Jumamosi, 21 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Dola ya Kiislamu Inautaka Uislamu Kuwa ndio Msingi wa Sheria na Hukmu Zote, Sio Baadhi ya Sheria Zilizopitishwa na Mahakama Bandia ya Shariah

(Imetafsiriwa)

Mjadala kuhusu Sheria ya Wanaobadili Jinsia

Hukmu kubwa imepitishwa na Mahakama ya Shirikisho ya Shariah ya Pakistan. Ilitangaza vifungu vichache vya sheria ya Waliobadili Jinsia ya 2018 kama kinyume na Uislamu. Kwa hivyo, vitakoma kutekelezwa, ilhali sheria iliyosalia itabaki kutekelezwa. Hili kwa mara nyingine tena limesababisha mjadala mkali kati ya wasomi wa sekula na wa kiliberali, kwa upande mmoja, na ‘Maulamaa na vyama vya kisiasa vyenye fikra ya Kiislamu kwa upande mwingine. Ili kuelewa athari kamili ya hukmu hii na sheria hii tunahitaji kuifupisha.

Kitambulisho cha Jinsia katika Sheria ya Wanaobadili Jinsia

Sheria ya Wanaobadili Jinsia Kifungu cha 2(f) kinajaribu kufafanua misamiati, kikisema, “kitambulisho cha kijinsia, maana yake ni hisia ya ndani kabisa ya mtu binafsi kama mwanamume, mwanamke au mchanganyiko wa wote wawili au kutokuwa yeyote katika hao: ambayo inalingana au isiyolingana na jinsia iliyopeanwa wakati wa kuzaliwa.”

Kifungu cha 2(n) kinasema, “Mtu aliyebadili jinsia” ni mtu ambaye ni, “(i) Khuntha (intersex) aliye na mchanganyiko wa sehemu za siri za kiume na za kike au utata katika sehemu zao za siri, au (ii) Mtu aliye hasiwa aliyepewa jinsia ya kiume wakati wa kuzaliwa, lakini anapitia kukatwa sehemu za siri au kuhasiwa; au (iii) Mwanamume Aliyebadili Jinsia, Mwanamke Aliyebadili Jinsia, Khawajasira au mtu yeyote ambaye kitambulisho chake cha kijinsia na/au muonekano wa kijinsia unatofautiana na desturi za kijamii na matarajio ya kitamaduni kulingana na jinsia waliyopewa wakati wa kuzaliwa."

Chaguo juu ya Kitambulisho cha Jinsia katika Sheria Hii

Suala la haki ya kuchagua kitambulisho cha kijinsia limeangaziwa katika Kifungu cha 3 cha sheria, ambacho kinasema chini ya kichwa, 'Kutambua kitambulisho cha mtu liyebadili jinsia' kwamba, “(1) Mtu aliyebadili jinsia atakuwa na haki ya kutambuliwa kwa mujibu wa ilivyojiainisha kitambulisho chake cha kijinsia, kama alivyo, kwa mujibu wa vifungu ya Sheria hii. (2) Mtu anayetambulika kama mtu aliyebadili jinsia chini ya kifungu kidogo cha (1) atakuwa na haki ya kusajiliwa kulingana na kitambulisho cha kijinsia anayoihisi yeye mwenyewe na idara zote za serikali ikiwemo, lakini sio tu NADRA. (3) Kila mtu aliyebadili jinsia, akiwa ni raia wa Pakistan, ambaye ametimiza umri wa miaka kumi na nane atakuwa na haki ya kusajiliwa kulingana na kitambulisho cha kijinsia anayoihisi mwenyewe na NADRA kwenye CNIC, CRC, Leseni ya Udereva na pasipoti kwa mujibu wa vifungu vya Sheria ya NADRA, 2000 au sheria nyingine yoyote husika. (4) Mtu aliyebadili jinsia ambaye tayari ashapewa CNIC na NADRA ataruhusiwa kubadilisha jina na jinsia kulingana na kitambulisho chake binafsi kwenye CNIC, CRC, Leseni ya Kuendesha gari na pasipoti kwa mujibu wa vifungu vya Sheria ya NADRA, 2000.”

Haki za Mtu Aliyebadili Jinsia Katika Sheria hii

Sehemu nyingine inafafanua zaidi juu ya haki zao, kifungu cha 7 cha sheria hiyo kinasema chini ya kichwa, “Haki ya Kurithi” kwamba, “(1) Hakutakuwa na ubaguzi dhidi ya Watu Waliobadili Jinsia katika kupata mgao kamili wa mali kama ilivyoainishwa chini ya sheria ya urithi. (2) Mgao wa watu waliobadili jinsia utaamuliwa kulingana na jinsia iliyotangazwa kwenye CNIC kwa mujibu wa sheria ya urithi nchini Pakistan (3) Sehemu ya urithi kwa watu waliobadili jinsia itakuwa kama ifuatavyo (i) Kwa Mwanamume aliyebadili jinsia, hisa ya urithi itakuwa ya mwanamume; (ii) Kwa Mwanamke Aliyebadili Jinsia, sehemu ya urithi itakuwa ya mwanamke (ii) Kwa mtu ambaye ana sifa za kiume na kike au zisizoeleweka, kama vile hali yake ni ngumu kubaini wakati wa kuzaliwa, yafuatayo yatatumika:- (a) Baada ya kufikisha umri wa miaka 18, ikiwa kitambulisho cha kijinsia anachojihisi yeye mwenyewe ni cha wanamume aliyebadili jinsia, sehemu ya urithi itakuwa ya mwanamume; (b) Baada ya kufikisha umri wa miaka 18, ikiwa kitambulisho cha kijinsia anachojihisi yeye mwenyewe ni cha Mwanamke Aliyebadilika Jinsia, sehemu ya urithi itakuwa ya mwanamke; (c) Baada ya kufikisha umri wa miaka 18, ikiwa kitambulisho cha kijinsia anachojihisi yeye mwenyewe wa si cha Mwanaume Aliyebadili Jinsia wala Mwanamke Aliyebadili Jinsia, mgao wa urithi utakuwa wastani wa migao miwili wa mwanamume na mwanamke; na (d) Chini ya umri wa miaka kumi na minane, jinsia ni kama, ilivyoamuliwa na afisa wa matibabu kwa msingi wa sifa kuu za kiume au za kike."

Uanaharakati Kuhusiana na Vifungu vya Ubaguzi na Uhangaishaji katika Sheria hii

Vifungu vilivyosalia vya Sheria hii vinahusiana na kuharamisha ubaguzi, uhangaishaji na haki za elimu, ajira, kura, afya, mikusanyiko na haki za kushikilia afisi ya umma na ufikiaji wa nafasi za umma na vile vile dhamana ya haki za kimsingi chini ya katiba ya Pakistan.

Hali ya sasa inahusiana na hatua ya Mahakama ya Sheria ya Shirikisho, ambayo imefuta kifungu cha 2(f) chenye ufafanuzi wa "kitambulisho cha kijinsia." Pia imefuta Kifungu cha 2(n) (iii), Kifungu cha 3 na Kifungu cha 7 cha Sheria tata, yenye kichwa, "Sheria ya Watu Waliobadili Jinsia (Ulinzi wa Haki) ya 2018." Imewashambulia kwa kusema kwamba wao wako kinyume na maamrisho ya Uislamu, kama yalivyobainishwa ndani ya Quran Tukufu na Sunnah za Mtukufu Mtume (saw). Imetangaza kuwa haya yatakoma kuwa na athari yoyote ya kisheria mara moja.

Msingi wa Kikatiba wa Mahakama ya Shariah

Kumekuwa na upinzani mkubwa kutoka kwa mashirika ya haki za binadamu na jumuiya ya LGBTQ nchini Pakistan dhidi ya hukmu hii. Kwa hiyo, ni muhimu kwanza kuelewa sio tu hukmu hii ya kina lakini pia thamani ya kikatiba ya mahakama ya Shariah ya Shirikisho yenyewe. Mahakama ya Sheria ya Shirikisho iliundwa mnamo tarehe 26 Mei, 1980 kwa Amri ya Rais Na.1 ya 1980 kama ilivyojumuishwa katika sehemu ya VII ya Katiba ya Pakistan, 1973 chini ya kichwa cha sura ya 3A.

Vifungu hivi na vyengine vichache vinavyoitwa vya Kiislamu vilifanywa kuwa sehemu ya katiba ili kutoa hisia kwa umma kwa jumla kwamba hii ni Katiba ya Kiislamu.

Utangulizi unasema, “Ubwana juu ya Ulimwengu mzima ni wa Mwenyezi Mungu peke yake, na mamlaka yatekelezwa na watu wa Pakistan ndani ya mipaka aliyoiweka Yeye ni amana takatifu.”

Kifungu cha 2(A) cha "Azimio la Malengo" kinasema, "Ubwana juu ya ulimwengu mzima ni wa Mwenyezi Mungu peke yake na mamlaka Ameyakabidhi kwa Dola ya Pakistan, kupitia watu wake kwa kutekelezwa ndani ya mipaka iliyoiwekwa Yeye ni amana takatifu.”

SEHEMU YA IX, “Vifungu vya Kiislamu” vinasema, “227. Vifungu vinavyohusiana na Qur’an Tukufu na Sunnah” na kufafanua, “(1) Sheria zote zilizopo zitaletwa kwa kufuata Maagizo ya Uislamu kama yalivyobainishwa ndani ya Qur’an Tukufu na Sunnah, katika Sehemu hii inayoitwa kama Maagizo ya Uislamu, na hakuna sheria itakayotungwa ambayo inagongana na Maagizo hayo.”

Katika Sehemu ya VII, "Mahakama," Sura ya 3A inapeana uundwaji wa Mahakama ya Shariah ya Shirikisho. Imeelezwa, chini ya "Mamlaka, Mamlaka ya 203D, Mamlaka na Kazi za Mahakama," kwamba, "(1) Mahakama inaweza, ima kwa hoja yake yenyewe au kwa rufaa ya raia wa Pakistan au Serikali ya Shirikisho au Serikali ya Mkoa, kuchunguza na kuamua swali kama sheria yoyote au kifungu cha sheria kinagongana au la na maamrisho ya Uislamu, kama yalivyobainishwa katika Qur'an Tukufu na Sunnah za Mtume Mtukufu (saw) zinazojulikana hapa kama Maagizo ya Uislamu."

Haki ya Kikatiba ya Kukata Rufaa dhidi ya Uamuzi wa Mahakama ya Shariah

Haki ya kukata rufaa imetolewa katika katiba dhidi ya agizo la Mahakama ya Shariah ya Shirikisho. Iko chini ya kifungu cha 203F Rufaa kwa Mahakama ya Upeo. Inasema kwamba, (1) Mhusika yeyote katika kesi zozote mbele ya Mahakama chini ya Kifungu cha 203D ambaye hajaridhika na uamuzi wa mwisho wa Mahakama katika kesi hizo anaweza, ndani ya siku sitini baada ya uamuzi huo, kupendelea kukata rufaa katika Mahakama ya Upeo: Isipokuwa rufaa kwa niaba ya Shirikisho au Mkoa inaweza kupendekezwa ndani ya miezi sita ya uamuzi huo.

Chini ya (2A), inasemekana "(2A) Rufaa itawekwa kwa Mahakama ya Upeo kutokana na hukmu yoyote, amri ya mwisho au hukmu ya Mahakama ya Shariah ya Shirikisho." Inaendelea kusema, "(3) Kwa madhumuni ya utekelezaji wa mamlaka iliyotolewa na Ibara hii, kutaundwa katika Mahakama ya Upeo Benchi litakaloitwa Mahakama ya Rufaa ya Shariah."

Mashirika ya haki za binadamu na wanaharakati waliobadili jinsia wamelaani hukmu iliyotajwa hapo juu na wanakusudia kuwasilisha rufaa katika Mahakama ya Upeo haraka iwezekanavyo kwani wanaona uamuzi huu kama ukiukaji wa haki zao. Wanadai kuwa hii itawafanya watendewe kinyama. Shirika la Amnesty International pia limeitaka Serikali ya Pakistan kuchukua hatua za haraka na za dharura kukomesha kubatilishwa kwa ulinzi muhimu. Wanasema kuwa bila uingiliaji kati huo, watu waliobadili jinsia na watu wenye jinsia tofauti tofauti watakuwa katika hatari zaidi ya kuhangaishwa, kubaguliwa na kunyanyaswa.

Masuala Kuhusiana na Hukmu ya Sheria ya Wanaobadili Jinsia

Mahakama ya Shariah ya Shirikisho imetoa hukmu ya kina yenye zaidi ya kurasa 108 baada ya kuwasikiliza walalamishi na washtakiwa wote wakiwemo baadhi ya makhuntha ambao pia walijiunga kama walalamishi kupinga sheria hii. Mahakama pia ilisikiliza wataalamu wa matibabu na wanasaikolojia katika suala hili.

Maswali muhimu hapa ni,

1. Ikiwa haki za makhuntha, watu waliohasiwa, na wanaume au wanawake waliobadili jinsia zinalindwa chini ya sheria hiyo, au hata Katiba ya Pakistan?

2. Je, ufafanuzi wa watu waliobadili jinsia ni sahihi kwa mujibu wa Uislamu?

3. Je, haki ya kukata rufaa katika Mahakama ya Upeo, dhidi ya Mahakama ya Shariah ya Shirikisho inatoa amri zake tu katika hali ya mapendekezo na hivyo si ya lazima?

4. Kwa kuwa Bunge ndiyo taasisi kuu kwa mujibu wa katiba na linaweza kutunga sheria katika jambo lolote kwa njia yoyote ambayo wajumbe wataona inafaa, je, lina haki ya kufuta hukmu yoyote ya mahakama ya Shariah au benchi la rufaa la Shariah la Mahakama ya Upeo?

5. Je, vifungu vya Kiislamu vya katiba vinaifanya Katiba huyo kuwa ya Kiislamu? Na kwanza je, ni kwa mujibu wa Uislamu kutunga sheria kulingana na akili ya mwanadamu kisha kujaribu kutafuta migongano yake na Quran na Sunnah?

6. Ni upi ufafanuzi sahihi wa makhuntha na ni zipi haki zao walizopewa na Uislamu?

Mgongano na Mitazamo ya Kimagharibi

Mashirika mengi ya haki za binadamu na wanaharakati waliobadili jinsia, ambao wanaibua suala hili, wanatabanni fikra na fahamu zao kutoka kwa ufafanuzi wa kimagharibi wa haki na wajibu. Wanajifunga uhuru wa Kimagharibi ukiwemo uhuru wa kujieleza na uhuru wa kibinafsi. Wanachukizwa kabisa na hata kutajwa kwa neno Uislamu au Shariah. Wanabeba fahamu zisizoeleweka, zenye dosari na zenye ufahamu wa kimakosa kabisa kuhusu Uislamu, shariah ya Kiislamu, na Ahkam za Shariah.

Kwa mtazamo wao, Uislamu hauwatambui makhuntha. Kisha wanadai kuwa wameharamishwa kuwepo katika jamii ya Kiislamu. Ni wazo la kipuuzi kabisa. Inaonekana kwamba wanajaribu kwa makusudi kuwakanganya makhuntha, ambao wamezaliwa na sehemu za siri zisizoeleweka, na watu waliohasiwa, ambao wamezaliwa wakiwa wanaume lakini wamepoteza sehemu za siri za kiume, kwa sababu ya ajali au jeraha la kimakusudi. Pia wanataka kuwakanganya makhuntha na kundi la watu wanaotaka kubadilisha jinsia zao kimakusudi, kwa msingi wa hisia na mitazamo yao wenyewe kama wanaume au wanawake, kufuatia ajenda ya mfumo wa kibepari wa Kimagharibi. Kwa hivyo, wamezua mkanganyiko huu kutokana na kwamba makhuntha pia walilazimika kupinga Sheria hii ya Wanaobadili jinsia, kama uvunjaji na ukiukaji wa haki zao.

Chini ya masharti ya sheria ya awali, iliwezekana kwa mtu yeyote kubadilisha kitambulisho chake kulingana na mtazamo wake uliochanganyikiwa wa yeye mwenyewe kama mwanamume au mwanamke. Kwa mapenzi ya kibinadamu pekee anaweza kujisajili katika nyaraka za serikali, taasisi na kupata Vitambulisho vya Kitaifa kwa msingi huu.

Hili lilizua fujo. Watu kama hao wakiwa wanaume wangeweza kupata nafasi zote za wanawake kama vile mabustani ya umma, vyoo, vyuo vya wasichana na hosteli. Tayari tunashuhudia fujo hili katika nchi za Magharibi ambako kuna mijadala mikubwa inayoendelea kuhusiana na masuala hayo.

Sheria ya Kiislamu Kuhusu Jinsia yenye Utata

Sheria ya Kiislamu kuhusu watu wenye jinsia mbili iko wazi kabisa, ambapo wanaitwa Khuntha. Neno khunthā kilugha linamaanisha "mara mbili" au "maradufu." Neno hilo hutumika kwa mtoto aliyezaliwa na viungo vya uzazi vya mwanaume na mwanamke au mwenye viungo vya uzazi visivyoeleweka. Maneno watu waliohasiwa (eunuch) na wenye sehemu mbili za uzazi (hermaphrodite) yanaepukwa hapa, kwani yanaweza kumaanisha vitu tofauti. Neno khunthā litatumika kuleta maana.

Mwenyezi Mungu (swt) asema,

[وَلَيْسَ الذَّكَرُ كَالْأُنثَىٰ]

“Na mwanamume si sawa na mwanamke.” [Surah Aali Imran 3:36]. Katika Uislamu, kiasili kuna jinsia mbili. Jinsia hizi mbili huamuliwa na mazingatio ya kibaolojia pekee. Jinsia haiamuliwi na uamuzi wa mtu binafsi au mtazamo wa kibinafsi. Jinsia isiyoeleweka inaamuliwa na wataalamu, kama moja ya jinsia mbili.

Neno ‘khuntha’ linatumika kwa mtu ambaye hawezi kutambulika kwa urahisi, kama mwanamume au mwanamke, kwa mazingatio ya kibaolojia. Ni mwanadamu ambaye ana viungo vya kiume na vya kike, au yule ambaye hana chochote. Katika Uislamu, mtaalamu anakabidhi jinsia isiyoeleweka kuwa moja ya jinsia mbili, mwanamume au mwanamke, baada ya kutafiti uhalisia wa kibaolojia. Mwanafaqihi wa kale Ibn Qudamah alisema katika kitabu chake Al-Mughni, kuhusiana na sehemu ya siri isiyoeleweka, “Haitengwi kutokana na kuwa mwanamume au mwanamke. Amesema Mwenyezi Mungu (swt):

[وَأَنَّهُ خَلَقَ الزَّوْجَيْنِ الذَّكَرَ وَالأُنْثَى]

“Na kwamba Yeye ndiye aliye umba jozi, dume na jike” [Surah An-Najm 53:45]. Na Yeye (swt) amesema,

[وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالا كَثِيرًا وَنِسَاءً]

“Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi.” [Surah An-Nisaa 4:1] na hivyo hakuna maumbile ya tatu.”

Kwa hivyo, Uislamu haujaweka jinsia ya tatu. Daktari Muislamu anayeaminika ambaye ni mtaalamu wa masuala ya ulemavu wa uzazi, viungo vya kijinsia, maumbile na tabia ya kijinsia, anathibitisha jinsia. Kwa hivyo yeye, kwa umakini na kwa usikivu, anachunguza kwa undani tabia za kibaolojia, za viungo, vya mwili, kwanza, ili kuona ni nini kinachozidi, cha sifa za kiume au za kike. Yeye huchunguza mambo ya kimwili, kama vile sehemu za siri, na sehemu ya siri ya kukojolea, na pia kuzingatia kromosomu za kijinsia za X na Y, zinazounda jinsia. Ikiwa, katika hali nadra sana, kwamba sifa za anatomiki na za kijeni pekee hazitatui utata huu, suala la baolojia ya mwanamume na mwanamke, mivutio na hamu ya kijinsia pia huzingatiwa, kabla ya kuamua jinsia. Baada ya hapo, hukmu za Kiislamu hutekelezwa kulingana na jinsia iliyoamuliwa, ikiwemo ndoa, dori za kijinsia na wajibu.

Uchunguzi wa mapema wa kimatibabu, kwa ombi la wazazi, au wakati kitambulisho cha kitaifa kinatolewa, unaweza kusaidia kutatua masuala magumu kwa kiwango kikubwa. Kwa hivyo, khuntha kisha hupewa hadhi ya kiume au ya kike.

Mambo hayo yanajulikana sana ndani ya Fiqh, ikiwemo Fiqh ya Hanafi, yenye rai na msimamo uliochukuliwa na Imam Abu Hanīfah, Imam Muḥammad ash-Shabaani na Imam Abu Yusuf. Sheria hizi za kina zina ukusanyaji mrefu katika vitabu vya Fiqh kwa karne nyingi na zilitabikishwa katika kote katika ardhi za Kiislamu kwa usahihi.

Kwa hivyo, mifano iliyotajwa hapo juu inaweka wazi kwamba Uislamu umetupa mkusanyiko wa kina wa hukmu na sheria kuhusu kila suala la jamii ya wanadamu. Mwenyezi Mungu (swt) ndiye Muumba wetu na ni nani mbora wa kutujua sisi zaidi Yake? Sheria zake ni adilifu, za haki, na zinaafikiana na umbile la mwanadamu. Ni balaa kabisa kuamini kwamba Shariah imenyamazia kimya juu ya baadhi ya masuala, hivyo basi wanadamu wanapaswa kujitengenezea sheria zao wenyewe. Akili ya mwanadamu ina kikomo katika ufahamu wake, kwa kuwa sisi sote tunajua mapungufu na kutokamilika kwetu. Pia, wanadamu wote wana uelewa wao wenyewe wa masuala, chini ya ushawishi wa mkusanyiko wao wenyewe wa imani sahihi au za makosa, malezi na ushawishi wa kijamii, ambayo kwayo kuna migongano mingi ndani ya sheria hizi, yenye kusababisha mkusanyiko mpya wa matatizo.

Jinsia si Haiamuliwi kwa Mtazamo wa Kibinafsi Pekee, katika Uislamu

Ufafanuzi wa watu waliobadili jinsia kama wale wanaozaliwa wakiwa wanaume wanaojiona au kujihisi kuwa ni wanawake, au kinyume chake hauna nafasi katika Shariah. Watu kama hao watachukuliwa kuwa wagonjwa wa akili au wagonjwa wa kisaikolojia. Wanahitaji matibabu ya haraka. Ikiwa si wagonjwa, wanaweza kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Hii ni ikiwa watatangazwa kuwa sawa kiakili, lakini wakasisitiza juu ya tabia mbaya kama hiyo. Kwa hivyo, ili kufafanua mkanganyiko huu ulioundwa na Magharibi, ni bora kuachana na istilahi zao na kushikamana na istilahi ya Shariah ya Khuntha kama ilivyoelezewa hapo juu.

Kufeli kwa Katiba ya Sasa ya Kuulinda Uislamu

Sasa tunakuja kwenye swali, je sheria inayozungumziwa au katiba ya Pakistan inaweza kulinda haki za Khuntha? Tunapoisoma katiba inadhihirika wazi kabisa kuwa sio katiba ya Kiislamu. Taarifa zenye dosari kwa jina la vifungu vya Kiislamu zimeongezwa kwa katiba ya wakoloni kikamilifu, kwa kuzingatia Sheria ya Serikali ya India, ya 1935.

Sheria hii ilibadilisha sura na awamu kama katiba ya 1956, 1962 na kisha 1973, ambapo marekebisho makubwa 26 yamefanywa hadi sasa. Vifungu vinavyoitwa vya Kiislamu si chochote ila ni ghilba na utapeli ili kulinda msingi wa kisekula na huria wa katiba hiyo.

Kwa mfano, zingatia kifungu kwamba “ubwana juu ya ulimwengu mzima ni wa Mwenyezi Mungu peke yake na mamlaka hutekelezwa na watu wa Pakistan ndani ya mipaka aliyoiweka ni amana takatifu.” Inatoa uwezo thabiti wa kutunga sheria kwa watu wa Pakistan kupitia wawakilishi wao, huku ikisema kwa uwazi kwamba ubwana ni wa Mwenyezi Mungu pekee. Kwa hivyo, utata ulio wazi katika kifungu hiki pekee ni dhahiri. Badala ya kusema kwamba chanzo cha sheria zote kitakuwa ni Qur'an Tukufu, Sunnah za Mtume, Ijma us-Sahaba na Qiyas, kifungu hiki kinaifanya akili ya mwanadamu kuwa chanzo cha sheria.

Inaendelea zaidi kusema kwamba hii ni amana takatifu na inapaswa kuwa ndani ya mipaka iliyowekwa na Mwenyezi Mungu (swt). Chini ya kifungu hiki inachukuliwa kuwa Shariah inatoa kanuni pana pekee, wakati mengine yameachiwa wanadamu kuamua. Kwa hivyo, Zakah inachukuliwa kuwa ni wajibu na riba inachukuliwa kuwa ni haramu, hata hivyo, mfumo uliosalia wa kiuchumi kama sarafu, hukmu za ardhi, muundo wa kampuni, umiliki wa mali za umma, hazina za serikali, kodi na ushuru wa forodha zinakuwa uwanja wa fikra za wanadamu. Aidha, serikali hailazimishi ulipaji Zaka. Ama kuhusu riba, imeenea, huku hali dhidi yake ikigeuzwa huku na huko, kwa miongo kadhaa.

Hivyo basi, wabunge wanaoketi katika mabunge hutunga sheria kuhusu masuala haya kulingana na matamanio na matakwa yao. Wanatabanni kutoka kwa ubepari au mifumo mingine ya ulimwengu, bila kujali ukweli kwamba tuna sheria za Kiislamu za kina kuhusu kila nyanja ya kiuchumi, kijamii, mahakama, mifumo ya utawala na elimu na sera za kigeni.

Inashangaza kuona kwamba wanazuoni mbalimbali mashuhuri wa Kiislamu walikuwa sehemu ya kuandaa katiba hii ya 1973. Hata hivyo kwa makusudi au kwa kutokusudia walipuuza sheria ya Kiislamu ya kina na Fiqh zilizoko katika maelfu ya vitabu na kutabikishwa hadi 1918. Ni dhahiri kwamba ibara hizi za Kiislamu zilikuwa zimeongezwa hivi punde ili kuwatuliza umma walio wengi ambao walikuwa wanaitisha utabikishaji wa Nidham ul-Mustafa na hukmu za Shariah. Watunzi na watangazaji walijua vyema kwamba hii si katiba ya Kiislamu na Uislamu hautabikishwa na kamwe hauwezi kutabikishwa chini yake. Kwa hiyo waliongeza vifungu ambavyo utabikishwaji wa hatua kwa hatua wa Uislamu ulisawiriwa kama lengo la dola ya Pakistan.

Kwa hiyo, chini ya kifungu cha 227, imeelezwa, “Sheria zote zilizopo zitaletwa kwa kuendana na Maagizo ya Uislamu kama yalivyobainishwa katika Quran Tukufu na Sunnah, katika Sehemu hii inayojulikana kama Maagizo ya Uislamu, na hakuna sheria itakayotungwa ambayo inagongana na Maagizo hayo.” Hili lilitekelezwa kupitia Baraza la Mfumo wa Kiislamu na mahakama ya Shariah ya Shirikisho. Hili linabainisha tena kwamba nia haikuwa kutabikisha sheria ya Kiislamu kwa njia kamilifu na pana kuanzia siku ya kwanza. Badala yake ilikuwa ni kuuhadaa umma kwa jina la Uislamu.

Mahakama ya Shariah ya Shirikisho ambayo iliundwa kuleta sheria za nchi kuendana na maamrisho ya Qur'an na Sunnah, haina mamlaka makuu. Hukmu na maagizo yake yanaweza kupingwa katika benchi la Rufaa ya Shariah la Mahakama ya Upeo, ambayo huamua kesi kulingana na katiba ya kisekula ya Pakistan. Katiba ya kisekula huamua kwamba haki za watu ziko chini ya ufafanuzi wa wanasheria wa Kimagharibi, maadili ya kisekula ya uhuru na haki za binadamu. Sheria za Kiislamu zimesalia hoi mbele ya matakwa ya wajumbe wa Bunge la Kitaifa na Baraza la Seneti, pamoja na Rais wa Pakistan. Shariah sio kanuni kuu nchini Pakistan kwani utawala ndio mamlaka kuu. Wana mamlaka ya kupitisha sheria yoyote ya Kiislamu katika mfumo wa mswada bungeni kwa idadi ya kura nyingi. Wanaweza kufuta sheria yoyote kwa 51% ya idadi ya wengi au hata kurekebisha katiba kwa theluthi mbili ya wengi. Kwa hivyo haki za Kiislamu za kundi lolote la watu zinawezaje kulindwa nchini Pakistan?

Kinyume chake, Uislamu unatoa haki za kupata mahitaji ya kimsingi kama vile chakula, malazi, mavazi, huduma ya afya na elimu kwa watu wote bila kujali dini zao, tabaka, itikadi, jinsia au kabila. Zaidi ya hayo, Uislamu unailazimisha serikali kumpa kila raia. Haki hizi zilitimizwa tangu mwanzo wa utawala wa Kiislamu chini ya Mtume Muhammad (saw), hadi mwisho wa Khilafah ya Uthmani. Nchini Pakistan, hata hivyo, chini ya katiba ya kibepari serikali inadai kutoa huduma hizi, lakini imeshindwa kufanya hivyo kwa zaidi ya miongo saba.

Sheria hii haitalinda haki za mtu yeyote, kwani serikali inaongozwa na mfumo na katiba ya kibepari. Marekebisho haya katika Sheria ya Wanaobadili jinsia yanaweza kubatilishwa na Mahakama ya Upeo chini ya katiba ya Pakistan. Hata kama uamuzi wa Mahakama ya Sharia utaidhinishwa na Mahakama ya Upeo, bunge linaweza kupitisha sheria mpya kulingana na matamanio na matakwa ya wabunge. Shariah imewekwa kupigiwa kura mbele ya wanadamu. Haina thamani yoyote nchini Pakistan.

Ili haki za watu wa Pakistan, bila kujali jinsia, tabaka, imani, kabila au dini zao zilindwe, kuna njia moja pekee ambayo ni kufutwa kabisa katiba na mfumo wa sasa, na utabikishaji wa sheria za Kiislamu kwa ukamilifu upana chini ya mfumo wa utawala wa Khilafah.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Irum Noreen

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoAlhamisi, 22 Juni 2023 19:21

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu