Alhamisi, 19 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/21
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 

Umbile la Bid'ah

(Imetafsiriwa)

 

Swali:

Katika moja ya mikutano yetu, tulijadili neno "Bid ́ah." Baadhi yetu walisema kwamba inahusisha kila kitu kinachopingana na amri ya Mtunga Sheria (Al-Shaari'), na wengine wakasema kwamba inahusisha tu kukiuka amri ya Mtunga Sheria katika mambo ya ‘Ibadaat (amali za ibada). Je, unaweza kufafanua suala hili tafadhali? Jazakum Allahu Khairan.

Jibu:

1- Maamrisho ya Mtunga Sheria (Mwenyezi Mungu) ni aina mbili: Aina ya kwanza ni katika Seeghat Al-Amr (umbo la amri) na kuambatanishwa na maelezo ya njia ya kukamilisha amri hii (yaani hatua za kivitendo za kuitekeleza kuanzia mwanzo hadi kumaliza). Kwa mfano, Mwenyezi Mungu سبحانه وتعالى asema:

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ﴿

“Na shikeni Swala” [Al-Baqara, 2:43] hii ni katika Seeghat Al-Amr, lakini haikuachiwa mwanadamu kuswali atakavyo, bali yameteremshwa maandiko mengine ambayo yanaeleza haswa jinsi swala inavyo swaliwa, ikiwemo nia, kusimama, kisomo, Rukuu, Sujuud, nk. Vilevile, Mwenyezi Mungu سبحانه وتعالى ameteremsha:

وَلِلّهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ﴿

Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo[Al-Imran, 3:97], na hii pia imo katika Seeghat Al-Amr, lakini kwa umbo la “habari katika muktadha wa amri,” na hii pia imeambatanishwa na maandiko yanayoeleza jinsi amri hii ya kuhiji inavyotakiwa kukamilishwa kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Aina ya pili pia iko katika Seeghat Al-Amr, lakini ni ya jumla (‘Aam) au isiyo na mipaka (Mutlaq), na haiambatani na njia ya kukamilisha amri (hatua za kivitendo za kuitekeleza). Kwa mfano, Mtume wa Mwenyezi Mungu صلى الله عليه وسلم amesema:

«مَنْ أَسْلَفَ فِي شَيْءٍ فَفِي كَيْلٍ مَعْلُومٍ وَوَزْنٍ مَعْلُومٍ إِلَى أَجَلٍ مَعْلُومٍ»

“Yeyote (aliye kopesha au kuuza kitu kwa mkopo), basi iwe kwa kipimo maalumu, uzito maalumu, na muda (mpaka malipo kufanywa) maalumu.” [Bukhari];

hapa, amri inayohusiana na kuuza kitu kwa mkopo iko katika Seeghat Al-Jumla Al-Shartiyyah (umbo la sentensi yenye masharti), ikituamrisha kujua kipimo, uzito na muda wa malipo, lakini Mtunga Sheria hakueleza hatua mahususi kukamilisha mkataba, kwa mfano, kuwasimamisha wanakandarasi wawili mbele ya kila mmoja wao, mmoja wao asome kitu kutoka katika Qur’an, kisha kila mmoja wao akapiga hatua moja mbele, kisha wakumbatiane, kisha wanajadiliane mkataba wa mkopo, ikifuatiwa na ofa na kukubali, nk.

Mfano mwingine ni Hadith za Mtume wa Mwenyezi Mungu صلى الله عليه وسلم:

“Dhahabu (inayouzwa) kwa dhahabu ni Riba, isipokuwa wakati (inapobadilishwa hapo kwa hapo katika mkutano mmoja)” [Bukhari] na

“Dhahabu (inayouzwa) kwa dhahabu, mithili kwa mithili, na karatasi (inayouzwa) kwa karatasi, mithili kwa mithili.” [Bukhari na Muslim].

Hadith hizi ni “amri katika umbo la habari,” lakini hatua mahususi za kukamilisha biashara hazikutolewa, kama ilivyoelezwa katika mifano iliyotangulia.

Katika mfano mwingine, imesimuliwa kwetu kupitia Hadith sahihi kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu صلى الله عليه وسلم alikuwa akisimama wakati msafara wa mazishi unapompitia. Imesimuliwa katika Sahih Muslim:

“Mnapouona msafara wa mazishi, basi usimamieni...”

na vitendo vya Mtume wa Mwenyezi Mungu صلى الله عليه وسلم ni aina ya Talab (maombi au amri), lakini yeye صلى الله عليه وسلم hakutuonyesha kwa uhakika jinsi ya kutekeleza hatua hasa zinazohusiana na amri hii, kama inavyoonyeshwa katika mfano wa kwanza.

Kwa hivyo, kuna amri kutoka kwa Mtunga Sheria ambazo zimeambatanishwa na maandiko yanayoelezea hatua za kiutendaji za utekelezaji, na kuna amri kutoka kwa Mtunga Sheria ambazo ni za jumla (‘Aam) au zisizo na kikomo (Mutlaq) ambazo hazikuambatana na hatua za kina za utekelezaji.

2- Neno (Istilaah) "Bid'ah" hutumika pale amri ya Mtunga Sheria, ambayo kwayo maandiko yanayoelezea kwa kina hatua za kiutendaji za utekelezaji pia zimeteremshwa, zinapovunjwa. Hii ni kwa sababu amri hiyo haikutekelezwa sawa na ilivyoagizwa na Mtunga Sheria. Maana ya kilugha (Lughawi) ya neno "Bid'ah," kama ilivyoelezwa katika Lisaan Al-Arab: "Mubtadi' (mtu anayefanya Bid'ah) ni mtu ambaye hutoa kitu kwa namna ambayo ni tofauti kuliko ilivyojulikana hapo awali [...] na ikiwa uta (Abda't) kitu, ina maana kwamba umekivumbua na ni cha kipekee."

Taarifu hiyo hapo juu pia inatumika kwa maana ya Istilaahi ya neno "Bid'ah," yaani kukiuka njia ya Kisheria, kama ilivyofafanuliwa na sheria za Kiislamu, ili kukamilisha jambo la Kisheria. Hivi ndivyo Hadith,

«وَمَنْ عَمِلَ عَمَلًا لَيْسَ عَلَيْهِ أَمْرُنَا فَهُوَ رَدٌّ»

Yeyote mwenye kufanya kitendo kisicho juu ya amri yetu basi kinakataliwa.” [Bukhari na Muslim]

inakusudia. Hivyo basi, mwenye kusujudu Sijda tatu badala ya mbili katika Swala yake atakuwa amefanya Bid ́ah, na mwenye kurusha vijiwe vinane kwenye Jamrat ya Mina badala ya saba atakuwa amefanya Bid ́ah. Kila Bid ́ah ni upotofu, na kila upotofu umo katika Moto wa Jahannam (yaani ni mwenye dhambi kwa kitendo hicho).

3- Kukiuka amri ya Mtunga Sheria ambayo haikuambatanishwa na hatua za kivitendo za utekelezaji iko chini ya uainishaji wa Hukmu Shari'e, na inafafanuliwa kama Haramu, Makruhu au Mubah ikiwa hotuba ni aina ya Khitaab Takleef (hotuba ya ukalifishaji), na Baatil au Faasid (potovu) ikiwa hotuba ni aina ya Khitaab Wadh' (hotuba ya maelezo). Hii, kwa upande wake, inategemea muundo wa Qareena (dalili unganishi) unaoambatana na amri, iwe katika muundo wa Jazm (kukatikiwa), Tarjeeh (iliyozidi uzito), au Takhyeer (chaguo).

Kwa hivyo, tukirudi kwenye mfano wetu wa kwanza, ikiwa mtu anauza kitu kwa mkopo (yaani amekamilisha mkataba wa mauzo) kinyume na amri ya Mtunga Sheria (yaani bila kujua kipimo, au uzito, au tarehe ya mwisho ya kulipa. ), haiwezi kusemwa kuwa amefanya Bid ́ah, bali inasemekana kuwa mkataba huu unakinzana na amri ya Mtunga Sheria na ni Baatil au Faasid kulingana na aina ya ukiukaji.

Na katika mfano wa pili, ikiwa mtu alifanya biashara ya dhahabu kwa dhahabu kinyume na amri:

“Dhahabu (inayouzwa) kwa dhahabu ni Riba, isipokuwa wakati (inapobadilishwa hapo kwa hapo katika mkutano mmoja)” na “...mithili kwa mithili (yaani, kutobadilishwa hapo kwa hapo na kwa mithili isiyofanana),

haiwezi kusemwa kuwa amefanya Bid ́ah kwa kukiuka amri, bali inasemekwa amefanya Haramu kwa kuhusika katika mkataba wa Riba.

Na kutosimama wakati msafara wa mazishi unapopita, ukichagua kubaki umekaa, haiwezi kuitwa Bid'ah, bali inaitwa Mubah (yenye kuruhusiwa) kwa sababu maandiko ya Kiislamu yamesimuliwa kwa matukio yote mawili. Imepokewa na Muslim kutoka kwa Ali Bin Abi Taalib (ra) ambaye amesema:

“Mtume wa Mwenyezi Mungu صلى الله عليه وسلم alisimama kisha akaketi” [Muslim].

Hii inatumika pia kwa amri ya Mtunga Sheria

«فَاظْفَرْ بِذَاتِ الدِّينِ تَرِبَتْ يَدَاكَ»

... tafuteni (mke) mwenye Dini (imara), mikono yako itaokoka” [Bukhari],

ambapo kukiuka amri hii hakuwezi kuitwa Bid ́ah, bali hukmu ya Kiislamu kuhusu kuoa mwanamke ambaye hana Dini imara inapaswa kufanyiwa utafiti. Hii ni kwa sababu hatua za kivitendo za kuchagua mke hazijatolewa, ambapo kwa mfano mwanamume anaweza kusimama mbele ya mwanamke na akasoma Ayat ul-Kursi, kisha akapiga hatua moja mbele na kusoma Mu’awidhaat mbili, kisha akapiga hatua moja mbele na kusema Bismillah, kisha akanyoosha mkono wake wa kulia mbele na kupendekeza ndoa, na kadhalika.

Haya pia yanahusu Hadith ya Mtume صلى الله عليه وسلم kwa wafanya biashara.

“Enyi wafanya biashara, ununuzi na uuzaji huu (au soko) unafanywa na Laghw (maneno ya uwongo) na kuapa viapo, basi jazeni kwa sadaka” [Abu Dawood na Ahmed]. Kutokana na viapo vyao kupita kiasi wakati wa biashara. Lakini Mtunga Sheria hakuweka wazi hatua mahususi za kutekeleza amri hiyo “...basi jazeni” na kwa hiyo haiwezi kusemwa kwamba ikiwa mtu aliuza kitu na akaapa, lakini hakutoa sadaka, kwamba amekuja na Bid' ah; bali hukmu ya Kiislamu kuhusu mfanyabiashara kutotoa sadaka baada ya kuapa ichunguzwe yenyewe.

Hii inatumika kwa ukiukaji wote wa amri za Mtunga Sheria ambao haukuambatana na hatua mahususi za utekelezaji.

4- Kwa kuangalia kwa undani zaidi (Istiqraa) maandiko ya kisheria ya Kiislamu, tunakuta kwamba idadi kubwa ya ́Ibaadaat (ibada) ndizo zinazoambatana na hatua za kivitendo za kutekeleza maamrisho ya Mtunga Sheria, na kwa hiyo Bid’ah haitokei nje ya  ́Ibadaat.

Tunasema “idadi kubwa ya Ibadaat” hapa kwa sababu baadhi yake hazikuambatana na hatua za kiutendaji za utekelezaji. Mfano mmoja wa hili ni Jihad. Ingawa ni kitendo cha ‘Ibaadah, lakini maamrisho yanayohusiana nayo yalikuja kwa njia isiyofungwa (Mutlaq) au ya jumla (‘Aam), kama vile Aya:

قَاتِلُواْ الَّذِينَ يَلُونَكُم مِّنَ الْكُفَّارِ﴿

“Enyi mlio amini! Piganeni na wale makafiri walio karibu yenu” [At-Tawba, 9:123]

Na ayah:

جَاهِدِ الْكُفَّارَ وَالْمُنَافِقِينَ وَاغْلُظْ عَلَيْهِمْ ﴿

Pambana na makafiri na wanaafiki, na wakazanie.” [At-Tawba, 9:73]

Amri hizi hazikuambatanishwa na maandiko ya Kiislamu yenye kueleza kwa undani hatua kamili za kuzitekeleza, kama vile jinsi ya kupigana: ikiwa utasoma Ayah, kisha piga risasi, kisha chukua hatua mbele, kisha piga risasi nyengine, kisha chukua hatua kulia, na kadhalika.

Hivyo basi, mtu ambaye hafanyi Jihad inapofaradhishwa juu yake haisemwi kuwa amekuja na Bid ́ah, bali amefanya Haramu kwa ajili ya kupuuza kwake Jihad.

5- Kwa kumalizia, kukiuka amri ya Mtunga Sheria iliyoambatana na maelezo kamili ya hatua zinazohitajika kukamilisha amri hiyo ni Bid ́ah. Na kukiuka amri isiyofungwa (Mutlaq) au ya jumla ('Aam) ya Mtunga Sheria ambayo haikuambatanishwa na maelezo kamili ya hatua zinazohitajika ili kukamilisha amri hiyo ni ukiukaji wa Hukmu za Shariah: Haramu, Makruhu, au Mubah ikiwa iko katika umbo la Khitaab Takleef (hotuba ya ukalifishaji), na Baatil au Faasid ikiwa katika Khitaab Wadh' (hotuba ya maelezo).

Na kwa kuangalia kwa undani zaidi (Istiqraa ́), tunakuta kwamba nyingi za ‘Ibadaat zimeambatana na hatua halisi za utekelezaji, na kwa hiyo kuzivunja sheria hizi kunaangukia kwenye uainishaji wa Bid’ah.

6- Ama kuhusu dalili zinazohusu Mu'amalaat (muamala) na Jihad, hizi ziliteremshwa kwa mtindo usio fungwa (Mutlaq) na wa jumla ('Aam), na kwa hiyo kuzivunja amri hizi iko chini ya uainishaji wa Hukmu za Shariah: Haramu, Makruhu, au Mubah ikiwa ni katika Khitaab Takleef (hotuba ya ukalifishaji), na Baatil au Faasid ikiwa katika Khitaab Wadh' (hotuba ya maelezo).

29 Ramadhan 1430 H

18/10/2009 M

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu