Jumapili, 20 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali
Kudai Haki Inayo Tambuliwa na Sheria Isiyo ya Kiislamu
Kwa: ‏‎ Rubhi Abu Muadh
(Imetafsiriwa)

Swali:

Sheria yawamwajibisha mwajiri kujifunga na sheria zinazo husiana na wafanyikazi na haki zao, lakini mwajiri anakwepa kutii sheria hiyo. Katika mgogoro wa kazi na ulafi wa waajiri, haki za mfanyikazi zinapotea, na hawezi kudai haki yake isipokuwa kupitia sheria hiyo ambayo inamwajibisha mwajiri kulipa haki za mfanyikazi kama zinavyo tambuliwa na sheria. Hivyo, je, ni haramu kuikimbilia sheria hiyo endapo mfanyikazi atahisi kudhulumiwa?

Jibu:

Wa Alaikum Assalam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Unauliza kuhusu hukmu ya mfanyikazi kudai haki yake kama inavyo tambuliwa na sheria hiyo.

Jibu ni inaruhusiwa katika hali ya kutafuta haki au kutaka dhulma iondolewe kwa mujibu wa Shariah; yaani, haki ni ile iliyo wekwa na sheria ya Kiislamu na dhulma ni ile iliyo wekwa na sheria ya Kiislamu, hivyo si haki kuitisha haki ambayo haitambuliwi kuwa ni haki kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Endapo mfanyikazi atadai haki kwa mujibu wa sheria hiyo lakini sio haki kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu, hairuhusiwi kwake kufanya hivyo. Endapo mfanyikazi atadai haki kwa mujibu wa sheria hiyo, ambayo pia ni haki kwa mujibu wa Sharia ya Kiislamu, hapo anaruhusiwa kuidai.

Kwa mfano, kwa mtu aliye kosewa na kukabiliwa na kifungo kwa sababu amesema neno la haki, Uislamu humtetea na kumtoa nje ya gereza, na hivyo basi inaruhusiwa kwake kumtafuta mtu wa kumtetea na kuondoa dhulma juu yake na kumwokoa kutokana na gereza.

Kwa mfano, kwa mtu aliye porwa, Uislamu humrudishia pesa zake alizo ibiwa, na inaruhusiwa kwake kumtafuta mtu wa kumtetea ili pesa zake zilizo ibiwa zirudishwe.

Katika mfano mwengine, endapo mtu atauza nyumba yake kwa kianzio cha malipo, na malipo yaliyo salia kulipwa kupitia mpango maalum wa malipo, lakini mnunuzi akaishia tu kulipa malipo ya kuanzia pekee, na kugoma kulipa malipo yaliyo salia au kukataa kuwa anadaiwa, licha ya ukweli kwamba ameinunua nyumba hiyo na anaishi ndani yake. Katika hali hii, Uislamu hurudisha haki za muuzaji kutoka kwa mnunuzi na hivyo basi, inaruhusiwa kwa muuzaji huyo kumtafuta mtu wa kumtetea ili kurudisha bei ya nyumba yake, ambayo mnunuzi anakatalia nayo.

Kwa hivyo, kwa mfanyikazi ambaye anafanya kazi kwa kiwango maalumu cha mshahara kwa mujibu wa mkataba wa kazi baina yake na mwajiri, lakini kisha mwajiri akaupunguza mshahara wake, Uislamu humlazimisha mwajiri huyo kumpa mfanyikazi mshahara wake kamili, na hivyo basi inaruhusiwa kwa mfanyikazi huyo kuwaendea wale watakaomtetea ili kupata mshahara wake kamili.

Yaani, endapo sheria ya Kiislamu imemwekea haki na akapunjwa haki hiyo, basi inaruhusiwa kwake kutafuta mtu wa kumtetea mbele ya mahakama ili kupata haki hiyo aliyo pewa na sheria ya Kiislamu. Kinyume chake, ikiwa haki hiyo ameekewa na sheria iliyo tungwa na mwanadamu lakini inagongana na sheria ya Kiislamu, basi hapo haruhusiwi kumtafuta mtu wa kumtetea mbele ya mahakama ili kuipata haki hiyo.

Kwa mfano, endapo mtu anamiliki hisa katika kampuni ya hisa, iliyo undwa juu ya mkataba batili, na pindi wakati unapo wadia wa kugawanya gawio la faida kwa wenye hisa, mtu akagundua kwamba gawio lake ni chache kuliko vile linavyo paswa kuwa. Katika hali hii, hairuhusiwi kwenda mahakamani kupata haki hii, maadamu haki hii imewekwa na sheria iliyo tungwa na mwanadamu na iko kinyume na Sheria ya Kiislamu kwa sababu muundo huo wa kampuni ni batili na faida zinazo tokamana nao hazikubaliwi na sheria ya Kiislamu. Hivyo basi, ni wajib juu ya Muislamu kujiondoa kutokana na muundo wa kampuni sampuli hii. 

Katika mfano mwengine, endapo mtu amewekwa pesa zake katika benki iliyo asisiwa juu ya msingi wa riba kwa kiwango maalumu cha riba, lakini pindi benki hiyo inapompa mgao wake, ikampigia hesabu kwa kiwango cha chini kuliko kile alicho kubaliana na benki hiyo. Katika hali hii, hairuhusiwi kwenda mahakamani ili kudai riba hii, maadamu ni haki iliyo wekwa na sheria iliyo tungwa na mwanadamu na ni kinyume na sheria ya Kiislamu, kwani "haki" hii imewekewa na sheria ya mwanadamu, inayo ruhusu benki za riba, lakini hakuwekewa na sheria ya Kiislamu. Hivyo basi, ni wajib juu ya Muislamu huyo kufutilia mbali mkataba huo wa riba na benki.

Kwa mukhtasari, ikiwa haki, anazodai mfanyikazi kwa mujibu wa sheria ya kibinadamu, pia ni haki kwa mujibu wa Shariah ya Kiislamu, kama zile zilizo ashiriwa na Shariah au ikiwa ni masharti katika mikataba ya kazi ambayo hayagongani na Shariah ya Kiislamu nk., hapo mfanyikazi anaruhusiwa kuzidai. Lakini, ikiwa haki hizo anazodai mfanyikazi ni haki kwa mujibu wa sheria ya mwanadamu na si haki katika Shariah ya Kiislamu, hapo mfanyikazi haruhusiwi kuzidai mbele ya mahakama.  

Nataraji hili litatosheleza, na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi na ni Mwingi wa hekima.

Ndugu yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

10 Sha’ban 1441 H

03/04/2020 M

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu