwa, imekifanya kuwa ni moja ya zana za nguvu nyepesi katika uvamizi wa kifikra na kisiasa ambayo lazima itahadharishwe.

Fikra ambayo mwandishi ameikazia kwa nguvu, na iliyovutia hisia kwa wengi au kuwadanganya ni ya kuwa nidhamu ya Kiislamu ya kiutawala imejengwa juu ya kuwa ubwana uko kwa Mwenyezi Mungu (swt), na kwamba Mwenyezi Mungu (swt) amefanya maadili kuwa kiini na nguzo msingi katika hukmu za Kiislamu na sheria za nidhamu ya utawala. Miongoni mwa maadili ya hukmu hizi ni kuwa hazimpendelei yeyote, hivyo lazima watu wazitii, watawala, mamlaka yote ya dola na watu wengine wote wako sawa mbele yake. Hii ni kinyume na dola ya kisasa ya kitaifa ya Kimagharibi, dola ya Westphalia, ambayo haina maadili na inabomoa ubinaadamu, na ambayo ubwana uko kwa serikali. Hivyo dola ndio daima, kitovu na mwisho wa sheria, na sheria zinazunguka maslahi yake na hakuna mwanya au jukumu la maadili ndani yake. Kama alivyosema: Kile ambacho usasa umekizalisha ni kuwa dola ni Mungu, na kwamba hakuna Mungu ila dola. Kwa kuwa watu ni moja ya nguzo za dola katika tafsiri ya Wamagharibi, ubwana wa dola kwa uoni wake ni ubwana wa utaifa, na hivyo anasema: kuwa utaifa ni kama mungu katika dola ya kisasa.

Hallaq anahoji kuwa ukinzani huu baina ya dola ya kisasa na sifa zake na sheria na baina ya nidhamu ya Kiislamu ya serikali na sheria za Kiislamu ndio kinachofanya uwepo wa dola ya Kiislamu kutowezekana. Nguvu ya Dola ya Kimagharibi hivi leo ni imara na imetawala. Haikubali msingi wowote mwengine kwa dola nyengine yoyote yenye kuibuka au mfumo wa serikali. Kwa hivyo, kusimamisha dola ya Kiislamu leo haiwezekani.

Na anajua, kama wengine walio na muelekeo wa Kimagharibi, kuwa hisia za kutowezekana huku hazipatikani miongoni mwa wenye muelekeo wa kisiasa wa Kiislamu, na anajua kuwa hamu ya kuhuisha dola ya Kiislamu ni lengo la Kiislamu lisiloepukika. Kwa hiyo, hakusita katika kushauri kutowezekana huku na kujaribu kulaghai kwa kusema kuwa dola ya Kimagharibi isiyo na maadili huenda ikavunjika kutokana na uzito wa maadili maovu yenye kuangamiza ya mwanadamu. Kwa hivyo, inahitaji maadili ya Kiislamu, kama ambavyo wale wanaofanya kazi ya kutekeleza Shariah wanavyohitaji dola. Katika hali hii ya mashaka, Hallaq ameonyesha uoni wake wa suluhisho, ambao ni ulazima wa ushirikiano baina ya wanazuoni wa Kiislamu wanaoshawishika na ufahamu huu pamoja na wanafalsafa wa kimaadili wa Kimagharibi. Anasema, “Waislamu na kipote cha wanafikra na wanasiasa wao, katika mchakato wa kujenga taasisi mpya inayohitaji kurekebisha hukmu za Shariah na kuweka dhana mpya ya jamii ya kisiasa, inaweza na inapaswa kuingiliana na wenzao Wamagharibi kuhusiana na ulazima wa kuyafanya maadili kuwa ndio kitovu cha mambo.” Baadhi wamelikuza suluhisho hili kuwa ni ongofu. Katika suluhisho hili linalodaiwa, na la kufikirika kuna udanganyifu, bali ni hadaa.

Kwa upande mmoja, Hallaq anaeneza mbawa zake na kupaa katika njozi zake na kupendekeza kuikinga dola ya kitaifa kwa maadili ya Kiislamu, na kuona kuwa suala hili linaweka mzigo juu ya wanachuoni wa Kiislamu na mujtahidina wanaopaswa kulibeba jukumu hili, na kuyakinisha kuwa kwa sasa hawapo.

Maelezo mafupi juu ya wazo hili: je ni ujinga au kutoelewa? Au ni udanganyifu wa kuwafanya wapumbavu wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu kuendea kuyafanyia kazi malengo ya kifikra na kifalsafa ya Wamagharibi? Au ni ujinga mkubwa kwa upande wa (Profesa) uliomfanya ashauri upumbavu huu; unaotaka kazi ya Uislamu iwe kuhudumia itikadi ya falsafa ya Wamagharibi iliojengwa juu ya kuukanusha Uislamu na kumkanusha Mwenyezi Mungu?

Kwa upande mwengine, anashauri mabadiliko ya hukmu za Shariah ya Kiislamu, na sheria zinazohusiana na nidhamu ya serikali na dola kuwa chini ya hukmu na sheria za dola ya Kimagharibi. Huu ni moja ya udanganyifu unaopaswa kutahadharishwa. Msomaji anaweza kushangazwa: kwa vipi Dkt. Hallaq anashauri kubadilishwa hukmu za Shariah katika nidhamu ya Kiislamu ya utawala baada ya kuwasifu wanazuoni wa Kiislamu na kuwa sheria zake zinazoegemea ubwana kwa Mwenyezi Mungu – kama alivyoweka mwenyewe – na kuwa Mwenyezi Mungu amefanya maadili kuwa ni kitovu cha maarifa ya sheria na hukmu zake na sheria za serikali? Hapa Hallaq amekuja na uongo wake: kuwa maadili yanabadilika kulingana na muda na mahali, na mabadiliko haya yanaongozwa na uthabiti wa maadili ambao ni mkubwa zaidi, na vyenginevyo yatashindwa.

Kwa hivyo (kama anavyodai), kumekuwa na nidhamu nyingi za hukmu za Kiislamu katika kipindi cha karne 12, na sio nidhamu moja. Hii imetokea kupitia maendeleo ya maarifa ya sheria, ambapo sayansi ya sheria imeibuka kutokana na kupitiwa na muda, kisha uchunguzi wa uzuri (Husn) na ubaya (Qubh), kisha fikra ya maafikiano ya wanazuoni yanawakilisha ubwana wa Mwenyezi Mungu. Hukmu juu ya maendeleo (hayo) hutolewa kama ni fatwa na wanazuoni ambao wana uzoefu katika kufahamu Shariah na kufahamu jamii, mahitaji yake na mambo yake, baada ya mchakato wa Ijtihad katika kuelewa na kuibainisha. Kile ambacho kwa kauli moja wamekivua kutoka kwenye Shariah, desturi zinazokubalika na kile ambacho uhalisia unakihitajia ni maarifa mapya ya sheria yanayojumuisha maadili yanayohusishwa na Shariah, yaani, kwa Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa Hallaq, ubwana wa Mwenyezi Mungu maana yake, ni kutoa mamlaka ya utungaji sheria kwa wanazuoni. Hawa ndio wenye kuunda fiqhi katika zama na muda wote, na Mwenyezi Mungu (swt) amewapa mamlaka haya kupitia vyanzo vya maafikiano ya wasomi au wanazuoni. Katika nyakati zote, wanawakilisha kama watu wenye busara wenye kuamua kipi kizuri na kipi kibaya.  

Kwa msingi huo, wanaamua hukmu ya utawala na sheria za nidhamu zake, na kuwashurutisha watawala na watu kwenye maarifa yao ya sheria waliyoyaamua, kwa sababu (eti) hukmu za Shariah zenye maafikiano (yao) ndio dalili yake. Hivyo, nidhamu ya utawala ya Kiislamu inabakia kuwa ni nidhamu iliyoegemea kiini cha maadili, ambayo imezalishwa na wanazuoni kwa namna ambayo inakidhi vidokezo vya Shariah na matakwa ya uhalisia na maarifa ya kawaida katika jamii. Anasema: “Tunapaswa kuuliza swali: Kama Sharia sio kazi ya mtawala wa Kiislamu au dola ya Kiislamu… ni nini au nani aliyeitengeneza? Jibu ni Ummah ndio ulioifanya, hiyo ndio dunia ya kijamii ya pamoja, kiasili inatengeneza wataalamu wake wa sheria, nao ni watu waliofuzu kutenda kazi mbali mbali za kisheria zilizosimamishwa kuwa kitu kimoja, nidhamu ya kisheria ya Kiislamu. Wanazuoni wa Kiislamu wanaishi na maadili na hukmu za dunia ya jamii jumla… Ujumbe wao umetambuliwa na hukmu hizo na maadili yenye msukumo ulio na nguvu wa tabia ya kupenda usawa iliyoenea katika Quran… Nazo zimekuwa ni jiwe la msingi la uhalali na mamlaka ya kidini na kimaadili.”

Ni muhimu kuangaliwa hapa kwamba japo fikra hii iliyopotoka ni kiini cha kitabu hichi, lakini hakuna katika wale niliosoma maoni yao aliyeligundua hili. Pia hawakutanabahi kuwa ubwana wa Mwenyezi Mungu (swt) – kwa uoni wa mwandishi – ni ubunifu wa pamoja katika jamii kwa kuwa ni kawaida isiyopingika, na uhalisia wake ni makubaliano ya wanasheria wakubwa. Kwa hivyo, anasema kuwa hakukuwa na nidhamu moja ya serikali katika kipindi chote cha historia ya Uislamu, bali kulikuwa na nidhamu tafauti. Japokuwa kauli hii ni uwongo wa wazi, lakini haikuzingatiwa na Waislamu waliopendezwa na kitabu hicho, na huenda moja ya sababu ya hili, ni  mfumo wenye utata wa mwandishi na kuyaeleza mambo kijumla jumla.

Moja ya kumbukumbu hatari katika maelezo haya ni kuwa kuna vijana wanaohisi kutowezekana kwa dola ya Kiislamu kulingana na uoni wao wa uzani wa nguvu uliopo, na umiliki wa dola ya kisasa wa teknolojia, kijeshi na kiuchumi. Kwa hivyo, wanadanganywa na maelezo ya kitabu na kukiona kina dhamira ya dhati ya mtu mwadilifu. Kumbukumbu nyengine hatari ni kuwa kuna uelewa mbaya ulio wa hatari miongoni mwa Waislamu, na pia miongoni mwa mashekhe na wasomi, kwamba hukmu za Shariah zinabadilika kulingana na kubadilika kwa muda au mahala. Hivyo ni muhimu kuwa macho na hatari hii, na mitego hii na udanganyifu, na kuikabili na kuifichua. 

Hivyo, ushauri wa Hallaq mwanzoni uliegemea juu ya fikra ya uthabiti wa maadili, na kisha kumalizia kinyume na alichoanza nacho, nayo ni kuwa vinabadilika. Na kwamba zibadilishwe na kuwa na uwezo wa kuvua hukmu na sheria zinazokubaliwa na kumezwa na dola ya kisasa. Pia, istilahi ya ubwana wa “Mwenyezi Mungu”, ambapo Hallaq ameanza kwa kuusifu Uislamu kuwa ni mfumo wa maadili, amemalizia kwa maana ya kuwa ubwana upo kwa wanasheria wa kimaadili, na kuwa Uislamu ni zao la wale ambao kihistoria wameumiliki ubwana, nao ni wanasheria na mujtahidina, na hii ni fikra sawa na ya wanafalsafa wa Kimagharibi, wanafikra wa kisekula wa kikasisi na kanisa. Kwa hivyo, anawasilisha falsafa za Kimagharibi, nidhamu ya kimaadili na kisekula, na hizi ni fikra za wanaokana Mungu na nadharia zao.

Ninahitimisha maoni haya mafupi juu ya kitabu hiki kwa kusisitiza kuwa ni chenye ainisho la kijumla jumla hadi kwenye nukta ya utata katika nyingi ya fikra zake, na katika viashirio vya sentensi zake nyingi na ibara, hali inayomlazimisha msomaji kusoma tena na tena, na kisha kufikiri na kufanya muunganisho na uchambuzi kama mwenye kujibu fumbo. Wachangiaji zaidi ya mmoja wameelezea kuwa ni lazima kukisoma kitabu zaidi ya mara moja ili kukifahamu. Wanadhani kuwa huo ndio usomi uliobobea kwenye kitabu na umuhimu wa mada zake. Kwa kweli, hii sio sawa. Utata sio jambo la kujivunia. Bali, ni kosa la ki-mbinu linalokishushia hadhi kitabu na kuzusha shaka kwa mwandishi. Uangalizi wa makini unaonyesha kuwa kuwacha wazi huku na utata wa ujumla jumla ni kutokana na dhumuni la kuupiga vita Uislamu. Kile kinachowakilishwa na maoni haya ni kipande kidogo tu cha dhamira ya uovu “Dola Isiyomkinika” katika kupambana na Uislamu na fikra za kisiasa za Kiislamu, na ni sehemu ndogo ya sera na ujanja wa Kituo cha Kiarabu cha Utafiti na Uchunguzi wa Sera waliokitoa kitabu na wa kituo cha Al-Jazeera waliokitangaza.

[وَيَمْكُرُونَ وَيَمْكُرُ اللهُ وَاللهُ خَيْرُ الْمَاكِرِين]

“Na wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa mipango.” [Al-Anfal: 30]

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Mahmoud Abdul Hadi

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu