Jumatano, 18 Rajab 1444 | 2023/02/08
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Miaka 100 ya Ufisadi, Mporomoko, Vita, Uharibifu na Tabu

Ummah wa Waislamu na dunia kwa ujumla imo katika machafuko tangu kuanguka kwa Khilafah mnamo 28 Rajab 1342 Hijria. Kutokuwepo kwa Khilafah kumesababisha pengo kubwa la kiungozi ambalo hakuna utawala duniani uliofaulu kuchukua mahali pake mpaka leo. Hakika hakuna serikali iliyo nyanyuka na kutoa muelekeo wa dharura uliohitajika. Badala yake, kumechipuza asasi dhalimu za serikali duniani ambazo zinajipiga kifua kwa kusababisha yafuatayo:

Ufisadi: Yale yanayoitwa mataifa ‘yenye nguvu’ yaliyochipuza baada ya kuivunja Khilafah, kwa haraka yalizidhibiti ardhi zilizobakia kwa kuzigawanya kwa vibaraka wao watiifu. Wakabuni vijidola 54 kutoka katika ile iliyokuwa Dola Moja ya Khilafah. Kwa kuongezea, waliwaagiza watumwa wao watawala vibaraka kuendeleza ‘ajenda ya kimishenari’ mpaka leo. Ambayo malengo yake yalikuwa: moja- kuziweka hai hisia za utaifa miongoni mwa raia ndani ya kila kijidola. Pili- kuubeba na kuulingania urasilimali katika ngazi ya kiserikali kwa njia ya siri na dhahiri.  

Natija yake ni kuwa tunayo mataifa na falme zilizotapakaa ndani ya ardhi ya Waislamu zinazodai kuwa ni za ‘Kiislamu’ lakini kiuhalisia wanajaribu tu kusema uwongo dhidi ya  Mwenyezi Mungu (swt) kwa kuwa SIZO. ٱنظُرۡ كَيۡفَ كَذَبُواْ عَلَىٰٓ أَنفُسِہِمۡ‌ۚ وَضَلَّ عَنۡہُم مَّا كَانُواْ يَفۡتَرُونَ﴿ “Tazama jinsi wanavyo jisemea uwongo wenyewe. Na yamewapotea waliyo kuwa wakiyazua.” [Al-Anaam: 24].قُلۡ إِنَّ ٱلَّذِينَ يَفۡتَرُونَ عَلَى ٱللَّهِ ٱلۡكَذِبَ لَا يُفۡلِحُونَ﴿ “Sema: Hao wanao mzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafanikiwa.” [Yunus: 69].

Zimesimama juu ya mfumo batili wa kikoloni wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake ovu kama vile demokrasia n.k. Zipo kudunisha dori ya Mwenyezi Mungu (swt) kama Mtungaji sheria kusimamia mambo ya mwanadamu. إِنِ ٱلۡحُكۡمُ إِلَّا لِلَّهِ‌ۚ﴿ “Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu tu. [Yusuf 12: 40]. Hivyo basi, wakatengeneza sheria za kibinadamu ili kuhukumu na kutawala watu kwazo. وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللهِ حُكْماً﴿ “Na nani aliye mwema Zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu.” [Al Ma’idah 5: 50].

Wanawaelekea na kuwataka mabwana zao Wamagharibi kuwapa muongozo juu ya sera, sheria na kanuni. Kwa hiyo kibla chao kipo katika miji ya Kimagharibi kama vile Washington, Paris, London na Moscow. Watawala vibaraka watiifu na mabwana zao Wamagharibi wamedumu katika kueneza ufisadi ardhini na baharini kwa jina la mageuzi! ﴿وَإِذَا قِيلَ لَهُمۡ لَا تُفۡسِدُواْ فِى ٱلۡأَرۡضِ قَالُوٓاْ إِنَّمَا نَحۡنُ مُصۡلِحُونَ “Na wanapo ambiwa: Msifanye uharibifu ulimwenguni. Husema: Bali sisi ni watengenezaji.” [Al-Baqarah: 11].

Mporomoko: Ni kupitia mikono yao na chuki zao ndio dunia imo katika mporomoko kama natija ya uenezaji uovu. ظَهَرَ ٱلۡفَسَادُ فِى ٱلۡبَرِّ وَٱلۡبَحۡرِ بِمَا كَسَبَتۡ أَيۡدِى ٱلنَّاسِ لِيُذِيقَهُم بَعۡضَ ٱلَّذِى عَمِلُواْ لَعَلَّهُمۡ يَرۡجِعُونَ﴿ “Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu.” [Ar-Rum: 41]. وَمَنۡ أَعۡرَضَ عَن ذِڪۡرِى فَإِنَّ لَهُ ۥ مَعِيشَةً۬ ضَنكً۬ا وَنَحۡشُرُهُ ۥ يَوۡمَ ٱلۡقِيَـٰمَةِ أَعۡمَىٰ﴿ “Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu.” [Ta Ha 20: 124].

Nidhamu ya kijamii iko katika mkanganyiko. Mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu yake ya kijamii yenye kipimo cha uhuru, imebuni njama feki ya ushindani baina ya wanaume na wanawake kwa sura ya ‘usawa wa jinsia.’ Njama hii inapigiwa upatu na watetezi wa wanawake na wamiliki wa viwanda. Wamewahadaa wanawake kwamba wanastahili kufanya kazi na kupata fursa sawa kama wanaume. Alas! Wamiliki wa viwanda walikuwa haja yao ni kupata waajiri watakao walipa mishahara duni kutokana na idadi kubwa ya wanawake ulimwenguni!  Kwa upande mwingine, watetezi wa wanawake walikuwa na lengo la kuwatoa wanawake majumbani mwao! Kwa kudunisha umama na kuwakejeli wanaoupa kipaumbele badala ya ‘ajira.’

Hatimaye. Imepelekea taasisi ya ndoa na uti wa familia kuvunjika. Wanandoa hawatizamani tena kama wandani walio na uwezo na dori za kipekee walizowekewa na Muumba - Mwenyezi Mungu (swt). Badala yake wanaitizama ndoa kuwa ni njia muafaka ya kukidhi mahitaji yao ya kighariza pasina na kuweko fungamano la kijamii. Kwa kuongezea, wanazingatia kuwa wao ni washirika walio na mamlaka yasiokuwa na mipaka na uhuru wa namna ya kuendesha muungano wao ‘familia.’ Natija yake ni kuongezeka kwa wazinifu, talaka, matatizo ya kiakili, msongo wa mawazo, kesi za kujiua, watoto waliopotoka n.k.

Nidhamu ya kiuchumi imekitwa katika kupatiliza utajiri wa watu kupitia utozaji ushuru wenye kukandamiza kisha baadaye ‘kuwekezwa’ katika miradi hewa inayowanufaisha wachache kwa njia ya hongo. Kwa kuongezea, nidhamu imetiwa kitanzi na kuzama ndani ya riba kiasi kwamba hakuna miamala iliyo salama.  Taasisi za Kimagharibi kama vile IMF na Benki ya Dunia huandaa sera, sheria na kanuni kisha kuwapa watawala wetu vibaraka wa wakoloni katika ardhi zetu ili kuzitekeleza!  Hivyo basi, utajiri wetu huporwa na kuhamishwa ng’ambo kwenda kuijenga na kuinawirisha miji ya Kimagharibi kwa gharama yetu!  Nidhamu ipo kwa ajili ya kuwalinda matajiri na kuwakandamiza masikini na hatimaye kuzidisha pengo baina ya matajiri na masikini!

Vita: Wamagharibi wakoloni wamedumu katika vita vyao dhidi ya kurudisha Khilafah. Daima wako mbioni kuchora mipango dhidi ya Uislamu na wafuasi wake.  Kwa hiyo, wamezindua vita vya kifikra na kijeshi ndani ya ardhi zetu. Vita vya kifikra vinatekelezwa kupitia mitaala ya elimu na mipango ya kithaqafa iliyowekwa kukuza utambulisho wa kisekula ndani yetu. Wanalenga kutufanya watumwa kwa mabwana wakoloni Wamagharibi na kudumisha utumwa wao juu yetu na ardhi zetu. Kwani, kufikiri kwetu kutakuwa kumefungika tu ndani ya sanduku la kisekula.

Vita vya kijeshi hufuatia pale ambapo vita vya kifikra vimeshindwa kutimiza ajenda zao ovu. Hutumika kututisha na kutufedhehesha ili kujisalimisha kikamilifu. Zana zao za mauaji hutumika kutumaliza kwa mamilioni kwa kisingizio chochote kitakachowafaa wao kwa mfano kutubandikiza kuwa ni magaidi au wenye misimamo mikali. Nyuma wakibakia wajane, mayatima, wazee n.k. wasiojiweza wakitafuta msaada.  

Uharibifu: ubomoaji mkubwa unashuhudiwa ndani ya ardhi zetu.  Kuangamizwa kwa miundo mbinu ya karne kama vile barabara, misikiti, vituo vya elimu, afya n.k. Inaweza kuthibitishwa ndani ya Syria, Libya, Iraq, Somalia, Afghanistan, Kashmir, Ardhi Tukufu ya Palestina n.k. Yote yakifanyika kwa jina la ukandamizaji wa kimfumo.

Tabu:  Kuteseka kunaendelea mpaka leo. Sio tu kwa Ummah wa Waislamu bali wanadamu kwa ujumla. Moto wa mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake umepenya ndani ya nyanja zote za maisha na unaendelea kuchoma kila kilichoko mbele yake! Hata yale yanayoitwa mataifa ‘yaliyoendelea’ yamo ndani ya fujo la kisiasa, kijamii na kiuchumi ambayo haijawahi kushuhudiwa hapo awali. Tafiti na fichuzi zimethibitisha kuwa kiwango cha matatizo wanayopitia wanadamu ni kikubwa mno.

Nukta hizo zimeangazia hali halisi iliyoko sasa katika ulimwengu tunamoishi kwa kukosekana Khilafah kwa miaka 100. Nidhamu ambayo ni makazi ya amani yenye kueneza amani na usalama kwa walio na mahitaji duniani kote. Hakika, ulimwengu una shauku ya kiongozi, Khalifah ambaye ataitikia vilio vya wenye matatizo. Atakayekuwa mlinzi na ngao yao dhidi ya njama na madhara yanayoletwa na maadui wa amani ya kweli. «إِنَّمَا الإِمَامُ جُنَّةٌ يُقَاتَلُ مِنْ وَرَائِهِ وَيُتَّقَى بِهِ» “Imamu  (Khalifah) ni ngao kwao. Wanapigana nyuma yake na kujilinda kwake.” [Muslim]. Hali itabakia hivi kwa kuwa Khilafah bado haijasimamishwa. Hii inawalingania wale wanaotafuta amani na utulivu wa kweli kufanya kazi kidharura kwa ajili ya kuirudisha kwa njia ya Utume.

#أقيموا_الخلافة               #خلافت_کو_قائم_کرو

#ReturnTheKhilafah          #YenidenHilafet          #TurudisheniKhilafah

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu