Ijumaa, 20 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Amiri wa Hizb ut Tahrir "Juu ya Maswali ya Wanaozuru Ukurasa Wake wa Facebook wa "Kifiqhi"

Jibu la Swali

Namna ya Kuamiliana na Ukaaji Uchi Ulioenea

Kwa: Abdullah Ibn Al-Mufakkir

(Imetafsiriwa)

Swali:

Assalamu alaikum wa rahmatullahi wa barakatuhu, sheikh wetu. Namuomba Mwenyezi Mungu Akuhifadhi na Akupe afya njema kwa ajili ya hii daawa na dini na Akupe maisha marefu katika ibadah Yake na Akujaalie uishuhudie Khilafah ya pili iliyoongoka. Namuomba Mwenyezi Mungu Aihifadhi na Aipe nguvu daawah, katika kulingania maisha ya Kiislamu, na kuunganisha Ummah wetu chini ya bendera moja. Ameen

Swali langu ni kuhusu wanaume kuangalia wanawake. Katika nchi za Magharibi, wanawake wengi hudhihirisha uchi (nywele na mikono kwa uchache - na karibia kila kitu majira ya joto). Mimi nafahamu kwamba kuona awrah (uchi) zao ni haram kwa wanaume, iwe ni wanawake wanaovutia au la, kama vile ilivyo haram kwa mwanamume kuona uchi wa mwanamume mwenziwe pamoja na kuwa hawavutiani.

Nafahamu kwamba "jicho la kwanza" halina makosa, na kuangalia tena baada ya hapo kwa hali yoyote ni haram. Katika maisha ya kila siku katika nchi za Magharibi, mwanamume hukutana na wanawake wanaodhihirisha awrah kila siku. Katika hali kama kuendesha gari au kutembea, huweza mtu akaangalia mara moja tu, lakini, hili kulitekeleza kazini, shule na madukani ni jambo lisilowezekana kutekelezwa.

Ni jambo lisilowezekana kabisa kwa mwanamume kuingililiana na wafanyakazi wenzake wa jinsia ya kike bila kuwaona awrah. Lau atamuona awrah yake kwa mara ya kwanza, basi kwa mara nyengine yoyote atakayokutana naye, itambidi afunge macho yake au aangalie sakafu/chini. Hapa simaanishi kumuangalia na matamanio kivyovyote. Huenda hata mwanamke mwenyewe sio wa kuvutia, lakini kwa maingiliano, mwanamume yambidi kumuangalia awrah yake - lakini ameruhusiwa tu jicho la kwanza (kama ninavyofahamu)

Mwanafunzi wa Kiislamu hatoweza kushiriki katika masomo darasa ambalo mwalimu ni mwanamke ambaye anadhihirisha awrah yake. Baada ya kumuangalia mwanzo wa masomo, basi itakuwa haram kwake kumuangalia tena mpaka mwisho wa masomo, hata kama ni mzee au havutii. Kwani anadhihirisha awrah, ambayo ni haram kuangalia.

Hali hii inafanana na madukani vilevile.

Mwanamume hatoweza kuingililiana na mwanamke ila kwa kuangalia chini au kufunga macho yake. Hata kama havutii, haruhusiwi kumuangalia awrah yake.

Swali langu:

Je dhana yangu iko sawa - kuwa kumuangalia mwanamke wa kando (ajnabiya) ni haramu ila kwa jicho la kwanza, hata kama havutii, kama vile kumuangalia awrah mwanamume ni haram pamoja na kuwa hakuna kuvutiwa kwake? Kama ni haram, je kufanya kazi ambayo ndani yake kuna kuingililiana na wanawake ambao hudhirisha awrah zao yaruhusiwa juu ya msingi wa kila jambo kwa hukmu yake, kwa msingi wa dharurah?

Naomba ueleze haswa kinachomaanishwa na "jicho la kwanza"?

Naomba pia ueleze maana haswa ya wanateremsha macho yao "Yaghuddhoo Absarihin/Absarihim" na hutekelezwa wakati gani?

Mwenyezi Mungu Awajazi kheri ewe Sheikh

Kutoka kwa: Saifudeen Abdullah) Mwisho

 

Jibu:

Waalaykum Salam Warahmatullahi Wabarakaatuh,

Kuhusu ukaaji uchi ulioenea ambapo ni vigumu kujikinga nako katika dhuruf ya Dola zilizopo sasa ambazo hazitabikishi Uislamu, kulingana na hali hizi Mwenyezi Mungu ametuamrisha mambo mawili:

Kwanza: Kufumba jicho, yaani tuinamishe macho kwa kiwango cha kuweza kutembea na kutekeleza kazi...

Pili: Tusifuatilize mtazamo wa ghafla kwa mtamazamo mwengine...

Na tumeyafafanua hayo katika kitabu cha Nidhamu ya Kijamii kuhusu jibu la swali lako tukasema:

(...Tangu tulipovamiwa na hadhara ya Kimagharibi, Na kutawala Miji ya Waislamu kwa nidhamu za kikafiri wanawake wasiokuwa wa Kiislamu wamekuwa wakitoka nje nusu uchi: Wanadhihirisha vifua vyao na migongo yao, Nywele na mikono na miundi. Wakawa baadhi ya wanawake Waislamu wanawaiga nao wanatoka kwenda masokoni kwa sura hii, mpaka ikawa mtu hawezi kutofautisha wanapokwenda sokoni baina ya mwanamke wa Kiislamu na asiyekuwa Muislamu, au akiwa amesimama Dukani anataradhia bei. Na wanaume Waislamu ambao wanaishi katika hii miji hawawezi wao peke yao kuondoa munkar hivi sasa, na hawawezi kuishi katika miji hii pasi na kuona hizi nyuchi. Kwa kuwa maumbile ya kimaisha ambayo wanaishi, na sampuli ya nyumba wanazoishi, yalazimisha mwanamume kuona uchi wa mwanamke, na mwanamume yeyote hawezi kujilinda asione nyuchi za wanawake, mikono yao, vifua vyao na migongo yao, miundi yao na nywele zao, namna atakavyojaribu asione, isipokuwa anapokaa nyumbani kwake na asitoke nje, na hili haliwezekani kabisa, kwani yeye anahitaji kuwa na mahusiano na watu katika kuuza na kununua, kuajiri na kufanya kazi, na mengineo ambayo ni katika dharura ya kimaisha. Na hawezi kuyafanya hayo huku akichunga asione hizi nyuchi. Na uharamu wa kuangalia uchi uko wazi katika Kitabu na Sunnah je afanye nini? Kutoka katika hili tatizo inakuwa katika sehemu mbili:

Kwanza, ni kuangalia kighafla bila kukusudia kile anachokishuhudia njiani na hili husamehewa mtazamo wa kwanza na ni juu yake asirudie mara ya pili, Kutokana na kile alichopokea Jarir bin Abdillah asema:

«سَأَلْتُ رَسُولَ اللَّهِ ﷺ عَنْ نَظْرَةِ الْفُجَاءَةِ فَأَمَرَنِي أَنْ أَصْرِفَ بَصَرِي»

"Nilimuiza Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kuhusu kuangalia ghafla akaniamrisha niangalie kando" [Amepokea Muslim]. Na kutoka kwa Ali radhi za Allah zimwendee asema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) aliniambia:

«لَا تُتْبِعِ النَّظْرَةَ النَّظْرَةَ، فَإِنَّمَا لَكَ الْأُولَى، وَلَيْسَتْ لَكَ الْآخِرَةُ»

"Usifuatilize mtazamo wa kwanza kwa mtazamo mwengine kwani jicho la kwanza ni halali, na la pili sio halali kwako" [Ameipokea Ahmad kutoka katika njia ya Buraydah].

Ama hali ya pili ambayo ni kuongea na mwanamke ambaye ameweka wazi kichwa chake na mikono yake na yale ambayo amazoea kifichua, basi huyu ni wajib kuangalia kando, na kufumba jicho lisimuangalie, kwa kile alichopokea al-Bukhari kutoka kwa Abdillah bin Abbas radhi za Mwenyezi Mungu ziwaendee asema:

«كَانَ الْفَضْلُ رَدِيفَ النَّبِيِّ ﷺ فَجَاءَتْ امْرَأَةٌ مِنْ خَثْعَمَ فَجَعَلَ الْفَضْلُ يَنْظُرُ إِلَيْهَا وَتَنْظُرُ إِلَيْهِ فَجَعَلَ النَّبِيُّ ﷺ يَصْرِفُ وَجْهَ الْفَضْلِ إِلَى الشِّقِّ الْآخَرِ»

"Al-Fadhlu alikuwa akimuandama Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akaja mwanamke kutoka Khatha'm (kuuliza hukmu fulani), ikawa Al-Fadhlu anamuangalia yule mwanamke na mwanamke anamuangalia. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akawa anaugeuza uso wa Al-Fadhlu upande mwengine". Na akasema Mwenyezi Mungu (swt):

(قُل لِّلۡمُؤۡمِنِینَ یَغُضُّوا۟ مِنۡ أَبۡصَـٰرِهِمۡ وَیَحۡفَظُوا۟ فُرُوجَهُمۡۚ)

"Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao." [An-Nur: 30]

Na maana ya kufumba jicho ni kuinamisha. Kwa hiyo kutatua hili tatizo ni kuinamisha macho upande wa Mwanamume, pamoja na kuendelea na kazi yake ya dharura anayoifanya pamoja na mwanamke kama yule, au kupanda gari, au kukaa ukumbini kwa sababu ya joto kali, au mfano wake. Hizi haja ni katika dharura jumla za kimaisha kwa Mwanamume, Hawezi kuzikimbia wala hana uwezo wa kuzuia huu mtihani wa kufichua uchi, basi ni juu yake kuinamisha macho kwa kulifanyia kazi andiko la ayah hii, na sio halali kwake jambo lengine kabisa.

Na wala haisemwi hapa: kwamba haya ni katika mitihani ilioenea, na ni vigumu kujichunga nayo, kwa hakika qaida hii inagongana na sheria, haramu haiwezi kuwa halali kwa kuenea mitihani, na wala halali haiwezi kuwa haramu ikawa mitihani imeenea. Wala haisemwi kuwa hawa ni wanawake wa kikafiri kwa hiyo wataamiliwa miamala ya watumwa, kwamba nyuchi zao ni nyuchi za vijakazi. Haisemwi hivyo kwa kuwa Hadith iko jumla (Aam) kwa wanawake wote, na haikusema mwanamke wa Kiislamu. Mtume (saw) asema:

«إنَّ الْجَارِيَةَ إذَا حَاضَتْ لَمْ تَصْلُحْ أَنْ يُرَى مِنْهَا إلَّا وَجْهُهَا وَيَدَاهَا إلَى الْمِفْصَلِ»

"Hakika kijakazi anapoanza kupata hedhi sio halali kuonekana isipokuwa uso wake na viganja vyake vya mkono hadi kwenye kifundo cha mkono" Na hadith hii iko wazi katika uharamu wa kumuangalia mwanamke, awe Muislamu au asiekuwa Muislamu, na ni jumla katika hali zote. Na wala Hafanyiwi qiyas mwanamke kafiri kwa kijakazi kwa kuwa hakuna sehemu ya kufanyia qiyas...

Na ni wajibu kwa wale wanaishi katika miji, na wanalazimika kupitia maisha ya mujtamaa' au kuamiliana na wanawake makafiri wenye kufichua nyuchi zao, kwa kununua kutoka kwako, au kuzungumza nao, au kukodi kutoka kwao, au kuwaajiri, au kuwauzia, au mengineo, wainamishe macho wakati huo, na wafupishe kwa kadri ya wanachohitajia kile ambacho ni cha dharura.) Mwisho wa Nukuu.

Nataraji jibu hili litakuwa limetosheleza swali lako, Na Mwenyezi Mungu Ndie Mjuzi Zaidi na Mwingi wa Hekima.

Ndugu Yenu,

Atwa Bin Khalil Abu Rashtah

9 Dhul Hijja 1442H

19/07/2021 M

Link ya jibu hili kutoka kwa ukurasa wa Amiri wa Facebook page.

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu