Ijumaa, 08 Jumada al-thani 1447 | 2025/11/28
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali

China na Ukombozi Wake Kutoka kwa Mtazamo Wake Mdogo wa Kikanda

(Imetafsiriwa)

Swali:

Ilitajwa katika Jibu la Swali, la tarehe 12/04/2014: “China inamiliki hisia ya nguvu na mapambano, na kama lengo la China halikufungika tu na kudumisha eneo lake, na kukubali kukabiliana na Amerika kama jibu tu kwa harakati za Amerika kuelekea eneo lake, China haisubutu kupambana na Amerika katika maeneo yao ya ushawishi... na kama isingeanza kutumia ubepari katika nyanja nyingi, haswa katika uchumi... ingekuwa na sauti kubwa kimataifa, na athari yake kwa maslahi ya Amerika ingekuwa na nguvu zaidi. China kwa vyovyote vile ina hisia kali ya nguvu, na inafanya kazi ili kudumisha ubwana wa eneo lake, hata kama iko katika eneo lake...” — Kwa hivyo, je, kizuizi cha China cha mauzo ya nje ya madini adimu ya ardhini kwenda Amerika, kuyauza kwa dhamana za Hazina ya Marekani, kulisasisha jeshi lake, na kujenga jengo kubwa zaidi la kijeshi duniani kusini magharibi mwa Beijing... je, hiki si kiashiria cha ukombozi wa China kutoka kwa mtazamo wake wa kisiasa uliofungika katika eneo lake na upanuzi wa mtazamo huu kushindana na Amerika duniani kote? Mwenyezi Mungu akulipe kheri.

Jibu:

Ili kufafanua jibu, ni muhimu kuhakiki mambo yafuatayo:

1- Jamhuri ya Watu wa China ilianzishwa mwaka wa 1949 na ushindi wa Mao baada ya mzozo kati ya Chama cha Kikomunisti kilichoongozwa na Mao na Chama cha Kizalendo kilichoongozwa na Chiang Kai-shek, ambacho kiliungwa mkono waziwazi na Marekani. Chama cha Kizalendo kilichoongozwa na Chiang Kai-shek kilikimbilia Taiwan na kuitangaza kuwa “Jamhuri ya China.” Pindi Deng Xiaoping alipochukua urais wa Chama cha Kikomunisti cha China mwaka wa 1978, tofauti na Mao, aliupa kipaumbele uchumi kuliko mfumo. Aliunda muundo wa kiuchumi unaoegemea juu ya mishahara midogo na mauzo ya juu ya nje, akafungua milango kwa wawekezaji wa kigeni, na kisha akaanzisha Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ) katika miji ya mashariki mwa China mwaka wa 1979.

2- Chini ya Deng, China iliachana na mfumo wa kikomunisti katika uchumi na sera za kigeni, nk., na ikaanza kuchanganya ubepari na ukomunisti katika vitendo! Tangu 1980, kwa kipindi cha miaka 45, ilipata ukuaji wa haraka sana wa uchumi na inaendelea kukua. Kuanzia mwaka 2010 na kuendelea, ikawa uchumi wa pili kwa ukubwa duniani baada ya Marekani, na inaendelea katika njia hii. “China ina nafasi nzuri ya kuongeza ukubwa wa uchumi wake mara mbili ifikapo mwaka 2035 - na kuipiku Marekani kama uchumi mkubwa zaidi duniani, alisema mwanauchumi mmoja kutoka Benki ya Amerika.” (CNBC; CBC Arabia, 27/2/2021). Hii ndiyo hali kiuchumi.

3- Kijeshi, China iko katika njia ya kubadilisha nguvu hii ya kiuchumi kuwa nguvu ya kijeshi; inaongeza matumizi yake ya kijeshi kila mwaka. “Leo, Jumatano, China ilitangaza kwamba inakusudia kuongeza bajeti ya ulinzi wa taifa kwa mwaka 2025 kwa 7.2%, ikiwakilisha mwaka wa kumi mfululizo wa ukuaji wa tarakimu moja katika bajeti ya ulinzi. Matumizi ya ulinzi yaliyopangwa yatakuwa yuan trilioni 1.784665 [karibu dolari bilioni 249 za Marekani] mwaka huu...” (Alarabiya News, 05/03/2025). Zaidi ya hayo, uwezo wa jeshi la kawaida la China na jeshi la nyuklia pia unaendelea; ripoti moja kutoka Idara ya Ulinzi ya Marekani kwa Bunge ilisema kwamba kufikia katikati ya 2024, “China imezidi makombora 600 ya nyuklia ya uendeshaji operehseni katika akiba yake kufikia katikati ya 2024 na itakuwa na makombora zaidi ya 1,000 ya nyuklia ya uendeshaji operesheni ifikapo 2030, mingi yao yatatumika katika viwango vya juu vya utayari.” (media.defense.gov; RT, 18/12/2024), na China ilionyesha silaha zake za hali ya juu katika gwaride la kijeshi mnamo 3/9/2025 kuadhimisha kumbukumbu ya miaka themanini ya ushindi dhidi ya Japan katika Vita vya Pili vya Dunia. Maendeleo ya silaha za kijeshi za China yalionekana.

4- Kisiasa, China ni dola kubwa huru ya kikanda ambayo haizunguki katika duara la Marekani, tofauti na nchi za kikanda kama vile Japan na Korea Kusini. Ina matarajio ya kisiasa katika eneo hilo, yanayoendeshwa na nia za kitaifa na maslahi ya kiuchumi, hata kama si ya kimfumo. Bahari ya Kusini mwa China ni muhimu sana kwa China; Ina njia muhimu za baharini, maeneo ya uvuvi, na akiba ya mafuta na gesi ya pwani muhimu kulisha sekta ya utengenezaji na uchumi wa China unaoendelea kukua. Kulingana na ripoti ya Idara ya Habari za Nishati ya Marekani ya 2013, inakadiriwa kuwa  “Bahari ya Kusini ya China ina takriban mapipa bilioni 11 ya mafuta na futi za ujazo trilioni 190 za gesi asilia zilizokadiriwa kuwa akiba iliyothibitishwa au inayowezekana” katika akiba zake za chini ya bahari. (Idara ya Habari za Nishati ya Marekani, 13/04/2013). Zaidi ya hayo, zaidi ya 80% ya biashara ya kimataifa hupitia Bahari ya Kusini ya China, inakadiriwa kuwa takriban dolari trilioni 5.3 za bidhaa zinazouzwa (China Power, 2016). Kwa hivyo, China ina nia katika eneo hili la kijiografia na inadai haki zake ndani yake.

5- Marekani, ikijifanya kama polisi wa dunia, na kwa mujibu wa mkakati wake wa Asia, ilijaribu kuzuia China kuinuka na kuidhibiti; wakati mwingine kwa kuhamisha wanajeshi na vifaa kutoka Ulaya hadi Pasifiki, wakati mwingine kwa kutumia vibaya mgogoro wa Taiwan, wakati mwingine kwa kutumia India, wakati mwingine kuanzisha ushirikiano wa kijeshi na nchi za kikanda kama vile AUKUS (Australia, Uingereza, na Marekani) na QUAD (Marekani, Australia, India, Japan), na wakati mwingine kuendesha vita vya kibiashara dhidi ya makampuni ya Kichina kama Huawei. Baada ya kuanguka kwa Muungano wa Kisovieti, Amerika iliuweka Uislamu kama adui wa kimfumo na China kama adui wa dola juu ya orodha yake ya mahasimu. Huku vita vya Iraq na Afghanistan vikichelewesha na kupunguza kasi ya mapambano yake na China, baada ya vita hivi, mwelekeo wake kamili ulihamia China, hasa vita vya kibiashara.

6- Baada ya ufafanuzi huu, sasa tunapitia jibu la swali:

a- Kuhusu usafirishaji wa madini adimu vya dunia: China inatambua umuhimu wake, hasa katika viwanda vya kisasa, vya teknolojia ya hali ya juu; kuna takriban aina 17 zinazotumika katika viwanda vya kisasa zaidi ya 200 duniani kote. Zinahitajika kwa viwanda vya kijeshi katika ndege, manuari, vyombo vya anga, na droni. Asilimia kubwa ya hizo zinachimbwa nchini China. China ilitumia vyuma hivi kama silaha dhidi ya Amerika ili kupata makubaliano katika vita vya biashara. Hii ilitokea wakati Trump alipotangaza kuongeza ushuru polepole kwa China hadi kufikia 104% mnamo 8 Aprili 2025. China ilijibu kwa kutangaza mnamo 9 Oktoba 2025, vikwazo vya usafirishaji wa madini adimu ya ardhini kwenda Amerika. China inashikilia 49% ya akiba adimu ya dunia na inachangia 69% ya uzalishaji wa kila mwaka duniani. Hiyo ni, hatua na mwitikio uliotokea mara kwa mara, huku ushuru hatimaye ukipunguzwa hadi takriban 47%. Baadaye Trump alisema baada ya mkutano wake na rais wa China huko Busan, Korea Kusini, mnamo 30 Oktoba  2025, wakati wa Kikao cha 32 cha Ushirikiano wa Kiuchumi la APEC: “Ushuru uliowekwa na Marekani kwa China utapunguzwa hadi 47% ... masuala yote yanayohusiana na madini adimu ya ardhi yametatuliwa, na makubaliano yataendelea kwa mwaka mmoja na uwezekano wa kupanuliwa” (Reuters; Al-Sharq Al-Awsat; Al-Araby Al-Jadeed, 30/10/2025). Kwa hivyo, kizuizi cha China kwa madini adimu ya ardhi hakionyeshi ukombozi kutoka kwa ruwaza finyo, lakini ni “mwitikio” kwa uamuzi wa Amerika, kimsingi ni chombo cha majadiliano. Uhalisia unathibitisha hili; ushuru ulipunguzwa na vikwazo vya madini adimu ya ardhi kusimamishwa kwa mwaka mmoja.

b- Kuhusu China kuuza sehemu ya dhamana za Hazina ya Marekani iliyokuwa nayo: ambazo zilifikia $1.189 trilioni mnamo Oktoba 2017; “Umiliki wa dhamana za Hazina ya Marekani nchini China ulishuka hadi kiwango cha chini kabisa tangu 2009… data iliyotolewa na Hazina ya Marekani mnamo Jumanne ilionyesha kuwa thamani ya deni la Marekani lililoshikiliwa na wawekezaji wa China ilipungua kwa dolari bilioni 57 hadi dolari bilioni 759 mwaka 2024, bila kujumuisha dhamana za Hazina zinazomilikiwa na Wachina zilizoshikiliwa katika akaunti katika nchi zengine.” (Al Jazeera Net, 19/02/2025), uamuzi huu ulichukuliwa kama hatua ya kujihami ili kupunguza hatari badala ya kutokea kutokana na mtazamo wa kikanuni (kimfumo). Baada ya vita vya Urusi dhidi ya Ukraine mwaka 2022, Amerika na Ulaya zilifungia mali za Urusi zenye thamani ya dolari bilioni 300 na kutumia mfumo wa SWIFT kama silaha. Kwa hivyo, China huenda ikabadilisha dhamana hizi kuwa akiba ya dhahabu ili kuzuia Amerika kufungia mali zake kama ilivyofanya kwa Urusi, iwapo kutakuwa na shambulizi dhidi ya Taiwan au sababu zengine kama vile vita vya kibiashara. “Mwaka jana pekee, China iliongeza tani kadhaa za dhahabu zenye thamani ya dolari bilioni 550 kwenye akiba yake. Mwezi uliopita, sehemu ya dhahabu katika akiba rasmi ya China ilipanda hadi kiwango cha juu zaidi katika historia kwa 4.9%...” (Artigercek.com, 18/05/2024). Madai kwamba kupungua kwa mali za China kunatokana na kuhamishiwa baadhi kwa taasisi kama vile Euroclear nchini Ubelgiji na Clearstream huko Luxembourg, kama baadhi ya wataalamu wanavyopendekeza, hayawezekani; kwa sababu katika kesi hii, mali zilizohamishwa kutoka Amerika hadi Ubeligiji na Luxembourg bado zinaweza kufungiwa chini ya shinikizo la Marekani. Kwa hivyo, dhahabu ndiyo kimbilio salama zaidi. Hatua hii, kama madini adimu ya ardhini, ni “hatua ya tahadhari”—vitendo vya China ni athari kwa vitendo vya Marekani.

c- Kuhusu uboreshaji wa jeshi la China na ujenzi wa eneo kubwa zaidi la kijeshi kusini-magharibi mwa Beijing: “Jeshi la China limethibitisha tena kujitolea kwake kufikia malengo yake ya miaka mia moja kwa Jeshi la Ukombozi wa Watu (PLA) mnamo 2027, likiahidi kuharakisha uboreshaji na kuongeza utayari wa mapigano. Wu Qian, msemaji wa ujumbe wa PLA na Jeshi la Polisi la Watu, alisisitiza kwamba kufikia malengo ya miaka mia moja na kuendeleza uwezo wa kijeshi ni “mambo muhimu ya kimkakati” katika juhudi pana za China za kuboresha ulinzi wake wa kitaifa. “Lazima tutoe juhudi zetu kuhakikisha kwamba tunafikia malengo yetu kwa utendaji mzuri kwa wakati,” Wu alisema. (Defence-blog; Defense-arabic.com, 13/03/2025). “Financial Times iliripoti kwamba jeshi la China linajenga jengo kubwa magharibi mwa Beijing ambalo ujasusi wa Marekani unaamini litatumika kama kituo cha amri cha wakati wa vita kikubwa zaidi kuliko Pentagon, kulingana na maafisa wa sasa na wa zamani wa Marekani. Picha za setilaiti zilizopatikana na ‘Financial Times’ ambazo zinachunguzwa na ujasusi wa Marekani zinaonyesha eneo la ujenzi la takriban ekari 1,500 kilomita 30 kusini-magharibi mwa Beijing lenye mashimo marefu ambayo wataalamu wa kijeshi wanatathmini yatakuwa na mabanda makubwa, magumu ili kuwalinda viongozi wa kijeshi wa China wakati wa mzozo wowote – ikiwa ni pamoja na uwezekano wa vita vya nyuklia.” (Financial Times, 30/1/2025; Al Jazeera Net, 31/01/2025). Kwa hivyo, uboreshaji wa jeshi na kujenga kituo hiki cha amri, kujenga visiwa bandia katika Bahari ya Kusini mwa China, au kupanua haraka meli za majini, zote ni “athari” kwa upelekaji wa Amerika wa 60% ya meli zake za majini katika eneo hilo. Haikusudiwi kuingia katika mzozo na Amerika katika koloni zake au kuchukua nafasi, tofauti na Marekani kuchukua nafasi ya Uingereza baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Vitendo hivi vinalenga kuzuia udhibiti wa Marekani juu ya kanda ya China – China imetosheka na kuhifadhi eneo lake – hasa kujibu kujaa kijeshi katika kanda hiyo.

7- Kwa kumalizia, China sasa ina uwezo wa kimada wa kuwa dola kubwa duniani, lakini hadi sasa haijasubutu kushindana na Amerika katika maeneo yake ya ushawishi au kwengineko. Kwa hivyo, haijainyakua Taiwan kwa nguvu kama ilivyokuwa imepanga na kutishia, baada ya kuona vikwazo vilivyowekwa na Amerika na nchi za Magharibi dhidi ya Urusi tangu 2022. Haipingi Amerika katika maeneo yake ya ushawishi barani Afrika, Asia, nk., imepunguza mipango ya kambi za kijeshi zilizopanuliwa kutoka pwani zake hadi Pasifiki, Bahari Hindi, na Afrika, ikiweka kambi moja tu nchini Djibouti. Haijachukua msimamo mkali dhidi ya vitisho vya Marekani kwa maslahi yake huko Panama, ambapo Panama ilishindwa na vitisho na kujiondoa kutoka makubaliano mapya ya Silk Road mnamo 6/2/2025, ambayo yalijumuisha usimamizi wa China wa Mkondo wa Panama. China inajibu tu harakati za Marekani zilizo karibu yake bila kuanzisha zake. Kwa hivyo, jibu letu la awali linabaki kuwa halali: China inaonyesha uwepo wa kikanda na inashindana ndani lakini sio kimataifa na Amerika—ingawa hii inaweza kubadilika ikiwa maendeleo mapya ya kisiasa na kimfumo yatasukuma China kuelekea ushiriki mkubwa wa kisiasa wa kimataifa, haswa inapojiendeleza kijeshi na kiuchumi.

8- Hatimaye, iwe nchi hizi ni Amerika, China, au zote mbili, zinashindana katika ulimwengu huu hazina kheri yoyote bali uovu tu unaozizunguka na wafuasi wao, na hadhara batili ambayo kwayo watu wake hawajafanikiwa. Kinachoonekana leo kama kuinuka kwao duniani ni kutokana na kutokuwepo kwa dola inayoeneza kheri duniani kote, ikikandamiza maovu yao na kuharibu miundo yao. Dola hiyo itarudi, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu: Khilafah Rashida, ambayo itawaondoa kama ilivyowaondoa watangulizi wao—Wafursi na Warumi. Umma wa Kiislamu ni taifa lililo hai, changamfu, linalokwenda kwa haraka kwenye njia yake ya asili uliopewa na Mwenyezi Mungu:

[كُنْتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنْكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ]

“Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu.” [Aal-i Imran:110].

Hakika, ndani ya Ummah kuna kundi aminifu kwa Mwenyezi Mungu, wakweli kwa Mtume Wake (swt), wakidumisha njia hiyo, mchana na usiku, hadi ahadi ya Mwenyezi Mungu na bishara njema za Mtume Wake zitakapotimizwa kupitia wao, bila kuogopa lawama yoyote kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Azma yao haitalegea, na azimio lao halitadhoofika, hadi ahadi ya Mwenyezi Mungu itimizwe kupitia wao, na Khilafah Rashida irudi, ikifungua Roma kwa mikono ya Waislamu kama Konstantinopoli ilivyofunguliwa. Ahmad amesimulia katika Musnad yake kutoka kwa Abdullah ibn Amr ibn al-As, ambaye alisema: Tulipokuwa karibu na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) tukiandika, aliulizwa: “Ni miji gani kati ya miwili itakayofunguliwa kwanza: Konstantinopoli au Roma?” Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema: «مَدِينَةُ هِرَقْلَ تُفْتَحُ أَوَّلاً يَعْنِي قُسْطَنْطِينِيَّةَ» “Mji wa Heraclius utafunguliwa kwanza, maana yake Konstantinopoli.”

[وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللَّهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ]

“Na siku hiyo Waumini watafurahi. Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.” [Ar-Rum:4-5]

1 Jumada al-Akhir 1447 H

22/11/2025 M

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu