Ijumaa, 20 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari na Maoni

Kanuni za Soko la Pamoja la Afrika Mashariki ni za Uongo

Mnamo Jumatano, 26 Juni 2019, Charles Njagua Kanyi, Mbunge wa Kenya Eneo Bunge la Starehe wa chama tawala cha Jubilee alikamatwa kwa mashtaka ya kuchochea ghasia kutokana na matamshi yake ya ubaguzi wa kitaifa dhidi ya wageni (Watanzania, Waganda, Wapakistani na Wachina) wanao endesha biashara na kutawala masoko ya Nairobi. [Daily Nation]

Maoni:

Matamshi hayo yalisababisha mvutano wa kidiplomasia hususan nchini Tanzania yaliyo pelekea Spika wa Bunge la Tanzania kuiamuru Serikali yake kutoa taarifa. Baadaye, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alisema kuwa serikali hiyo imelichukulia jambo hilo kwa uzito na kumtaka balozi wa Kenya nchini humo kufafanua. Balozi huyo wa Kenya alisema, “Hayo yalikuwa matamshi ya kibinafsi ambayo hayana mahusiano yoyote na msimamo wa Serikali ya Kenya.” Fauka ya hayo, Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Kenya ilitoa taarifa na kusema, “Matamshi ya Mbunge huyo hayakuwa ya busara na yalikuwa ya uchochezi ikitaja kuwa lugha ya uadui na chuki iliyo tumiwa na Bw Njagua iko dhidi ya utamaduni wa ukarimu wa Kenya na vilevile katiba.” Yanayojiri kwa sasa yanajitokeza takriban wiki mbili baada ya Waziri wa Ndani Matiang’i kuagiza kurudishwa makwao Wachina waliopatikana wakiuza nguo za mitumba katika soko la Nairobi la Gikomba. [Daily Nation, 26/6/2019]. Fauka ya hayo, Kiongozi wa Wengi anaye wakilisha serikali tawala ya Jubilee katika Bunge la Kitaifa la Kenya aliliomba Bunge kutathmini mahusiano yake na Tanzania; akisema kuwa Watanzania wanaoishi Kenya wananufaika zaidi ikilinganishwa na Wakenya wanaoishi nchini Tanzania kwa upande wa kazi na biashara. Alitoa mifano ya wataalamu wa Kenya kunyimwa vibali vya kazi, Ng’ombe wa Kenya kupigwa mnada na vifaranga wa kuku wa Kenya kuteketezwa moto miongoni mwa kadhia nyinginezo zinazo tekelezwa na serikali ya Tanzania!

Mvutano huo unathibitisha kuwa kwa hakika kutoaminiana kunaendelea kuongezeka baina ya vibaraka wa dola za kikoloni ambao kila uchao wanasukuma ajenda ya mabwana zao katika eneo la Afrika Mashariki. Kwa mfano, vipaombele vya Kenya viko sambamba na vya Uingereza/Umoja wa Ulaya huku vipaumbele vyaTanzania viko sambamba na Amerika. Hii imepelekea kuganda kwa zile zinazoitwa Kanuni za Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki kuwa dola moja huru. Kanuni hizo zilipasa kupelekea usambaaji huru wa kazi, mtaji, bidhaa na huduma ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Nchi sita wanachama wa EAC zimesimama juu ya msingi wa mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu yake ya utawala ya kidemokrasia. Hivyo basi, kuwepo kwao ni kwa lengo tu la kulinda mipaka ya mabwana zao wa kikoloni waliyo chorewa nao na daima zinaegemea mafungamano ya kihamasa ya utaifa na uzalendo.  Hivyo basi, raia wao wanatazamana kama wageni wasiostahili kufurahia chochote ndani ya mipaka ya mwengine! Kwa yakini, alichofanya Mbunge wa Kenya ndicho kile kile walichofanya wakoloni wa Kimagharibi katika nchi walizo zikoloni kifikra pamoja na kinguvu. Hivyo basi, serikali zote zililazimika kujihusisha na hatua za uokozi wa nyuso na hivyo kuziokoa nyuso za mabwana wao wa Kimagharibi wanao pigia debe matamshi kama hayo ya ubaguzi wa kitaifa kote duniani hususan dhidi ya Waislamu na Uislamu!

Ni muhimu mno kwa kila mmoja anayetaka kuwa na mdahalo wenye natija juu ya ubaguzi wa kitaifa; kwanza kusafisha sumu ya thaqafa ya Kimagharibi na ushawishi wake katika kupigia debe ukoloni moja kwa moja katika karne ya 16 barani Amerika, Asia na Afrika; na hadi leo ukoloni mambo leo kote ulimwenguni. Hatimaye, itatambuliwa kuwa hakika ubaguzi wa kitaifa na misamiati yote inayo husiana nao ni natija ya mfumo wa Kimagharibi wa kisekula wa kirasilimali unao ipa kipaombele thamani ya kimada juu ya thamani nyinginezo! Kinyume chake tunao mfumo safi wa Kiislamu uliojaribiwa kwa takribani karne 14 kuwa ndio mfumo unaounganisha watu pamoja na kutoa fursa nyingi mno kwa wale wote walio ndani ya himaya yake iliyo panuka mabara mengi chini ya Dola ya Kiislamu ya Khilafah.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 09 Agosti 2020 06:20

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu