Alhamisi, 16 Rajab 1446 | 2025/01/16
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Umuhimu wa Kuwa na Fahamu Sahihi za Kisiasa kwa ajili ya Kuhuisha Umma wa Kiislamu

(وَإِذا قيلَ لَهُم لا تُفسِدوا فِي الأَرضِ قالوا إِنَّما نَحنُ مُصلِحونَ)

“Na wanapo ambiwa: Msifanye uharibifu ulimwenguni. Husema: Bali sisi ni watengenezaji.” [Surah Al-Baqarah, 2:11]

(Imetafsiriwa)

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliteremsha aya hii mjini Madina akizungumzia matendo ya wanafiki ambapo walikuwa wakiwafanyia matatizo Waislamu waliokuwa wakiishi katika Dola ya Kiislamu. Qur’an iliteremshwa kwa ajili ya wanadamu mpaka Siku ya Kiyama, na tunaangalia maana ya jumla ya aya bila ya kuweka mipaka kwenye sababu mahususi ambayo kwayo aya hiyo iliteremshwa. Ingawa wanafiki wa Madina walikuwa ndio sababu ya kuteremshwa kwa Aya hii, lakini matumizi ya ujumbe wake ndio maana ya jumla. Kwa mujibu wa qaidah maarufu ya kiusuli (kanuni) العِبرةُ بعموم اللفظ لا بخصوص السبب maana yake, “Mazingatio ni kwa ujumla wa lafudhi, sio maalum kwa sababu ya kuteremshiwa hukmu”, Aya hii ina maana ya jumla na inawahusu wote wanaosababisha matatizo kwa Waislamu. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anatwambia baadhi ya ujumbe muhimu sana kuhusu ulimwengu katika aya hii fupi sana. 1) Katika ulimwengu huu, kutakuwa na watu ambao wanafanya shida kwa watu wengine. 2) Watu wengine watajaribu kuwazuia. 3) Lakini wachokozi wataukanusha uchokozi wao na kwa hakika hufunika vitendo vyao vya uadui kwa maneno mazuri ya kujaribu kuwahadaa watu. 4) Mwenyezi Mungu (swt) hapendi uchokozi dhidi ya watu; kwa hivyo, Anawafichua hawa wavamizi na uchokozi wao.

Kwa kuzingatia aya hii na kwa maana hizi, hapa tunajadili fahamu muhimu za kisiasa ambazo Ummah lazima uwe nazo ili upate mwamko.

Kwa nini Ummah unapaswa kuwa na fahamu sahihi za kisiasa?          

Kuna sababu tatu muhimu za kushughulikia mada hii.

Kwanza, mada ya mahusiano ya kimataifa ni muhimu katika Uislamu kwa sababu Mwenyezi Mungu (swt) aliteremsha Sura huko Makka ili kuonyesha umuhimu wake kwa Waislamu.

)الم غُلِبَتِ ٱلرُّومُ فِى أَدْنَى ٱلْأَرْضِ وَهُم مِّن بَعْدِ غَلَبِهِمْ سَيَغْلِبُونَ فِى بِضْعِ سِنِينَ لِلَّهِ ٱلْأَمْرُ مِن قَبْلُ وَمِن بَعْدُ وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ ٱلْمُؤْمِنُونَ)

“Alif Lam Mim (A.L.M.) Warumi wameshindwa, Katika nchi iliyo karibu. Nao baada ya kushindwa kwao watashinda Katika nchi iliyo karibu. Nao baada ya kushindwa kwao watashinda Katika miaka michache. Amri ni ya Mwenyezi Mungu kabla yake na baada yake. Na siku hiyo Waumini watafurahi.” [Surah Ar-Rum, 30:1-4]

Kama tunavyojua kwamba Qur'an iliteremshwa kwa miaka 23 na kwa ujumla inakubaliwa na wanazuoni kwamba sehemu ya kwanza ya wahyi, hasa katika mji wa Makka, ilikuwa kwa sababu ya kujenga imani za Waislamu wapya. Hata hivyo, inafurahisha kutambua kwamba Sura hii na aya hizi, ambazo zinazungumzia mahusiano ya kimataifa, zilifunuliwa miaka 5 tu baada ya ufunuo kuanza mapema kabisa. Katika aya hizi, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaonyesha wazi kwamba imani yetu ni pana, yaani, ya kiroho, ya kisiasa na ya kimataifa.

Sababu ya pili ya kujadili umuhimu wa fahamu za kisiasa ni kwamba somo hili linaendana kabisa na hali yetu ya sasa kama Waislamu. Hivi sasa, tumekuwa wahasiriwa wa moja kwa moja wa jinsi uhusiano wa kimataifa unavyoendeshwa kwa sasa na Mataifa ya ulimwengu. Nchi, zenye nguvu na dhaifu, hubadilishana zamu, kudhulumu, kudhuru, kuwanyanyasa Waislamu kama ilivyoelezwa:

(وَإِذا قيلَ لَهُم لا تُفسِدوا فِي الأَرضِ قالوا إِنَّما نَحنُ مُصلِحونَ)

“Na wanapoambiwa: Msifanye uharibifu ulimwenguni. Husema: Bali sisi ni watengenezaji.”  [Surah Al-Baqarah, 2:11].

Umbile la Kiyahudi linawakandamiza Waislamu huko Palestina; Dola ya India inakandamiza na kuwadhuru Waislamu huko Kashmir na kote India; Dola ya China inawakandamiza na kuwadhuru Waislamu wa Uyghur; Dola ya Burma inakandamiza na kuwadhuru Waislamu wa Rohingya; Dola ya Saudia inawakandamiza na kuwadhuru Waislamu wa Yemen na orodha inaendelea.

Sababu ya tatu muhimu ni kwamba Umma wa Kiislamu ulikuwa umepewa wajibu na jukumu muhimu la kuupeleka Uislamu ulimwenguni kote, na hiyo ina maana kwamba ni lazima tuufikishe Uislamu kwa watu wote katika sayari hii.

(وَما أَرسَلناكَ إِلّا رَحمَةً لِلعالَمينَ) 

“Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.” [Surah Al-Anbiya, 21:107]

Ibn Abbas amesema ‘Aalamiin’ maana yake ni rehema kwa Waislamu na makafiri. Ibn Masoud anasema, Uislamu utaifikia dunia nzima. Ili kutimiza wajibu huu, inatulazimu tufahamu jinsi ulimwengu umepangwa na jinsi unavyofanya kazi, ili tuweze kuufikisha Uislamu ulimwenguni.

Kwa mukhtasari utafiti na ufahamu wa uhusiano wa kimataifa ni muhimu kwa sababu Mwenyezi Mungu (swt) aliashiria umuhimu wake katika Quran; sisi ni wahanga wa jinsi mahusiano ya kimataifa yanavyoendeshwa hivi sasa na pia tuna wajibu wa kuupeleka Uislamu ulimwenguni.

Katika muktadha huu, fahamu tano muhimu za kisiasa ambazo Umma wa Kiislamu unatakiwa kuzifahamu ili upate mwamko ni hizi zifuatazo,

1.Siasa. 2. Msukumo wa sera ya kigeni, 3. Uhusiano wa kimataifa 4. Mipango ya kisiasa, 5. Mbinu za kisiasa.

1. Siasa

Siasa inafafanuliwa kuwa ni “kuchunga mambo ya ummah – ndani na nje”. Inafanywa kivitendo na serikali, wakati Ummah unaihesabu serikali kuwa na jukumu juu ya hilo. Kuchunga mambo ya Umma kwa ndani kunafanywa kwa kutekeleza idiolojia ya Kiislamu. Hii inawakilisha sera ya ndani ya dola ya Kiislamu na inashughulikia masuala kama vile mahakama, kodi, usalama, masuala ya kijamii, afya, elimu, n.k. Kushughulikia mambo ya Ummah nje hufanywa kwa kuanzisha mahusiano na mataifa mengine na kubeba idiolojia ya Kiislamu kwa ulimwengu, na hii inawakilisha sera ya kigeni ya dola ya Kiislamu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema,

«كَانَتْ بَنُو إِسْرَائِيلَ تَسُوسُهُمْ الْأَنْبِيَاءُ كُلَّمَا هَلَكَ نَبِيٌّ خَلَفَهُ نَبِيٌّ وَإِنَّهُ لَا نَبِيَّ بَعْدِي وَسَيَكُونُ خُلَفَاءُ فَيَكْثُرُونَ»

“Mambo ya Bani Israil yalishughulikiwa na Manabii. Wakati wowote Nabii alipokufa, alifuatwa na Nabii. Kwa hakika yake hakutakuwa na Nabii baada yangu. Kutakuwepo na Makhalifa na watakuwa wengi.”

Mtume akaulizwa,

«فَمَا تأمرنا؟» “Unatuamrisha nini?” Akawaambia (saw),

«فُوا بِبَيْعَةِ الْأَوَّلِ فَالْأَوَّلِ أَعْطُوهُمْ حَقَّهُمْ فَإِنَّ اللَّهَ سَائِلُهُمْ عَمَّا اسْتَرْعَاهُمْ»

"Mpeni ba’yah (ahadi ya utiifu) mmoja baada ya mwengine na wapeni haki yao, kwani Mwenyezi Mungu atawauliza juu ya yote aliyowapa usimamizi kwayo." [Bukhari na Muslim].

Imam An-Nawawi anasema katika maelezo yake (sharh) kuhusu hii

Hadithi ya Nabii (saw), «يَتَوَلَّوْنَ أُمُورهمْ كَمَا تَفْعَل الْأُمَرَاء وَالْوُلَاة بِالرَّعِيَّةِ» “Walikuwa ni wachungaji katika mambo yao, kama Maamiri wa Kiislamu na Mawalii walivyo kwa raia.” Hivyo kama vile Manabii (as) walivyosuluhisha mambo kwa Wahyi wa Mwenyezi Mungu, vivyo hivyo lazima wafanye Maamiri na Magavana wa Kiislamu. Aidha alisema, وَالسِّيَاسَة الْقِيَام عَلَى الشَّيْء بِمَا يُصْلِحهُ "Siasa: ni utekelezaji juu ya jambo, kwa lile linalorekebisha." Hivyo basi, kuchunga mambo ya watu kwa shari’ah ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt) ambayo tutahesabiwa juu yake ikiwa tutaghafilika, tunapokusanywa mbele yake (swt).

Kwa mukhtasari, ni muhimu kuelewa na kutekeleza fahamu ya kisiasa ya siasa na kuelewa kwamba watu binafsi hujipanga katika mataifa. Mataifa haya kwa asili yataunda dola/serikali ambayo inapaswa/itashughulikia mambo ya ndani na nje ya mataifa. Kwa sasa, mataifa yamejipanga kwa mtindo wa kitaifa na mataifa haya yatatangamana kupitia sera za kigeni.

2. Motisha kwa sera ya kigeni:

Mataifa yote yanafanya siasa, lakini mengine ni bora kuliko mengine. Kwa nini mataifa yanaendeleza sera za kigeni? Ni nini kinachochochea taifa kwenda nje ya mipaka yake na kuingiliana na mataifa mengine. Mataifa yatavuka mipaka yao na kuingiliana na kukamilishana na mataifa mengine ili kufikia maslahi yao wenyewe. Kuna aina mbili za maslahi ambayo yanahamasisha mataifa yote kuingiliana na kushindana 1) Maslahi yasiyo ya kimada: mataifa hutafuta kuingiliana na kushindana kwa sababu yanapenda watu wao wenyewe au yanapenda idiolojia yao wenyewe, njia yao ya maisha, utamaduni na ustaarabu. Kiasi kwamba wanahisi watu wao au idiolojia yao inapaswa kuwa nambari moja ulimwenguni. Upendo na hamu hii ya kuwa nambari moja ulimwenguni inawasukuma kutawala mataifa mengine na idiolojia zingine. Hii ni sababu moja kuu kwa nini baadhi ya mataifa yanataka kuwadhuru Waislamu, kwa sababu yanauchukulia Uislamu na Waislamu kuwa ni tishio kwa idiolojia zao au mfumo wao wa maisha na hii inawasukuma kushambulia fikra za Uislamu na kupigana vita vya kifikra na kithaqafa dhidi ya Uislamu. Na hivyo kuwadhuru Waislamu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anakumbusha ukweli huu katika Quran:

(يَـٰأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا لَا تَتَّخِذُوا بِطَانَةً مِّن دُونِكُمْ لَا يَأْلُونَكُمْ خَبَالًا وَدُّوا مَا عَنِتُّمْ قَدْ بَدَتِ ٱلْبَغْضَاءُ مِنْ أَفْوَٰهِهِمْ وَمَا تُخْفِى صُدُورُهُمْ أَكْبَرُ قَدْ بَيَّنَّا لَكُمُ ٱلْـَٔايَـٰتِ إِن كُنتُمْ تَعْقِلُونَ)

“Hivyo basi nyinyi ndio mnawapenda watu hao, wala wao hawakupendeni. Nanyi mnaviamini Vitabu vyote. Na wanapo kutana nanyi husema: Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao wanakuumieni vidole kwa chuki. Sema: Kufeni kwa chuki yenu! Hakika Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo vifuani.”  [Surah Ali ‘Imran, 3:118].

Hii ndiyo sababu ya kwanza inayochochea baadhi ya mataifa kuunda sera ya mambo ya nje. Wanatafuta maslahi yasiyo ya kimada.

Sababu ya pili kwa nini mataifa yanaanzisha sera za kigeni ni kwa sababu ya maslahi ya kimada wanayotafuta nje ya mipaka yao. Hii inaweza kuwa kudhibiti rasilimali kama vile mafuta, kupata wafanyikazi (kama biashara ya utumwa), kufungua masoko ya bidhaa na huduma zao, kupata njia za biashara, au hata kudhoofisha mataifa mengine ambayo yanataka kuwadhuru. Hapana shaka kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amebariki ardhi za Waislamu kwa rasilimali nyingi na ametupa maeneo ya kimkakati duniani. Baadhi ya mataifa yasiyo ya Kiislamu yanataka kuiba rasilimali hizi na kuchukua udhibiti wa maeneo yetu kwa mahitaji yao ya kibinafsi.

Misukumo hii miwili inatufanya sisi Waislamu na ardhi zetu kuwa shabaha ya moja kwa moja kwa baadhi ya mataifa na tunakuwa walengwa wa sera zao za kigeni.

Ufahamu wa motisha ni muhimu kwa sababu utatoa ufahamu bora wa vitendo vya kisiasa vinavyotokea ulimwenguni kwa njia iliyo karibu na ukweli na kukubaliana na ukweli kadiri iwezekanavyo. Tutaweza kuona zaidi ya uwongo uliotajwa na wanasiasa na tutajua nia ya kweli ya sera za kigeni. Silaha za vita dhidi ya ugaidi, silaha za maangamizi, amani, utulivu, ustawi, kurejesha demokrasia, kuwapa watu uhuru, kulinda mazingira, kuingilia kati kwa sababu za kibinadamu ni baadhi ya kauli mbiu ambazo zimekuwa zikitumika kuhalalisha uchokozi dhidi ya Waislamu hata dhidi ya Wasiokuwa Waislamu. Lakini haya ni maneno tu yanayofunika nia zao mbaya.

Kwa mukhtasari, mataifa yataanzisha sera za kigeni ili kuingiliana na kushindana ili kufikia maslahi ya kimada na yasiyo ya kimada. Uislamu, Waislamu na ardhi zetu zimekuwa lengo la maslahi yao. Ni maingiliano haya kupitia sera za kigeni za mataifa haya ambayo yanaunda hali ya kimataifa ambayo Waislamu wanapaswa kuisoma na kuielewa kwa usahihi ikiwa tunataka kujilinda na kuibeba idiolojia hii duniani.

3. Hali ya Kimataifa:

Ufafanuzi wa hali ya kimataifa ni "muundo wa mahusiano ya kimataifa yenye ufanisi kati ya dola".

Kwa kuwa ulimwengu umepangiliwa kwa muundo wa dola ya kitaifa, je, tunajua ni dola ngapi za kitaifa ziliyopo duniani leo? Kulingana na UN, kuna dola 206 za kitaifa. Lakini hapa kuna jambo kuu la kuelewa, kwamba dola hizi zote 206 za kitaifa si sawa linapokuja suala la sera zao za nje, kuingiliana na kushindana kwa maslahi yao wenyewe. Ukweli ni kwamba baadhi yad ola za kitaifa zina uwezo mkubwa wa kushawishi matukio nje ya mipaka yao ili kufikia maslahi yao binafsi. Ili kusaidia kuelewa ufahamu huu muhimu wa hali ya kimataifa, kielelezo cha kuainisha dola kulingana na uwezo wao wa kushawishi matukio nje ya mipaka yao na kufikia maslahi yao ni muhimu.

Aina tofauti za dola

Kupitia mtindo huu, tunasema kwamba kuelewa hali ya kimataifa, yaani, muingiliano na uhusiano kati ya dola za kitaifa kupitia sera zao za kigeni kwa kweli, inakuja chini ya kuzingatia dola hizo za kitaifa ambazo zina ushawishi mkubwa zaidi kwa mataifa mengine inapokuja sera ya mambo ya nje na mataifa haya zinaitwa dola kubwa/dola zenye nguvu na taifa linaloweza kuwa na ushawishi mkubwa katika sera yake ya mambo ya nje. Dola hizi ziliorodheshwa kama dola zinazoongoza. Kwa maana nyengine, hali ya kimataifa ni kuelewa sera ya mambo ya nje ya dola inayoongoza na zile dola ambazo zinashindana na dola kubwa, kwa sababu dola hizo kubwa zitatengeneza kwa kiasi kikubwa kile kinachotokea duniani na sio mataifa yote 206 duniani. Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ufaransa Hubert Védrine, katika kitabu chake ‘France in an Age of Globalization’, alitoa uainishaji wake mwenyewe wa dola katika suala la nguvu na ushawishi, akisema kwa maoni yake. ‘Marekani inawakilisha nafasi ya 1 duniani bila mpinzani. Katika safu ya pili inakuja, dola saba ambazo zina ushawishi wa kimataifa ambazo ni Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Urusi, China, Japan na India kwa sharti kwamba watapanua maono yao ambayo bado ni ya kikanda'.

Ni muhimu kujua kwamba ushawishi ambao mataifa haya hutoa ndani ya sera zao za kigeni juu ya mataifa mengine ili kufikia maslahi yao haujakomewa; maana unaweza kuhama na kubadilika. Kwa hiyo dola kubwa zinaweza kudhoofika, kushuka na kuwa dola huru au dola tegemezi. Vile vile, dola ambayo inaitwa tegemezi, yaani, ambayo haidhibiti sera yake ya kigeni, kwa kweli inaweza kuwa dola kubwa hatimaye. Kwa hivyo hali ni nyumbufu sana. Kwa hivyo, kutokana na mtindo huu, tunaweza kuhisi kwamba kuna dola inayoongoza, ambayo tunahisi ni Marekani sasa hivi. Linapokuja suala la sera za kigeni, Marekani ina ushawishi mkubwa zaidi kwa mataifa na dola zengine ambazo zinashindania nayo nguvu kubwa ikiwemo Uingereza, Ufaransa, Urusi na China nk.

Kisha kuna dola huru ambazo zinaendesha sera zao za nje na za ndani kulingana na matakwa yake na maslahi yake yenyewe, kama vile, Uswizi, Uhispania, Uholanzi, Italia, Uswidi, Japan, India (hivi sasa) na nchi nyingi za Ulaya.

Na kisha kuna dola tegemezi ambazo zinaunganishwa na dola zengine katika sera zao za nje na hata katika masuala yao ya ndani. Haya ni mataifa dhaifu zaidi duniani katika suala la nguvu na ushawishi linapokuja suala la hali ya kimataifa na sera ya kigeni na kwa bahati mbaya unaweza kuona nchi nyingi za Kiislamu ikiwa sio zote, pamoja na Afrika na Amerika Kusini ziko chini ya kundi hili.

Ili kuelewa mtindo huu, tuchukulie mashambulizi ya hivi karibuni ya kijeshi ya Saudia dhidi ya Yemen na kuua maelfu ya Waislamu. Saudi Arabia ilisema kwamba ilitekeleza vitendo hivi katika sera yake ya kigeni ili kujilinda dhidi ya 'magaidi' nchini Yemen. Swali tunalopaswa kujiuliza juu ya ukweli huu ni je, Saudi Arabia inaona na kuchukua hatua hizi inapokuja kwenye sera yake ya mambo ya nje kama dola kuu, au kama dola huru au dola tegemezi? Kwa maana nyengine, je, Saudi Arabia ilifanya shambulizi hili nje ya mipaka yake, kwa sababu ina uwezo wa kujipambanua maslahi yake linapokuja suala la siasa za nje au ilifanya mashambulizi haya katika siasa zake za nje kwa maslahi ya dola kubwa zaidi? Je, twadhani kwamba Saudi Arabia ina uwezo wa kuamua sera yake ya mambo ya nje? Kutumia mfumo huu kutatusaidia kuelewa kinachoendelea Yemen na kwa nini kinatokea.

Kwa mukhtasari, fahamu hii na mfano wa aina mbalimbali za serikali itatusaidia kuelewa kwamba mataifa machache yenye nguvu ndiyo yatawajibika kwa matukio mengi ya kimataifa yanayotokea duniani. Matukio mengi ya kimataifa yanayotokea mara nyingi husababishwa na nchi chache zenye nguvu. Kwa hivyo, kama Waislamu, tunapaswa kuzingatia sera za kigeni za zile dola za kitaifa zenye kumiliki nguvu kubwa, kwani zina uwezekano mkubwa wa kuwajibika kwa kile kinachotokea ulimwenguni na haswa kwa Waislamu. Na bila shaka zitakuwa kikwazo kikubwa zaidi, tunapojaribu kuupeleka Uislamu ulimwenguni kote.

Mipango ya Kisiasa

Fahamu muhimu inayofuata ya kisiasa ni mipango ya kisiasa. Kama ilivyotajwa hapo awali, sera za kigeni hutengenezwa na mataifa ili kufikia maslahi yake nje ya mipaka yake. Kuna sehemu nyingi za sera ya kigeni. Sehemu muhimu zaidi za sera ya kigeni ni mipango ya kisiasa na mitindo ya kisiasa. Mataifa huunda mipango ya kisiasa. Inafafanuliwa kama "sera jumla ambayo inaundwa na dola ya kitaifa kwa ajili ya kupata moja ya maslahi yake". Kwa hivyo, baada ya kutambua maslahi yake, dola hizi za kitaifa zitaendeleza mipango ya kisiasa ya kufikia maslahi haya nje ya mipaka yake. Mipango ya kisiasa iliyoandaliwa na dola ya kitaifa itachukua muda kufikia maslahi yake. Kwa hivyo, mara nyingi itakuwa ya muda mrefu na haibadiliki mara nyingi. Mipango mingi ya kisiasa huwekwa siri. Mataifa yenye nguvu mara chache hukagua mipango ya kisiasa hadharani. Dola za kitaifa, hasa dola kubwa, kwa kawaida zina maslahi mengi nje ya mipaka yao.

Kwa hivyo, wataunda mipango mingi ya kisiasa. Kwa kuzingatia kwamba tunapaswa kuzingatia sera ya kigeni ya dola kubwa, ni dhahiri kwamba tunatafuta kutambua mipango ya kisiasa ya mataifa kama Amerika. Hapana shaka kwamba Marekani ina maslahi duniani kote. Kwa hivyo, itakuwa na mipango maalum ya kisiasa kwa kanda kama vile Ulaya, Urusi, Mashariki ya Kati, Mashariki ya Mbali na Afrika. Kwa hivyo, mipango ya kisiasa ya Marekani inaweza kuwa ni ipi kwa maeneo haya ikizingatiwa kwamba inajaribu kuiweka siri? Baadhi ya mifano ya jumla ya mipango ya kisiasa ambayo imeendelezwa na mataifa kihistoria ili kufikia maslahi yao ni. 1) Ukaliaji dhahiri wa nchi nyingine au kunyakua sehemu ya ardhi yake; 2) Kuchukua rasilimali za taifa; 3) Kuunda mhimili wa nchi; 4) Kubadilisha hali ya taifa kutoka kujitegemea hadi tegemezi n.k. 5) Kudhibiti na kuzuia ushawishi wa mataifa mengine yanayoongoza au yaliyo huru katika eneo au kanda ya dunia; 6) Kusaidia taifa jingine kuongeza ushawishi wake ili kufikia maslahi ya taifa lake. Hii ni baadhi ya mifano ya mipango ya kisiasa.

Mbinu za Kisiasa:

Kipengele kinachofuata muhimu cha sera ya kigeni ni mbinu za kisiasa. "Ni sera maalum inayohusiana na moja ya maelezo ambayo husaidia katika kukamilisha na kuimarisha mpango". Kwa maana nyengine, ni hatua mahususi ambayo taifa linabeba kufikia mpango wa kisiasa. Dola nyingi ni za vitendo; kwa hivyo, zitafuata mbinu za kisiasa ambazo mara nyingi zinaweza kukiuka kanuni zao wenyewe ikiwa mbinu hiyo itafikia lengo [Lengo huhalalisha njia]. Baadhi ya mifano ya mbinu za kisiasa ni 1) Vita; 2) Kuweka au kuondoa watawala vibaraka; 3) Mapinduzi ya kijeshi; 4) Kushawishi uchaguzi; 5) Mikopo ya misaada ya kiuchumi, miradi ya maendeleo kwa kutumia wataalam; 6) Ufumbuzi wa kijeshi, droni, na uvamizi; 7) Miungano ya kijeshi, mikataba na kambi za Kijeshi 8) Mikataba ya kiuchumi 9) Mikataba ya silaha 10) Kusitishwa kwa mapigano; 11) Kuanzisha, kushajiisha na kusaidia mapinduzi katika nchi nk.

Nukta ya jumla ya kukumbuka kuhusu mbinu za kisiasa na mipango ya kisiasa ni kwamba zote mbili zinatumika kufikia maslahi ya mataifa na zinaunda sehemu muhimu ya sera ya kigeni ya nchi. Mipango na mbinu za kisiasa hupangwa kwa ajili ya hatua za haraka. Mitindo hiyo inaweza kubadilika inapofichuliwa au kutofaa, ilhali mipango ya kisiasa inaweza kubadilika ikiwa haina maana au kusababisha matatizo yasiyo ya lazima kwa dola ya kitaifa. Dola hiyo ya kitaifa, hasa dola kubwa, kamwe haitaacha kuunda, kubuni, kupitia upya, au kuhakiki mipango na mitindo yake ya kisiasa hadi itakapokuwa dhaifu na kushuka kutoka kiwango chake katika hali ya kimataifa, kama ilivyotokea kwa Japan, Italia, Ubelgiji, Uholanzi, Ureno, ambazo kihistoria zilikuwa dola zenye nguvu kubwa.

Fahamu hizi tano za kisiasa ni sehemu ya mfumo utakaosaidia kuelewa uhusiano wa kimataifa na sera halisi ya mambo ya nje ya dola kubwa zilizopo; kutusaidia kutengeneza sera ya kigeni ya dola ya Kiislamu ambayo italinda na kuhifadhi maslahi ya Ummah; ili kutuwezesha kuubeba Uislamu ulimwengu mzima unaoishi kwa sasa kama dola ya kitaifa.

Ili kuelewa fahanu hizi za kisiasa ambazo hapa zimetolewa kama dhahania tu, hapa tunataja tafiti mbili ili kuzielewa kwa njia bora na jinsi zinavyotumika kivitendo.

Utafiti 01

Uhusiano wa kimataifa na makabila ya Waarabu katika Peninsula ya Arabia na dola ya kwanza ya Kiislamu huko Madina na Mtume (saw) kama mtawala wake.

 

Bara Arabu mwaka wa 1 Hijria

Wakati wa kuhama kwa Mtume (saw) kwenda Madina, wengi wa makabila ya Waarabu walikuwa wasiokuwa Waislamu. Walikuwa wakiabudu masanamu katika maeneo ndani ya Arabuni ambayo waliyadhibiti kisiasa na kiuchumi. Jambo la ukweli ni kwamba ndani ya miaka 10 ya kuhama kwenda Madina, Mtume Muhammad (saw) alibadilisha mazingira yote ya kisiasa ya Arabia. Mengi kama si makabila haya yote ya Waarabu kwenye ramani hii na maeneo yao yakawa sehemu ya Darul Islam, yaani eneo la Uislamu, na Madina kama mji wake mkuu na Muhammad (saw) kama mkuu wa dola. Na wote walitoa zaka, ambayo ilitolewa kwenye mfuko mmoja na ikawekwa Madina.

Je, ni vipi Mtume wetu (saw) alipata mabadiliko makubwa namna hii katika muda mfupi namna hii? Kumbuka, kwa muda wa miaka 13 Mtume (saw) hakuweza kulibadilisha kabila moja la Maquraishi katika mji mmoja wa Makka kuwa la Kiislamu. Lakini ndani ya miaka 10, yeye (saw) hakuwafikia Maquraishi tu, bali makabila yote ya Waarabu na kuwa Waislamu. Ni vipi (SAW) alifanikisha haya?

Je, Mtume (saw) alisafiri kwa kila kabila, akazungumza nao kibinafsi, akatabasamu nao, akaishi nao, akawaonyesha maadili na tabia yake nzuri, na wakaguswa sana na shakhsia yake (saw) kiasi kwamba wakayatupilia mbali masanamu yao, wakawa Waislamu, wakaacha kumiliki ardhi zao na wakatoa zaka? Hapana shaka kwamba Mtume wetu (saw) alikuwa na shakhsiya bora, maadili bora na tabia bora lakini ni kutojua na kwa kweli ni makosa kuamini kwamba mabadiliko haya katika Arabuni yalitokea kwa njia ya madhihirisho ya kiroho na kimaadili.

Kwa hakika, tukiielewa kwa usahihi Sunnah ya dawa yake (saw) itadhihirisha kwamba Mtume (saw) aliweza kufikia mabadiliko haya si kwa njia ya fahamu za kiroho au za kimaadili bali kwa kufanyia kazi fahamu za kisiasa zinazoongozwa na sharia. Kutoka kwake (saw) tunaelewa fahamu za kisiasa za ‘siasa’; njia pekee ya kuchunga mambo ya watu ilikuwa ni kusimamisha dola ya Kiislamu. Na ni kwa ajili hiyo ndio maana Mtume (saw) na Maswahaba zake walihama kwenda Madina, ambako (saw) alianzisha dola ya kwanza ya Kiislamu.

Mara moja (saw) aliichunguza mandhari na akabainisha makabila mbalimbali ambayo alipaswa kuingiliana nayo na kushindana nayo huko Arabuni. Kwa hili, yeye (saw) aliendeleza sera ya kigeni. Baada ya kusimamisha dola ya Kiislamu huko Madina, Mtume (saw) alibainisha maslahi yake muhimu. Maslahi yake makuu yalikuwa ni kuubeba Uislamu kama fikra na njia kwa makabila haya yote ya Kiarabu na kuyaweka chini ya utawala wa Uislamu.

Msukumo wake wa kuingiliana na kwenda nje ya kuta za Madina na kushindana na makabila haya kimsingi ulikuwa ni maslahi yasiyo ya kimada; maslahi yake yalikuwa kwa mfumo. Alitaka kuupeleka Uislamu kwenye makabila yote haya. Na pia alitambua kwamba makabila haya yangeichukulia dola yake mpya ya Kiislamu na mfumo wake mpya wa maisha kuwa ni tishio kwa maslahi yao ya kimada na kwa maisha yao ya kuabudu masanamu na hilo lingeyatia hamasa makabila haya ya Kiarabu kutaka kuwadhuru Waislamu. Kwa hiyo (saw) alianzisha sera ya kigeni ambayo 1) ingewalinda Waislamu waishio Madina dhidi ya kudhuriwa na makabila mengine; 2) kubeba Uislamu kwa Waarabu wote wanaoabudu masanamu ambao walipangwa katika muundo wa kikabila. Kwa hiyo (saw) aliyaainisha makabila yaliyoizunguka katika makundi tofauti, yaani, yale yaliyokuwa na athari kubwa katika eneo hilo na (saw) akaamua kwamba Maquraishi huko Makka ni miongoni mwa makabila yanayoongoza. Pia alibainisha kwamba Banu Thaqeef, Banu Najran, Banu Tamim, pia walikuwa makabila muhimu ya Kiarabu katika Arabuni. Alibainisha kwamba baadhi ya makabila yalikuwa na uhusiano wa karibu na tegemezi kwa Maquraishi kama makabila ya Banu Kinana na Banu Al-Akhdhari na hivyo yangeweza kufanya vitendo dhidi ya Waislamu chini ya ushawishi wa Maquraishi. Pia alibainisha makabila ambayo yanajitegemea na yaliyo karibu na Madina, makabila ya Kiyahudi ya Banu Nadhir, Banu Qaynuqa, Banu Quraydha. Baada ya kuyaainisha makabila haya katika aina tofauti, yeye (saw) alibainisha kwamba Maquraishi ndilo kabila alilolihisi, ambalo liliweka kikwazo kikubwa kwa maslahi yake makuu ya kuupeleka Uislamu kwa makabila yote haya ya Kiarabu. Kwa hiyo (saw) alianzisha mpango wa kisiasa wa kuwashinda Maquraishi na kuuweka mji wa Makka chini ya udhibiti wa dola ya Kiislamu. Mpango huu ulimchukua miaka 8 kufikia na mpango huu haukubadilika kamwe. Ili kufanikisha mpango huu wa kisiasa, (saw) alianzisha na kutekeleza mitindo mingi ya kibunifu ya kisiasa. Kwa Maquraishi, yeye (saw) aliendesha ghadhabu isiyopungua 3 kwenye msafara wa Maquraishi uliokuwa umebeba bidhaa za bei ghali kutoka Syria kwenda Makka. Ndani ya miaka michache baada ya hijrah, yeye (saw) alitafuta kujenga mashirikiano na akafanya mapatano na makabila mbalimbali ya Kiarabu kama vile Banu Dhamrah na Banu Mudlij. Alikuwa akituma majasusi na misheni pelelezi ili kumjuza na kumpa habari kuhusu Maquraishi na shughuli zao. Alifanya mapigano na vita na Maquraishi; vingine alishinda na vingine hakushinda. Yeye (saw) wakati mwingine alivunja kivitendo miungano iliyofanywa kati ya makabila ya Kiarabu ambayo yalikuwa yakitishia dola ya Kiislamu. Alilitolea kabila la Banu Ghatafan, 1/3 ya mazao ya Madina kama wangekubali kuvunja mashirikiano yao na Maquraishi wakati wa vita vya Khandaq (handaki). Aliweza hata kutia saini usitishaji vita wa muda na Maquraishi, ili kwamba aweze kulitenganisha kabila la Kiyahudi la Khaybar (Kaskazini mwa Madina) bila kuwa na wasiwasi juu ya mashambulizi ya kushtukiza kutoka kwa Maquraishi kutoka kusini mwa Madina. Mitindo ya Mtume ilianza kuzaa matunda na aliweza kudhoofisha nguvu za Maquraishi na kuongeza nguvu zake mwenyewe. Muungano wake na makabila tofauti ya Kiarabu ulimwezesha kuongeza jeshi lake kutoka askari 313 hadi askari 10,000 katika muda wa miaka mitano tu. Ilikuwa ni kwa mchanganyiko wa mashirikiano, uvamizi, misafara, mikataba, vita, usitishaji mapigano ambapo hatimaye aliweza kufanikisha mpango wake wa kisiasa na baada ya miaka 8, mji wa Makka ukawa sehemu ya dola ya Kiislamu na baada ya miaka miwili zaidi, sehemu kubwa ya makabila katika Bara Arabu yenyewe walikuwa wakitoa zaka kwa Muhammad (saw) au walikuwa wakitoa Jizya. Katika miaka hii 10, Maswahaba wake (ra) walijifunza na kutekeleza fahamu hizi za kisiasa ambazo bwana wao Muhammad (saw) alizitumia kuyaleta makabila haya ya Kiarabu chini ya dola ya Kiislamu. Sahaba (ra) waliendelea kutumia fahamu hiyo hiyo ya kisiasa kuendeleza dola ya Kiislamu na wakafanikiwa kununua Dola chini ya dola ya Kiislamu. Milki ya Uajemi na Rumi ilianguka wakati dola ya Kiislamu chini ya uongozi wa Khulafaa ar-Rashidoon (Makhalifa waongofu) ilipanuka hadi Iraq ya sasa, Syria na Misri n.k.

Utafiti 02:

Uvamizi wa Iraq na Amerika mnamo 2003

Taifa la Marekani lilielewa fahamu ya siasa, hivyo wakaanzisha nchi huru ili kushughulikia mambo yao ndani na nje mwaka 1776. Katika mwaka wa 2003 Marekani ilikuwa taifa linaloongoza duniani kwa kuiona Urusi ya kikomunisti zaidi ya muongo mmoja. Msukumo wake wa kuingiliana na ulimwengu ulikuwa ni wa kimfumo na kimada; hata hivyo, ilipokuja katika vita vya Iraq, ni vya maslahi ya kimada. Moja ya masilahi ya Wamarekani ilikuwa kutawala na kudhibiti soko la kimataifa la mafuta. Kwa kuzingatia hili na maslahi yake ya kimada, Amerika ilibainisha mataifa mengine ambayo yanaweza kupinga maslahi yake. Kwa hiyo wakabainisha Ufaransa, Uingereza, Urusi, Ujerumani mataifa ambayo yanashindana nayo na mataifa mengine huru kama China na India n.k. Hivyo ili kutimiza nia yake ya mafuta, iliandaa mpango muhimu wa kuikalia Iraq moja kwa moja na kuigawanya. Na mtindo wa kisiasa ambao Amerika iliutumia kufanikisha mpango huu ulikuwa ni kutengeneza kitisho cha kufikirika cha silaha za maangamizi makubwa ili kuhalalisha kuikalia kwa mabavu Iraq. Ilitumia Umoja wa Mataifa kama kifuniko. Ilitaka kuzuia mataifa mengine kuingilia mpango wa Marekani. Ilitaka kupuuza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na haja ya azimio la uvamizi huo. Iliunda muungano wa walio tayari. Ilichochea migawanyiko ya kimadhehebu, hivyo Waislamu watapigana wao kwa wao huko Iraq badala ya kujishughulisha na kumuondoa mnyakuzi. Iliunda serikali iliyochaguliwa ndani ambayo ingeipa umiliki wa Amerika uhalali kwa kuomba msaada kutoka kwa vikosi vya Amerika. Kwa hivyo Amerika ilikuwa na nia, ina sera ya kigeni, ilikuwa na mpango kwa Iraq na ilitumia mitindo tofauti kufanikisha mpango huo. Hata hivyo, mataifa mengine makubwa pia yalikuwa na maslahi katika uhusiano na mafuta na Mashariki ya Kati.

Ufaransa kama nchi yenye nguvu kubwa iliitikia mpango huu wa Marekani na ikatengeneza mpango wake wa kisiasa ili kufikia maslahi yake kuhusiana na mafuta na Mashariki ya Kati. Mpango wa Ufaransa kwa Iraq ulikuwa kuunda chini ya uongozi wake na ufikiaji wa nchi kuzuia mpango wa Amerika wa kuikalia kwa mabavu Iraq. Mtindo ambao Wafaransa walitumia ni kujaribu kutumia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukomesha uvamizi huo. Mtindo huu ulifanya kazi, kwani UN ilishindwa katika Baraza la Usalama. Ufaransa ilitaka kushinda mataifa mengine ili kuvuruga mpango wa Marekani. Ufaransa iliweza kushinda Urusi na Ujerumani kwa upande wake na hii ilifanya Marekani ionekane kama dola dhalimu na kuifanya Ufaransa ionekane kama mtetezi wa sheria za kimataifa.

Uingereza pia ina maslahi kama dola kubwa katika Mashariki ya Kati. Kwa hiyo ilikuwa na mpango wake ambao ulikuwa ni kupata manufaa fulani na wakati huo huo kuzuia udhibiti wa Marekani wa Iraq. Mitindo ambayo Uingereza ilitumia ilikuwa kuunga mkono Marekani hadharani, ili kupata manufaa fulani kutoka kwayo, lakini pia kwa siri kudhoofisha udhibiti wake. Ilikubaliana na Marekani hadharani kuhusu uwongo wa silaha za maangamizi makubwa, lakini ilitaka kuisukuma Marekani katika Baraza la Usalama pamoja na Ufaransa. Licha ya kujua, haikuwezekana kupata azimio lililofanya kazi kuunga mkono upinzani dhidi ya Marekani kwa siri kwa kuunga mkono Marekani hadharani kwa manufaa yake yote na kudhoofisha matumizi kwa wakati mmoja.

Mafunzo kwa Waislamu:

  1. Tafakari

Inatubidi kutafakari majibu yetu kama Waislamu kwa vita vya Iraq 2003 ambapo tunaona sera za kigeni zilitekelezwa na mataifa mengine kwenye ardhi yetu. Mambo yetu ya ndani kama Waislamu yaliathiriwa moja kwa moja. Nchini Iraq tulikuwa wahanga wa uchokozi huu lakini bila majibu. Wafaransa walikuwa na jibu, Wafaransa walikuwa na mpango, Waingereza walikuwa na mpango, Amerika walikuwa na mpango, lakini sisi Waislamu hatukuwa na mpango. Kwa nini? Kwa sababu inapokuja katika fahamu ya siasa hatuna dola ya Kiislamu inayotulinda na sera za kigeni za serikali hizi za kitaifa. Nchi tulizo nazo, zote bila ubaguzi, ni tegemezi kwa mataifa hayo makuu yanayotaka kutudhuru. Tunapoangalia maslahi yetu katika dunia kwa huzuni kama Waislamu hatuna maslahi katika dunia. Tumesadikishwa kwamba tunapaswa kushughulika tu na Aakhirah na tusiifukuze dunia hii (dunya); kwa hivyo, hatuna maslahi na mafuta, maeneo ya kimkakati, ulinzi n.k. dori yetu duniani ni kulinda maslahi ya Marekani, Ufaransa, Uingereza, Urusi au China kwa kuwafuata na kuwaunga mkono na kutekeleza mitindo yao kwa ajili ya mipango yao, ili waweze kufikia maslahi yao na sisi kupata madhara makubwa katika mchakato huo.

  1. Sababu za udhaifu wetu

Sababu kuu za udhaifu wetu ni, 1) Hatuna fahamu zozote za kisiasa kwa sababu tumeuwekea mipaka Uislamu na Sunna za Muhammad (saw) kwenye mkusanyiko wa imani, ibada na maadili au tumechukua fahamu za kisiasa kutoka Magharibi. 2) Tunaelewa uhusiano wa kimataifa kwa kutumia fahamu muhimu ambazo Magharibi hutupa; fahamu kama dola za kitaifa, sheria za kimataifa, kanuni za kimataifa. 3) Imani yetu kwamba njia pekee ya kuathiri mahusiano ya kimataifa ni kwa kusaidia mataifa makubwa kuhifadhi na kulinda maslahi yao ni uelewa wetu dhaifu wa fahamu za kisiasa zinazodumisha mfumo wa sasa wa kiulimwengu ambao sisi ni waathirika.

Hatimaye, tunakosa utaratibu muhimu zaidi wa kutekeleza fahamu hizi za kisiasa, yaani, serikali yetu wenyewe ya Kiislamu, na sera yetu ya kigeni inayojitegemea. Bila fahamu hizi za kisiasa, bila serikali yetu wenyewe na sera yetu ya kigeni, hatutaweza kamwe kuathiri ulimwengu kwa njia yoyote muhimu, tu kutoka kwa shida moja hadi nyingine. Matokeo yake, tutanaswa daima katika mitego iliyowekwa na mataifa makubwa.

Mwenyezi Mungu anakumbusha, (وَيَمْكُرُونَ وَيَمْكُرُ ٱللَّهُ وَٱللَّهُ خَيْرُ ٱلْمَـٰكِرِينَ)  Wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa mipango.” [Surah Al-Anfal, 8:30].

  1. Haja ya kuwa na fahamu za kisiasa

Ili kukabiliana na udhaifu huu, ni lazima tutake kuathiri hali ya kimataifa kwa kusoma, kuangaza na kutumia kivitendo fahamu hizi za kisiasa zilizotajwa katika makala hii zinazoonyesha ulazima na thamani kubwa ya fahamu za kisiasa kwa Waislamu. Kwa kutumia fahamu hizi za kisiasa si tu kwamba hatutafanikiwa tu kujilinda na mipango yenye madhara iliyopangwa na dola kubwa bali InshaAllah tutaweza kutengeneza tukio la dunia kulingana na maslahi na mipango yetu.

Ni muhimu kwamba tujaribu na kutumia fahamu hizi za kisiasa kujua mipango ya kisiasa ya kila taifa kuu na kuweza kutambua kwa usahihi mitindo yao. Lazima tujaribu kufichua mipango yao ya kisiasa hadharani. Ni lazima pia tulenge kuharibu mipango yao ya kisiasa kwa kukatisha mitindo yao ya kisiasa. Mapambano yetu ya kisiasa kama Waislamu yanapaswa kuelekezwa dhidi ya mipango na mitindo ya kisiasa kwa kuifichua na kuipinga.

Hitimisho

Kuhitimisha, dols za kitaifa zinatafuta kufikia maslahi yao na hii inazilazimu kuingiliana na kuwa na uhusiano na nchi zingine. Wakati mwingine masilahi haya ni yale yale lakini zaidi masilahi haya yanakinzana. Kwa hivyo, dols hizi za kitaifa zinashindana kila mara ili kufikia maslahi yao wenyewe. Kwa kufanya hivyo, watajaribu kushindana wao kwa wao. Hii inaleta ushindani wa mara kwa mara kati ya dola hizi za kitaifa zinapopambana na kushindana juu ya maslahi haya. Kama Waislamu, tutake au tusitake, hivi ndivyo Mwenyezi Mungu (swt) alivyoumba ulimwengu. Tupende tusipende, sisi ni sehemu ya ulimwengu huu na sisi ni sehemu ya mashindano na mapambano haya. Swali tunalopaswa kujibu ni je, tunataka kuwa washindwa na wahanga wa mapambano? Au tunataka kuwa washindi wa mapambano? Ni lazima tutambue kuwa, katika mapambano haya ya kudumu, wenye nguvu zaidi watasalia na walio dhaifu watakufa na hivi sasa tunakufa lakini Waislamu haturuhusiwi kufa kwa sababu Aqedah wetu inatuambia kuwa tuna misheni ya pekee sana hapa duniani. Ni kweli hatuifukuzii dunia hii bali ni lazima tuubebe Uislamu duniani kote na hiyo ina maana kwamba tunapaswa kuwa taifa linaloongoza duniani.       

(كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِٱلْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ ٱلْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِٱللَّهِ وَلَوْ ءَامَنَ أَهْلُ ٱلْكِتَـٰبِ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُم مِّنْهُمُ ٱلْمُؤْمِنُونَ وَأَكْثَرُهُمُ ٱلْفَـٰسِقُونَ)

“Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Watu wa Kitabu nao wameamini ingeli kuwa bora kwao. Wapo miongoni mwao waumini, lakini wengi wao wapotovu.”  [Surah Aali ‘Imran, 3:110]

Kwa hiyo, sisi Waislamu, ni lazima tuingie kwenye mashindano haya; lazima tuingie kwenye mchezo huu wa mataifa na lazima tushinde. Mtume (saw) alipambana na makabila ya kuabudu masanamu na kuyashinda kwa kufuata fahamu hizi za kisiasa. Maswahaba (ra), kwa kutumia fahamu hizo hizo za kisiasa, walizichukua himaya za kipagani zenye nguvu na kuzishinda. Sisi leo hii inatubidi kutumia fahamu hizi hizi za kisiasa kuyachukua mataifa haya yenye nguvu ya kibepari na hatuna budi kuyashinda. Inatubidi kumuabudu muumba wa dunia hii kwa kuifanya ayah hii kuwa na uhalisia. Mwisho, tunamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atusaidie kuzielewa na kuzifanyia kazi fahamu hizi za kisiasa. Tunamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atusaidie kusimamisha Dola ya Kiislamu itakayotekeleza fahamu hizi za kisiasa na sera zake za kigeni. Ninamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atusaidie kusimamisha tena dola ya Kiislamu, chombo ambacho kwacho tunaupeleka Uislamu duniani kote.

Alhamdulillahi Rabbil ‘Alameen

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Hameed bin Ahmed

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu