Jumamosi, 11 Rajab 1446 | 2025/01/11
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Je Malengo ya NEMC Ni Kupiga Marufuku Adhana Zinazotumia Vipaza Sauti?

(Imetafsiriwa)

Habari:

Siku ya Jumatatu tarehe 08/05/2023, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilitangaza kuwa limefunga biashara 89 kwa uchafuzi wa kimazingira wa kelele. Biashara zilizofungwa ni pamoja na baa na vituo vya burudani ambavyo vilipatikana vikitoa kelele zinazozidi viwango vinavyokubalika.

Maoni:

Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilianzishwa mnamo mwaka 1983 ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Stockholm wa mwaka 1972 ulioyataka mataifa yote kuanzisha na kuimarisha mabaraza ya kitaifa ya mazingira ili kushauri serikali na jumuiya ya kimataifa kuhusu masuala ya mazingira. Amma kuhusu uchafuzi wa kimazingira wa kelele, Shirika la Afya Duniani (WHO) linafafanua kuwa wingi wa kelele zaidi ya 65dB huwa ni uchafuzi wa mazingira, na linapendekeza kuwekwa chini ya 65dB wakati wa mchana, na linaonyesha kuwa usingizi wa utulivu hauwezekani kupatikana kwa viwango vya kelele vya usiku vinavyozidi 30dB.

Kwa hivyo, NEMC inaagiza kufanya utekelezaji, uzingatiaji, uhakiki na ufuatiliaji wa shughuli za kimazingira kulingana na miongozo na matakwa ya kilimwengu ya kisekula. Kwa mtazamo huu, na kwa vile mtazamo wa kisekula haujali dini, kelele za vilabu vya usiku, baa na vituo vya burudani vitachukuliwa kuwa sawa na mwito wa swala Msikitini (Adhana). Hivyo, kwa NEMC kupiga marufuku baadhi ya baa na vituo vya burudani na hatua hizo kupanuliwa hadi kwenye nyumba za ibada kuna uwezekano mkubwa wa kufika misikitini kwa lengo la kupiga marufuku adhana ya kutumia vipaza sauti (mwito wa swala). 

Licha ya maagizo ya hivi karibuni ya Waziri wa Nchi, Afisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jaffo, kwamba sehemu za burudani na nyumba za ibada zinatakiwa kutumia vipima kelele na vifyonza sauti, lazima iwe  wazi kuwa mwito wa swala (adhana) haupaswi kulinganishwa na kelele za baa na vituo vya burudani, kwa kuwa adhana ni wajibu wa kiibada katika Uislamu, matukufu muhimu na ishara ya uwepo wa jamii ya Kiislamu mahali husika.

Iwapo NEMC inajali sana ustawi wa watu, ingeweza kupiga marufuku baa na sehemu zote za burudani (munkari) za maovu bila kujali kelele kwa vile zinaeneza kila aina ya maovu katika jamii. Kupiga marufuku baa chache kwa uchafuzi wa kimazingira wa kelele hakutaokoa jamii kutokana na usumbufu au kuleta utulivu wa mfumo wa kijamii. Lakini kwa taswira pana zaidi ukiachana na uchafuzi wa kelele, kuna mambo mengi yasiyofaa yanayofanywa ndani ya baa hizi na vituo vya burudani kama uasherati, ulawiti, matumizi ya dawa za kulevya, ulevi nk ambayo yote ni hatari kwa jamii.

Wakati mataifa ya Magharibi yanasukuma mataifa yanayoendelea katika ajenda ya utunzaji wa mazingira, tumeshuhudia uongo mwingi katika kutekelezaji wake, kwa nini baadhi ya maeneo kama vile kelele za magari, kelele za vyombo vya anga, maeneo ya ujenzi, kelele za umati katika miji nk. hazipewi kipaumbele zaidi ya kulenga nyumba ya ibada? Zaidi ya hayo, kuna unafiki (katika kadhia ya kupambana na yanayoharibu mazingira) mfano kujiondoa kwa Marekani kutoka katika Maafikiano ya Kyoto ya kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa (CO2) na kuwepo kwa gesi chafuzi (GHG) katika angahewa kwa misingi kwamba mkataba huo ungeathiri uchumi wake. Bila shaka ni kwamba kwa vile ajenda ya kukabiliana na matatizo ya kimazingira inasukumwa na mataifa ya kikoloni kwa kuzingatia maslahi ya mataifa hayo, na kwa vile wanaichukulia itikadi ya Uislamu kuwa ni adui wao nambari moja, hapana shaka watatumia kisingizio hicho kuushambulia Uislamu kwa kuhujumu matukufu ya adhana.

Ingawaje hatuungi mkono uchafuzi wa kelele kutoka katika mabaa, vituo vya burudani viovu nk., tunapinga kwa nguvu zote na hatukubaliani na hatua yoyote itakayochukuliwa kuathiri misikiti kwa kupiga marufuku adhana ya kutumia vipaza sauti, hatua hiyo chafu itakabiliwa na upinzani mkali kutoka katika jamii ya Kiislamu kwa vile inapingana na Uislamu.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu