Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali:

Kuswali Swala ya Ijumaa katika Uga wa Msikiti Uliofungwa na Mamlaka

Kwa: Mohammed Amin Al-Jadidi
(Imetafsiriwa)

Swali:

Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Baadhi ya Mashababu na watu nchini Tunisia waliswali swala ya Ijumaa mbele ya misikiti baada ya kufungwa na mamlaka. Baadhi ya maimamu waliwakana na wakazichukulia swala zao kuwa batili, ikizingatiwa kuwa swala za Ijumaa huswaliwa ndani ya msikiti pekee.

Tunatumai kuwa utatuongoza kwa hukmu ya Sharia katika hali kama hiyo, na kile ambacho watu wa nchi lazima wakifanye ikiwa misikiti yao itaendelea kufungwa.

Mwenyezi Mungu akubariki na akulipe kwa juhudi zako.

Jibu:

Wa Alaikum Assalam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Swala ya Ijumaa (Jumu'ah) inaruhusiwa ndani ya msikiti na katika uwanja wa umma, na ikiwa hizo mbili zinapatikana, yaani ikiwa msikiti uko wazi na sio mdogo kwa wenye kuabudu, basi swala ya Ijumaa inapaswa kuswaliwa ndani yake na ikiwa msikiti sio mkubwa wa kuwatosha wenye kuabudu, basi swala inaweza kufanywa mahali pa wazi, lakini jambo muhimu katika yote hayo ni kwamba mahali hapo pasiwe ni nafasi ya kibinafsi; yaani swala ya Ijumaa hairuhusiwi katika nyumba; badala yake, ni lazima iwe ndani ya msikiti au nafasi ya wazi ili mtu yeyote asizuiliwe kuingia ndani kuswali. Lakini ikiwa misikiti imefungwa, basi kuswali katika eneo la wazi ni sahihi na hakuna chochote ndani yake, na anayeizuia anatenda dhambi, na tayari tumeshatoa kuhusu hilo, na kutokana na yale tuliyoyatoa:

1- Mnamo 18 Shaaban 1441 H - 11/4/2020 M: (... na dola itabeba mzigo wa madhambi kwa kuzuia swala ya Ijumaa kuswaliwa misikitini au uwanjani, kwa sababu nususi zimefafanua jambo hili, na hili linafahamika katika maneno ya Mwenyezi Mungu:

]يَا أيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِنْ يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَى ذِكْرِ اللَّهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ذَلِكُمْ خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ تَعْلَمُونَ[

“Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara. Hayo ni bora kwenu, lau kama mnajua.” [Al-Jumu’a: 9]. Muislamu anastahiki kuswali bila ya kuzuiwa

فَاسْعَوْا إِلَى ذِكْرِ اللَّهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ[

“nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara.” [Al-Jumu’a: 9].

Kuiendea swala hii ni wajib kwa sababu imehusishwa na kuacha jambo la mubah… na dola inayofunga misikiti itabeba dhambi kubwa kama tulivyotaja katika Jibu hilo la Swali.)

2- Hili limefafanuliwa kwa kina katika Kitabu cha Hukmu za Swala (Ahkam As-Swalah) kilichotolewa na Hizb, na kinasema:

[Swala ya Ijumaa ni sahihi katika mji, kijiji, msikiti, na majengo ya nchi na nafasi yake:

- Hii ni kwa sababu Mtume aliswali Ijumaa mjini Madina; imesimuliwa kutoka kwa Ibn Abbas (ra) kwamba alisema: "Swala ya kwanza ya Ijumaa ambayo iliswaliwa baada ya swala ya Ijumaa iliyo swaliwa kwenye msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu  ilifanyika katika msikiti wa kabila la Abdul Qais huko Jawathi nchini Bahrain.” na Jawathi ni kijiji cha Bahrain. Abu Huraira alisimulia: "Alimwandikia Umar akimuuliza juu ya swala ya Ijumaa huko Bahrain na yeye alikuwa 'Amil (gavana) wake juu yake, kwa hivyo Umar alimwandikia kwamba swali swala ya Jumu'ah mahali ulipokuwa".  Ama kuhusu yale yaliyosimuliwa kutoka kwa Mtume (saw), kwamba alisema: "Hakutakuwa na swala ya Ijumaa (Jumu'ah) na hakuna swala kwa Siku ya Tashreeq isipokuwa katika mji mkuu (misr)." hadith hii haijathibitishwa, Ahmad amesema hii si Hadith.

- Ama kuhusu kuiswali katika nafasi ya wazi, hakuna andiko la kusema kwamba ni sharti, na swala ya Ijumaa ni kama swala yoyote nyengine inayotakiwa kuswaliwa. ikiwa kuna sharti ndani yake kwa kitu chengine kando na hukmu jumla kinachohitaji kufanywa, basi lazima kuwe na andiko lenye kutoa hilo.

- Inaruhusiwa kuswali swala kadhaa za Ijumaa katika mji mmoja. Ikiwa mji huo ni mkubwa, inaruhusiwa kuswali swala za Ijumaa ndani yake katika misikiti kadhaa, bila kujali ikiwa kuna haja au la, kwa sababu hakuna andiko kuhusiana na kukataza swala kadhaa za Ijumaa na hakuna andiko kuhusiana na hitaji au la, kwa hivyo andiko lisilokuwa na kizuizi (Mutlaq) linabakia bila ya kizuizi. Ama ukweli kwamba Mtume (saw) hakuswali swala ya Ijumaa isipokuwa katika msikiti mmoja, hii haiashirii kuwa hairuhusiwi kuswali swala ya Ijumaa katika msikiti zaidi ya mmoja, kwa sababu ikiwa Mtume (saw) hakufanya jambo, hii haiashirii kuwa kitendo chake ni marufuku. Badala yake, alikuwa na msikiti mmoja ambamo aliswali, na hii haiashirii kwamba hakutaka kuswali katika msikiti zaidi ya mmoja.] Mwisho.

3- Katika kitabu: Al-Fiqh 'Ala al-Madhahib al-Arba (Fiqh ya Kiislamu kwa Mujibu wa Madhehebu Manne ya Kisunni) cha Abdul Rahman al-Jaziri (aliyefariki: 1360 H) kinasema:

] … Je! Swala ya Ijumaa ni sahihi katika uwanja wa wazi? Maimamu watatu walikubaliana juu ya ruhusa ya kuswali swala ya Ijumaa katika uwanja wa wazi; lakini, Malik hushikilia kuwa sio sahihi:

- WanaMaliki wamesema: swala ya Ijumaa kwa jamaa ni sio sahihi katika nyumba za watu wala nje; badala yake, lazima iswaliwe msikitini:

- WanaHanbali wamesema: swala ya Ijumaa kwa jamaa ni sahihi ikiwa itafanywa nje maadamu eneo ambalo inaswaliwa liko karibu na (jengo la) msikiti, na ukaribu huzingatiwa kulingana na viwango vinavyokubalika kwa kawaida. Ikiwa haliko karibu basi swala hiyo ni batili. Kwa kuongezea, ikiwa imamu anaongoza swala ya Ijumaa jangwani, lazima amteue mtu mwengine kuongoza swala msikitini kwa wale walio dhaifu sana kutoka.

- WanaShaf'i wamesema: Ijumaa ni sahihi nje ikiwa eneo liko karibu na msikiti, ambapo "karibu" hufafanuliwa kama hatokuwa mbali zaidi na msikiti kuliko hatua ambayo, ikiwa msafiri angeifikia, bado hangeruhusiwa kufupisha swala zake.

- WanaHanafi wamesema: Sio lazima kwamba swala ya Ijumaa iswaliwe msikitini ili iwe sahihi; badala yake, inaweza kuswaliwa nje maadamu eneo hilo haliko mbali zaidi ya Farsakh moja (kipimo cha umbali) kutoka mjini na kwamba imam anatoa idhini ya iswaliwe huko, kama walivyo eleza masharti yanayohusiana na Swala ya Ijumaa.)

4- Hitimisho ni:

a- Kama unavyoona, Imam Malik anasema kwamba lazima iswaliwe msikitini, na kwa hivyo, kufungwa kwa misikiti na mtawala husababisha kusitishwa kwa swala ya Ijumaa, na Ummah unapaswa kusimama mbele ya mtawala ikiwa anazuia kuswaliwa msikitini.

b- Ama Fuqaha ’(wanachuoni wa fiqh) wengine, haswa wale wa Madhehebu hayo, wanaruhusu katika msikiti na katika uwanja wa umma.

c- Ama yale tunayopendelea sisi, ni yale tuliyoelezea hapo juu: (Swala ya Ijumaa (Jumu'ah) inaruhusiwa ndani ya msikiti na katika uwanja wa umma, na ikiwa hizo mbili zinapatikana, yaani ikiwa msikiti uko wazi na sio mdogo kwa wenye kuabudu, basi swala ya Ijumaa inapaswa kuswaliwa ndani yake na ikiwa msikiti sio mkubwa wa kuwatosha wenye kuabudu, basi swala inaweza kufanywa mahali pa wazi, lakini jambo muhimu katika yote hayo ni kwamba mahali hapo pasiwe ni nafasi ya kibinafsi; yaani swala ya Ijumaa hairuhusiwi katika nyumba; badala yake, ni lazima iwe ndani ya msikiti au nafasi ya wazi ili mtu yeyote asizuiliwe kuingia ndani kuswali. Lakini ikiwa misikiti imefungwa, basi kuswali katika eneo la wazi ni sahihi na hakuna chochote ndani yake, na anayeizuia anatenda dhambi).

d- Kwa msingi wa hayo, swala yenu katika uwanja wa msikiti ni sahihi na serikali imetenda dhambi mara mbili: la kwanza ni kwamba imefunga msikiti, na la pili ni kwamba ilijaribu kuzuia swala katika uwanja wa msikiti ... na tunamuomba Mwenyezi Mungu (swt) kuharakisha kusimama kwa Khilafah, ili Waislamu watekeleze swala hiyo kwa njia yake sahihi.

]وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ وَذَلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ]

“Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu, na washike Sala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Dini madhubuti.” [Al-Bayyinah: 5[.

Ndugu yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

22 Jumada al-Awwal 1442 H

06/01/2021 M

Link ya jibu hili kutoka kwa ukurasa wa Amiri wa Facebook.

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumatano, 13 Januari 2021 15:57

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu