Jumapili, 22 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/24
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Uislamu Pekee ndio Utakaonusuru Wanadamu na Ukandamizaji wa Kodi

(Imetafsiriwa)

Habari:

Mnamo tarehe 4 Oktoba 2024, Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi ilizinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam. Tume hiyo itakuwa na jukumu la kufanya mapitio ya sera zilizopo za kodi na kuainisha maeneo ya marekebisho, kuboresha mfumo wa kodi na kuhimiza watu wote wanaostahiki kulipa kodi kulipa kwa khiyari.

Maoni:

Mfumo wa uchumi wa kibepari hutegemea kodi kandamizi pekee kama chanzo kikuu cha mapato. Katika hali hiyo inatarajiwa serikali daima itabuni na kulazimisha kodi mbalimbali ambazo ni wazi zitakuwa mzigo kwa raia wa kawaida. Serikali za kidemokrasia za kibepari badala ya kufanya bidii kuondoa mzigo wa kodi, zenyewe zihakikisha kila mtu analipa kodi. Rais Samia alisema: “Kila mtu lazima achangie; kila mtu alipe kodi kulingana na uwezo wake ili tufanikiwe zaidi kama taifa. (Daily News, 05/10/2024)

Uzinduzi wa Tume hii ya Rais hautakuwa mwisho wa mzigo wa kodi kwa wananchi wa Tanzania kwa sababu kwa mujibu wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa 2021 mpaka 2026, ongezeko la mapato ya kodi linapaswa kufikia 14.4% ya Pato la Taifa ifikapo 2026. Hata hivyo, kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mwaka 2024, mapato ya kikodi nchini Tanzania yamefikia takribani asilimia 12 ya Pato la Taifa ikiwa na maana kwamba ni chini ya lengo linalotakiwa. Kwa hivyo, kodi zaidi zitabuniwa na kukusanywa kutoka kwa watu ili kufikia lengo lililoainishwa la serikali.

Kwa upande mwingine, Uislamu umekataza serikali (mamlaka) kutoza kodi (maks, inayojumuisha aina zote za kodi chini ya mfumo wa uchumi wa kibepari) kwa watu. Mtume Muhammad (saw) amesema:

«لا يَدْخُلُ الْجَنَّةَ صَاحِبُ مَكْسٍ»

“Hataingia peponi mwenye kuchukua kodi” (sahib masks)” (Ahmad).

Mfumo wa uchumi wa Kiislamu hautegemei kodi, bali kuna vyanzo kadhaa vya kudumu na endelevu vya mapato ya serikali, ambavyo ni kama: Al Fai’, Al Ghanaa’im, Al Anfal, Al Kharaj n.k.

Pia kuna mapato ya mali zinazomilikiwa na Umma pamoja na aina zake mbalimbali, mapato ya mali zinazomilikiwa na serikali kama vile Ushoor, Khumus nk. Vyanzo hivi vya fedha za Bayt al-Mal (hazina ya Serikali) vimekuwa msingi wa mapato katika historia yote vikiipatia serikali zaidi ya mahitaji ya kugharamia majukumu yake yote na ya majukumu ya Umma.

Hata hivyo, kuna hali fulani katika sharia ya Kiislamu ambapo serikali inaruhusiwa kuweka mchango wa dharura (siyo kodi kwa maana ya kodi kama hizi tulizo nazo leo katika mfumo wa kibepari) ambayo inaitwa “adhwaribah”, lakini kuwekwa kwake kuna masharti manne lazima yatimizwe:

1. Kutokuwepo kwa fedha za kutosha ndani ya Bayt al-Mal za kutumia kwa mahitaji kama hayo.

2. Sheria ya Kiislamu iwe imebainisha kwamba matumizi yanayohitajika katika hali hii ni wajibu kwa serikali.

3. Mchango uliowekwa hauzidi kiasi cha matumizi kinachohitajika kwa hitajio hilo.

4. Mchango unawekwa kwa wenye uwezo peke yao.

Hivi ndivyo Uislamu chini ya dola ya Khilafah Rashida utakavyojiweka mbali na kukwapua mali za watu kwa jina la kodi kutokana na kuogopa kuhesabiwa kwa ukali na Muumba kesho Akhera.

وَلاَ تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ وَلاَ تَعْثَوْا فِي الأَرْضِ مُفْسِدِينَ

Wala msiwapunguzie watu vitu vyao, wala msiende katika ardhi kwa kueneza ufisadi.” [Hud: 85]

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu