Jumamosi, 16 Rabi' al-awwal 1443 | 2021/10/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Mafunzo Kutokana na Kufeli Kwa Harakati za Kisiasa za Kiislamu Zilizopita kwa Ummah kwa Jumla na kwa Wale Wanaochukua Mamlaka Haswa kwa Ajili Ya Kusimamisha Mamlaka Halisi ya Kiislamu

(Imetafsiriwa)

Ummah wa Kiislamu una hamu ya kweli ya Khilafah kwa njia ya Utume kama ilivyotajwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Katikati ya magofu ya udhalilishaji na uharibifu unaousibu ulimwengu wa Kiislamu, leo, Ummah wa Kiislamu unasubiri siku ya ushindi. Wasomi wa dola za kikafiri pia wanalijua hili vizuri na wanasiasa ndani ya nchi kubwa wanaogopeshwa kwa kurejea kwa Uislamu. Wanaogopa kurejea kwa Uislamu leo kutoka nchi yenye uwezo kama vile Uturuki ambayo watu wake wana ndoto ya kusimamisha tena utukufu wa Uislamu kama ilivyopandikizwa mizizi ndani ya historia ya Uthmani huku Istanbul ikiwa ndio kitovu cha dola ya Kiislamu na Ummah mzima, au kutoka nchi imara kama Pakistan au Afghanistan pamoja na nchi nyengine za Asia ya kati au Misri kwa kuwa zote kwa pamoja zinamiliki jeshi kubwa na zimefungamanishwa na bahari ya Mediterrania, bahari nyekundu na (mkondo wa) Suez, ambao ni ukanda wa biashara za dunia. Wasiwasi huu unawapaza usingizi wanasiasa wa nchi kubwa, hasa Amerika, dola kuu ya zama hizi.

Hofu ya Amerika na mataifa ya Ulaya kwa kuwasili kwa dola ya Khilafah ya kweli zinatambulika wakati walipoona hali ya upinzani ndani ya Ummah wa Kiislamu. Ushuhuda wa kwanza mkubwa kuonekana upinzani ilikuwa ndani ya mwaka 2001 kipindi ambacho Taliban – Afghanistan walikataa kuachana na Al-Qaida, ambayo Amerika iliishutumu kwa tukio la Septemba 11 na Taliban walipendelea kupigana lakini walipoteza nguvu kutokana na Amerika kuivamia Afghanistan. Hata hivyo, Taliban ilikataa kutii na iliendeleza mapambano ya silaha dhidi ya taifa lenye nguvu Amerika. Baada ya mwanzo huu wa uvamizi wa Amerika, kisha ukaja uvamizi wa Iraq mwaka 2003. Kipindi ambacho Amerika ilijitangazia ushindi dhidi ya jeshi la Iraq, ilijikuta yenyewe imekabiliwa na upinzani mkali ambao haukuogopa jeshi la Amerika. Upinzani huu uliilazimisha Amerika ndani ya tope la Iraq na ilikaribia kuishinda.

Kisha, ndani ya 2011, kulikuwa na machafuko ya Mapinduzi ya Kiarabu yakitoa wito wa kupinduliwa kwa serikali za vibaraka wa Amerika na Ulaya, baada ya umaarufu wa ushawishi wao kuoza na kumong’onyoka kufikia hatua ambayo wako kwenye ukingo wa kuanguka. Mapigano haya hayakutarajiwa na mashirika ya Kijasusi ya Amerika na Ulaya. Hili liligonga kengele za hatari kubwa ya hali ya upinzani ambayo ilianza kulipuka. Zaidi ya hayo, ni wito wa kupindua tawala ulioambatana pamoja na wito mwengine mkubwa sana wa kusimamisha Khilafah Rashidah. Kwa hivyo, mapinduzi haya yameifanya Amerika itetemeke kwa sababu ilikuwa mlangoni mwa kusimamishwa tena Khilafah kwa njia ya Utume.

Hata hivyo, kuliibuka mambo mawili; La kwanza ni kufeli kuanzisha mamlaka halisi ya Kiislamu kwa vyama vilivyodai kurejesha Khilafah ya Kiislamu, kama vile Ikhwan al-Muslimin ya Misri na En-Nahdah ya Tunisia; na la pili ni tangazo la Khilafah ya uongo ndani ya mji wa Mosul lililotangazwa na kikundi cha wapiganaji wa ISIS.

Ndani ya nchi zote mbili, Misri na Tunisia, Ikhwan al-Muslimin na En-Nahdah walipiga kampeni kuhusu utawala wa Kiislamu, na hatimaye, watu waliwapigia kura wote kuingia madarakani, hivyo kuashiria mwanzo wa zama mpya ndani ya Mashariki ya Kati. Licha ya kiasi kikubwa cha kuungwa mkono walichokua nacho, vyama vyote daima vilifuata makubaliano ya pamoja na, matokeo yake, mara kwa mara waka umeulaghai Uislamu kwa matumaini ya kupata uhalali kwa jamii yao na jamii ya Kimataifa. En-Nahdah iliacha kuifanya Shari’ah kuwa ndio chanzo kikuu cha sheria zote ndani ya katiba mpya na wakatangaza kuwa walitaka kudumisha usekula asili wa nchi. Kiongozi wa En-Nahdah, Rachid Ghannouchi, alidokeza kuhusiana na kusimamisha Khilafah: “Kwa hakika, Sisi ni dola ya kitaifa. Tunataka hali ya mabadiliko kwa Watunisia, kwa Dola ya Tunisia. Ama kuhusu suala la Khilafah, hili ni suala moja ambalo si la uhalisia. Suala la uhalisia wa leo ni kwamba sisi ni Dola ya Tunisia inayotaka mabadiliko, ili iwe dola kwa ajili ya watu wa Tunisia, na si dhidi yao.”

Vivyo hivyo, MB nchini Misri ilienda kwa marefu zaidi kuelezea maboresho yao. Katika kukimbilia kwake kutuliza yanayoitwa maoni ya kimataifa, wakaachana na yote ya wajibu kuhusu kutawala kwa Uislamu. Ilipokuja katika kufanyia kazi misingi ya Kiislamu, walinukuu vizuizi vya kikatiba na haja ya kuweka machache katika hali ya makubaliano. Ilipokuja katika kufanyia kazi uchumi wa Kiislamu, walinukuu haja ya kuepuka kutishia wawekezaji wa kimataifa na watalii.

Moja ya hatua ya kwanza aliyoichukua raisi Mohammed Morsi kama raisi wa Misri, juu ya mambo yote, ilikuwa ni kutuma mazungumzo ya kuthibitisha uwajibu wa Misri wa kuweka mahusiano ya amani na ‘Israeli’! Miito ya awali ya Uislamu iliondolewa kabisa katika kauli za Morsi wakati alipokaa madarakani. Licha ya miaka 80 ya kupiga kelele ‘Uislamu ndio Suluhisho’, wakati fursa ilipojitokeza yenyewe MB walishindwa kukabiliana na changamoto ya utawala uliowekwa.

Sababu muhimu zaidi kwa nini vyama hivi vilifeli vibaya mno, baada ya kuingia madarakani ni kuridhishana na kufanya kazi kupitia mfumo uliopo, kutokuwa na mpango sahihi wa kisiasa na kushindwa kushughulika na upinzani nk. Ama kuhusu kuridhishana na kufanya kazi ndani ya mfumo uliopo, miongoni mwa vyama vingi vya Kiislamu vilitawala katika nafasi ya udhaifu ambapo walizingatia zaidi kuridhisha wengine, kinyume na kubeba amri ya kurejesha utawala wa Kiislamu. Kwa mfano En-Nahdah, daima iliruhusu vyama vya kisekula ndani ya Tunisia, mwishowe wakapiga kura ya kuruhusu watu kutoka utawala uliopita kugombea katika uchaguzi wa ubunge. Ikhwan al-Muslimin walipitisha mtazamo kama huo; walifanyia kazi matakwa ya wengine na wakafanya kazi na nchi kubwa za kimataifa kwa kisingizio cha ‘kulinda utalii’ kwa kusaini makubaliano ya kiusalama na umbile la Kiyahudi. Vyama vyote viwili kamwe havikutambua ya kuwa sera kama hizo zinawafanya wao waonekane dhaifu na wasio na ufanisi. Hivyo, makundi yote hayakuwafikiana na yaliachana na misingi ya kisiasa ya Kiislamu na wakathibitisha kwa tawala za kisekula zilizopo kwa kuchagua kufanya kazi kupitia makundi hayo. Hii haifanyi chochote isipokuwa kurudisha imani ndani ya mfumo unaokufa uliowekwa na nchi za wakoloni na ambao kufikia sasa haujaupa Ulimwengu wa Kiislamu chochote isipokuwa matatizo. Ama kuhusu kutokuwa na mpango sahihi wa kisiasa, vyama hivi vya kisiasa vilikuwepo kwa miongo kadhaa na walikuwa na nafasi ya kuandaa mpango wa kisiasa kwa ajili ya siku watakayoingia madarakani, lakini hawakuwa nao. Maandalizi yake yalipaswa kuja katika mfumo wa katiba, ramani ya njia ya kisiasa au mipango na sera, ambayo inatakiwa kufuatwa. Uhalisia ulikuwa, kwa bahati mbaya, kwamba wote En-Nahdah na Ikhwan al-Muslimin (MB) hawakuwa na kimoja wapo katika mambo haya, na wakafanya matatizo ya kimuundo, kiuchumi na kijamii kuwa mabaya zaidi. Misri kwa mfano ilikuwa na asilimia 40 ya watu wake wanaoishi chini ya mstari wa umaskini. Badala ya kufanya kazi ya kurekebisha miundo na ugavi mpya wa rasilimali nyingi zilizomo ndani ya Misri, MB ilifanya maamuzi ya kuuendea Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ambao wanajulikana vibaya kwa kuziweka nchi ndani ya mzunguko wa deni la kudumu linalopelekea umaskini zaidi. Kuhusu kushindwa kushughulika na Upinzani, vyama hivi vya kisiasa licha ya kuwa na uungwaji mkono mkubwa wa watu na kuchaguliwa kuingia madarakani, wote En-Nahdah na MB walisimama wakishangaa mbele ya wakosoaji wao. Ndani ya zote Misri na Tunisia, watawala wa zamani kamwe wahangekukubali kuwa nje ya madaraka na wakachukua kila maamuzi ya serikali mpya zilizochaguliwa kuwa ni igizo na majibizano mengi mitaani. Badala ya kuushinda upinzani, kwa msaada wa watu walithibitisha kuwa hawana uwezo na ni dhaifu katika kuwashughulikia waasi hawa. Nchini Misri, Morsi hakuwashinda wapinzani, wala hakuwanyamazisha, lakini mwisho wake aliathiri nafasi yake mwenyewe kwa ajili ya kuwatuliza wao na mwishowe akatolewa kwa kupinduliwa na hivyo wote En-Nahdah na MB walishindwa kushughulika na wapinzani wao. Hivyo, matokeo yake, licha ya kushinda uchaguzi, vyama vyote vilipiga domo tupu tu kwa Uislamu wakati vilipofika madarakani na wakapoteza nia njema ya watu waliowaunga wao mkono kuingia madarakani na mwishowe wakashindwa kurejesha Khilafah ya kweli ya Kiislamu kutokana na shughuli zao na mahesabu yao ya kisiasa ya muda mfupi.

Ama kuhusu kutangazwa kwa Khilafah ya Kiislamu ya uwongo na kikundi cha wapiganaji wa ISIS, kwanza hawakumiliki hata mamlaka ya ukweli ya kutangaza utawala. Sheria ya Kiislamu inataka chama (kundi/Hizb) chochote kinachotaka kutangaza Khilafah katika eneo kinapaswa kuwa na mamlaka ya wazi inayoonekana kwenye hilo eneo, ambapo kitadumisha usalama ndani na nje na kwamba hili eneo linapaswa kuwa na vipengele vya utawala ndani ya eneo ambalo Khilafah itatangazwa. ISIS haikuwa na mamlaka ndani ya Syria au Iraq wala haikuwa na usalama wa ndani au ulinzi wa nje. Hivyo, utangazaji wa ISIS wa Khilafah ni wa usemi tu bila ya uzito wowote. Hata hivyo, tamko la Baghdadi lilidai kuwa Khilafah ndani ya Mosul imeifaidisha sana Marekani; faida hiyo ilikuwa katika mfumo wa kudhoofisha hali iliyomo ndani ya Syria ambayo ilikuwa ya wito wa Khilafah. Khilafah ya Baghdadi iliibuka kama mchanganyiko wa Umwagaji damu, starehe ya wanawake kama Masuria, sheria za mashimo ya kuzikia, makaburi na maeneo matukufu, hivyo kuwasilisha picha hasi ya dola tukufu ya Khilafah.

Licha ya majaribio haya yaliyofeli ya harakati hizi za Kiislamu na kuanzishwa kwa Khilafah bandia, Alhamdulillah, bado hali ya upinzani katika Umma wa Kiislamu inakua kwa njia ambayo Amerika imetishika kwa mshangao kama vile matukio ya Mapinduzi ya Kiarabu na hivi karibuni zaidi, kuingia kwa Taliban madarakani nchini Afghanistan. Hata hivyo, Amerika ni dola kuu inayopima mikakati yake na kuitekeleza ima moja kwa moja au kwa kutumia vibaraka wake, ili masilahi yake ya kimataifa yawe salama. Kwa hivyo, kitendo cha Amerika kutafuta mbinu mpya ni dhahiri kutaka kutatua hali ya upinzani katika ulimwengu wa Kiislamu, na kwa sasa, nchini Afghanistan na sio kuyawacha matukio kuwashangaza ambayo huenda yakaleta Khilafah kuu na ya kweli.

Kwa kuongezea, ni muhimu kutambua kwamba Taliban imetangaza muundo wao wa serikali kuwa tu ‘Imarati ya Kiislamu’ badala ya kuianzisha kama Khilafah ya Kiislamu; pia walitafuta msaada kutoka kwa serikali za vibaraka kama Uturuki na Qatar kuendesha uwanja wa ndege wa Kabul. Je! Watu wa Afghanistan hawawezi kuendesha uwanja huo wa ndege? Je! Afghanistan haina uwezo wa kisayansi, uhandisi na kiutawala wenye uwezo wa kusimamia hata uwanja wa ndege? Hii inaonyesha kuwa Taliban haina mkakati wa wazi wa kisiasa na uwezo wa kuendesha serikali kwa uhuru bila msaada wowote kutoka dola nyengine.

Kwa kuongezea, Taliban bado haikuweza kuunganisha vikosi vyote vya upinzani kama vile uwepo wa msuguano wa vikosi vya Uzbek-Tajik katika bonde la Panjshir (Kaskazini mwa Afghanistan).

Kuhusiana na hili, Hizb ut Tahrir (ambayo jina lake ni sanjari katika uwanja wa Kiisalmu na Da’awah uliolenga kazi ya kusimamisha tena Khilafah) inaishauri sana Taliban kuzingatia kwa uangalifu yaliyofanywa na harakati zilizopita na sio kurudia makosa sawa na waliowatangulia. Alhamdulillah, Taliban imetimiza moja ya amri muhimu ya Mwenyezi Mungu kuhusu kuwaondoa wakoloni katika ardhi za Kiislamu; Hata hivyo, hawapaswi kuanzisha mamlaka yao kama “Imarati ya Kiislamu” kwani haina msingi katika Uislamu na inakwenda kinyume na dalili za Shari’ah ya Kiislamu. Zaidi ya hayo, Taliban wanapaswa kuwa makini kisiasa na kuwa na uwezo wa kuendesha serikali bila kuwa na maafikiano kwa namna yoyote ile. Taliban haipaswi kuanzisha serikali inayojumuisha mchanganyiko wa Uislamu na Usekula, kwani Mwenyezi Mungu (swt) hakubali isipokuwa Uislamu pekee. Taliban haipaswi kuzingatia masharti yoyote ya Amerika katika kuanzisha mamlaka ya Kiislamu na inapaswa kukataa taasisi zote za Kikafiri kama UN, Amnesty international, IMF, WB, n.k.

Ili kuyafanya mamlaka haya kuwa mamlaka sahihi ya dola ya kweli na madhubuti ya Kiislamu, wanapaswa  kuungana na Hizb ut Tahrir, waanzilishi wa uwazi na usafi wa fikra za Kiislamu na njia sahihi ya mabadiliko katika zama zilizokumbwa na moshi, na umbali kutoka mwongozo wa kinabii. Tangu kuanzishwa kwake, Hizb ut Tahrir inafanya kazi bila kuchoka mchana na usiku ili kuanzishwa tena kwa dola ya Kiislamu ya Khilafah, ambayo itarejesha tena mfumo wa maisha ya Kiislamu katika ulimwengu wa Kiislamu na kueneza Uislamu ulimwengu mzima. Katika mwenendo wa kazi yake, Hizb inamcha Mungu na kujitoa kidhati kwa hukmu za Shari’a pekee, imejikomboa kutokana na kushawishiwa na kitu chochote ambacho sio halali, iwe ni matamanio au masilahi, au kushawishiwa na thaqafa nyengine yoyote, na iha ikhlasi katika kufanya kazi ya Mwenyezi Mungu (swt) peke yake ili isije ikamshirikisha na chochote chengine. Hizb ina uwezo wa kutosha kuchukua mamlaka na kutimiza malengo yake ya Kiislamu.

Kwa hili, Hizb ut Tahrir imeelezea kwa kina ufafanuzi wa kuutambua Uislamu, na kwamba Uislamu unaweza kutabikishwa katika maisha haya kwa kuanzishwa kwa Dola ya Kiislamu, kwa hivyo, ikaweka muongoza kamili wa serikali, msingi wake, nguzo zake, na mifumo yake. Imeonyesha haya yote katika vitabu vyake, machapisho, na nakala kama vile “Dola ya Kiislamu”, “Nidhamu ya utawala katika Uislamu”, “Taasisi za Dola ya Khilafah katika Utawala na Idara”, “Nidhamu ya Kiuchumi katika Uislamu”, “Nidhamu ya Kijamii katika Uislamu”, “Nidhamu ya Kuadhibu”, “Mali katika Dola ya Khilafah” na vitabu vyengine, vijitabu, na machapisho ambayo haziwezi kutajwa zote. Kupitia njia hii, Hizb imechora njia kamili na wazi ya kuendelea na kazi inayofanya.

Katika nyanja za kisiasa, Hizb imeweka kanuni za kisiasa za kufuata katika kuitambua siasa, uchambuzi, na utekelezaji, kwa hivyo ikafafanua siasa kuwa ni kusimamia mambo ya Ummah ndani na nje. Imezingatia kuwa itikadi ya Kiislamu ni itikadi ya kisiasa na kiroho na imetazama mwamko wa kisiasa wa ulimwengu kwa mtazamo wa kiulimwengu na kutoka mtazamo maalumu ambayo ni itikadi ya Kiislamu. Kwa hivyo, inachambua na kufuata habari za kisiasa kwa mtazamo wa itikadi ya Kiislamu, kwa hivyo, ikachapisha kitabu cha “Fikra za Kisiasa”, “Fahamu za Kisiasa”, “Mitazamo ya Kisiasa” na “Kadhia za Kisiasa”. Kwa hili, Hizb imekusanya ufahamu kamili wa msimamo wa kimataifa na duara la kimataifa, na hivyo kuweza kufichua mipango na njama zinazopangwa dhidi ya Ummah wa Kiislamu. Kwa hiyo, Hizb ina picha nzuri ya jinsi ya kushughulika na nchi za wakoloni ambazo zina ulafi kwa nchi za Kiislamu wakati utakapofika wa kusimamisha Dola ya Khilafah, kuonyesha sababu kwa nini kila nchi ina nguvu, hatari zake, udhaifu wake, nukta za nguvu yake na mengineyo. 

Kwa kuongezea, la muhimu zaidi, kwa ajili ya kusimamisha Khilafah mara tu inapopata fursa, ikaweka rasimu ya katiba iliyojumuisha vifungu 191 vilivyovuliwa kupitia ijitihad sahihi na dalili zenye nguvu, na iliyojengwa juu ya machimbuko ya Sharia, hukmu za Sharia ilizozitabanni, na kuonesha usahihi wake kwa nyanja zote za maisha. Hizb inasema haya kwa kupeleka sifa zote njema kwa Mwenyezi Mungu (swt) pekee na kumuomba Mwenyezi Mungu (swt) aipe ushindi Hizb, kama anavyosema Mwenyezi Mungu (swt):

(فَلَا تُزَكُّواْ أَنفُسَكُم هُوَ أَعلَمُ بِمَنِ ٱتَّقَى)

 “Basi msijisifu usafi. Yeye anamjua sana mwenye kujikinga na maovu.” [An-Najm: 32].

Kwa hivyo, ikiwa Taliban kweli inajali Uislamu na Ummah wa Kiislamu, hawapaswi kuchelewesha muda zaidi na wanapaswa kuungana na Hizb ut Tahrir ili kuanzisha Khilafah na kuziunganisha ardhi za Waislamu katika maeneo kama Pakistan, Tajikistan, Kazakhstan na Uzbekistan pamoja na Afghanistan kutengeneza dola moja yenye nguvu ya Kiislamu ya Khilafah. Mlango bado uko wazi kwa Taliban kubeba mpango wa kisiasa wa Hizb ut Tahrir na kuutekeleza, na mlango bado uko wazi kwao kukabidhi utawala nchini Afghanistan kuanzisha mpango wa Khilafah Rashidah ya pili kwa njia ya Utume. Tunamuomba Mwenyezi Mungu kwamba jambo hili liwe hivi karibuni katika siku zijazo Insha Allah, na siku hiyo Waumini watafurahi kwa ushindi wa Mwenyezi Mungu na utukufu mkubwa kwa Uislamu. Amiin

(وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ ٱلْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ ٱللَّهِ يَنصُرُ مَن يَشَاءُ وَهُوَ ٱلْعَزِيزُ ٱلرَّحِيمُ)

“Na siku hiyo Waumini watafurahi. Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.” [Ar-Rum 4-5]

أفغانستان#                      #Afganistan            #Afghanistan

 Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Hameed Bin Ahmad

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu