Jumamosi, 11 Rajab 1446 | 2025/01/11
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Vipi Khilafah Itakavyo Angazia Uraia na Wasiokuwa Waislamu

Mwenyezi Mungu (swt) asema:(وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ) “Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.” [21:107]

Uislamu ulikuja kama angazo kwa wanadamu wote, bila ya kuzingatia dini, dhehebu, tabaka au jinsia. Ndani ya Khilafah raia wote watafurahia manufaa ya nidhamu ya Kiislamu na ulinzi kamili wa maisha yao, mali yao na heshima yao bila ya ubaguzi.

 “Raia wote wa Dola ya Kiislamu wanastahiki kufurahia haki na majukumu ya kiShari'ah.”  (Kifungu cha 5 – Katiba Kielelezo ya Khilafah ya Hizb ut Tahrir)

Uislamu unapinga fikra zote za kiaswabia, ambazo zilikuwa ndicho kiini cha kuundwa kwa mataifa ya Kimagharibi. Uislamu unayavuka yote haya kwa sababu yananyima kitambulisho kwa msingi wa mtazamo mpana wa ulimwengu. Mtazamo huu umejengwa juu ya ufahamu kuwa viumbe vyote vimeumbwa na Muumba – Mwenyezi Mungu (swt) – na ni vitiifu kwa kanuni yake ya kimaumbile. Kwa mtazamo wa kijamii Uislamu huwatazama wakaazi wote kama wanadamu kuliko kuwatazama kwa makabila au matabaka yao. Natija yake ni wale wanaoishi katika maeneo ya Kiislamu hutazamwa kama raia, bila ya kujali itikadi, rangi au kabila.  

Uraia umejengwa juu ya msingi wa ukaazi kuliko kuzaliwa au ndoa. Wale wote wanaobeba uraia ni raia wa Dola, uchungaji wao na usimamizi wa mambo yao ni jukumu la Dola, pasi na ubaguzi wowote. Hivyo basi watu wote wanaobeba uraia wa Kiislamu wanapaswa kutendewa usawa, pasi na kubaguliwa baina yao ima na mtawala, katika upande wa kuangalia mambo yao na katika upande wa kulinda maisha yao, heshima yao na mali yao, au kadhi katika upande wa usawa na uadilifu.

“Raia wote wa Dola watatendewa usawa bila ya kuzingatia dini, tabaka, rangi au jambo jengine lolote. Serikali inaharamishwa kubagua miongoni mwa raia wake katika mambo yote, iwe katika utawala au mahakama, au uchungaji wa mambo.” (Kifungu cha 6 – Katiba Kielelezo ya Khilafah ya Hizb ut Tahrir)

Uraia katika Uislamu umo ndani ya mtu aishiye kwa kudumu ndani ya ardhi za Khilafah bila ya kuzingatia makabila yao au itikadi zao. Sio sharti mtu awe Muislamu na kutabanni vipimo vya Uislamu ndio aweze kuwa raia wa dola. Hili limevuliwa kutoka katika Hadith ifuatayo. Mtume (saw) amesema:    

«ادْعُهُمْ إِلَى الْإِسْلَامِ فَإِنْ أَجَابُوكَ فَاقْبَلْ مِنْهُمْ، وَكُفَّ عَنْهُمْ، ثُمَّ ادْعُهُمْ إِلَى التَّحَوُّلِ مِنْ دَارِهِمْ إِلَى دَارِ الْمُهَاجِرِينَ، وَأَعْلِمْهُمْ أَنَّهُمْ إِنْ فَعَلُوا ذَلِكَ أَنَّ لَهُمْ مَا لِلْمُهَاجِرِينَ، وَأَنَّ عَلَيْهِمْ مَا عَلَى الْمُهَاجِرِينَ»

Waite katika Uislamu, na ikiwa watakuitikia wakubalie na ujiepushe kupigana dhidi yao, kisha waite kuhama kutoka katika ardhi yao kuja katika ardhi ya waliohama (Muhajirina), na uwajuze kuwa wakifanya hivyo, watakuwa na haki kama za Muhajirina na juu yao watakuwa na majukumu kama ya Muhajirina.’

Raia wasiokuwa Waislamu wanaoishi chini ya Khilafah huitwa katika Shari'ah, kama dhimmi. Neno “dhimma,” lamaanisha “wajibu wa kutimiza mkataba.” Uislamu umekuja na hukumu kadhaa kuhusiana na watu wa dhimmah, ambazo kwazo ulidhamini haki za uraia kwao na kuwalazimisha juu yao majukumu yake. Uislamu pia ulifafanua kuwa dhimmi afurahiye uadilifu ule ule wanaofurahia Waislamu na kwamba wanapaswa kujifunga kwa hukumu zile zile ambazo Waislamu wanajifunga kwazo. Ama kwa yale wanayofurahia katika uadilifu na usawa, hili limevuliwa kutoka katika amri jumla inayojitokeza katika maneno ya Mwenyezi Mungu (swt):

[وَإِذَا حَكَمْتُم بَيْنَ النَّاسِ أَن تَحْكُمُوا بِالْعَدْلِ]

Na mnapo hukumu baina ya watu hukumuni kwa uadilifu.” (4:58)

Na katika maneno yake (swt):

[وَلاَ يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَى أَلاَّ تَعْدِلُواْ اعْدِلُواْ هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَى]

Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamngu(5:8)

Na pia inamulikwa katika maneno ya Mwenyezi Mungu (swt) kuhusiana na kuhukumu baina ya watu wa Kitabu

[وَإِنْ حَكَمْتَ فَاحْكُم بَيْنَهُم بِالْقِسْطِ]

Na ukiwahukumu, basi hukumu baina yao kwa uadilifu(5:42).

Dola haitaingilia imani au ibada za dhimmi. Wataruhusiwa kushikamana na sheria zao katika mambo ya ndoa na talaka kwa mujibu wa dini yao. Dola itamteua kadhi miongoni mwa watu wao wenyewe ili kutatua mizozo yao kwa msingi wa dini yao katika mahakama za Dola. Katika mambo yanayo husiana na chakula na mavazi wasiokuwa Waislamu wataamiliwa kwa mujibu wa imani yao na ndani ya upeo wa yale ambayo hukumu za kiShari'ah zinazo yaruhusu. Mambo yote mengine yaliyosalia ya sheria na hukumu, kama vile: utekelezaji wa miamala, adhabu na ushahidi (mahakamani), nidhamu za utawala na uchumi hutabikishwa na Dola juu ya kila mmoja, Muislamu na asiyekuwa Muislamu wote sawa sawa. (Kifungu cha 7, Katiba Kielelezo ya Khilafah ya Hizb ut Tahrir). Adam Metz, mwanahistoria wa Kimagharibi, aliandika kuhusiana na Khilafah katika karne ya 4 Hijria, “… dola ya Kiislamu iliwaruhusu watu wa dini nyenginezo kutumia mahakama zao wenyewe. Tunachojua kuhusu mahakama hizi ni kuwa zilikuwa mahakama za kanisa na viongozi maarufu wa kiroho walikuwa ndio mahakimu wakuu.”  

Kuna Hadith nyingi zinazo amrisha kuwatendea wema dhimmi na kutowadhuru au kuwachukulia kama raia wa tabaka la pili. Mtume (saw) amesema:

«أَلَا مَنْ ظَلَمَ مُعَاهِدًا، أَوِ انْتَقَصَهُ، أَوْ كَلَّفَهُ فَوْقَ طَاقَتِهِ، أَوْ أَخَذَ مِنْهُ شَيْئًا بِغَيْرِ طِيبِ نَفْسٍ، فَأَنَا حَجِيجُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ»

“Jueni kuwa yeyote atakaye mdhulumu aliyehifadhiwa kwa mkataba, au akamlazimisha zaidi ya uwezo wake, akachukua chochote kutoka kwake bila ya ridhaa ya nafsi yake, basi mimi nitakuwa mtetezi wake Siku ya Kiyama.”

Wanazuoni wa kale wa Uislamu pia walifafanua haki za Waislamu kwa dhimmi. Mwanachuoni wa kifiqhi maarufu wa dhehebu la Malik, Shaha al-Deen al-Qarafi ameeleza, “Ni jukumu la Waislamu kwa watu wa dhimmi kuwachunga madhaifu wao, kutimiza mahitaji ya maskini, kuwalisha walio na njaa, kuwapa mavazi, kuwahutubia kwa upole, na hata kuvumilia madhara yao hata kama yanatoka kwa jirani, ingawa Waislamu ndio wenye mkono wa juu. Waislamu pia wawashauri kwa ikhlasi juu ya mambo yao na kuwalinda dhidi ya yeyote anayejaribu kuwadhuru wao au familia zao, kuwaibia mali yao, au kukiuka haki zao.”

Mwanahistoria wa Kiingereza T. W. Arnold katika kitabu chake, Kuulingania Uislamu, aliandika kuhusiana na muamala wa wasiokuwa Waislamu walioishi chini ya Khilafah Uthmaniya, “… ingawa wayunani kiidadi walikuwa wengi kuliko Waturuki katika mikoa yote ya Ulaya ya himaya hiyo, uvumilivu wa kidini waliopewa, na ulinzi wa maisha na mali waliofurahia, punde tu yaliwaridhisha kupendelea kutawaliwa na Sultan kuliko kutawaliwa na utawala wowote ule wa kinaswara.” Mwandishi wa Kiingereza, H.G. Wells, aliandika yafuatayo katika utekelezwaji wa uadilifu na Khilafah: “Waliasisi tamaduni kuu za uvumilivu adilifu. Waliwashajiisha watu kwa hisia ya ukarimu na uvumilivu, na ni wenye utu na uhalisia. Waliunda jamii ya kiutu ambayo ndani yake ilikuwa ni nadra kuona ukatili na madhila ya kijamii, kinyume na jamii nyenginezo zilizokuja kabla yake.” 

Dhimmi hufurahia manufaa yale yale ya kiuchumi kama Waislamu. Wanaweza kuwa waajiriwa, kuasisi makampuni, kuwa washirika pamoja na Waislamu na kununua na kuuza bidhaa. Mali zao zinahifadhiwa na endapo watakuwa ni masikini na kushindwa kupata kazi wanastahiki kupata ruzuku za dola kutoka katika Hazina ya Khilafah (Bait ul-Mal).

Wasiokuwa Waislamu wanaruhusiwa kuwa wanachama wa Majlis al-Ummah – kitengo cha dola kinachomhisabu Khalifah na kuwakilisha na kuelezea maoni ya watu kwake. Kama mwanachama wa kitengo hiki, wasiokuwa Waislamu wanaweza kusema malalamishi yao kuhusiana na vitendo vya kidhuluma vinavyofanywa na watawala au utabikishaji mbaya wa hukumu za Kiislamu juu yao au ukosefu wa huduma au mfano wake. (Kifungu cha 105, Katiba Kielelezo ya Khilafah ya Hizb ut Tahrir)-

Kihistoria, dhimmi walipata ufanisi ndani ya ardhi za Khilafah. Mwanahistoria wa Kiingereza mwenye asili ya Kiyahudi Cecil Roth anataja kuwa kuamiliwa kwa Mayahudi mikononi mwa Dola ya Uthmaniya kuliwavutia Mayahudi kote barani Ulaya Magharibi. Ardhi ya Uislamu ikawa ndiyo ardhi ya ufanisi. Madaktari wa Kiyahudi kutoka katika chuo cha Salanca waliajiriwa kumhudumia Sultan na mawaziri (Viziers). Katika maeneo mengi utengezaji vioo na uhunzi zikawa ni ukiritimba kwa Mayahudi, na kwa ujuzi wao wa lugha za kigeni, wakawa ndio washindani wakuu kwa wafanyi biashara wa Veneti.

Kodi ya Kiislamu inayofahamika kimakosa zaidi ni jizya. Baadhi ya wanahistoria wanaonyesha sura ya kirongo kuwa kodi ya jizya ilikuwa juu sana hadi dhimmi walilazimika kusilimu ili kuiepuka. Wengine wanaonyesha viwango vya jizya visokuwa na mashiko kama vile asilimia 50. 

Uwajibu wa jizya unavuliwa katika Ayah ya Qur’an ifuatayo. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

 [قَاتِلُوا الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَلَا بِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَلَا يُحَرِّمُونَ مَا حَرَّمَ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَلَا يَدِينُونَ دِينَ الْحَقِّ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حَتَّىٰ يُعْطُوا الْجِزْيَةَ عَن يَدٍ وَهُمْ صَاغِرُونَ]

“Piganeni na wasio muamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho, wala hawaharamishi alivyo haramisha Mwenyezi Mungu na Mtume, wala hawafuati Dini ya Haki miongoni mwa waliopewa Kitabu, mpaka walipe kodi (Jizyah) kwa khiyari yao ilhali wao ni wanyonge (saghiroon).”  (9:29).

‘Unyonge’ (sighar) huu uliotajwa katika Ayah hii unamaanisha kuwa dhimmi ni lazima ajisalimishe kwa hukumu za Uislamu. Haimaanishi unyonge wa kimwili.

Kodi ya jizya hutekelezwa kwa dhimmi wote watu wazima, wanamume walio na uwezo wa kulipa. Wanawake na watoto wameepushwa na kulipa kama walivyo masikini wasio na njia za kujikimu kimaisha. Jizya hutekelezwa kwa mujibu wa ufanisi wa dhimmi. Katika zama za ‘Umar ibn al-Khattab (ra) aliweka vigawanyo vitatu vya jizya kulingana na ufanisi wa mtu. Viwango vya jizya vya wilaya tofauti tofauti za Khilafah katika zama za ‘Umar ibn al-Khattab (ra) vimeonyeshwa hapo chini.

Ni haramu kwa Khilafah kuwabebesha mzigo mkubwa dhimmi kwa utozaji wa kodi kubwa kwani hili huwasababishia wao madhara. Mtume (saw) amesema,

«أَلَا مَنْ ظَلَمَ مُعَاهِدًا، أَوِ انْتَقَصَهُ، أَوْ كَلَّفَهُ فَوْقَ طَاقَتِهِ، أَوْ أَخَذَ مِنْهُ شَيْئًا بِغَيْرِ طِيبِ نَفْسٍ، فَأَنَا حَجِيجُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ»

“Jueni kuwa yeyote atakaye mdhulumu aliyehifadhiwa kwa mkataba, au akamlazimisha zaidi ya uwezo wake, akachukua chochote kutoka kwake bila ya ridhaa ya nafsi yake, basi mimi nitakuwa mtetezi wake Siku ya Kiyama.”

Umar bin Al Khattab (ra) kama Khalifah aliletewa mali nyingi. Abu Ubayd akasema, ‘Naamini, alisema “Ni ya Jizya” – na yeye (Umar) akasema: “Nadhani ni lazima utakuwa umewatia watu uzito (kwa mali kama hiyo).” Wakasema: “Hapana, Wallahi, hatukukusanya chochote ambacho hakikutolewa kwa khiyari bali ni kwa khiyari yao wenyewe.” Akasema: “Pasina kutumia fimbo na pasina kuwafunga kamba?” Wakasema: “Ndio.” Akasema: Namshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye hakujaalia haya kutokea mikononi mwangu au wakati wa utawala wangu.” 

“Wakati wa Khilafah ya Umawiyya, dhimmi, Manaswara, Majusi, Mayahudi na Masabi, wote walifurahia kiwango fulani cha uvumilivu ambacho leo hatukioni katika nchi za Kinaswara. Walikuwa huru kufanya ibada za dini zao na makanisa yao na mahekalu yao yalihifadhiwa. Walifurahia uhuru ambapo walikuwa ni wafuasi wa sheria za kidini za wasomi na makadhi.” (Will Durant, mwandishi na mwanahistoria wa Kiamerika, Hadithi ya Hadhara – Umri wa Imani)

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Tsuroyya Amal Yasna
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 26 Aprili 2020 10:57

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu