Jumamosi, 11 Shawwal 1445 | 2024/04/20
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Uhakiki wa Habari 08/10/2022

Vita vya Kiuchumi vya Kiulimwengu vya Biden Vyatumia Mafuta na Mfumko wa Bei

Ushindani mkali kati ya dola kuu za ulimwengu umekuja kuathiri karibu kila sehemu ya maisha. Wiki hii, kibaraka wa Marekani, Saudi Arabia ilipunguza kidogo uzalishaji mafuta ghafi ili kuendeleza bei ya juu ya mafuta. Hii inawasilishwa kama hatua dhidi ya Rais wa Marekani Joe Biden lakini inafahamika vyema kwa wale wenye ufahamu mzuri wa siasa za kimataifa kwamba Mfalme Salman na mwanawe hawachukui hatua isipokuwa kwa mujibu wa sera za Marekani. Kulingana na Washington Post:

Wanauchumi wa Ulaya wana wasiwasi kuhusu hatari kubwa ya kudorora kwa uchumi na Urusi iliyoimarishwa siku ya Alhamisi, baada ya OPEC Plus, muungano wa mataifa yanayozalisha mafuta unaoongozwa na Urusi na Saudi Arabia, ulitangaza kwamba utapunguza uzalishaji wa mafuta kwa mapipa milioni 2 kwa siku.

Mipango ya muungano huo ilisababisha mwitiko mkali kutoka kwa maafisa katika Ikulu ya White House, ambao walikuwa wameushawishi kwa ukali muungano huo kuendelea na uzalishaji katika viwango vya sasa au zaidi.

Ingawa maoni ya awali yalinyamazishwa zaidi katika Muungano wa Ulaya, kupunguzwa kwa uzalishaji kunakuja wakati kambi ya mataifa 27 ikikabiliana na kushuka kwa kasi kwa ukuaji wa uchumi unaohusishwa na bei ya juu ya kawi. Gwiji wa viwanda wa Muungano wa Ulaya, Ujerumani, iliripoti kushuka vibaya zaidi kuliko ilivyotarajiwa kwa oda za utengenezaji siku ya Alhamisi, na kuongeza hofu ya kushuka kwa uchumi.

Simone Tagliapietra, mwandamizi mkuu katika taasisi ya wataalam wa masuala ya kiuchumi yenye makao yake jijini Brussels Bruegel, alisema kupunguza uzalishaji "kutadumisha mfumko wa bei na kusababisha mgogoro wa kawi wa Ulaya kuwa hata mgumu zaidi."

Ikiwa Marekani inataka, inaweza kulazimisha kupunguzwa kwa bei ya mafuta duniani kwa urahisi, lakini Amerika inataka kutumia hata hili katika ushindani wake mkubwa wa nguvu, hata wakati ambapo vita viko mlangoni mwa Ulaya. Hakika, mfumko wa bei wa juu ambao tayari umeregelewa hapa umekuwa ni matokeo ya sera za Marekani. Rais wa Marekani Joe Biden aliingiza ufadhili mwingi katika uchumi wa Amerika mwaka jana wakati wa janga la Uviko ili kuharakisha Amerika kutoka kwa mdororo wake, akijua vyema jinsi mfumko wa bei utakavyokuwa. Kisha mwaka huu, Marekani inapandisha pakubwa viwango vya riba, ili kudhibiti mfumko wa bei yake mwenyewe lakini kwa gharama ya kunyonya mtiririko mkubwa wa fedha kutoka kwengine duniani, ambapo kwa mara nyengine tena inaharibu shughuli zao za kiuchumi. Kwa mujibu wa nakala ya mwezi uliopita katika jarida la Business Insider:

Ulaya inaonekana kuelekea kwenye mdororo wa uchumi - na hasara yake inaweza kuwa faida kwa Marekani kwani inaonekana kuepusha mdororo wake.

Mnamo Agosti, wachambuzi wa Goldman Sachs waliweka uwezekano wa kushuka kwa uchumi katika kipindi cha miezi 12 ijayo kwa 60% kwa Ulaya na 30% kwa Amerika.

Ikiwa utabiri huu utathibitishwa kuwa wa kweli, na Ulaya ikakumbwa na mdororo wa kiuchumi kabla ya Marekani, inaweza kupunguza uwezekano wa Marekani kukumbwa na hatima kama hiyo.

"Marekani, kama nchi yenye uchumi mkubwa zaidi duniani, mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta na gesi asilia, na ikiwa na moja ya maboresho makubwa zaidi, inapaswa kuwa na uwezo wa kukabiliana na dhoruba huko Ulaya," mwanauchumi wa zamani wa Hifadhi ya Amerika Claudia Sahm aliandika katika Chapisho la Septemba. "Hali ngumu yao utapunguza mahitaji yao na kusaidia kupunguza mfumko wetu wa bei."

Nchini Marekani, Hifadhi ya Serikali inaongeza viwango vya riba ili kukabiliana na mfumko wa bei. Kadiri Hazina inavyozidi kwenda ili kuona bei zikiwa za wastani, ndivyo uwezekano wa uchumi kukwepa "mdororo wa ukuaji" unakuwa mkubwa na kukumbwa na mtikisiko chungu zaidi. Inawezekana mdororo wa uchumi barani Ulaya, hata hivyo, unaweza kusaidia Marekani kupunguza mfumko wa bei, kuepuka mdororo wa hali yake ya kiuchumi, na kuokoa mamilioni ya nafasi za kazi za Marekani.

Ushindani kati ya dola kubwa za ulimwengu ni jambo lisiloepukika. Hata hivyo, chini ya Ubepari, ushindani huu unawezekana ukawa uchungu na mkali zaidi kwa wanadamu kuwahi kuujua. Lakini kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (swt), Ummah wa Kiislamu hivi karibuni utasimama na kusimamisha tena Dola ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Mtume (saw) ambayo itaziunganisha ardhi za Waislamu, kukomboa ardhi zao zilizokaliwa kwa mabavu, kutabikisha sharia ya Kiislamu, kuregesha mfumo kamili wa maisha wa Kiislamu, na kubeba ulinganizi wa Uislamu kwa ulimwengu mzima. Dola ya Khilafah karibu tangu kuanzishwa kwake itajiunga na safu za dola kubwa kwa sababu ya ukubwa eneo lake, idadi kubwa ya watu wake, rasilimali nyingi, jiografia isiyo na kifani na mfumo wa kipekee wa Kiislamu. Dola ya Khilafah itafanya kazi ya kukabiliana, kudhibiti na kutuliza dola zengine kubwa za dunia, kuiregesha dunia katika amani na ustawi jumla uliokuwepo katika kipindi cha miaka elfu moja ambayo hapo awali Uislamu ulitawala masuala ya dunia na kuleta maadili ya hali ya juu, thaqafa na hadhara kwa wanadamu wote.

Khamenei Ajibu Maandamano Nchini Iran

Wiki hii, kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, alijibu hadharani maandamano yaliyochochewa na kifo cha msichana mdogo chini ya ulinzi wa polisi na yamesababisha vifo vya makumi ya watu. Kulingana na Aljazeera:

Kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amezilaumu Marekani na Israel kwa maandamano ambayo yameikumba nchi hiyo kwa zaidi ya wiki mbili, akizishutumu nchi hizo kwa kujaribu kuzuia "maendeleo" ya Iran ...

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 83 alisalia kimya juu ya maandamano hayo, ambayo yalizuka baada ya mwanamke wa Kikurdi mwenye umri wa miaka 22, Mahsa Amini, kufariki mwezi uliopita akiwa chini ya ulinzi wa polisi wa maadili wa Iran.

"Ninasema wazi wazi kwamba ghasia hizi na ukosefu huu wa usalama ulikuwa ni mpango wa Marekani na utawala bandia vamizi wa Kizayuni [Israeli] na wale wanaolipwa nao, na baadhi ya Wairani wasaliti walioko ng’ambo waliwasaidia," Khamenei aliwaambia wanafunzi wa waliohitimu katika chuo kikuu cha polisi jijini Tehran.

"Katika ajali iliyotokea, mwanamke mdogo aliaga dunia, jambo ambalo pia lilituumiza, lakini mwitiko wa kifo chake kabla ya uchunguzi [kufanyika] ... wakati baadhi ya watu walikuja kuzifanya barabara kutokuwa salama, kuchoma Quran, kuvua hijab kwa wanawake waliojifinika, na kuchoma misikiti na magari ya watu – haya sio mwitiko wa kawaida, wa kimaumbile,” Khamenei alisema huku akiwa amezungukwa na wakuu wa polisi, jeshi na Askari wa Jeshi la Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Khamenei alitaka kuyafanya zaidi machafuko hayo kuwa kama sehemu ya juhudi za kigeni za kuivuruga Iran, akisema "kisingizio" chengine kingepatikana kuiyumbisha nchi ikiwa sio kifo cha Amini.

Khamenei yuko sahihi kuituhumu Magharibi kwa kupatiliza hali hiyo. Bila shaka, wao daima wako tayari na wepesi kupatiliza fursa ya usumbufu wowote katika nchi za Kiislamu. Msimamo unaodaiwa wa Magharibi wa kutolazimisha kanuni za mavazi wenyewe unajigonga na ni wa kinafiki. Hata hivyo, chimbuko la machafuko ya sasa kwa hakika ni matokeo ya utiifu wa siri wa muda mrefu wa Khamenei na Iran kwa sera za kigeni za Marekani. Dola ya Iran iko katika mizani ya nguzo mbili, serikali ya kiraia na Walinzi wa Mapinduzi au IRGC. Nguzo hizi zote mbili kwa kweli zinafanya kazi kwa mujibu wa sera ya Marekani lakini mara nyingi moja hupendelewa zaidi ya nyingine. Wakati wa vita vikali vya Marekani vya Iraq, Amerika ilipanua dori ya IRGC, ili kusaidia katika kuleta Iraq chini ya udhibiti. Kisha Amerika ikapanua dori yao hadi Syria wakati mapinduzi yalipotokea huko kwani majeshi ya makafiri wakati huo yalikuwa na hofu ya kuingia moja kwa moja katika ardhi za Waislamu. Lakini katika miaka michache iliyopita, kwa kuwa Iraq na Syria zimetulia, Marekani imekuwa ikitaka kupunguza dori ya IRGC. Ili kujibu msukumo juu ya hili kutoka kwa IRGC, serikali ya Iran ilifanya igizo la kuimarisha utekelezaji wa polisi wa mavazi ya wanawake. Hili ndilo lililochochea maandamano ya sasa.

Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (swt), Umma wa Kiislamu hivi karibuni utalipindua tabaka kibaraka la watawala na kisiasa linalotafuta nguvu katika muungano na makafiri.

Mwenyezi Mungu (swt) asema katika Qur’an Tukufu:

(وَلَن یَجْعَلَ اللَّهُ لِلْكَافِرِینَ عَلَى الْمُؤْمِنِینَ سَبِیلًا)

“wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini.” [An-Nisa: 141].

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu