Jumatatu, 06 Rajab 1446 | 2025/01/06
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Msururu wa Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata bin Khalil Abu Rashtah Amiri wa Hizb ut Tahrir

Juu ya Maswali ya Wanaozuru Ukurasa Wake wa "Fiqh" wa Facebook 

Jibu la Swali

Maswali Kuhusu Qiyas

 Kwa: Zahid Talib Naim

Swali:

Assalam Aleykum wa Rahmatullah wa Barakatuh

Shekhe wetu mkubwa, Mwenyezi Mungu azibariki juhudi zenu, aziongoze hatua zenu, akupeni kilicho bora zaidi, akudhalilishieni magumu, na atupe nguvu ya nusra ya dini yake. Hakika Yeye ni Msikizi na Mwenye kujibu dua.

Maudhui: Maswali kuhusu Qiyas

Kwanza kabisa, nisamehe kwa kurefusha, Mwenyezi Mungu awasaidie katika kumtii na aijaaliye subira yenu iwe katika mizani ya matendo yenu mema.

Kwanza: Ilitajwa katika jibu la swali, la tarehe 07/02/2014

(Ama angalizo lako kuhusu kile kilichoelezwa katika kitabu: "Imethubutu umbile la Qiyas kuwa ni dalili ya kisheria kupitia dalili iliyokatikiwa (qat'i), na dalili isiyo ya kukatikiwa (dhanni)", Kwa hivyo kauli yako ina upande uliosahihi, licha ya kuwa dalili hutolewa katika usul na katika fiqh, lakini maana yake huhitilafiana katika upande wa kukatikiwa na kutokatikiwa, na kwa sababu maudhui hapa yanahusu dalili za usul, hivyo basi ni bora kuyafunga juu ya dalili ya kukatikiwa (qat'i) na sio isiyo ya kukatikiwa (dhanni), na kwa hivyo ni bora kuyasahihisha, na tutayasahihisha, Mwenyezi Mungu akipenda.) Mwisho

Marekebisho hayo yametajwa katika toleo jipya la tarehe 16/07/2019 uk. 322 katika sehemu mbili,

Lakini pindi nilipoyamaliza maudhui haya, baadhi ya sentensi zilinipa changamoto ambapo zilitatiza ufahamu wangu, na sikuweza kuzioanisha baina yazo na baina ya yale mapya yaliyokuja kusahihisha nayo ni kama yafuatavyo:

Uk. 323 (Hadithi hizi zote ni dalili kuwa qiyas ni hoja, na upande wake wa hoja ni kwamba Mtume aliambatanisha deni la Mwenyezi Mungu na deni la mwanadamu katika wajibu wa kulilipa na kunufaika nalo, ambapo ndicho kiini cha qiyas.)

Uk. 325 (Matukio haya hayakujulikana kwamba walipatikana walioyakanusha na yalikuwa ni mashuhuri miongoni mwa Maswahaba ingawaje ni katika mambo yanayoweza kukanushwa, kwa hivyo kuyanyamazia kwao na ilhali ni katika yale ambayo hawayanyamazii, ni ijma' miongoni mwao kwamba qiyas ni hoja ya kisheria.)

Uk.326 (Kutokana na hili inakuwa wazi kuwa hadithi, ijma' ya Maswahaba, na maelezo ya Mtume juu ya hukmu nyingi ni dalili kwamba qiyas ni dalili ya kisheria miongoni mwa dalili ambazo zinakuwa ni hoja kwamba hukmu iliyovuliwa kutokana nayo ni hukmu ya kisheria ... na kwa sababu hii dalili hizi haziwi ni hoja juu ya qiyas jumla, bali ni hoja juu ya qiyas ambayo 'illahh (sababu ya kisheria) iliyo ndani yake imepatikana juu yake dalili kutoka kwa Shariah, na hii ndio qiyas inayozingatiwa kuwa ya kisheria.)

Kwa hivyo ikajitokeza kwangu kana kwamba nukta hizi tatu hazioani na kile kilichotajwa hapo awali katika sehemu mbili zilizotajwa hapo juu, Nataraji kutoka kwenu ukarimu kwa kuyaweka wazi yale ambayo yamenitatiza.

Pili: Katika kitabu Bahri al-Muhit cha al-Zarkashi - Mlango wa Qiyas - Sehemu ya tatu katika wajibu kuifanyia kazi Qiyas (Na ya pili yao: Je! Ni maana ya kuisikia ni ya kukatikiwa (qat'i) au isiyo ya kukatikiwa (dhanni)? Ya kwanza wengi wameisema, na ya pili imesemwa na Abu Hussein na al-Aamidi.) Mwisho. Vilevile amesema katika sehemu nyengine (Ya tatu: ni ijma' ya Maswahaba: hakika wao walikubaliana katika kuifanyia kazi Qiyas, na imepokewa kutoka kwao kwa maneno na vitendo. Ibn 'Aqeel al-Hambali amesema: imefikishwa kwa wingi (tawatur) wa maana kutoka kwa Maswahaba utumiaji wake, hivyo imekatikiwa (qat'i).) Mwisho.

Je! Inawezekana kwa dalili dhanni za kusikia zilizofikia kiwango cha wingi (tawatur) wa kimaana kuwa dalili iliyo katikiwa juu ya hoja ya qiyas?

Tatu: Imetajwa katika Kitabu cha Shakhsiya, Juzuu ya Tatu, uk. 323 (Hadithi hizi zote ni dalili kuwa qiyas ni hoja, na upande wake wa hoja ni kwamba Mtume aliambatanisha deni la Mwenyezi Mungu na deni la binadamu katika wajibu wa kulilipa na kunufaika nalo, na hicho ndicho kiini cha qiyas.)

1- Je! Qiyas uliyoifanya Mtume (saw), iliyotajwa katika aya juu ya maana ya kilugha ya kukaribisha picha na kusahilisha fahamu ya msikilizaji, au kuitumia kwa maana ya kiistilahi, na kutabikika juu yake ufafanuzi uliotajwa katika Kitabu cha Shakhsiyya, Juzuu ya Tatu, uk. 321, (Qiyas ilifafanuliwa kuwa ni uthibitisho wa mfano wa hukmu inayojulikana kwa nyengine inayojulikana kwa sababu ya ushiriki wao katika sababu ya kisheria (illah) ya hukumu ile yenye kuthibitisha)?

2- Je! sababu ya kisheria (illah) ya kulipa deni, ambalo kwa umbile lake ni lenye kunufaisha inatoka katika maandiko yaliyofanyiwa qiyas juu yake, kama vile mtu kumlipia deni babake ambaye alikufa naye ni mwenye kuacha kuswali swala zote za faradhi ambazo babake alizipuuza maishani mwake kwa kufanya qiyas ya kulipa hijja kwa sababu ya ushirika wao katika illah (kuwa ni deni),  pamoja na kuzingatia kuwa ibada hazifanyiwi illah (sababu ya kisheria)? 

3- Kwa nini hijja ya mtoto kwa niaba ya babake ambaye hana uwezo wa kuifanya inakadiriwa kuwa ni deni la Mwenyezi Mungu, wakati inajulikana kuwa faradhi hajj inategemea uwezo? 

Nne: Imetajwa katika Kitabu cha Shakhsiya, Juzuu ya Tatu, uk. 336, katika masharti ya furuu' (matagaa) (la nne: ni kwamba hukmu ya matagaa haipaswi kuainishwa, vinginevyo ndani yake muwe na qiyas ya maandiko. Na hakuna hata moja kati yazo iliyo na qiyas kwa nyingine iliyo bora isipokuwa ni kinyume. Na wala haisemwi kwamba kufafananisha dalili juu ya suala moja lenye kupewa dalili inajuzu. Kwa sababu hili linakuwa bila ya qiyas. Kama vile kuthubutu hukmu kupitia Qur’an na Sunnah na ijma ya Maswahaba. Ama kuhusu qiyas hiyo, kile kinachothibitishwa ndani yake ni illah na ukiukaji wake kwa hukmu ya tagaa ndio ambao ulifanya qiyas hiyo iwepo. Endapo kutakuwa na andiko juu ya hukmu ya tagaa basi wakati huo hukmu hiyo itakuwa imethubutu kupitia andiko na sio kwa illah hivyo hakuna nafasi ya qiyas.) mwisho. Vipi qiyas itatoka kwa Mtume (saw), na inajulikana kuwa kila kitu ambacho kimetoka kwake (saw), kinachukuliwa kuwa ni andiko la kisheria ambalo linaloondoa qiyas? Kama alivyoashiria Imam Al-Shawkani maana hii katika kitabu chake, Irshad Al-Fahul, akiwajibu wale wanaozichukulia hadithi hizo kama dalili ya hoja ya qiyas. (jibu ya hilo ni: qiyas zilizopatikana kutoka kwa Al-Shari' asiye na makosa (ma'sum), ambaye Mwenyezi Mungu (swt) anasema kuhusu yale aliyokuja nayo kwetu:

إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوْحَى﴿

"Wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa" [An-Najm: 3-4], Na pia anasema wajibu wa kumfuata:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانْتَهُوا﴿

"Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho" [Al-Hashr: 7] na hilo liko nje ya mahali pa mzozo, kwa sababu qiyas ambayo tunaizungumzia ni ile qiyas ya mtu ambaye haijathubutu kwake kutokuwa na makosa, na uwajibu wa kumfuata, wala maneno yake sio wahyi, bali yanatoka kwa mamlaka ya nafsi yake, na katika akili yake iliyo na uwezo wa kukosea, na tumetangulia kusema kuwa itifaki ilitokea katika kutoa hoja kwa qiyas zilizotoka kwake (saw)) Mwisho.

Tano: Imetajwa katika Kitabu cha Shakhsiya, Juzuu ya Tatu, uk. 335: (Matumizi ya qiyas yanahitaji ufahamu wa kina. Hairuhusiwi kutumia qiyas kuvua hukmu isipokuwa kwa mujtahid, hata kama yeye ni mujtahid wa maswala fulani pekee.) Je! Tunawezaje kunasibisha qiyas kwa Mtume (saw), wakati ambapo haijuzu katika haki yake ya utume (saw), kuwa mujtahid?

Ewe Mwenyezi Mungu tuelimishe yale yanayotunufaisha na utunufaishe kwa yale uliotuelimisha hakika wewe ni Mjuzi Mwingi wa hekima, na dua yetu ya mwisho ni Alhamdulillah rabi al-'Alamin.

Jibu:

Waaleykum Salaam wa Rahmatullah wa Barakatuh

Mwanzo kabisa Mwenyezi Mungu akubariki kwa dua yako njema kwetu, na sisi vilevile tunakuombea kheri…

Hakika yako ewe ndugu yangu umekithirisha maswali yako kwa mpigo mmoja na ilikuwa yatosheleza kuuliza swali moja na pindi tutakapo kujibu ingewezekana kufuatisha na swali jengine sio kwa kutuma maswali saba kwa pamoja… lakini pamoja na hivyo hakika sisi tunaona tuyajibu kwa sababu yanahusiana na vitabu vyetu na thaqafa yetu… lakini siku za mbeleni usitume maswali mengi kwa wakati mmoja, hivyo tuhafifishie Mwenyezi Mungu akurehemu.

1- Kuhusiana na swali lako la kwanza juu ya maswala hayo matatu katika kitabu cha Shakhsiya ya Kiislamu, Juzuu ya Tatu:

Ni kweli kwamba tumefanya marekebisho katika kitabu cha Shakhsiya ya Kiislamu, Juzuu ya Tatu katika mlango wa qiyas, kwa msingi wa yale yaliyokuja katika jibu letu la tarehe 7 Rabi` al-Akhir 1435 Hijria sawia na tarehe 02/07/2014 M ... Lakini tulikuwa makini katika marekebisho hayo kwa kuugawanya mlango huo katika sehemu mbili:

- Sehemu ya kwanza inahusiana na dalili za uthibitisho wa qiyas, kwa hivyo tulilifunga suala hilo kwa dalili iliyokatikiwa (qat'i) na hatukujumuisha ndani yake dalili zisizo za kukatikiwa (dhanni).

- Na sehemu ya pili inahusiana na mwongozo katika qiyas na ubainishaji wa uhalisia wake, na sehemu hii tumetumia ndani yake dalili kutoka kwa Sunnah na Ijma, na hatukulifunga suala hili kwa dalili zilizokatikiwa (qat'i) kwa sababu si katika upande wa kudhibitisha umbile la qiyas kuwa ni dalili ya kisheria, ambapo hilo tulilithibitisha katika sehemu ya kwanza ya mlango huu.

Hakuna shaka kwamba dalili ambazo tumezitumia katika sehemu ya pili ya mlango huu kutoka katika Sunnah na Ijma ni dalili zisizo za kukatikiwa (dhanni) ambazo zinabainisha uhalisi wa qiyas, lakini sio dalili za kukatikiwa (qat'i) juu ya hoja ya qiyas, na hili halidhuru kwa sababu hatukuzitumia kama dalili kwake katika muktadha wa kuthibitisha hoja ya qiyas kama nilivyotaja hapo juu, lakini katika muktadha mwingine, ambao ni mwongozo wa qiyas na ubainifu wa uhalisia wake ... na ili kufafanua jambo hili zaidi, ninakuletea msimamo wa lazima kutoka kwa nakala iliyotangulia kutoka katika kitabu cha Shakhsiya ya Kiislamu, Juzuu ya Tatu kabla ya marekebisho, kisha msimamo uliofuata kutoka kwa nakala mpya baada ya marekebisho:

A- Nakala kabla ya marekebisho: 

(Qiyas ni dalili ya kisheria juu ya hukmu za kisheria, nayo ni hoja ya kuthibitisha kuwa hukmu fulani ni hukmu ya kisheria. Na limethubutu umbile la qiyas kuwa ni dalili ya kisheria kwa dalili ya kukatikiwa na dalili zisizo za kukatikiwa. Ama dalili ya kukatikiwa ni kuwa mahali pa kuzingatia qiyas kuwa ni dalili ya kisheria ni katika hali ambayo hutarajiwa ndani yake qiyas katika andiko hilo hilo, ...

Ama dalili zisizo za kukatikiwa (dhanni), ni dalili vilevile kwamba qiyas hukadiriwa kuwa ni dalili ya kisheria. Na imethubutu qiyas kuwa ni hoja katika upande wa ijma ya Maswahaba,  Imethubu kuwa Mtume (saw) aliotoa mwongozo katika qiyas na akakubali qiyas, kutoka kwa Ibn Abbas...) Mwisho.

 B- Nakala baada ya marekebisho: 

(Qiyas ni dalili ya kisheria juu ya hukmu za kisheria, kwani ni hoja ya kuthibitisha kuwa hukmu fulani ni hukmu ya kisheria. Na imethubutu kuwa qiyas ni dalili ya kisheria kupitia dalili ya kukatikiwa (qat'i) nayo ni kuwa mahali pa kuzingatia qiyas kama dalili ya kisheria ni katika hali ambayo inatarajiwa ndani yake qiyas katika andiko lilo hilo;...

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ametoa mwongozo juu ya qiyas, na akakubali qiyas. kutoka kwa Ibn Abbas...) Mwisho.

Kama ilivyo wazi kutoka kwa marekebisho, sisi katika aya ya kwanza wakati tunathibitisha kuwa qiyas ni hoja ya kiusuli (msingi), tumeifunga kwa dalili ya kukatikiwa (qat'i) wala hatukushughulika na dalili zisizo za kukatikiwa (dhanni) ...  Ama mwanzo wa aya ya pili, ambayo kabla ya marekebisho ilikuwa ikithibitisha kufuata dalili za kuthibitisha qiyas, tumefanya marekebisho kwa njia ambayo inayafanya kuwa maudhui mengine, kando na kuthibitisha kuwa qiyas ni moja katika misingi ya sheria (usul), bali tumeijaalia kuhusiana na mwongozo wa qiyas na kuhusiana na ufafanuzi wa uhalisia wake ... na haya inatosheleza ndani yake dalili zisizo za kukatikiwa (dhanni) ambazo tumezitaja kutoka katika Sunnah na Ijma ... Kwa hivyo hakuna haja ya kurekebisha mambo hayo matatu ambayo yameashiriwa kuwa hayapo katika muktadha wa kuthibitisha qiyas kama moja ya misingi ya sheria (usul). Badala yake, ni katika muktadha mwingine, kama tulivyoeleza awali (mwongozo wa qiyas na ufafanuzi wa uhalisia wake) ...

Labda umechanganyikiwa na hadithi ambazo tumezitaja baada ya hapo ambazo ni dalili ya qiyas, na tukasema: (Hadithi hizi zote ni dalili kwamba qiyas ni hoja, na upande wake wa kuitumia kama hoja ni kwamba Mtume aliambatanisha deni la Mwenyezi Mungu kwa deni la mwanadamu katika wajibu wa kulilipa na kunufaika nalo, ambacho ndicho kiini cha qiyas.) hakuna tatizo hapa, maadamu tumetoa dalili ya kukatikiwa ambayo ndani yake hutumiwa kama hoja juu ya qiyas ... Na sisi tulipofanya marekebisho hayo ilikuwa ni katika mlango wa kuzingatia kwanza kukatikiwa kwa dalili juu ya qiyas na sio kukataa uwepo wa dalili zisizo za kukatikiwa (dhanni) ...

2- Kuhusu swali la pili juu ya kwamba dalili za kusikia ni za upokezi wa walio wengi (Mutawatir) wingi wa kimaana:

Hizi hazitengi kuwa dalili juu ya qiyas ziwe zinatoka kwa Sunnah na kutoka kwa ijma ya Maswahaba. Hazitengi kuwa wingi wake na aina zake tofauti ziwe zimefikia kiwango cha upokezi wa walio wengi wa kimaana kama ilivyotajwa na Imam Al-Zarkashi katika Al-Bahri al-Muhit sambamba na nukuu yako kutoka kwake katika swali lako ... lakini sisi hatuegemei njia hii ya utoaji dalili katika kuthibitisha hoja ya qiyas kwa sababu jambo hili huenda likawa na mzozo wa kiikhtilafu...  na kwa kuwa dalili ya kukatikiwa tulioitaja katika kuthibitisha qiyas ni dalili ya kina iliyokatikiwa inatosha peke yake kuthibitisha hoja ya qiyas na ni vigumu kwa anayekiuka kuipinga… 

3- Kuhusiana na swali lako la tatu, la sita na la saba, yote yanatoka katika mlango mmoja:

Hakika Mtume (saw) alitoa mwongozo wa qiyas na hakufanya qiyas kwa sababu Mtume (saw) anajua hukmu ya kisheria kupitia kwa wahyi na sio kupitia kwa ijtihadi yake, kwa hivyo haiswihi katika haki yake kama mtume kuwa mujtahid kama inavyoonyeshwa katika wadhifa wake ... Mifano ambayo tumeitaja kutoka katika Sunnah nzima ina mwongozo kutoka kwa Mtume (saw) wa qiyas na jinsi ya kuitumia, na hii ni katika mlango wa elimu kwa Waislamu ... lakini haimaanishi kuwa Mtume (saw) alifanya qiyas kwa sababu matunda ya qiyas ni ufikiaji wa hukmu ya kisheria ambayo mujtahid haijui, na Mtume (saw) anajua hukmu ya kisheria kupitia wahyi na hahitaji kufanya qiyas wala ijtihadi ili kujua hukmu ya kisheria. ... Nimeweka wazi jambo hili katika kitabu changu "Taysir al-Wusul ila al-Usul" kwa njia ya ukamilifu katika mzungumzo kuhusu hoja ya qiyas kama ifuatavyo: 

[Mtume (saw) alitoa mwongozo wa kutumia qiyas, yeye (saw) wakati alipoulizwa juu ya kulipa Hijja na juu ya busu la mwenye kufunga, hakumpa hukmu yule aliyeuliza moja kwa moja, bali alimjibu baada ya kupata Illah kamili (sababu ya kisheria) ya kulipa deni la kibinadamu na katika kusukutua, akiwaongoza Waislamu katika matumizi ya qiyas.

(Amesimulia kutoka kwake kwamba mtu mmoja kutoka Khath'am alimuuliza, akasema: Hakika Babangu Uislamu umemfikia akiwa mzee sana, hawezi kupanda kipando cha usafiri, na Hijja ni faradhi juu yake, je, naweza kuhiji kwa niaba yake? Akasema: «أَنْتَ أَكْبَرُ وَلَدِهِ؟» "Je, wewe ndiye mwanawe mkubwa kabisa?" Akasema: Ndio, akasema:

«أَرَأَيْتَ لَوْ كَانَ عَلَى أَبِيكَ دَيْنٌ فَقَضَيْتَهُ عَنْهُ، أَكَانَ ذَلِكَ يُجْزِئُ عَنْهُ؟»

"Waonaje lau Babako angekuwa na deni kisha ukamlipia, je, hilo lingetosha kwake?" Akasema: Ndio, akasema: «فَاحْجُجْ عَنْهُ» "Basi hiji kwa niaba yake").

Kutoka kwa Umar amesema: Nifikwa na hisia siku moja kikambusu (mke wangu) hali mimi nimefunga, nikaja kwa Mtume (saw) nikasema: leo nimefanya jambo kikubwa sana! Nimebusu (mke wangu) hali ya kuwa nimefunga. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw): «أَرَأَيْتَ لَوْ تَمَضْمَضْتَ بِمَاءٍ وَأَنْتَ صائِمٌ؟» "Je! Waonaje kama ungesukutua kwa maji na hali ya kuwa umefunga?" Nikasema: Hakuna ubaya. Akasema (saw) «فَفِيمَ؟» "Basi hapo kuna kosa gani?").

Mbali na kuwa, hukmu hii haimaanishi kuwa Mtume alifanya qiyas, bali ni kwamba yeye (saw) "alipeana hukmu kama wahyi utokao kwa Mwenyezi Mungu uliokuja kwake, kwa njia ambayo inatoa mwongozo katika utumiaji wa qiyas, kwa sababu kila kitu ambacho kimepatikana kutoka kwa Mtume katika kauli, kitendo au kukiri ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama tulivyo bainisha katika mlango wa Sunnah uliotangulia.) Mwisho wa nukuu kutoka kwa kitabu Al-Taysir.

4- Kuhusiana na swali lako la nne kuhusu qiyas ya swala inayodaiwa: 

Qiyas ambayo hadithi zimetoa mwongozo kwake katika maudhui ya hajj ndani yake mna mambo mawili: 

 A- Qiyas ya deni la Mwenyezi Mungu (swt) juu ya deni la mwanadamu katika wajibu wa kulilipa na kunufaika nalo, ikimaanisha kuwa ibada ambayo mtu hakuifanya ni deni lililo katika dhima yake ni lazima ilipwe na kwamba kulipwa kwake ndio huliondoa deni hilo lililo katika dhima yake kikamilifu kama ambavyo ni wajibu kulipa deni la mwanadamu lililo katika dhima na kwamba kulipwa kwake huondoa deni hilo lililo katika dhima ...

B- Kwamba mtu kulipa deni ambalo ni la Mwenyezi Mungu lililo katika dhima yake huondoa deni hili, na vile vile ulipaji wa mwengine (mtoto) deni ambalo ni la Mwenyezi Mungu lililo katika dhima ya mtu huondoa deni hilo kwa mtu huyu pamoja na kuwa yeye siye aliyelilipa deni hilo, na hiyo ni qiyas juu ya deni la kibinadamu ambalo humuondokea mtu kwa kulipiwa na mtu mwengine ... 

Na kwa kutabikisha hilo juu ya maudhui ya swala yanabainika yafuatayo:

- Kwamba swala ambayo mtu anadaiwa ambayo hakuiswali bila udhuru wa kisheria ni lazima ailipe, na pindi mtu anapoilipa yeye mwenyewe basi itamuondokea kwa kulipa huku, na hilo ni kwa qiyas ya deni la mwanadamu ambalo ni lazima lilipwe na anapolilipa humuondokea kwa ulipaji huo, na qiyas hii ni sahihi kwa kuwa inamtambua mdeni... na katika hali ya kawaida, kuondoka kwa deni la Mwenyezi Mungu (swt) kwa kulipa swala haimaanishi kuondoka kwa dhambi kwa mtu huyo kwa sababu ya kuchelewesha swala na kutoswali kwa wakati, bali yamaanisha tu kuondoka kwa deni analodaiwa pekee, ambapo ni kuwa, hahitajiki tena kuitekeleza swala hiyo ambayo anadaiwa kwa sababu tayari ameshailipa ... Hivyo basi maudhui ya dhambi kwa sababu ya kuchelewesha swala kupita wakati wake ni maudhui mengine ...

- Ama kufanya qiyas deni la Mwenyezi Mungu juu ya deni la mwanadamu katika kuondoka kwa deni kwa kupitia ulipaji wa wengine (mtoto) kuhusiana na ulipaji wa mtoto swala kwa niaba ya babake, qiyas hii haimsalimishi mdeni hivyo sio sahihi, na hilo ni kwa sababu katika moja ya masharti ya tagaa linalofanyiwa qiyas (linapaswa kuwa huru kutoka na kutanguliwa na pingamizi wazi zinazo kinzana na lile linaloekewa illah ya qiyas, ili qiyas hiyo iwe yenye manufaa.) Na tagaa hapa, ambalo ni swala, kuna dalili za kumwajibisha mtu kuswali yeye mwenyewe na kwamba haiondoki kwa mtu huyu kwa kufanyiwa na mtu mwengine, na wala haikubali nia wala wakala kama majukumu mengine yote. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

وَأَنْ لَيْسَ لِلْإِنْسَانِ إِلَّا مَا سَعَى﴿

"Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyo yafanya mwenyewe?" [An-Najm: 39].

Shariah anamwajibisha Muislamu kuswali kwa kuketi ikiwa hana uwezo wa kusimama, na kwa kuashiria ishara ikiwa hawezi hayo na haikuruhusu mtu yeyote mwengine kuchukua nafasi yake ndani yake... Na ufahamu wa kuitekeleza katika hali hizi kali za ugonjwa ina maana kwamba hairuhusiwi kwake kufanyiwa na wengine, na kwa hivyo qiyas ya swala juu ya deni la mwanadamu katika upande wa kuondoka kwake kupitia ulipaji wa mtu  mwengine, qiyas hii sio sahihi wala haisimami sawa kwa sababu ya uwepo wa dalili zenye kupinga ambazo zinazuia utendaji wa jukumu hili kwa mtu mwengine isipo yeye mwenyewe, kwa hivyo anatenda kupitia dalili hizo sahihi zenye kupinga na masharti ya qiyas huachwa kama ilivyo thibitishwa katika elimu ya usul...

Wala haisemwi kwamba deni la Mwenyezi Mungu (swt), limeondoka katika Hijja, kufunga, zakat na kadhalika kwa kulipwa na wengine kuwa ni kutokana na qiyas ya deni la mwanadamu, hivyo basi pia kuondoka deni kupitia kulipwa swala na wengine kama qiyas kwa deni la mwanadamu ... haisemwi hivyo kwa sababu kuondoka kwa Hijja, kufunga, zakat ... n.k., kwa kulipwa na wengine hayakuthubutu kupitia qiyas. Badala yake, yamethubutu kupitia andiko juu yake katika hadithi tukufu za Mtume zilizotoa mwongozo wa qiyas, kwa hivyo zikayafunga kwa yale maandiko (nusus) yaliyokuja nayo... na ulipaji wa wengine katika swala haukupatikana katika Sunnah kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) hivyo basi inabaki katika asili yake ambayo ni wajibu wa kuitekeleza na kuilipa mtu yeye mwenyewe na kutokubalika niaba wala wakala ndani yake... maandiko (nusus) yaliyoko katika kuilipa swala yanahusiana na yule ambaye swala imempita na sio wengine, miongoni mwake ni:

 - Amepokea Muslim katika Sahih yake kutoka kwa Abu Huraira kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema,

«مَنْ نَسِيَ الصَّلَاةَ فَلْيُصَلِّهَا إِذَا ذَكَرَهَا فَإِنَّ اللَّهَ قَالَ: ﴿أَقِمْ الصَّلَاةَ لِذِكْرِي﴾».

"Yeyote anayesahau swala basi naaswali pindi tu anapokumbuka kwani hakika Mwenyezi Mungu anasema: 'Simamisheni swala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi'"

- Imepokewa na Ibn Abi Shayba katika Musanif yake kutoka kwa Anas asema: Mtume (saw) amesema:

«مَنْ نَسِيَ صَلَاةً أَوْ نَامَ عَنْهَا فَكَفَّارَتُهُ أَنْ يُصَلِّيَهَا إذَا ذَكَرَهَا».

"Yeyote mwenye kusahau swala au akalala basi kafara yake ni aswali pindi anapokumbuka"

- Na imepokewa na Ad-Daraqutni katika Sunan yake kutoka kwa Bilal asema: tulikuwa pamoja na Mtume (saw) katika safari "akalala mpaka jua likachomoza akamwamrisha Bilal akaadhini kisha akatawadha kisha akaswali rakaa mbili kisha wakaswalI swala ya Fajr."

 Na lililo dhahiri katika nususi hizi ni kwamba zinahusiana na mtu aliyepitwa na swala na halipatikana andiko ambapo inaruhusiwa kwa mwengine kumlipia yeye swala kama mtoto kumlipia babake, na kwa hilo ulipaji unabakia unahusiana na yule tu aliyepitwa na swala kwa wakati wake.

5- Kuhusiana na swali lako: (Na kwa nini huitwa hijja ya mtoto kwa niaba ya babake ambaye hana uwezo wa kuilipa na kuzingatiwa hajj kuwa ni deni la Mwenyezi Mungu wakati inajulikana kuwa faradhi ya hajj inategemea uwezo?

Jibu la hilo ni kwamba tumeelezea katika Shakhsiya juzuu ya tatu katika mlango (lafdhi jumla katika sababu maalum) kwamba ujumla uko katika maudhui ya tukio na swali na sio ujumla katika kila kitu, na tukasema: (Hakika hotuba jumla katika tukio na jibu la swali linahusiana na maudhui ya swali na sio jumla katika kila kitu. Yaani, ni ya jumla kwa maudhui hayo katika tukio hilo na mengine ... na ipasavyo, ujumla ni juu ya maudhui, maudhui ya tukio na swali, kwa hivyo ni maalum kwake na haijumuishi mengine, kwa hivyo maudhui hiyo haiingii katika qaida (msingi) ya tafakuri kwa lafdhi jumla na sio kwa sababu maalum; kwa sababu hiyo sio sababu, yaani sio tukio na silo swali, na kwa kuwa maneno yamepatikana juu yake na sio kwengine. Na ubadilishe swali, na kwa sababu hotuba hiyo imo ndani yake na sio kwa wengine, kwa hivyo ni maalum kwake; kwa sababu lafdhi ya Mtume inahusiana na maudhui ya swali na maudhui ya tukio, , kwa hivyo hukmu hiyo inahusiana na maudhui hayo. Andiko ambalo linazungumziwa kuhusu tukio fulani, na andiko ambalo ni jibu la swali, yanapaswa kufungwa maalum kwa maudhui ya swali au tukio hilo wala haiswihi kuwa jumla kwa kila kitu; kwa sababu swali linarudi katika jibu, na kwa sababu maneno hayo ni juu ya maudhui maalum, hukmu ni lazima ifungwe kwa maudhui hayo, kwa sababu lafdhi ya Mtume ambayo ndani yake ameelezea hukmu ya swali au tukio hilo inahusiana na swali hilo peke yake na tukio hilo peke yake, na haihusiani na kitu chengine chochote kabisa. Kwa hivyo hukmu hiyo inahusiana na maudhui ya swali na maudhui ya tukio hilo, yaani kwa kumwamrisha yule anayeulizwa kwa hilo au yule anayepitikiwa na tukio, na wala haihusiani na kitu chengine, kwa hivyo haijumuishi mengine yasiyokuwa maudhui haya, bali ni maalum kwake ... Ujumla wa lafdhi katika sababu maalum sio ujumla katika kila kitu, bali ni ujumla katika maudhui ambayo hadithi imeyapitia, au swali limeyapitia.)  Hapa, maudhui ambayo yameulizwa juu ya hadithi hiyo ni (Hajj ya mtoto mwenye uwezo kwa niaba ya babake ambaye hana uwezo) na sio mengine, kwa hivyo ujumla wa hajj ya mtoto kwa babake utabakia ikiwa mtoto ana uwezo na baba hana uwezo, basi mtoto atamhijia babake, hata kama hajj sio wajib juu ya baba huyo ambaye hana uwezo, na maswala mengine yasiyokuwa hili, yatalazimu dalili nyingine ...

Tumetangulia nyuma kujibu mithili ya swali kama hili mnamo 04 Rajab 1434 H / 14 Mei 2013 M, na jibu linasomeka kama ifuatavyo:

(... kuhusiana na Hadithi niliyoitaja: kutoka kwa Yusuf bin Zubair, kutoka kwa Abdullah ibn al-Zubayr, alisema: Mtu mmoja alikuja kutoka Khath'am mpaka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema: Hakika babangu ni mtu mzima sana, hawezi kupanda kipando, na faradhi ya Mwenyezi Mungu ya Hajj imemkuta, Je! Inaruhusiwa kumfanyia Hajj kwa niaba yake? Akasema:

  «آنْتَ أَكْبَرُ وَلَدِهِ؟» "Je! Wewe ndiye mwanawe mkubwa kabisa?" Akasema: Ndio, akasema: «أَرَأَيْتَ لَوْ كَانَ عَلَيْهِ دَيْنٌ أَكُنْتَ تَقْضِيهِ؟» "Je! Waonaje lau alikuwa na deni, je! Ungelilipa?" Akasema: Ndio, Akasema: «فَحُجَّ عَنْهُ» "Basi mhijie"

Imepokewa na Al-Nasa’i, na Yusuf bin Al-Zubayr akalichagua neno "Wewe ndiye mwanawe mkubwa kabisa", Kwa hivyo, baadhi ya wahakikishaji wakasema maneno juu yake kwa sababu ya jambo hili. Ama kilicho bakia katika hadithi ni sahihi kulingana na wahakikishaji wengi, na wapo walioisahihisha hata kwa lafdhi "mwanawe mkubwa kabisa". Lakini pamoja na hivyo, hadithi hii ilisimuliwa bila ya kutajwa "mwanawe mkubwa kabisa" kutoka kwa Ibn Abbas:

Amepokea Ibn Hibban katika Sahih yake kutoka kwa Suleiman bin Yasar amesema: Abdullah bin Abbas alinihadithia, kwamba mtu mmoja alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Hakika babangu ameingia katika Uislamu ilhali yeye ni mtu mzima sana, na iwapo nitamkazania katika safari yangu, nahofia nisije nikamuua, na iwapo sitamkazania, hata simama kidete juu yake, je naweza kumhijia? Akasema: «أَرَأَيْتَ لَوَ كَانَ عَلَى أَبِيكَ دَيْنٌ فَقَضَيْتَهُ عَنْهُ أَكَانَ يُجْزِئُ عَنْهُ؟» "Je, wanaonaje lau babako angekuwa na deni kisha ukamlipia je, ingeruhusiwa kwake?" akasema: ndio, akasema: «فَاحْجُجْ عَنْ أَبِيكَ» "Basi mhijie babako".

Wanachuoni wa fiqh wamezungumza kuhusu hadithi hiyo wakizingatia kwamba Mwenyezi Mungu (swt) alifaradhisha Hajj kwa kuiambatanisha na kuweza.

وَلِلَّهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلاً﴿

"Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea." [Aali-Imran: 97] Baadhi ya wanachuoni wa fiqh wameijaalia hadith ya mtu mzima sana kuwa ni maalum kwa mtu huyo aliyeuliza pekee na sio kwa wengine ili hadithi hii isigongane na kuweza ambako kumetajwa na aya. Na katika hali nyingine zisizokuwa hii, mtoto halazimiki kufanya Hajj kwa niaba ya babake ambaye hana uwezo isipokuwa kwa mlango wa kuwaheshimu wazazi, ikizingatiwa kuwa hukmu hii ni maalum kwa yule anayeuliza, kama vile hukmu maalum juu ya Abu Barda kuhusu kichinjo (udh'hiya) mbuzi aina ya al-jadha', ambayo imepokewa na Al-Bukhari kutoka kwa Al-Bara 'Ibn Azib, (ra) Alisema ... Abu Burda Ibn Nayyar alisema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika sisi tuna mbuzi aina ya al-Jadha' naye nampenda kuliko mbuzi wawili, je, itaruhusiwa kwangu?" Akasema:

«نَعَمْ وَلَنْ تَجْزِيَ عَنْ أَحَدٍ بَعْدَكَ»

"Ndio, na kamwe haitaruhusiwa kwa mwengine baada yako." Na Al-Jadha' ni miongoni mwa mbuzi ambaye haruhusiwi kuchinjwa kama udh'hiya, lakini ni maalum kwa Abu Barda.

Rai niionayo kuwa yenye nguvu zaidi ni kuunganisha baina ya hadithi na aya kabla ya kwenda kwa ukhasisishaji kwa sababu asili ni kwamba hukmu huwahutubia watu, na hakuna hata moja kati yao inayotumiwa katika ukhasisishaji isipokuwa kunapo patikana andiko katika hilo, mithili ya kisa cha Abu Barda, na maneno ya Mtume (saw) kwake

 «نَعَمْ وَلَنْ تَجْزِيَ عَنْ أَحَدٍ بَعْدَكَ» "Ndio, na haitaruhusiwa kwa mtu mwengine baada yako." Na isipokuwa kunapopatikana udhuru wa kuchanganya ... na hapa hakujapatikana andiko lenye kukhasisisha, na vivyo hivyo hakuna udhuru wa kutochanganya, kwa hivyo inawezekana kuchanganya aya na hadithi kwa sababu Hajj sio lazima isipokuwa kunapokuwa na uwezo wa mali na mwili, na hufanywa takhsisi katika hilo hali ya mtoto pamoja na babake, ikiwa mtoto ana uwezo na baba hana, basi lazima mtoto kufanya Hajj kwa niaba ya babake kwa sababu Mtume (saw) alichukulia Hajj kwa niaba ya baba katika hali hii kama deni ambalo mtoto anapaswa kulilipa kwa niaba ya babake ...) Mwisho wa nukuu kutoka kwa jibu la swali lililotangulia, ikimaanisha kuwa hadithi hiyo sio maalum kwa mtu aliyeuliza peke yake, bali ni ya jumla, lakini ndani ya maudhui ya swali hilo pekee  yaani, katika hali ya (mtoto mwenye uwezo hufanya Hajj kwa niaba ya baba asiye na uwezo) ... Hii ndio ninayoipa uzito katika suala hili, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi  Zaidi na Mwingi wa Hekima. 

Nataraji majibu haya yaliyoko juu yameondoa mkanganyiko wowote katika ufahamu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Ndugu yenu,

Ata bin Khalil Abu Rashtah

 14 Safar Al-Khair 1442 H

Sawia na 01/10/2020 M

Link ya jibu hili katika ukurasa wa Amiri (Mwenyezi Mungu amuhifadhi) wa Facebook

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu