Jumamosi, 21 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Amiri wa Hizb ut Tahrir "Juu ya Maswali ya Wanaozuru Ukurasa Wake wa Facebook wa "Kifiqhi"

Jibu la Swali

Jambo Lisiloweza Kupatikana Lote, Haliachwi Lile Linalowezekana Kupatikana kwa Urahisi Kutokana Nalo

Kwa: Abu Umar

Swali:

Ewe Amir Wetu, Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakaatuh.

Mwenyezi Mungu awahifadhi, awachunge, na awafungulie kheri kupitia mikono yenu.

Ni upi usahihi wa huu msingi wa kisheria? Na je yafaa kuutumia kama dalili ya kutekeleza hukmu za kisheria polepole? [msingi wenyewe ni:

"ما لا يدرك كله لا يترك ما تيسر منه" “Jambo lisiloweza kupatikana lote, Haliachwi lile linalowezekana kupatikana kwa urahisi kutokana nalo.” Mwenyezi Mungu awabariki.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakaatuh.

Kwanza: Mwenyezi Mungu akubariki kwa kutuombea dua zako nzuri, nasi twakuombea kheri.

Bila shaka, wauliza kuhusu mambo mawili:

Kwanza:

Ni upi usahihi wa msingi wa kisheria usemao: “Jambo lisiloweza kupatikana lote, Haliachwi lile linalowezekana kupatikana kwa urahisi kutokana nalo.”

Na pilii: waulizia ikiwa yafaa kuutumia kama dalili ya kutekeleza hukmu za kisheria polepole?

Na jibu juu ya hayo ni kama ifuatavyo:

1- Ama kuhusu swali lako juu ya usahihi wa msingi huu “Jambo lisiloweza kupatikana lote, Haliachwi lile linalowezekana kupatikana kwa urahisi kutokana nalo”. Huu msemo una matamshi mengi yanayokaribiana, yanayozunguka katika vitabu vya wanazuoni. Kama vile “lisilowezekana lote, haliachwi lote” ama “lisilowezekana lote hakiachwi kingi chake” ama “lisilowezekana lote, kichache chake hakiachwi” ama “lisilowezekana lote, kichache chake zaidi pia hakiachwi” ama “lisilowezekana lote, haliachwi baadhi yake” pamoja na kuongezea tamshi lilokuja kwenye swali lako: “jambo lisiloweza kupatikana lote, “lisilowezekana kupatika lote haliachwi lile linalowezekana... na baadhi husema kuwa hiyo ni “mifano” au ni “misemo” na wengine wanaieleza kuwa ni “misingi ya kisheria”... bali ni kana kwamba imepita kwenye midomo ya baadhi ya watu wakiizingatia kuwa ni hadithi kutoka kwa Mtume (saw), jambo lilomfanya mwanahadith wa Sham katika zama zake ambaye ni Ismail bin Muhammad bin Abd al-Haadi al-Jirahi, al-Ajluni, ad-Dimashqiy, Abu al-Fidaa, aliyekufa mwaka 1162 H, [Jambo hilo lilimfanya mwanachuoni huyu] kuitaja katika kitabu chake cha “Kashfu al-Khafaa” na kisha akasema: “lisowezekana lote, haliachwi lote” msingi huu ina maana ya aya isemayo: ﴿فَاتَّقُوا اللَّهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ﴾ "Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo" [At-Taghaabun: 16] na hadithi isemayo «اتَّقِ اللهَ مَا اسْتَطَعْتَ» “Mtii Mwenyezi Mungu kadiri unavyoweza”. Na hilo tamko ni Qaaidah (msingi) na wala sio hadith”.

Ametaja msingi huu pia Ahmad bin Abdilkarim al-Ghazy, al-Amiri, alokufa mwaka 1143 H kwenye kitabu chake “Al-Jidul Hathith fii Bayani Maa Laisa bi Hadith” akasema: “lisowezekana lote, haliachwi lote” hii ni Qaidah na sio hadith, na ina maana ya aya فَاتَّقُوا اللَّهَ مَا اسْتَطَعْتُم﴿ "Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo" [At-Taghaabun: 16]

2- Kutokana na uchunguzi wa kina kuhusu hilo jambo, imebainika kwamba huo msemo “lisowezekana lote, haliachwi lote” marejeo yake ni kwenye Qaidah ya kisheria isemayo: “jambo linalowezekana haliondoki kwa sababu ya lisowezekana” ikiwa na maana kwamba, hayo ni matamshi mengine ya hii Qaida. Na hii Qaida [iliyotangulia hivi punde] ni Qaidah ilotajwa ndani ya vitabu vya misingi ya kisheria pamoja na dalili zake. Kwa mfano: anasema As-Suyutwi kwenye kitabu chake “Al-Ashbaahu wa Nadhair” [Qaidah ya thalathini na nane: "الْمَيْسُورُ لَا يَسْقُطُ بِالْمَعْسُورِ" "Linalowezekana kupatikana kwa urahisi halipomoshwi na jambo lisiloweza kupatikana kwa urahisi". Amesema Ibn Subki: [nayo hii Qaidah ni kati ya misingi mashuhuri iliyotolewa kwenye neno lake Mtume (saw): «إذَا أَمَرْتُكُمْ بِأَمْرٍ فَأْتُوا مِنْهُ مَا اسْتَطَعْتُمْ» yaani: “Pindi ninapowaamrisha jambo lolote basi lifanyeni kwa kadri mnavyoweza”. Na pia Zarkashi ameitaja hii Qaidah ndani ya kitabu chake “Al-Manthur fil Qawaaid” akasema: “Hii Qaidah isemayo: lisowezekana lote, haliachwi lote” yarudi kwenye Qaidah ya “uwezo” juu ya baadhi ya msingi]. Na kwa hakika, aliifafanua na kubainisha mipaka yake pale alipozungumzia kuhusu maudhui ya “kitu kinachowezekana baadhi, je ni lazima?”

3- Wanazuoni wametolea dalili hii Qaidah "الْمَيْسُورُ لَا يَسْقُطُ بِالْمَعْسُورِ" "Linalowezekana kupatikana kwa urahisi halipomoshwi na jambo lisiloweza kupatikana kwa urahisi" na zengine zinazofanana nayo, au kwa maudhui ya “kitu kinachowezekana baadhi, je ni lazima?” [walizitolea dalili] kwa neno lake Mwenyezi Mungu (swt) aliposema:

 فَاتَّقُوا اللَّهَ مَا اسْتَطَعْتُم﴿ "Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo" [At-Taghaabun: 16] na kwa kauli yake Mtume (saw) aliposema: «إذَا أَمَرْتُكُمْ بِأَمْرٍ فَأْتُوا مِنْهُ مَا اسْتَطَعْتُمْ» yaani... “Pindi ninapowaamrisha jambo lolote basi lifanyeni kwa kadri mnavyoweza” (imepokewa na Bukhari kwenye Sahih yake, kutoka kwa Abu Huraira r.a) na hizi qaida wamezitolea mifano mingi ya ufafanuzi ili kuweka wazi uhalisia wake. Ametaja [As-Suyutwi] katika kitabu “Al-Ashbaahu wa Nadhair” matawi yake mingi, na tutataja tu baadhi yake:

 “Ikiwa mtu amekatwa baadhi ya viungo, itamlazimu [katika udhu] kuosha viungo vilivyobakia”. Pia: mtu mwenye uwezo wa kupata baadhi ya [nguo] ya kujistiri, atawajibika kujisitiri nayo kwa namna itakayowezekana. Pia: mwenye uwezo wa kusoma baadhi ya Suratul Fatiha, ni lazima aisome tu, hakuna ikhtilafu [kwa wanazuoni]... pia: lau mtu atashindwa kurukuu na kusujudu, na [hakushindwa] kusimama, basi ni wajibu kusimama, hilo halina ikhtilaaf kwetu... pia: mwenye kupata baadhi ya pishi kwenye Idd ul Fitri, inamlazimu kuitoa [hiyo hiyo] kulingana na kauli sahihi zaidi...”

4- Kutokana na kutafiti mifano waliotolea wanazuoni juu ya msingi huu usemao: (الميسور لا يسقط بالمعسور) "Linalowezekana kupatikana kwa urahisi halipomoshwi na jambo lisiloweza kupatikana kwa urahisi" na iliyofanana nao, inabainika kwamba wao wanakusudia kwa msingi huu kuwa, hukmu maalumu iliyoamrishwa kisheria, na mukallaf akawa hana uwezo wa kutekeleza baadhi yake [ima] kwa sababu ya kushindwa, au kwa sababu ya uzito wake, basi kutekeleza yaliyobakia katika kitendo kilichaomrishwa hakupomoki kwake. Bali ni lazima kwake kufanya anayoweza kutokana na hicho alichoamrishwa. Kwa sababu, mukallaf anatakiwa kisheria kutekeleza anachoweza kutokana na maamrisho, kulingana na matamshi ya Kitabu [Qur`an] na Sunnah

 فَاتَّقُوا اللَّهَ مَا اسْتَطَعْتُم﴿، "Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo" [At-Taghaabun: 16] na kauli yake Mtume (saw): «إذَا أَمَرْتُكُمْ بِأَمْرٍ فَأْتُوا مِنْهُ مَا اسْتَطَعْتُمْ» yaani... “Pindi ninapowaamrisha jambo lolote basi lifanyeni kulingana na mnavyoweza”. Kwa mfano: mwenye kuswali ni lazima asome Surat ul-Faatiha kamili katika kila rakaa, lakini mtu anaposilimu na akataka kuswali hali ya kuwa hajui kwenye Surat ul-Faatiha isipokuwa baadhi yake tu, je hapo ni wajib kwake katika swala yake asome aya anazozijua katika Surat ul-Faatiha? Ama aache kabisa [asisome chochote] kwa sababu hajui isipokuwa tu baadhi yake? Jibu juu ya hilo: kulingana na hii qaidah ni wajib kwake asome kiasi anachojua katika sa Surat ul-Faatiha, na haitoswihi kwake kuacha kuisoma. Kwa sababu “kinachowezekana - ambapo hapa ni kusoma aya anazozijua katika Surat ul-Faatiha - hakiachwi - kwa ajili ya - lile lisilowezekana” [hapa ni kusoma aya asizozijua katika Faatiha]... na kwa mfano: ni lazima mukallaf anapotawadha aoshe mikono yake miwili hadi kwenye visusuku, lakini akiwa amekatwa kiganja, je ni lazima aoshe sehemu zengine za mikono yake? Ama uoshaji wa hizo sehemu zengine za mkono utaondoka, kwa kuwa yeye hawezi kuosha baadhi ya mkono [kiganja]? Na jibu juu ya hilo: kulingana na hii qaaidah ni lazima kwake kuosha sehemu ilobakia [ndio “kinachowezekana]  hata kama kuosha kiganja haiwezekani [kisichowezekana] kwa sababu, “linalowezekana haliachwi -kwa ajili ya - lile lisilowezekana”... kwa hiyo basi, bila shaka maudhui ya hii qaidah kwa wanazuoni ni “hukmu ya kisheria iliyoamrishwa, na ikawa mukallaf hawezi kutekeleza baadhi yake kwa sababu ya uzito, basi hilo halitamuondolea ulazima wa kutekeleza kile anachoweza kutokana na kitendo kinachotakiwa”...

5- Hakika, qaidah isemayo ““linalowezekana haliachwi -kwa ajili ya - lile lisilowezekana” na mfano wake, ni misingi isiyodhibitika. Ndio ni sahihi katika baadhi ya hali na sio sahihi katika hali zengine. Kwa mfano: mtu asoweza kufunga baadhi ya siku katika mwezi wa Ramadhan, sio wajib kwake kujizuia baki ya siku na awe kana kwamba kafunga siku nzima, [eti] kwa hoja kuwa ““linalowezekana haliachwi -kwa ajili ya - lile lisilowezekana”! bali ni afungue [swaum] na atalipa swaum ya siku iliyompita... na hivyo ndivyo inavyodhihirika kwamba hizi qaaidah hazidhibitiki, kwa hiyo zaweza kutumika katika baadhi ya hali tu na haziwezi kutumika katika hali zengine. Na ili kutumika kwake kunahitajika ijtihaad katika kutafiti uhalisia [wa hali] inayotakiwa kutumika hizo qaida, na kujua hukmu za kisheria zenye kuhusiana nayo... na hakika wanazuoni walitanabahi kwamba hizi qaidah hazidhibitiki:

a) Ametaja As-Suyutwi kwenye “Al-Ashbaahu wa Nadhair” haya yafuatayo: [“Tanbihi: kuna mambo kadhaa yanatoka nje ya hizi qaidah, miongoni mwayo: mwenye kumiliki baadhi ya mtumwa katika kafara hatoacha huru, bali atahamia kwenye badali, bila ya ikhtilaaf. Na imeelekezwa kwamba, kulazimisha kuacha huru baadhi ya mtumwa pamoja na kufunga miezi miwili, itakuwa ni kuweka pamoja badali na kilichobadilishiwa, na kufunga mwezi mmoja pamoja na kuacha huru nusu ya mtumwa, hapo kutakuwa na utekelezaji baadhi ya kafara na hilo haliwezekani, hasa kwa kuwa Mwenyezi Mungu (swt) amesema: فَمَنْ لَمْ يَجِدْ﴾) “Na ambaye hakupata...” [An-Nisa: 92]. Na mwenye kuwa na baadhi ya mtumwa huyo basi [anahisabiwa kuwa] hajapata mtumwa... na miongoni mwayo: mwenye kuweza kufunga baadhi ya siku na akashindwa na kufunga siku nzima, huyo si lazima kwake kujizuia...”]

 b) Kadhalika Zarkashiy amebainisha hili jambo katika kitabu “Al-Manthur fil Qawaaid” akasema: “[na baadhi inalowezekana je, ni wajib? Kuna vigawanyo vinne:

Kwanza: kuna linalowajibika kwa kukatikiwa, kama vile ikiwa mwenye kuswali aweza kusoma baadhi ya Faatiha, basi itamlazimu kwa kukatikiwa...

Pili: kuna linalowajibika kulingana na kauli sahihi zaidi... na lau kwenye mwili wake kuna majeraha yanayomzuia kueneza maji, basi kulingana na Madh-hab ni aoshe viungo vizima, na atayammam badala ya kiungo chenye jeraha...

Tatu: kuna lisilowajibika kwa kukatikiwa. Kama vile akipata baadhi ya mtumwa katika kafara inayompasa, basi hatolazimika kwa kukatikiwa, kwa sababu sheria kusudio lake ni kukamilisha uachaji huru kadri inavyowezekana... na ataendea badali yake...

Nne: na kuna yasiyowajibika kulingana na kauli sahihi zaidi. Kama vile lau mtu mwenye hadath [asiye na udhu] aliyekosa maji, akipata theluji au umande, na ikashindikana kuziyeyusha, basi hapo hatowajibika kupangusa kichwa nayo, kulingana na Madh-hab. Kwa sababu, mpangilio ni wajib, na haiwezekani kutumia hii [theluji] kwenye kichwa kabla ya kutayammam kwa ajili ya uso na mikono miwili...”]

Kwa hiyo, yadhihirika kwamba hiyo/hizo qaidah zilizoashiriwa sio sahihi moja kwa moja, wala sio makosa moja kwa moja. Bali huwa ni sahihi na zilonyooka katika baadhi ya sehemu, na haziwi sahihi katika sehemu zengine.

Pili:

Kuhusu kutumia hii qaidah (ما يدرك كله لا يترك ما تيسر منه) “Jambo lisiloweza kupatikana lote, Haliachwi lile linalowezekana kupatikana kwa urahisi kutokana nalo.” au  (الميسور لا يسقط بالمعسور) "Linalowezekana kupatikana kwa urahisi halipomoshwi na jambo lisiloweza kupatikana kwa urahisi" kama dalili juu maudhui ya utabikishaji polepole wa hukmu za kisheria:

Bila shaka, kutumia hizi qaidah kama dalili ya kufaa kutabikisha polepole hukmu za kisheria, huko ni katika kuwahadaa watu, na katika kuizulia uongo dini ya Mwenyezi Mungu. Na hiyo ni kwa sababu, hakuna nafasi kabisa kutumia hizi qaaidah kama dalili ya kufaa kutekeleza sheria polepole. Na [nasema] hivyo kwa milango [hoja] nyingi:

1- Maana ya kutabikisha polepole hukmu za kisheria: ni kutekeleza sehemu kutokana na hukmu za kisheria katika baadhi ya mambo, na kutekeleza hukmu za ukafiri katika mambo mengine. Hilo ni kama vile: mikataba ya ndoa ifungwe kulingana na hukmu za Kiislamu, lakini riba, zinaa, unywaji pombe [hizi] ziruhusiwe! Adhabu ya mwizi ifanywe ni kukatwa mkono, lakini mzinifu na mlevi hawapewi adhabu...! Hivyo, itakuwa maana halisi ya “kutabikisha polepole hukmu za kisheria” ni kuhukumu kwa hukmu za ukafiri katika mambo maalumu badala ya kuhukumu kwa sharia. Na hili - bila shaka - liko mbali sana na maudhui ya qaidah [ما يدرك كله لا يترك ما تيسر منه] “Jambo lisiloweza kupatikana lote, Haliachwi lile linalowezekana kupatikana kwa urahisi kutokana nalo.” Kwa sababu, hii qaaidah yasema kwamba, kitendo ambacho kimeamrishwa na sheria ni lazima kitekelezwe baadhi yake kinachowezekana ikiwa baadhi nyengine sio rahisi kwa kukosekana uwezo. Kwa hiyo, qaaidah haisemi kwamba, yaruhusiwa kufanya haramu au kutekeleza ukafiri ikiwa hakuna uwezo wa kutekeleza uliyoamrishwa...!

2- Hizi qaidah zazungumzia kitendo kilicho amrishwa wala sio kitendo kilicho katazwa. Kwani kitendo kilichoamrishwa ni “kutekeleza sheria” ama kutekeleza isiyokuwa sheria bila shaka ni “jambo lilokatazwa” bali hilo miongoni mwa madhambi makubwa zaidi! Sasa vipi hizi qaaidah zitumiwe kama dalili juu ya kufaa kutekeleza hukmu za ukafiri?! Hivi hili si ni jambo la ajabu?!

3- Hakika wenye msimamo wa tadarruj wanakusudia kwa hilo: mtawala kutekeleza sheria polepole, na mtawala hakuna kitu kinachomzuia kutekeleza sheria, hivyo haitokuwa na nafasi hapa maudhui ya kutokuwa na uwezo, kwa sababu yeye ndiye mtawala! Kwa mfano: kitu gani kinamzuia mtawala Muislamu kutekeleza hukmu zote za kisheria badala ya kutekeleza hukmu za ukafiri kwenye sehemu nyingi za nyanja za maisha? Kwani yeye si ndiye mtawala hakika wa nchi?! Basi kwa nini hatabikishi hukmu za sheria? Bali hutanguliza hukmu za ukafiri?! Je, uhalisia wa mtawala ni mfano wa mtu asiyeweza kusimama katika swala kwa sababu ya maradhi aliyo nayo? Ikawa ulazima wa kusimama umeondoka kwake, na akaswali bila ya kusimama?! Zafanana kivipi hizi hali?

4- Na kabla ya yote hayo na baada yake, hakika nususi za kisheria zilizotumiwa kuwa dalili ya hizi qawaid hazijulishi kamwe suala la tadarruj:

(a) Kwa sababu neno lake Mwenyezi Mungu (swt): فَاتَّقُوا اللَّهَ مَا اسْتَطَعْتُم﴿  "Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo" [At-Taghaabun: 16] haina ufahamu wa kinyume, yaani haifahamiki kutokana na aya kwamba uchamungu hauamrishwi wakati inapokuwa hapana uwezo, bali ni kinyume na hivyo, aya inajulisha ulazima wa kutumia juhudi katika upatikani wa uchaji mungu na kujifunga na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake. na imamu Twabari amedhihirisha hii maana katika tafsiri yake aliposema: "Neno lake Mwenyezi Mungu (swt): فَاتَّقُوا اللَّهَ مَا اسْتَطَعْتُم﴿  "Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo" [At-Taghaabun: 16]: asema Mwenyezi Mungu (swt), na kuweni na tahadharini na Mwenyezi Mungu (swt) enyi waumini, na ogopeni mateso yake, na jiepusheni na adhabu yake kwa kutekeleza aliyowafaradhishia na kujiweka mbali na maasi yake, na kwa kutenda yanayowakaribisha kwake kadri ya uwezo wenu]… na amefanya vizuri ibn Ashur katika tafsir yake [at-Tahrir wa at-Tanwiir] pale alipoifafanua aya hii, kwa kusema:

فَاتَّقُوا اللَّهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ وَاسْمَعُوا وَأَطِيعُوا وَأَنْفِقُوا خَيْراً لِأَنْفُسِكُمْ وَمَنْ يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴿

"Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo, na sikieni, na t'iini, na toeni, itakuwa kheri kwa nafsi zenu. Na mwenye kuepushwa na uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio walio fanikiwa." [At-Taghaabun: 16]  herufi “faa” ni “faswiha” nayo ni kutanua yaliyotangulia, yaani ikiwa mumelijua hili basi mcheni Mwenyezi Mungu (swt) katika yanayopasa kutokana na taqwa... na kuondoshwa yanayohusiana na neno (اتَّقُوا) ni kwa kusudio la kueneza yanayohusiana na uchamungu katika hali zote zilizotajwa na nyenginezo. Kwa hiyo, maneno haya ni kama ukamilishaji, kwa sababu yaliyo ndani yake ni mapana zaidi kuliko yaliyo kabla yake. Na ilivyo “taqwa” ni kama tu mengine yaliyotajwa [ambapo] mtu mwenye taqwa anaweza kupatwa na mapungufu katika kutekeleza, kwa sababu ya pupa yake ya kutaka kuridhisha utashi wa nafsi yake katika hali nyingi ya hivyo vitu, ndio maana ikazidishwa kusisitizwa jambo la taqwa kwa kusema: (مَا اسْتَطَعْتُمْ) “kwa kadri mnavyoweza”. Na neno “maa” ni ya “maswdar” na “dhwarfu” yaani, [mcheni Mwenyezi Mungu] kwa mda wa uwezo wenu, ili [neno hilo] lienee zama zote, na ili lienee hali zote kutokana na kuenea kwake zama, na lienee pia uwezo wote. Hivyo basi wasijitenge na taqwa katika zama zozote, na zama zimefanywa ni dhwarfu ya uwezo ili wasizembee katika jambo lolote ambalo wanaliweza katika mambo waliyoamrishwa kuwa na taqwa nayo maadamu halitoki nje ya kipimo cha uwezo na kwenda kwenye kiwango cha mashaka/mazito...]” mwisho wa nukuu.

Kwa hiyo, aya inajulisha kwa uwazi kabisa juu ya ulazima wa kutumia juhudi katika kumcha Mwenyezi Mungu (swt), na kutoenda kombo na kuacha maamrisho yake na makatazo yake kwa kiasi anachoweza Muislamu. Wala haijulishi kwa namna yoyote ile juu ya tadarruj, yaani juu ya ufaaji wa kutekeleza hukmu za ukafiri kando na hukmu za sheria, bali [aya] inataka tujifunge na sheria kwa daraja ya juu zaidi ya kujifunga.

(b) Hadith tukufu ambayo imetumiwa kuwa dalili ya hizo qawaid zilizoashiriwa [huko mwanzo] ni kama ilivyopokewa na Bukhari katika Sahih yake kutoka kwa Abu Huraira, kutoka kwa Mtume (saw) akisema:

»دَعُونِي مَا تَرَكْتُكُمْ إِنَّمَا هَلَكَ مَنْ كَانَ قَبْلَكُمْ بِسُؤَالِهِمْ وَاخْتِلَافِهِمْ عَلَى أَنْبِيَائِهِمْ فَإِذَا نَهَيْتُكُمْ عَنْ شَيْءٍ فَاجْتَنِبُوهُ وَإِذَا أَمَرْتُكُمْ بِأَمْرٍ فَأْتُوا مِنْهُ مَا اسْتَطَعْتُمْ«

“[Niacheni madamu nimewaacha, kwani si kwa lengine waliangamia walokuwa kabla yenu kwa maswali yao na kutafautiana kwao na mitume wao. Hivyo basi, nitakapowakataza kitu kiepukeni, na nitakapowaamrisha jambo basi litekelezeni kwa kadri ya uwezo wenu]”. Hii hadith yasema - kuhusu yalokatazwa - kwamba hakuna budi ila kujiepusha nayo, kwa hiyo yaloharamishwa ni wajib kujiweka mbali nayo moja kwa moja. Ama yaloamrishwa ndio ambayo yamefungamanishwa na uwezo. Na hapana shaka kwamba, kutekeleza hukmu za ukafiri kando na hukmu za Uislamu kwa madai ya tadarruj, hilo ni miongoni mwa mambo ambayo sheria imekataza tena kwa dalili za kukata. Kwani hakika amesema Mwenyezi Mungu (swt):

وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنْزَلَ اللَّهُ فَأُولَئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ﴿

"Na wasio hukumu kwa aliyo teremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri." [Al-Maidah: 44]

  ﴾وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنْزَلَ اللَّهُ فَأُولَئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴿

"Na wasio hukumu kwa yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhaalimu." [Al-Maidah: 45]

 ﴾وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنْزَلَ اللَّهُ فَأُولَئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ﴿

"Na wasio hukumu kwa yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio wapotofu." [Al-Maidah: 45]

 ﴾وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْراً أَنْ يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَنْ يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالاً مُبِيناً﴿

"Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapo kata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi." [Al-Ahzab: 36]

Basi kwa hiyo, hiyo hadith haijulishi kwa namna yoyote ile juu ya kufaa kuzembea katika kuhukumu na sheria na [badala yake] kutabikisha hukmu za ukafiri kwa madai ya tadarruj. Kwa sababu, kuhukumu kwa sheria isiyokuwa aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu (swt) hilo ni miongoni mwa mambo yaliyoharamishwa, na ni katika makatazo ambayo hadith imewajibisha kujiepusha nayo.

Kwa misingi hiyo basi, bila shaka kutumia qaaidah hii kama dalili ya tadarruj katika kuzitabikishaa hukmu za sheria, huo ni utoaji dalili ulio batili ambao hoja kamwe haiwezi kusimama kwayo.

Ndugu Yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

05 Rabi ul-Akhir 1443 H

10/11/2021 M

Link ya jibu hili kutoka ukurasa wa Amiri wa Facebook

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu