Ijumaa, 25 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/27
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Amiri wa Hizb ut Tahrir "Juu ya Maswali ya Wanaozuru Ukurasa Wake wa Facebook wa "Kifiqhi"

Jibu la Swali

Kuamiliana na Benki za Kiislamu

Kwa: Abdulkarim Zaid

(Imetafsiriwa)

Swali:

Assalamu Alaikum wa Rahamtullahi wa Barakaatuh.

Je, benki za Kiislamu hufanya kazi kulingana na sheria za Kiislamu mjini Tulkarm, na mikoa ya Ukingoni wa Magharibi?

Je, Yafaa Kuweka Pesa Kwenye Hizo Benki? Ama Hizo Benki Ni Majina Tu Ya Kuzibia Kazi Za Riba? Na Hayo Tutahakikisha Vipi?

Jibu:

Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Kwanza: Tulishawahi kujibu mfano wa hili swali zaidi ya mara moja. Mnamo 20/8/2010, na 5/3/2011… na nitarudia yaliyo lazima kuhusiana na swali lako kutokana na hayo majibu:

[ Kwa hakika, mikataba katika Uislamu sio ya kutatiana, wala sio kwamba haijulikani bali ni mepesi na inajulikana, na imebainishwa katika sheria kwa uwazi kabisa:

1- Muuzaji wa bidhaa yoyote, anapaswa awe anaimiliki, kisha aionyeshe kwa ajili ya kuuza, na mnunuaji naye aione, halafu akiikubali basi mkataba umetimia, na kama si hivyo basi mwenye bidhaa abaki na bidhaa yake. Na haiswihi na haifai katika Uislamu, mtu kuuza bidhaa isiyoimilikiwa na muuzaji. Na miongoni mwa dalili juu ya hilo:

Imepokewa kutoka kwa Hakim bin Hizam akisema:

«قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ يَأْتِينِي الرَّجُلُ يَسْأَلُنِي الْبَيْعَ لَيْسَ عِنْدِي مَا أَبِيعُهُ مِنْهُ، ثُمَّ أَبِيعُهُ مِنْ السُّوقِ»

فَقَالَ: «لَا تَبِعْ مَا لَيْسَ عِنْدَكَ»

Nilisema: "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, huwa najiwa na mtu akitaka nimuuzie kitu hali ya kuwa sina cha kumuuzia. Kisha namnunua kutoka sokoni. Akasema: usiuze kitu usicho kuwa nacho" (Imepokewa na Ahmad).

Na imepokewa kutoka kwa Amr bin Shuaib, kutoka kwa babake, kutoka kwa babu yake, amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):

«لَا يَحِلُّ سَلَفٌ وَبَيْعٌ، وَلَا شَرْطَانِ فِي بَيْعٍ، وَلَا رِبْحُ مَا لَمْ تَضْمَنْ، وَلَا بَيْعُ مَا لَيْسَ عِنْدَكَ»

“Si halali mauzo ya mbeleni (salaf) na mauzo ya hapo kwa hapo (ba'i), wala (si halali) sharti mbili ndani ya mkataba mmoja wa mauzo. Wala (si halali) faida ya ambacho hujakidhamini. Wala (si halali) kuuza kitu usichokuwa nacho” (Imepokewa na Abu Daud).

2- Na mfano wa hayo, ni akiwa Khalifah atataka kuwagawia watu mali ya Ummah, au kuwagawia chakula kutokana na mali ya serikali, na kila mmoja akajua fungu lake, hapo haifai kwake kuuza funga lake kwa kutanguliza kabla ya kulipokea kutoka kwa serikali.

Na hiyo ndio hali waliyokuwa nayo Maswahaba wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (saw).

Imepokewa na Malik, kutoka kwa Naafi, kwamba Hakim bin Hizam aliuza chakula ambacho alikitoa Umar ibn Khatwab na kuwapa watu kabla ya (Hakim) kukipokea. Hilo likamfikia Umar ibn Khatwab akamkosoa, na akamwambia: “Usiuze chakula ulichonunua hadi ukipokee”.

Na amepokea tena Malik kwamba ilimfikia kuwa misaada kutokana na chakula cha huko Jaar kilitoka kwa ajili ya watu, zama za Marwaan ibn al-Hakam. Watu wakaanza kuuziana hiyo misaada kabla hawajaipokea. Akaingia Zaid bin Thaabit na mtu mwengine kati ya Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) wakaingia kwa Marwaan ibn al-Hakam wakamwambia: “Ewe Marwaan wahalalisha kuuza riba?! Akajibu: "Najikinga kwa Mwenyezi Mungu (nimehalalisha) kivipi?" Wakasema: "Hii misaada, watu wanauziana hata kabla hawajaipokea! Basi, Marwaan akatuma walinzi waifuate na kuwanyang`anya watu mikononi, na kuwarudishia wenyewe”.

3- Lakini imedhihiri katika miji ya Waislamu taasisi zinazofanyia hila sheria na kujiita “za Kiislamu”. Mfano benki zinazoitwa “za Kiislamu”, zinaamiliana kwa riba, lakini sio kwa njia za riba kama zinavyofanya benki zingine bali zinafuata njia zingine zilizoharamishwa:

a- Pindi unapoenda kwa benki za kawaida ukitaka mkopo, basi benki itakupa mkopo kwa faida maalum ya riba. Na unapoenda kwa benki inayoitwa “ya Kiislamu” na ukataka mkopo, basi haitokupa bila ya ziada, kwa sababu hiyo ni benki wala sio taasisi inayosaidia watu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Nayo yataka ziada, lakini sio kwa uwazi kama zinavyofanya benki za kawaida, kwa kuwa jina lake ni la Kiislamu! Kwa hiyo haitaki kuamiliana kwa riba iliyo haramu, uharamu ambao unajulikana na hata watu wa kawaida. Lakini itakwambia: kwa nini wataka mkopo? Utasema: ili ninunue gari, au bidhaa fulani… na similiki thamani yake. Benki itakwambia: vizuri! sisi tutakununulia, na tutalipa thamani yake taslimu, na tutakuuzia kwa malipo ya polepole kwa ziada fulani… na itapitisha makubaliano nawe kabla ya benki kununua yaani, mauzo kati ya benki na wewe kulipa polepole yamepitishwa na mkataba umetimia na tayari imekuwa lazima hata ya benki kununua bidhaa. Hivyo basi unalazimika kuichukua hiyo bidhaa baada ya benki kununua! Ikiwa na maana, mkataba wa mauzo umepita kabla ya benki kumiliki bidhaa. Wewe hukuinunua baada ya benki kuimilki na kukuonyesha ili ukubali au ukatae, bali hapa huwezi kukataa kwa sababu, kimsingi benki ilikununulia wewe na wala si yao. Hivyo, hii ni kuuza usichokimiliki, na hilo halifai kisheria…lau hiyo benki ina mahala pa maonyesho ya magari ambayo wanayamiliki, na wanayaonyesha kwa watu na kuwauzia watakao kwa malipo ya polepole, basi hayo mauzo yangekuwa sahihi. Lakini, benki sio mfanyibiashara kwa maana inayojulikana bali ni benki inayotaka faida kwa mali wanazotoa. Sasa badala ya wao kuchukua ziada ya riba isiyoendana na jina lake la kuwa benki ya “Kiislamu” wanaipata hiyo riba na zaidi yake kupitia muamala usiokuwa wa kisheria, ambao ni: kuuza usichomiliki, ambao ni muamala haramu katika Uislamu!.

b- Wao huita ni “murabaha” lakini sio hivyo kwa sababu, murabaha kisheria: ni uwe wamiliki bidhaa, na uionyeshe kwa ajili ya kuuza, aje anayetaka kununua na muelewane bei, wamuambia nipe faida kadhaa juu ya bei niliyonunua nayo hii bidhaa, basi naye akubali, baada ya kumjulisha bei uliyogharamika kununua nayo hiyo bidhaa, naye pia apate utulivu kwa hilo. Halafu akulipe hiyo bei na faida mliyokubaliana. Na kama unavyoona, hapa muuzaji anamiliki bidhaa pale alipoionyesha kwa mnunuzi. Na  ni wazi hivi sivyo yanavyoamiliana mabenki yaitwayo ya Kiislamu ama taasisi zinazofanana nayo!.

c- Wakati mwengine huita ni “ahadi” wala si “mauzo”. Na hii pia ni “mughalatwa” (ujanja tu wa kucheza na maneno) na ni kauli isio sahihi. Kwa sababu, ahadi au kuahidiana hailazimishi, lakini katika kuamiliana na benki yalazimisha. Kwa kuwa makubaliano yamepitishwa hata kabla benki haijamilki bidhaa. Kwa hiyo, mtu hawezi kuiambia benki: sitaki tena kununua, baada ya benki kumiliki gari. Hilo haliwezekani katika kuamiliana na benki, kwa sababu mkataba ushapita kabla ya wao kununua gari, hivyo huwa yalazimisha na sio ahadi. Ama ahadi ya kuuza au kununua: huwa kikawaida hailazimishi.

Hakika ahadi ya kununua hailazimishi bali kinacho lazimisha ni mkataba kwa ijab na qabul tu. Na hapo mkataba umeshakamilika kati ya mtu na benki kabla benki haijailiki gari. Kwa hiyo, kilichotimia kati yao ni: mkataba wa mauzo unaomlazimisha mtu. Hivyo, biashara kivitendo ishamalizika kati ya benki na mtu kabla benki haijamiliki gari. Kwa dalili kwamba benki inapomiliki ile gari basi mtu hawezi tena kukataa kununua, na hilo ni kinyume kabisa na hukmu za kisheria ambazo zimebainisha wazi biashara katika Uislamu.

d- Na mara nyingine huita kwamba ni “kununua” na sio mauzo, na kwamba yule mtu ndiye aliyeamrisha kununua, kwa kuiambia benki: ninunulieni gari... hii nayo pia maneno mengine ya makosa. Kwa sababu, huu muamala kwa sifa hii ni “uwakilishi”. Yaani: mtu ndiye ameiwakilisha benki imnunulie gari kwa kiasi fulani cha pesa, naye atailipa benki kiasi fulani kwa sababu ya uwakilishi wao... lakini kinachofanyika si hivyo! Kwa sababu, gari litasajiliwa kwa jina la benki kwa kuwa ndio walionunua gari kutoka kwenye maonyesho ya magari, nayo (benki) yamuuzia mtu kwa malipo ya polepole. Na itabakia imesajiliwa kwa jina la benki hadi pale mtu atakapokamilisha kulipa thamani yake inayoitwa malipo ya polepole. Kwa hiyo, haisajiliwi kwa jina la yule mtu, na benki kuwa muwakilishi wake katika kununua kwa malipo maalumu. Bali hivyo sivyo kabisa... kwa hiyo, hiyo sio “uwakilishi” kwa pande zote. Na lau yule mtu angekuwa ana uwezo wa kimali na ataka kuiwakilisha benki imnunulie gari kwa malipo kadhaa... angekuwa na huo uwezo asingeiendea benki. Bali angeenda kwa aliye bora na mwenye uzoefu zaidi wa kununua na mwenye gharama hafifu kuliko benki!...

Kwa hiyo, hicho wanachokiita “mauzo” kwa hali hii hakikubaliki.

Na kwa ufupi: huu muamala hauruhusiwi kisheria.

Na kwa hakika nimefurahishwa na maoni ya mmoja wao kuhusiana na benki za Kiislamu aliposema: “Hakika benki za kawaida huvuta mali za watu ambao hawajali kuamiliana kwa riba, na hubakia wale watu wenye kujifunga na dini, ambao hawaamiliani kwa riba, hivyo mali zao hubakia nje ya benki za kawaida. Kwa hiyo, benki zinazoitwa “za Kiislamu” zikawa ndio za kuwinda mali za watu wenye kujifunga na dini, hizi benki zikapatiliza kwa njia za miamala mingine isiyokuwa ya riba inayojulikana uharamu wake hata kwa watu kawaida. Wanazipatiliza mali zao kwa miamala isiyo ya kisheria, lakini inakuwa rahisi kuwakinaisha watu wa kawaida kwamba ni katika sheria. Kama vile: kutafuta jina katika (misamiati ya) kisheria kama neno “murabaha” kwa mfano... nalo ni neno lisilokuwa wazi kama riba, bali huenda wengi katika wajifungao na dini hawalijui na hudhani kua yafaa ] Mwisho wa nukuu.

Pili: Ama swali lako kuhusu kuweka pesa kama amana kwenye hizi benki... tushawahi kujibu swali kama hili mnamo 14/10/2012 na hii ndio kama ilivyo:

[ Kinachopelekea kwenye jambo la haramu pia huwa ni haramu. Ndio hii hutumika kwenye kila kitendo, ni sawa iwe ni kitendo cha mtu binafsi anachofanya mwenyewe kwa upande mmoja, ama kiwe kutoka kwa pande mbili, yaani ... mkataba kati ya mikataba. Tofauti pekee ni kwamba, wakati unapofanya kinachopeleka kwenye haramu basi wewe utawajibikia hiyo haramu. Ama unapokuwa wewe ni sehemu katika mkataba, basi uharamu itakuwa tu kwa ule upande ambao ndio uliotumia njia inayopeleka kwenye haramu. Na ikiwa pande zote zimefuata hiyo njia basi madhambi yatakuwa juu yao wote.

Na wewe kuweka amana, yaani akaunti endelevu (current account) isiyo na faida ya riba kwenye benki, basi utakapokuwa na dhana ya nguvu kwamba benki itatumia pesa zako katika riba, hapo haitofaa kuweka amana (current account) kwenye benki. Ila benki hutafautisha kati ya amana za faida ya riba na zile ambazo ni akaunti endelevu (current account) bila faida ya riba. Ama hiyo ya kwanza ambayo huwekwa amana kwa faida hutumiwa katika riba na hilo halina shaka. Ama ile akaunti endelevu: huenda ikatumika hivyo, ima kutokana na akaunti yako endelevu au kutoka kwa akaunti ya mtu mwengine. Na hilo ni kwa sababu, akaunti endelevu (current account) huwa kuna uwezekano wakati wowote kutolewa pesa pale mwenyewe anapotaka... hivyo basi yafanana zaidi na hali ya kuweka amana kwa mtu muovu. Kwa hiyo, kama utasongeka (lazimika) kufanya hivyo basi haina neno kwako, na atakayepata madhambi ni kwao pindi wakiitumia amana kwa isiyo sawa, maadamu hukujua hilo wala hukuridhia. Ni vivyo hivyo benki, kama utajua kuwa watatumia akaunti yako endelevu katika riba, basi haitofaa

Na kwa hali ya kawaida, bora zaidi ni usiweke kwenye benki au kwa mtu muovu.

Lakini yote hayo, ni pale ambapo benki itakuwa imefunga mkataba sahihi. Kama vile ikiwa ni umiliki binafsi, au umiliki wa serikali, au kampuni ya Kiislamu, au kampuni ya hisa iliyofungwa kwa wenyewe... wala sio kampuni ya hisa yenye mkataba batili. La sivyo basi haitaruhusiwa kuamiliana nayo katika hali zote ] Mwisho wa nukuu

 

Ndugu Yenu,

Atwa Bin Khalil Abu Rashtah

9 Dhul Hijja 1442H

19/07/2021 M

Link ya jibu hili kutoka kwa ukurasa wa Amiri wa Facebook page.

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu