Jumatatu, 03 Dhu al-Qi'dah 1442 | 2021/06/14
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Mafunzo Kutoka Ukombozi wa Palestina wa Salahuddin

(Imetafsiriwa)

Wengi wanaendelea kuangalia kwa hofu mauwaji ya watu wengi yanayofanyika Palestina. Kile kilichoanzia Sheikh Jarrah na kuendelea al-Quds kwa kushambuliwa Msikiti wa al-Aqsa kimewashitua wengi duniani kote. Mgeuko huu wa matukio ni safari ya karibuni zaidi ya ukaliaji wa miongo kadhaa wa Wazayuni na waungaji mkono wao na ufukuzwaji wa wazawa unaoendeshwa kwa hatua ndogo ndogo. Baada ya miaka kadhaa ya wito wa maazimio kwa Umoja wa Mataifa na Wamagharibi ili kuingilia, watu wengi hivi sasa wametambua kuwa uvamizi unahitaji kugeuzwa kupitia ukombozi kwa majeshi ya Waislamu.

Maandiko ya Kiislamu na historia yamejaa ushahidi na mifano ya mapambano ya ukombozi yaliomaliza ukaliaji. Ushahidi na mfano muwafaka zaidi wa haya na kuchukua mafunzo kwayo ni ukombozi wa Palestina wa Salahuddin mwaka 1187, baada ya miaka 88 ya ukaliaji wa Makruseda wa Ulaya.

Siasa za Kieneo za Karne ya 11

Nishati ya kisiasa katika karne ya 11 ya washindani na uzani wa nguvu kisiasa haikuwa tofauti sana na hali ya leo katika ulimwengu wa Kiislamu.

Khilafah ya Abbasiyah ilikuwa ni uongozi mkuu wa Ummah, lakini hadi karne ya 11 ilikuwa imeshapitwa na utukufu wake wa awali na ilikuwa ni kama gamba tu la ukuu wake. Kiini cha ulimwengu wa Waislamu baina ya Misri na Uajemi kilikuwa kimetengana. Uongozi wa kisiasa usiomakinishwa mahala pamoja ulipelekea kuibuka kwa tawala za kurithishana zilizopelekea kuundwa kwa maeneo ya ushindani wa madaraka dhidi ya Khilafah.

Washindani wakuu walikuwa Fatimiya, kipote cha Ismailia waliodai kuwa na haki ya kutawala kwa kuwa ni vizazi vya Imam Ali (ra) na Fatima (ra), iliyopelekea jina la “Fatimiya”. Wa-Fatimiya walilifanya kuwa ni jukumu lao kuuchukuwa ulimwengu wa Kiislamu na kusimamisha utawala wa Ismailia na kutoka mwaka 909, walipingana na mamlaka ya Abbasiyah. Walipoiteka Misri mwaka 969, wakawa ni wenye nguvu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu. Mwishoni mwa karne ya 11, Fatimiya wakaitawala Afrika ya Kaskazini, Misri, Makkah na Madinah na sehemu za Syria na Palestina.

Wadau wakuu wengine wa kisiasa walikuwa ni Seljuks. Wakati wa zama za utawanywaji wa mamlaka usiomakinishwa chini ya uongozi mmoja, Abbasiyyah ilitumia askari watumwa walioletwa kutokea ardhi za Turkic za Asia ya Kati kuhudumu katika majeshi yao ili kuweka uzani dhidi ya Fatimiya. Makabila haya ya Turkic yalihamia kwenye ardhi za Kiislamu na kuufuata Uislamu na kisha kuweka nchi zao wenyewe katika vurugu za kisiasa za karne ya 10. Waseljuk waliunda dola iliomakinika ilioenea kutoka Syria hadi Asia ya Kati. Lakini Waseljuk walibeba jukumu la walinzi wa Khilafah. Ilikuwa ni Waseljuk ambao walizuia ueneaji wa Fatimiya katika karne ya 11. Mwishoni mwa karne ya 11, Waseljuk walienea Anatolia kote hadi wakajitokeza fukweni mkabala na Konstantinopli.

Ukoloni wa Wazungu wa Karne ya 11

Pindi Mfalme wa Byzantine Alexios alipotambua kuwa hatoweza kupambana na Waislamu mnamo 1095, ili kuihifadhi kutokana na kuanguka kwa Himaya ya Byzantine, alimuomba usaidizi mshindani wake Papa Urban II wa Roma. Papa Urban aliitumia fursa hiyo kukusanya jeshi la Wakristo wote wa Ulaya kwa jina la Kristo lililofikia makumi ya maelfu. Kwa kweli Papa alikuwa na uoni wake kwa Jerusalem na kutoa wito kwa Wakristo wote kuunga mkono safari ya vikosi kuukomboa mji na kusimamisha Utawala wa Kruseda wa Palestina, chini ya mamlaka ya Upapa.

Kutokea 1096, majeshi yakiongozwa na watukufu na mashujaa yalianza kusonga kuelekea Ulaya Mashariki kutoka Ufaransa ya leo, Ujerumani na Italia. Wakiwa safarini, Mayahudi wa Ulaya waliuliwa kutokana na ta’asubi za kidini zilizochochewa na Kanisa. Wakati Makruseda walipofika kwenye kuta za Konstantinopli, Mfalme Alexios alikataa kuwaruhusu kuingia katika mji, kwa kuhofia kuwa wataweza kupora kama walivyofanya kwenye makumi ya miji na vijiji walimopitia.

Makruseda walipofika mji wa zamani wa Antioch kwenye mpaka wa Syria na Uturuki (Antakya ya leo ya Uturuki), hali ya siasa katika eneo ilikuwa yenye maslahi upande wao. Antioch, kama ilivyo miji na vijiji vingi, ulikuwa ni kisiwa kilichojitenga. Ufalme wa Seljuk haukuwa tena ulioungana kisiasa. Badala yake Maamir wadogo wadogo wa Turkic wakiongoza miji binafsi, na mara kwa mara wakizozana. Miji mikubwa ya Damascus, Aleppo, Mosul yote haikuwa imeungana, na Maamir wao walikuwa ni wenye kupambana vita vya kuendelea. Wakati mtawala wa Antioch alipotaka msaada kutoka kwa Maamir wengine dhidi ya Makruseda waliouzunguka mji wake, hakupata msaada wowote.

Baada ya Makruseda kuushika mji, wakaazi wake waliuliwa. Mauwaji makubwa ya Antioch na miji mengine kuelekea Jerusalem yaliingiza hofu katika maeneo yaliozunguka. Maamir Waislamu walipendelea kuepuka mapambano na Makruseda, na mara walipotambua lengo lilikuwa ni Jerusalem, wengi waliwasaidia Makruseda kwa vyakula, silaha na kuwasafishia njia salama badala ya kupigana nao. Mnamo msimu wa kiangazi 1099, Makruseda walifika kwenye ngome za Jerusalem. Tarehe 15 Julai 1099, baada ya mzingiro wa wiki moja tu, Makruseda waliweza kuishika Jerusalem kutoka kwa Waislamu. Kwa mara ya mwanzo tokea Umar (ra) alipoingia mji huo miaka 462 iliopita nyuma yake, Jerusalem ilipotezwa. Yote haya yaliwezekana kutokana na kutoungana kwa viongozi wa Kiislamu na kina “Sharif Hussain” na “Mir Jafar” wa wakati huo waliowasaidia Makruseda.

Takriban wakaazi wote, zaidi ya 70,000 waliuliwa. Katika al-Aqsa, damu ya Waislamu ilifikia magotini mwa wakoloni. Misikiti na masinagogi yaliharibiwa kote. Hata Wakristo waliathirika, wakati Makruseda walipotaka kuweka tafsiri zao wenyewe za Kikatoliki badala ya zile za kiasili za Kigiriki, Armenia, Georgia na za makanisa mengine.

Nchi Vibaraka

Huku ulimwengu wa Kiislamu ukiwa katika hali ya mvurugiko, Makruseda waliweza kuimarisha nafasi yao Jerusalem. Ndani ya miaka minne, Himaya nne za Makruseda zilianzishwa – Kaunti (Wilaya) ya Edessa, Manispaa ya Antioch, Manispaa ya Armenia Cilicia, Kaunti ya Tripoli ikiwa na Himaya ya Jerusalem.

Kutokana na mgawanyiko wa ndani na kutengana, ulimwengu wa Kiislamu ulikuwa dhaifu mno na mvunjiko usioweza kutoa upinzani wowote. Vituo vya asili vya utawala katika Baghdad, Damascus au Cairo havikuwa na uwezo wa kujibu mashambulizi kutokana na mazingira hayo. Baadhi ya miji na vijiji vya Waislamu vya pembezoni vilianza pia kufanya biashara na nchi za Makruseda hali ambayo iliweza kuimarisha uwepo wao.

Kuimarisha Umoja

Iliwachukuwa Waislamu nusu karne kuweza kujijenga upya tokea kuipoteza al-Quds. Ilianzia kutoka kwa Amir wa Turkic, Imad al-Din Zengi, aliyetawala mji wa Mosul kaskazini ya Iraq. Aliunganisha Mosul na Aleppo kuwa jimbo moja na kwa nguvu zilizoungana za miji miwili mikubwa zaidi katika eneo, jeshi lake liliikomboa Wilaya ya Edessa, jimbo la kaskazini zaidi la Makruseda mwaka 1044. Wakati huo Edessa ilikuwa ni jimbo dhaifu zaidi la Makruseda na Makruseda waliangalia kupotea kwake kama Maamir wadogo wadogo walivyofanya kwa Antioch, na hili lilikuwa ni kosa kubwa.

Mkakati wa Imad al-Din ni kubuni Syria ilioungana kukabiliana na tishio la Makruseda kwa kuileta Damascus chini ya udhibiti wake, lakini mji huu wa kale ulibakia nje ya udhibiti wake kwa kuwa Amir wa Damascus hakutaka kuachilia mamlaka yake, hata kwa jina la umoja wa Waislamu.

Imad al-Din Zengi alikufa mnamo 1146 na mwanawe Nur al-Din Zengi aliendeleza mapambano kuunganisha ulimwengu wa Waislamu. Imad al-Din alikomboa maeneo mengi pembezoni mwa Antioch mnamo 1149, na mwaka 1154 alimng'oa Amir wa Damascus kwa msaada wa wakaazi wake waliomchoka kwa kuungana kwake na majimbo ya Makruseda.

Kwa kuungana kwa Syria chini ya mtawala mmoja, likabakia suala la Misri tu. kwa kipindi hichi, Makruseda waligeukia kusini kuivamia Misri ili kutanua uwepo wake katika eneo. Fatimiya walipohisi watashindwa, waliomba msaada kwa Imad al-Din, aliyepeleka jeshi kwa jina la umoja wa Kiislamu, lakini mara tu baada ya Makruseda kushindwa, Fatimiya waliunda muungano na Makruseda walioshindwa punde tu kulifukuza jeshi la Nur al-Din kutoka Misri. Huu ulikuwa ni usaliti wa hali ya juu. Jeshi la Nur al-Din lilijiondoa kutoka Misri lakini baada ya miaka minne tu, hatimaye Fatimiya walilazimika kutaka tena msaada kwa Nur al-Din, baada ya Makruseda kurudi tena kuiteka Misri. Mara hii Nur al-Din Zengi aliwashinda Makruseda Misri na kisha kuwashinda Fatimiya. Akamuweka jenerali wake mkuu Shirkuh kuwa Wali. Alifariki miezi michache baadaye kutokana na maradhi na mpwa wake Yusuf akashika nafasi yake Misri mwaka 1169, ambaye sote twamjua, alikuwa ni Salahuddin al-Ayubi.

Kuwazingira Maadui 

Maandalizi kwa ajili ya ukombozi wa al-Quds yalikwisha wekwa kwa Salahuddin na alianza moja kwa moja kujenga juu ya hayo na kuikomboa al-Quds. Alianza kwa kuimakinisha Misri na kuyatia mabaki yote ya Fatimiya ndani ya debe la taka la historia. Fatimiya ambao hutafautiana na Waislamu walio wengi, na ambao walikuwa ni usumbufu katika ulimwengu wa Kiislamu kwa karne kadhaa, walipigwa marufuku rasmi. Chuo Kikuu cha al-Azhar, ambacho kwa kipindi fulani kilikuwa ni ukumbusho wa propaganda ya Uismailiya, kiligeuzwa kuwa ni shule ya kiasili ya Kiislamu, na imebakia hivyo hivi leo.

Salahuddin alitia saini mkataba wa amani na Himaya ya Jerusalem ili kupatia muda wa kuziunganisha ardhi za Waislamu Jirani na Jerusalem. Alipofariki Nur al-Din mwaka 1174 kutokana na maradhi, Salahuddin akiwa Wali alisonga hadi Syria bila upinzani na kwa uungwaji mkono mkubwa wa ummah aliweza kuiunganisha Misri na Syria kwa ukamilifu kwa mara ya kwanza tokea kuibuka kwa Fatimiya. Salahuddin kisha akaiunganisha Iraq chini ya mamlaka yake na hii ikamaanisha kuwa Himaya ya Makruseda ya Jerusalem imezungukwa na dola ilio na nguvu, ilioungana chini ya mtawala aliyeamini kuwa lilikuwa ni jukumu lake kuikomboa Jerusalem.

Katika Vita vya Hattin mnamo 1187, jeshi la Salahuddin lililishinda kabisa jeshi la Makruseda la Jerusalem. Mashujaa wachache tu walibakia katika mji mtakatifu, ambao walijisalimisha kwa Salahuddin. Kinyume na Makruseda ambao walimuuwa kila mtu katika mji, Salahuddin aliwapatia wakaazi wote njia salama kuelekea kwenye ardhi za Wakristo na waliruhusiwa kuchukua vifaa vyao pamoja nao. Vituo vya Kikristo katika mji vilihifadhiwa na waliruhusiwa kufanya hija zao.

Kuna mafunzo mengi tunayoweza kujifunza kutokana na kukombolewa kwa al-Quds ambayo yanatekelezeka katika mazingira yetu hivi leo.

Mtengano - Makruseda waliweza kupata mahala salama katika ulimwengu wa Waislamu kutokana na kukosekana kwa umoja miongoni mwa watawala wa Waislamu. Tofauti zao ndogo ndogo ziliwafanya wawe washindani wao kwa wao na walikuwa wakishughulishwa sana na kupigana wao kwa wao kuliko kushughulikia tishio la Makruseda. Hii ni kama ilivyo hali ya sasa ya ulimwengu wa Waislamu ambapo tumegawanywa katika dola za kitaifa na kushindana wenyewe kwa wenyewe huku makafiri Wamagharibi wakitumia tofauti hizi za kitaifa kufikia maslahi yao.

Kuwang'oa Watawala – Salahuddin ametuonyesha namna ya kushudhulikia mtengano. Alipigana na kuwaondoa watawala wote waliokataa kuungana katika kuiteka tena Jerusalem. Alipoongoza kuiteka Misri ya Wa-Fatimiya, alipata uungwaji mkono wa watu ambao sio tu walitaka ukombozi kuondokana na Fatimiya bali pia walitaka al-Qudsi ikombolewe. Salahuddin alikuwa yupo sambamba na hisia za watu kuliko walivyokuwa watawala wa Fatimiya. Leo tunakabiliana na hali sawa ambapo tuna watawala ambao wako kinyume kabisa na hisia za Ummah. wakati Ummah ukitamani ukombozi kwa Palestina, watawala hutoa sababu kuhusu udhaifu walionao Waislamu, na nguvu kubwa ilizonazo umbile la Kiyahudi na namna mikono yao ilivyofungwa. Salahuddin ametuonyesha mazingira ya matukio haya kwamba watawala hawa wanahitaji kung'olewa na kuwekwa badala yake wale ambao hisia zao ziko sambamba na za Ummah.

Watawala vibaraka - Dola za Makruseda ziliweza kujiimarisha katika eneo wakati watawala wadogo wadogo wa Kiislamu Jirani na Jerusalem kuwapesishia. Lengo la Himaya ya Makruseda ilikuwa ni kuitumia Jerusalem ili kuimarisha nafasi yake katika Sham na kujitanua. Hivi leo umbile la Kiyahudi linatekeleza jukumu hili kama ilivyo Himaya ya Makruseda ya kane ya 21 na utawala wa Misri, Jordan na Syria ulivyokuwa na mikataba na mahusiano ambayo yanaimarisha umbile la Kiyahudi, ambapo bila ya hiyo haitoweza kubakia. Salahuddin, akikabiliana na uhalisia kama huo, aliyateka maeneo yote yalioizunguka Jerusalem, kuwaondoa watawala hawa vibaraka na kwa kweli ni kukata mirija iliyoinufaisha Himaya ya Makruseda.

Kambi Tangulizi ya Kimkakati – Majimbo ya Makruseda yalianzishwa na Kanisa katika Ulaya ili kuwa ni kambi tangulizi za kimkakati za kuipata Ardhi Takatifu na kulitawala eneo hilo. Licha ya vita vingi vya Krusedi, wakoloni wa Kikristo wa Ulaya hawakuweza kudhibiti eneo lao tangulizi la kimkakati. Eneo kubwa lao ni hili lililodumu miaka 88 ambalo Salahuddin alilimaliza. Hili ndilo jukumu la umbile la Kizayuni katika eneo hivi leo. Limeanzishwa kutumika kuwa ni msingi wa kuingilia katika eneo na hii ndio sababu Wamagharibi hutoa silaha, fedha na msaada kwa umbile la Kizayuni. Kama yalivyokuwa majimbo ya Makruseda ambayo yalifanya mikataba na makubaliano pamoja na viongozi wadogo wadogo wa Kiislamu kwa lengo la kumakinisha nafasi zao na kuwa ni kambi tangulizi za kimkakati kwa Ndugu zao wa Kikristo katika Ulaya, umbile la Kiyahudi ni kama mbebaji wa ndege za kivita kwa ajili ya Amerika katika eneo hilo hivi leo. Ni moja ya zana zinazotumiwa na Amerika kuimarisha ushawishi wake katika eneo. Kwa kuondoa Himaya ya Makruseda kutoka eneo hilo kama alivyofanya Salahuddin mnamo karne ya 11 ni sawa na kile kinachohitajika hivi leo ili kukikata kifaa hichi kwa uingiliaji wa kigeni katika eneo.

Salahuddin ametuonyesha kuwa kurejesha umoja miongoni mwa Waislamu na kuwaondosha viongozi mawakala kutoka miongoni mwetu na kuikomboa Palestina ndio namna ya kuikomboa ardhi iliobarkiwa, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (swt). Haya yanahitaji kuwa ni kipaumbele na ni kwa namna hii tu ndio tutaweza kumaliza hali tunayoishuhudia leo.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Adnan Khan   

 #Aqsa_calls_armies                                                #AqsaCallsArmies
 #OrdularAksaya                                   #الأقصى_يستصرخ_الجيوش
 #AqsaYawaitaMajeshi

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu