Jumapili, 22 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/24
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali
Matukio ya Kisiasa nchini Iraq
Na Dori ya Al-Kadhimi katika Kuitumikia Amerika

(Imetafsiriwa)

Swali: Kama ilivyo mashuhuri, Al-Kadhimi alijishindia imani ya idadi kubwa ya Bunge linalo unga mkono Iran, ingawa anatuhumiwa na pande zilizo tiifu kwa Iran na watu wake nchini Iraq kushirikiana na Amerika katika mauaji ya Soleimani, na baadhi ya watu wa Iran wanamtaja kama mtu wa Amerika. Hivyo je, hili lina maana kuwa Al-Kadhimi ana uungwaji mkono mkubwa kutoka Amerika, na hivyo hajali kuhusu uingiliaji kati wa Iran na watu wake nchini Iraq? Na je, Amerika ingali inaichukulia Iraq kuwa kitovu cha nguvu, na kwamba Al-Kadhimi ni mtumwa wa Amerika wa kudumisha ushawishi wake katika kitovu hiki cha nguvu? Mwenyezi Mungu akulipe kheri.

Jibu: Ili kupata jibu la ufafanuzi kwa maswali hayo ya juu, tutatathmini mambo yafuatayo:

1- Amerika inaipa umuhimu mkubwa Iraq, kama alivyo sema Raisi wa Amerika hivi majuzi: ["Iraq ni nchi imara na muhimu, na ina dori kubwa katika eneo hilo na katika kupata utulivu wa kieneo na kimataifa" na kusisitiza "umakini wa Amerika katika kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizi mbili na kuwa tayari kwa nchi yake kutoa msaada muhimu wa kiuchumi ili kuusadia uchumi wa Iraq…" (Chanzo: gazeti la 'The Independent na 'The World', 11/5/2020)]. Hii ndio sababu Amerika imeiangazia, hivyo ikatuma jeshi kubwa lenye idadi ya wanajeshi 250 elfu, kuikalia na kuunda muungano wa nchi 49 zilizo shiriki na takriban wanajeshi 50 elfu, pamoja na kampuni ovu za usalama, kama vile American Blackwater, ambayo makao makuu yake yako katika jimbo la Carolina Kaskazini, ili kutekeleza misheni chafu kuanzia ubanduaji, mauaji, wizi, na ulinzi wa maafisa wa Kiamerika, makao yao makuu na misheni zao, na imeasisi kambi za kijeshi kuwa za kudumu ambapo kwa sasa ziko kambi kuu tatu: Ain al-Asad katika mkoa wa Anbar, Kambi ya Anga ya Balad katika mkoa wa Salah al-Din na Kambi ya Al-Taji kaskazini mwa Baghdad. Kuna Makubaliano ya Mpangilio wa Kistratejia, yaliyo chapishwa na Amerika na Iraq mnamo 17/11/2008.

Imeelezwa katika Makubaliano hayo ya Mpangilio wa Kistratejia: "…kuthibitisha hamu ya kikweli ya nchi zao mbili kuasisi uhusiano wa muda mrefu wa ushirikiano na urafiki… na kusisitiza uhusiano huu wa muda mrefu katika nyanja za kiuchumi, kidiplomasia, kitamaduni na usalama… makubaliano haya yatabakia katika utekelezaji isipokuwa ikiwa pande zote mbili zitawasilisha arifu ya kimaandishi kwa upande wa pili kwamba wanataka kumaliza makubaliano haya, na umalizaji huo utatekelezeka mwaka mmoja baada ya tarehe ya arifu hiyo… na ili kuimarisha usalama na utulivu nchini Iraq, pande mbili hizi zitaendelea kufanya kazi ili kuunda uhusiano wa ushirikiano wa karibu baina yao kuhusiana na mipangilio ya ulinzi na usalama … nk." Haya ni makubaliano ya kikoloni kwa maana halisi ya neno hili, yanayoipa Amerika haki ya kuingilia mambo ya Iraq chini ya jina "uhusiano wa ushirikiano wa karibu baina yao kuhusiana na mipangilio ya ulinzi na usalama"!  

2- Maandamano yalianza nchini Iraq dhidi ya ufisadi, mapendeleo na ufujaji wa maafisa, kukithiri kwa ukosefu wa ajira miongoni mwa watu, kuzorota kwa huduma za umma na kuzorota kwa hali za maisha na bei za juu, hususan bei za umeme. Hili limejumuisha eneo lenye uungaji mkono mkubwa kwa serikali. Maandamano yalianza tangu 2010 na huwaka na kuzima kila mwaka ima baada ya kugandamizwa kwake au baada ya ahadi za urongo kutoka kwa mamlaka za kufikia matakwa ya waandamanaji, au kupitia baadhi ya nguvu za kisiasa zilizomo ndani ya serikali kufanya kazi kuyadhibiti. Lakini, maandamano ya hivi karibuni yaliyo lipuka tangu mwanzoni mwa Oktoba 2019 yalikuwa tofauti, kwa sababu waandamanaji walikataa kuacha kuandamana licha ya kukandamizwa kwao, na walizikataa nguvu hizo za kisiasa zilizo kuwa zikifanya kazi kuyadhibiti maandamano hayo, hivyo ukandamizaji ukaongezeka juu ya waandamanaji kuanzia mauaji, kujeruhiwa, na kifungo. Wakati huu, maandamano yalijumuisha shambulizi juu ya Iran na waandamanaji walimwaga hasira zao juu yake na balozi zake na vituo vyake kwa sababu ya majibu ya mashirika ya Iran nchini Iraq kwao, na kwa sababu waliona kiasi cha mafungamano ambayo serikali, mirengo ya kisiasa na wanamgambo waliyo nayo kwa Amerika ima kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja, na kasi ya maandamano hayo ikawa ya nguvu. Serikali na Waziri Mkuu, Adel Al Mahdi, walionyesha kwamba wameshindwa kudhibiti hali, ili kutatua tatizo hilo, na kufikia matakwa ya waandamanaji wanaolingania kupinduliwa kwa serikali, ikimlazimu Abdul-Mahdi kutangaza kujiuzuli kwake mnamo 30/11/2019 ili kuiokoa serikali, na siku iliyo fuatia, Bunge lilikubali kujiuzulu kwake mara moja. Abdul-Mahdi akawa kinara wa serikali ya muda. Na Raisi wa Jamhuri, Barham Salih, mnamo 26/12/2019 akalazimika kukiuka katiba kwa kukataa kumpa Asaad Al-Eidani, mgombeaji wa mrengo kubwa zaidi bungeni (Al-Banaa), jukumu la kuunda serikali, kwa sababu waandamanaji walimkataa mgombeaji huyu kutokana na dori yake kama gavana wa Basra katika majiribio ya kuwakanyaga kanyaga waandamanaji huko. Maandamano haya yalivutia zaidi kuliko yaliyo tangulia.

3- Wakati huo huo, imetokea kwamba mapote yanayo nasibishwa na kundi maarufu, Al-Hashd Ash-Shaabi, yalirusha makombora katika kambi ya Kiamerika karibu na Kirkuk mnamo 28/12/2019 bila ya sababu, yakimuuwa Mwamerika mmoja anaye fanya kazi kambini humo, na inaonekana kana kwamba hili lilifanywa nje ya muktadha kwa sababu kinara wa kundi hilo maarufu, Al-Hashd Ash-Shaabi, Falih Al-Fayyadh alikuwa amezuru Washington miezi miwili iliyo pita mnamo 19/10/2019, na kukutana na Waziri wa Ulinzi, Mark Esper, akiwepo Mwenyekiti wa Muungano wa Wakuu wa Kijeshi, Mark Milley. Alitangaza kuwa uhusiano baina ya nchi mbili hizi, hususan ushirikiano wa kijeshi, umezungumziwa, na sasa mauaji haya yanatokea! Kutokana na mauaji haya ya Mwamerika, jeshi la Kiamerika lilitekeleza mashambulizi ya angani mnamo 29/12/2019, dhidi ya kundi la wanamgambo la Hezbollah, mojawapo ya mapote ya kundi hilo maarufu. Na likatangazwa kuwa kwa uchache wanachama 27 waliuwawa na 62 wa brigedi hiyo kujeruhiwa. Amerika ilifanya shambulizi la angani kupitia droni mnamo 3/1/2020 karibu na Uwanja wa Ndege wa Baghdad, ambapo ilitangazwa kuuwawa kwa Qasem Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Askari wa Mapinduzi wa Iran, aliyekuwa na ushawishi juu ya kundi maarufu, pamoja na naibu kamanda wa kundi maarufu, Abu Mahdi al-Muhandis, na maafisa wengine wanne kutoka katika Askari wa Mapinduzi wenye vyeo vya: brigedia jenerali, kanali, meja, na kapteni. Amerika imepatiliza matukio haya kwa manufaa ya raisi wake, ambaye anataka kujishindia alama ili kuimarisha nafasi zake za muhula wa pili wa uraisi wa Amerika.

Lakini, inaonekana kwamba matukio haya yalitia joto anga dhidi ya Amerika, na hii ndio sababu bunge la Iraq lilichukua uamuzi mnamo 5/1/2020 kufanya kazi kumaliza uwepo wowote wa majeshi ya kigeni, na wakatoa wito kwa Waziri Mkuu kutekeleza uamuzi wao. Raisi wa serikali ya muda, Abdul Mahdi, akashirikiana nao. Majibu ya Amerika kwa bunge la Iraq yalifanywa na Raisi Trump kupitia kutishia kuiwekea vikwazo Iraq, na akasema, "Amerika haitaondoka Iraq isipokuwa ikiwa serikali ya Iraq italipa gharama ya kambi hiyo ya Amerika huko", na akasema, "Tuna kambi ya anga huko ambayo ni ghali mno. Ilihitaji mabilioni ya dolari kuijenga muda mrefu kabla ya kuja kwangu. Hatutaondoka Iraq isipokuwa ikiwa watatulipa gharama zake, na endapo Iraq itataka kuondoka kwa majeshi ya Amerika, na hili halitafanywa kwa msingi wa kirafiki, tutawaekea vikwazo juu yao ambavyo hawajapatapo kuviona. Vikwazo vya Iran ubavuni mwake itakuwa ni jambo dogo." (Chanzo: Sky News 5/1/2020)

4- Iran kisha ikatangaza kuwa imeanzisha mashambulizi ya makombora mnamo saa 1:20 mchana kwa saa za Tehran, mwanzoni mwa siku mnamo 8/1/2020 juu ya kambi za Amerika nchini Iraq, na wakawauwa kwa uchache Waamerika 80 katika shambulizi hilo la makombora la Iran juu ya kambi za Amerika. Katika runinga kichwa cha habari kilikuwa "Tumelipiza kisasi cha Soleimani", lakini Amerika ilitambua shambulizi hilo na kukataa kuuwawa kwa yeyote katika watu wake! Kisha kasi ya matukio haya ikawa sahali na kupoa pasi na kuongezeka zaidi! Kisha Muhammad Tawfiq Allawi, aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano katika serikali ya Al-Maliki, akatangaza mnamo 1/2/2020 kuwa Raisi wa Jamhuri alimwagiza kuunda serikali. Waandamanaji wakatangaza kupinga kwao uteuzi wa Allawi, huku wakitangaza kuwa wanapinga kila mwanasiasa aliye husishwa katika serikali tangu uvamizi wa Amerika mnamo 2003, na kabla ya kazi yake kurefushwa, alijiuzulu. Kisha, mnamo 16/3/2020, Raisi wa Jamhuri akamwagiza Adnan Al-Zarfi kuunda serikali.

Alishikilia nyadhifa nyingi za usalama katika serikali na alikuwa ni gavana wa Najaf baada ya kuvamiwa kwake, lakini Al-Zarfi akaomba msamaha mnamo 9/4/2020 kwa kushindwa kwake kuunda serikali. Mnamo 9/4/2020, Raisi wa Iraq Barham Salih alitangaza kuwa kinara wa Shirika la Ujasusi la Iraq, Mustafa Al-Kadhimi, amepewa jukumu la kuunda serikali ambayo haiegemei upande wowote, na huu ni ukiukaji mwengine wa katiba. Imeripotiwa kwamba Mustafa Al-Kadhimi alikuwa anafanya kazi kama mpinzani wa serikali ya Saddam ng'ambo, na baada ya 2003 alirudi Iraq kwa Sulaimaniyah. Huku akifanya kazi kama mhariri mkuu wa mambo ya Iraq katika mtandao wa habari wa Kiamerika wa Al-Monitor, alikuwa akitetea kwa dhati kwamba mahusiano kati ya Iraq na Amerika ni lazima yawe imara kabisa, hivyo alisema katika makala moja: ["Ufuatiliaji wake juu ya mahusiano kati ya Iraq na Amerika baada ya 2003 unaonyesha kwamba pindi yanapo kuwa dhaifu na duni, upande mmoja huenda yakafungua ule mlango kwa watu wengine kutoka nje kuingia, na pia kusababisha hasara kwa maslahi ya pamoja ya Iraq na Amerika katika eneo hili na hivyo basi Iraq na Amerika zinapaswa kutathmini upya uhusiano wao ili kuunda uhusiano imara na wa kistratejia unaosaidia kuregesha mizani baina ya dola katika eneo hili, na kuhakikisha maslahi ya pamoja ya pande mbili hizi" (Chanzo: Al-Monitor, tovuti ya Kiamerika, 2/10/2015)]. Anafanya kazi kwa siri na dhahiri kwa ajili ya maslahi ya huduma za usalama za Kiamerika, na kwa uratibu kamili na majeshi vamizi ya Amerika nchini Iraq tangu kurudi kwake Iraq baada ya 2003, na kwa sababu hivyo ndivyo alivyo, Wairaqi wengi walishangazwa na Al-Abadi kumwasilisha kwa ghafla mnamo 2016 kama mkurugenzi wa ujasusi, wadhifa nyeti mno, na unaohitaji mtu wa kutegemewa sana nchini Amerika. ["Mnamo 2016, Waziri Mkuu Haidar al-Abadi aliwashangaza Wairaqi kwa kumteua mtu kama Mustafa al-Kadhimi, mwanahabari na mtetezi wa haki za kibinadamu, kuongoza ujasusi. Huu ndio upeo wa juu wa vita dhidi ya ISIS ambayo imeikali sehemu ya nchi hii katika kipindi fulani kabla ya jeshi la Iraq, kwa usaidizi kutoka kwa muungano wa kimataifa, kufaulu kuishinda…" (Chanzo: France 24, 8/5/2020)].

Zaidi ya hayo, Amerika haikuficha uhusiano wake naye alipo kuwa katika ujasusi (na ripoti moja iliyo chapishwa na Jarida la Kiamerika la 'Wall Street' ilimnukuu David Schenker, Waziri Msaidizi wa Kigeni wa Mambo ya Mashariki ya Karibu, akisema kuwa Al-Kadhimi alifanya "kazi nzuri" alipo kuwa kinara wa ujasusi na yuko tayari kushirikiana naye kama waziri mkuu.) (Chanzo: Mtandao wa Al-Jazeera Net kutoka jarida la Wall Street, 30/5/2020). Alikuwa amezuru Saudi Arabia mnamo 2017 pamoja na Waziri Mkuu wa zamani Haider al-Abadi, na alionekana akimkumbatia kwa kipindi kirefu rafiki yake binafsi, Mfalme Mtarajiwa wa Saudia Muhammad bin Salman, anayejitolea kuwatumikia Waamerika!

5- Mnamo 7/5/2020, bunge la Iraq liliipa imani serikali ya Al-Kadhimi kwa kura 255 za wabunge kati ya wabunge 329, hata ingawa Al-Kadhimi anatuhumiwa kutoa usaidizi kwa Amerika katika mauaji ya Qasem Soleimani na Al-Muhandis. Abu Ali Al-Askari, afisa wa usalama katika Brigedi ya Hezbollah katika wanamgambo wa Iraq, alimshambulia, "na kumtuhumu kinara wa Huduma ya Ujasusi ya Iraq, Mustafa al-Kazemi, "kusaidia" katika mauaji ya Kamanda wa Iran wa Kikosi cha Quds, Qasem Soleimani, na naibu wa mkuu wa Kundi Maarufu, Abu Mahdi al-Muhandis" (Chanzo: Al-Hurra, 3/3/2020). Na katika jibu la kwanza kutoka kwa ushawishi wa Iran, ["Kiongozi shupavu wa kidini Ali Al-Kurani, ambaye yuko karibu na wanamgambo wa Lebanon wa Hezbollah, alimshambulia Al-Kadhimi na kumtuhumu kubeba ajenda za Kiamerika" (Chanzo: Habari za Al-Ain, 15/5/2020)]. Kwa kutazama kwa karibu, tunapata kuwa pande zilizo tiifu kwa Iran zilimpigia kura na kumpa imani yao, na sasa wanamtuhumu kufanya kazi kwa ajili ya Amerika na kumtuhumu kushirikiana nayo katika kuwaua watoto wao, na kumuua Soleimani na Al-Muhandis.

Sio hayo tu, bali alikataa matakwa yao yote na kukataa ugavi maarufu, yaani, kuzinyima pande hizo "ngawira" za uwaziri. Yote haya yanaashiria kwamba Amerika ina ushawishi mkubwa juu ya pande hizi moja kwa moja au kupitia Iran. Na uhasama iliyo tangazwa na Iran ni ya kupotosha tu. Hadi kufikia kuuwawa kwa Soleimani ni dhoruba ya kimaneno pekee ndio iliyo kuwa ikiendelea jijini Tehran ambayo ilimalizika kwa muda mchache, kana kwamba hakuna kilicho tokea kwa sababu ya mafungamano yake na Amerika nyuma ya pazia. Pengine pande hizo za kimadhehebu hazikutambua kwamba kuwanyima nyadhifa za uwaziri sio adhabu kwao, bali ni ili kulififisha wimbi la hasira ninalo fagia barabara za Iraq, baada ya wimbi hilo

kurudi tena upya baada ya kuhafifishwa kwa hatua dhidi ya virusi vya Korona nchini Iraq. Hii yamaanisha kuwa nyingi ya pande hizi zimedhamini utiifu kwa Amerika wa moja kwa moja au kupitia Iran, na uonyeshaji imani kwa njia hii imevipelekea vyombo vya habari kuzungumzia kuhusu makubaliano au mpango!

Ibrahim al-Zubaidi alieleza katika gazeti la London la Al-Arab, "kwamba baadhi ya miungano na mawimbi ya kisiasa nchini Iraq yalimkataa Mustafa al-Kadhimi na kutoa taarifa dhidi yake zilizombandika jina la kuwa kibaraka wa Amerika, zikimtuhumu kupanga mauaji ya Qasem Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis" na al-Zubaidi aliendelea kusema, "Kama mulivyo ona na munavyo ona kuwa mawimbi ya kisiasa yalikubaliana kupitisha Bungeni, kana kwamba hakuna kitu kilicho tokea, isipokuwa tu wakati amri na maagizo yalipotolewa kwake na ubalozi wa Wilayat Al Faqih jijini Baghdad, au kutoka katika ubalozi wa Mjomba Donald Trump. Je, hii si aina ya usanii wa kipuzi?" (Chanzo: Al Aran, gazeti la London  mnamo 8/5/2020), na kisha Al-Kadhimi akajishindia imani licha ya tuhuma! Hii ni kuongezewa na yale yanayo weza kutokea kuanzia "upigaji msasa" hadi Al-Kadhimi katika taarifa ambayo itatolewa kuhusu mazungumzo ya kistratejia kati ya Amerika na Iraq, yanayo tarajiwa katikati ya mwezi huu. ["na nchi mbili hili hizi zinapanga kufanya mazungumzo ya kistratejia katikati ya mwezi ujao, ili kufafanua masharti ya uhusiano wao wa mustakbali" (Chanzo: mtandao wa Al-Jazeera Net kutoka kwa Jarida la Wall Street, 30/5/2020)].

6- Katika kikao hicho hicho cha kujenga imani, Al-Kadhimi aliichukulia serikali yake kuwa ya muda mfupi, na kwamba anatafuta uchaguzi wa mapema, na akasema: "Mojawapo ya vipaumbele vya serikali yake ni kufanya uchaguzi wa mapema katika kuitikia matakwa ya haki ya watu", katika jaribio la kuwamiliki waandamanaji na wapinzani na kwa hili aliongeza: ["Kufanya matayarisho kwa ajili ya uchaguzi wa haki yahitaji madai ya ubwana wa dola katika maeneo yote, na mbele kabisa, kudhibiti silaha mikononi mwa dola na majeshi yake na kwa amri ya amiri jeshi mkuu wa vikosi vya majeshi, na sio kuigeuza nchi kuwa uwanja wa kulipiziana visasi, na kuzuia utumiaji wa ardhi ya Iraq kushambulia wengine" (Chanzo: BBC, 7/5/2020)]. Upataji ujasiri wa Al-Kadhimi ulikuwa ni mafanikio muhimu na habari njema kwa Amerika, inayotaka kuifanya serikali iliyoiasisi kuwa imara ili kupata utulivu wa ushawishi nchini Iraq na kuihalalisha, na hii ndio sababu Waziri wa Kigeni wa Amerika, Mike Pompeo, kwa haraka alizungumza kwa simu na Mustafa Al-Kadhimi ili kuyabariki mafanikio yake ya imani ya Bunge na kuwa Waziri Mkuu wa Iraq, na akaandika katika akaunti yake ya Twitter mnamo 7/5/2020 akisema: "Ni jambo la kufurahisha leo kuzungumza na Waziri Mkuu mpya wa Iraq Mustafa Al-Kadhimi, sasa kazi ya haraka na umakini inakuja kutekeleza mabadiliko yanayo takikana na watu wa Iraq", na akaongeza, "Naahidi kumsaidia kutekeleza ajenda yake ya kijasiri"

Na msemaji wa Wizara ya Kigeni ya Amerika Morgan Ortagus alisema katika taarifa kuwa: ["Katika kuiunga mkono serikali mpya, Amerika itaisukuma mbele kwa afueni inayo husiana na umeme "kuagiza umeme kutoka Iran ndani ya siku 120" kama ofa ya hamu yetu kusaidia kupatikana kwa hali nzuri kwa ajili ya mafanikio …" (Chanzo: KUNA, 7/5/2020)]. Kisha, Raisi wa Amerika yeye mwenyewe akazungumza na Al-Kadhimi. Msemaji wa Ikulu ya White House, Jad Dair, alisema katika taarifa moja kwamba: ("Mnamo Jumatatu 11/5/2020 Raisi Trump alizungumza na Al-Kadhimi kwa njia ya simu kumpongeza kwa kuidhinishwa na bunge la Iraq kwa ajili ya serikali yake… Na Raisi ameelezea usaidizi wa Amerika kwa Iraq wakati huu wa janga la maambukizi ya virusi vya Korona linalo endelea, na kusisitiza maslahi ya pamoja na Iraq ili kupata ushindi wa kudumu dhidi ya ISIS… na kwamba Raisi pia anamshajiisha Waziri Mkuu kuzungumzia matakwa ya watu wa Iraq ya mabadiliko na uchaguzi wa mapema …" (Chanzo: Reuters, Al-Hurra (ya Kiamerika), 12/5/2020).

7- Miongoni mwa hatua za kwanza za Al-Kadhimi alipo kutana kwa mara ya kwanza na mawaziri mnamo 9/5/2020 ni tangazo lake la kumteua tena Abdel-Wahab Al-Saadi kama mkuu wa vile vinavyo itwa vyombo vya kupambana na ugaidi nchini Iraq, na katika taarifa za vyombo vya habari, alisema: "Tumeamua kumrudisha shujaa, ndugu, Abdel-Wahab Al-Saadi, katika wadhifa wake kama mkuu wa vyombo vya kupambana na ugaidi". (Vikosi vya kupambana na ugaidi hukadiriwa kuwa vikosi bora zaidi katika jeshi la Iraq, kwani vimepewa mafunzo na silaha na vikosi vya Amerika, na vimetumika kama nguvu ya msukumo katika vita dhidi ya ISIS kwa kipindi cha miaka mitatu 2014-2017) (Chanzo: Shirika la Kituruki la Anatolia, 9/5/2020). Runinga ya Al-Arabi iliripoti mnamo 11/5/2020 kuwa uamuzi wa Al-Kadhimi wa kumteua tena Abdel-Wahab al-Saadi na kupandishwa cheo kwake hadi kiongozi wa shirika la kupambana na ugadi imekuja kama jibu kwa matakwa ya barabarani, kwani vyombo vya kupambana na ugaidi nchini Iraq kimsingi huitegemea Amerika, (katikati mwa 2017 ripoti moja ya Amerika iliitaja "huduma ya kupambana na ugaidi" kuwa bora zaidi kuwahi kuundwa na Amerika nchini Iraq).  

Vyombo vya jeshi la Iraq viliasisiwa na Amerika kwa vipimo vya uteuzi na mafunzo ambayo huenda yakawa maalumu kama yale yanayo tumiwa katika kusajili vikosi vya Amerika vya Operesheni Maalumu, kwa mujibu wa ripoti iliyo chapishwa na Taasisi ya Washington ya Sera ya Mashariki ya Kati, (Chanzo: Arabic 21, 30/9/2019). Al-Saadi, kwa mujibu wa chanzo kilicho tangulia, alipandishwa cheo katika nyadhifa za kipekee za luteni jenerali mnamo 2016, na kisha katika Brigedi mnamo 2008 mikononi mwa kibaraka wa Amerika Al-Maliki, ambapo inaashiria kiwango cha kutosheka kwa Amerika na afisa huyu wa Iraq. Vyombo hivi vimepata umaarufu unaotokana na vitu viwili ambavyo Wairaqi wanao andamana barabarani hawakuvitambua: cha kwanza ni kuwa Amerika yenyewe ilivizuia vyombo vya kupambana na ugaidi kutowauwa waandamanaji, na mbinu hii hii ya Amerika ndio iliyo tumika nchini Misri mnamo 2011 wakati ambapo jeshi la Misri lilipo apa kutotumia nguvu dhidi ya waandamanaji, na ilikubaliwa na halaiki ya waandamanaji kuundwa kwa baraza la kijeshi baada ya kubanduliwa Hosni Mubarak, ikimaanisha kuwa Amerika ilitaka mkono 'msafi' kwa shirika la kupambana na ugaidi la Iraq ili liwe badili ya mabadiliko. Ama jambo la pili, watu wa Iraq walidhani kuwa Al-Saadi, kwa sababu ya kufutwa (kuhamishwa) Abdel-Mahdi kutokana na kupambana na ugaidi, kulipingwa na serikali inayo ongozwa na Abdel-Mahdi, hivyo walimtaka Al-Saadi kama badali; vyenginevyo, waandamanaji wa Iraq walipinga vikali ushawishi wa Iran pamoja na wa Amerika nchini Iraq.

Na tulitaja kitu kuhusiana na hilo katika chapisho letu la tarehe 04/12/2019, ambapo tulisema: "Kuhusu Iraq: Amerika inaitawala Iraq takriban moja kwa moja nyuma ya pazia. Ubalozi wake jijini Baghdad una wafanyi kazi 16,000, wanaofuatilia kazi za wizara zote za Iraq, hususan sekta za mafuta na usalama, na ndio ubalozi mkubwa zaidi wa Amerika duniani. Ina kambi nyingi za kijeshi nchini Iraq, maarufu zaidi ya hizo ni kambi ya Ain al-Asad iliyoko Anbar. Katika wiki ya mwisho ya mwezi uliopita, Amerika ilikoleza ujumbe wake, hivyo kumekuweko na ziara ya ghafla ya Makamu wa Raisi, Pence, mnamo 23/11/2019 katika kambi ya Ain al-Asad, na kabla ya wiki kupita baada ya ziara ya Makamu wa Raisi Iraq, Amerika ilimtuma Kamanda wa Muungano wa Wakuu wa Kijeshi wa Amerika Mark Milley hadi Baghdad mnamo 27/11/2019. Huu ndio ushahidi wa ufuatiliaji wa kudumu wa Amerika, hususan kwa kuwa Iraq ni kesi nyeti kwa Amerika. Imegunduliwa kuwa vyombo vya kupambana na ugaidi nchini Iraq, ambacho ni kikosi kubwa cha kijeshi kilicho undwa na Waamerika na kupewa zana bora zaidi za kijeshi, viko mbali na sera ya kuangamiza maandamanao, na inaonekana kwamba waandamanaji katika Uwanja wa Tahrir wanakitazama kikosi hiki kama mwokozi wao kutokana na wanasiasa wafisadi kwani wananyanyua picha kubwa ya Jenerali Abdel-Wahab Al-Saadi mmoja wa viongozi wa shirika hilo baada ya kufutwa kwake na Abdel-Mahdi, kana kwamba kikosi hiki kinakubalina na waandamanaji hao kuwa na dori katika kupangilia suluhisho." Mwisho wa Nukuu. 

8- Tamati ni kuwa Al-Kadhimi ni mtumwa wa Amerika nchini Iraq

A- Katika kazi yake ya kihistoria: Alipokuwa anafanya kazi kama mhariri mkuu wa mambo ya Iraq katika mtandao wa habari wa Kiamerika Al-Monitor, na kutetea vikali, mnamo 2015, kuwa uhusiano kati ya Amerika na Iraq ni lazima uwe imara mno.

B- Katika jukumu lake mnamo 2016 kama Mkurugenzi wa Ujasusi, na kukubaliwa kwake na Amerika kama ilivyo nukuliwa na Jarida la Kiamerika la 'Wall Street' kutoka kwa David Schenker, Waziri Msaidizi wa Kigeni, kuwa Al-Kadhimi alifanya "kazi nzuri" alipokuwa mkuu wa ujasusi, na akakubali kushirikiana naye kama Waziri Mkuu.

C- Kisha uhusiano wake dhahiri na rafiki yake Muhammad bin Salman, hususan alipo zuru Saudi Arabia mnamo 2017 pamoja na Waziri Mkuu wa zamani Haider al-Abadi na kuonekana akimkumbatia kwa muda mrefu "rafiki yake wa kibinafsi", Mfalme Mtarajiwa Mohammad bin Salman, aliyejitolea kuwatumikia Waamerika".

D- Kupata imani ya Bunge mnamo 7/5/2020, kwa usaidizi wa Amerika wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja kutoka Iran, kupitia kuzishinikiza pande ambazo ni tiifu kwa iran, ingawa al-Kadhimi anatuhumiwa kwa kutoa usaidizi kwa Amerika katika mauaji ya Qasem Soleimani na al-Muhandis, na kwamba anatekeleza "Ajenda za Waamerika". Na yote haya yanaashiria kwamba Amerika ina ushawishi mkubwa nchini Iran, na uhasama ilio tangazwa na Iran si chochote ila ni upotoshaji tu!

E- Kisha Abdel Wahab Al-Saadi, mnamo 9/2/2020, alimteua tena kama kinara wa Vyombo vya Kupambana na Ugaidi nchini Iraq, na vikosi vyake vimepewa mafunzo na vikosi vya Amerika. Ripoti moja ya Amerika iliyo chapishwa na Taasisi ya Sera ya Mashariki ya Kati ya Washington katikati mwa 2017 ilivitaja vyombo hivi kama "vyombo bora zaidi kuwahi kuundwa na Amerika nchini Iraq…" (Chanzo: Arabic 21,30/9/2019)

Yote haya yanaonyesha kiwango cha "msimamo uliopendelewa" ambao Amerika anampa al-Kadhimi na watu wa Iraq ni lazima watambue hili kabla hawajajutia!

9- Natamatisha kwa ujumbe mmoja, na nasema kwamba hakuna uokozi kwa Iraq wala kurudi kwa utukufu na ngumu yake ili iwe nchi muhimu na kitovu cha dola kuu yenye kuzikomboa Amerika, Uingereza na nchi nyenginezo za kikoloni isipokuwa kwa kurudisha chimbuko la fahari yake, nalo ni Uislamu kupitia kusimamisha dola yake, Khilafah Rashidah kwa njia ya Utume na Mwenyezi Mungu Al-Aziz Al Qawi ndiye Mkweli:

 [وَلِلّٰهِ العِزَّةُ وَلِرَسُولِه وَلِلمُؤمِنِينَ وَلَكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لا يَعلَمُونَ]

“Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui.” [Al-Munafiqoon: 8].

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumatatu, 29 Juni 2020 09:21

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu