Jumatano, 22 Rajab 1446 | 2025/01/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Mafunzo kwa Ummah Wakati Chama cha Kikomunisti cha China Kikitimiza Miaka 100

(Imetafsiriwa)

Ni vigumu kupita siku bila ya kuwepo habari kutoka China, ima itakuwa ni katika GDP yake, meli za kubebea ndege, akili bandia, mabwawa yake ya umeme, reli za kasi au miji ya kifahari. Hakuna ubishi kuwa China inanyakua vichwa vingi vya habari. Mnamo Julai 2021, chama pekee cha China – Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) kilisherehekea miaka mia moja. Kuna vyama vichache sana duniani vinavyoweza kudai vimedumu kwa miaka mia moja, lakini CCP kimejitokeza kuwaonyesha watu wake kuwa utumishi wake kwa China umekifanya kuwa ni kiongozi pekee halali wa nchi. Kwa maeneo yaliobaki ya dunia, China inajaribu kujionyesha kuwa ni nguvu inayoibuka inayohitaji kuheshimiwa. China imepitia kutoka kuwa nchi ilioathiriwa na umasikini katika kipindi cha miongo minne tu iliopita na kuwa nchi ya kibabe ya kiviwanda inayounda bidhaa nyingi sana zinazotumika duniani. China ikiwa inawakilisha mfano wa taifa ambalo limeendelea katika kipindi hichi cha maisha yetu, je mafunzo gani ambayo ulimwengu wa Kiislamu unajifunza katika safari ya nchi ya China, na je inatuonyesha kuwa ni kigezo tunachoweza kukifuata?

Jamhuri ya Watu wa China (PRC) ilianzishwa na Wakomunisti walioongozwa na Mao Zedong mnamo 1948. Historia ya China hadi wakati huo ilikuwa ni sawa na Ulimwengu wa Kiislamu hivi leo. China ilipitia karne ya udhalilifu kutokea 1839 wakati Uingereza ilipoigeuza kuwa pwani yake ili kupata fursa za biashara ambapo baadaye kugeukia kuzitawala bandari za China. Hivi ndivyo namna Uingereza ilivyoitawala Hong Kong hadi 1997. Baada ya Uingereza kufika, Ufaransa, Amerika, Urusi, Ubelgiji na Uholanzi zote zilianza kuchukuwa maeneo ya China, kama ulimwengu wa Kiislamu ulivyopitia katika karne za 18 na 19. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, mambo yalibadilika. Wachina walijihisi kuwa ni taifa kubwa duniani la kihistoria ambalo uwezo wake ulichukuliwa na ukoloni wa Kimagharibi. Udhalilifu ulistahiki umalizike! Njia pekee ya kusonga mbele ni kuwafukuza wakoloni, kuondoa uingiliaji wa kigeni na kuhakikisha Wachina wanaiendesha China. Hichi ndio Mao na Wakomunisti walichokifanya, wakitambua kuwa hakuna uhuru kwa kushirikiana au kufanya kazi na taifa lolote la kikoloni.

Ulimwengu wa Kiislamu umekuwa vile vile ukipitia karne ya udhalilifu. Miongoni mwa watawala wa Waislamu, wakoloni waliona watu wa maslahi na vikaragosi wanaoweza kufanya chochote kubakisha falme zao. Mabwana zao wakoloni wanaendelea kuwadhalilisha, lakini wanafanya kila jitihada kuhifadhi maslahi ya mabwana zao wakifikiri kuwa hiyo itahifadhi utawala wao. Matokeo yake, na ambapo ni tafauti na China hivi leo, ulimwengu wa Kiislamu umekuwa eneo mwanana kwa njama za wageni kwa sababu watawala wa Waislamu ni mlango ambao mataifa ya kikoloni hutumia kuingilia kwenye ardhi zetu.

Mipango ya Muda Mrefu

Wakati CCP iliposhika hatamu, walirithi taifa ambalo lilikuwa nyuma kabisa ya mataifa mengine yenye nguvu duniani. Hawakuwa na maendeleo ya kisasa ya kiviwanda na wakihangaika hata katika kuwalisha watu wake wenyewe. Mao na wandani wenzake walifahamu kuwa walihitaji kubadilisha hali hii na kuweka mipango ya muda mrefu ya maendeleo ya China. Kumbuka kuwa wakati huo China ilishakuwa na idadi kubwa zaidi ya watu duniani.  

CCP ilijaribu kuiendeleza China chini ya misingi ya uchumi wa kikomunisti, na hii ilipelekea kuwa na matatizo makubwa. Mao Zedong alipofariki mnamo 1975, China ilibaki kuwa nchi masikini; matumaini yake ya kuwa na maendeleo kiviwanda bado yakiitatiza, na watu wake bado ikawa hawawezi kujilisha wenyewe. CCP ilitambua kuwa ukomunisti ulikuwa umefeli na wakaachana nao, na pia wakaacha kuulingania duniani. Utawala mpya wa CCP ukiongozwa na Deng Xiaoping ulimalizia kwa China kukosa utaalamu, teknolojia na ujuzi wa mbinu za utekelezaji katika kushindana na mataifa mengi ya dunia yalio na usemi.

Mabingwa wa CCP walikuja na mpango wa kuifanya China kuwa mahala rahisi kwa makampuni ya kigeni kutengenezea bidhaa zao. Kwa kuwa China imekuwa na idadi kubwa zaidi ya watu, ikawa na idadi ya kutosha ya wafanya kazi. Nchi ikawa na mpango mpana wa maendeleo katika miundombinu kuyashawishi makampuni ya kigeni kuhamisha uundaji wao wa bidhaa hadi China. Miundombinu hii iliunganisha sehemu kubwa ya nchi kwa barabara, mikondo na bandari, na ikaweka mitambo ya kuzalisha umeme na mifumo ya mawasiliano ili China mpya ya kiviwanda ifanyike kwa ufanisi na kufungua biashara za kimataifa. Mwaka 1979 China ilikuwa na maili 33,000 tu ya njia za reli; hadi 2016 ilipindukia maili 100,000 – mtandao mrefu zaidi wa reli duniani. Zaidi ya asilimia 80 ya watu wa China waliishi katika maeneo ya vijijini mwaka 1979. Hivi leo ni asilimia 50 tu wanaishi vijijini. CCP imeunda miji na majiji kwa mamia ya milioni ya raia wake katika kipindi cha miongo michache tu.

Lakini CCP haikutaka China kuwa ni mahala pa viwanda kwa Wamagharibi tu. ilitaka kutumia teknolojia ya kigeni, ujuzi na utaalamu ili iweze kujitegemea kwa kipindi cha mbeleni. China iliunda Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ) yakiwa na unafuu mpana wa kodi kwa makampuni ya kigeni kuelekeza viwanda vyao China na kutumia fursa ya wafanyakazi wa malipo ya chini. Wale wanaoingiza teknolojia mpya na ya kisasa waliamiliwa kwa ubora zaidi, ikiwemo viwango vya chini zaidi vya kodi. Mkakati huu uliiwezesha China kukabiliana na nchi za Magharibi katika maeneo kama ya akili bandia (artificial intelligence) na maendeleo ya viwango vya juu katika kompyuta. Kwa hivyo China imetekeleza mpango wa muda mrefu wa kujenga miundombinu ambayo ni njia ya mataifa mfano, kama Japan na Ujerumani, na pia ilitekeleza na kuhakikisha kuwa ‘utaalamu na ufundi’ vimesafirishwa nchini ambao hivi sasa inautumia na kuweza kujitegemea na kuvumbua.

Licha ya kumiliki baadhi ya rasilimali muhimu za dunia, hakuna mkakati kama huo wa muda mrefu uliopo katika ulimwengu wa Kiislamu, bali imefuatwa miradi ya kiuchumi ya muda mfupi au mikakati iliozaliwa ugenini ikitekelezwa chini ya kisingizio cha soko huru na biashara huru. Mataifa ya Mashariki ya Kati, ambayo yana rasilimali nyingi ya nishati, hayakuzitumia hizi kujenga nchi ya miundombinu ya kisanaa (mbali ya maduka makubwa na hoteli) au kupatia teknolojia za kisasa. Saudi Arabia ingeweza kununa teknolojia na utaalamu na kutumia kizazi kimoja tu kuhakikisha kuwa hizi zinasomwa na kutumiwa na watu wake wa ndani, lakini familia ya Kisaudi inashughulishwa zaidi na kudhibiti ufalme wake na kuuwekeza utajiri wa Ummah katika masoko ya fedha ya Magharibi na kuyadhamini mashirika ya Kimagharibi.

Matatizo ya Kijamii Yapo Mbeleni

Wakati kuna mambo ya kuchukua kutoka njia ya China kuelekea kwenye maendeleo, kuna pia mafunzo tunayoweza kujifunza yanayoonyesha ukomo wa maendeleo ya China na vitu tunavyopaswa kuvikwepa.

Mageuzi nchini China yamesukumwa na nadharia ya vitendo na yamechukuliwa pole pole kuongoza mabadiliko. China hivi leo ina uchumi wenye mambo mengi ya kibepari, lakini CCP imechukuwa kile kinachofanya kazi kwa ajili ya nchi kuliko kuangalia upande wa kuwa ni nchi ya kimfumo. Mfumo wa siasa wa China una chama kimoja tu cha siasa – CCP. China inatumia utaifa na historia kuiunganisha nchi na katika sera zake za kigeni China haipiganii maadili yoyote; inahitaji kushughulikia masuala ya kiuchumi, uwekezaji na masoko. Ukosefu huu wa mfumo umeleta matatizo kadhaa kwa China.

Hong Kong na Taiwan ni maeneo mawili ambayo China inayaangalia kama yalioasi, lakini baada ya jitihada za miongo kadhaa, imeshindwa kuyaunganisha kwenye maadili ya China bara. Hong Kong ilitawaliwa na Uingereza kwa miaka 150 hadi 1997 na katika kipindi hichi, Uingereza ilibuni taasisi na maadili ya Kimagharibi. Uingereza ilipoondoka, wakaazi milioni sita wa kisiwa hichi hawakujiona na hawajioni kuwa Wachina wa Han bali ni wa-Hong Kong. Licha ya kuitawala Hong Kong hivi sasa kwa takriban miaka 25, China bado haijakaribia kuwavutia watu wa Hong Kong, wanaobishana na Beijing wazi wazi hivi sasa na wanajiona wao kama ni Wamagharibi kuliko Wachina wa Han. China inakabiliana na tatizo kama hilo Taiwan ambapo imeshindwa kuwashawishi wakaazi wake, licha ya kumimina fedha, vitega uchumi na kuzalisha kazi kwa kisiwa hichi kilicho asi. Yote haya ni kwa sababu China haina mfumo wala maadili kwa watu hawa katika kuukumbatia muungano na China bara. China imekumbatia vipande vya Ukomunisti na vipande vya Ubepari; na utaifa ambao haukusaidia kuliunganisha tena eneo lolote kati ya hayo. Hali ya kiuchumi ya Taiwan na Hong Kong haitoiruhusu China kuwavutia watu huko. Kukosa maadili ya uunganishaji imepelekea njia ya utumiaji nguvu kuudhibiti utawala wa zaidi ya Waislamu milioni 25 wa Xinjiang. China imegundua kuwa uchumi, miundo mbinu na teknolojia havitoshinda hapa.

Kukosekana huku kwa mfumo kumepelekea kuibuka kwa idadi kadhaa ya matatizo ambayo China inajaribu kuyatatua. Kuongezeka kwa utajiri kumepelekea kukua kwa GDP mara 86 tokea 1979. Takwimu zinaonyesha kuwa China imemaliza umasikini – kama inavyoelezwa hakuna katika watu wake anayeishi kwa chini ya dolari 1.90 kwa siku. Lakini wengi ya Wachina wanaishi kwa chini ya dolari 5 kwa siku ambacho ni kiwango kizuri kuliko kuwa katika umasikini. Wakati ikiwa katika utajiri mkubwa zaidi, ukosefu wake wa mfumo maana yake haikuweza kusambaza utajiri huu katika namna yoyote iliyo ya usawa.

Maendeleo ya China pia yamesababisha masuala nyeti ya kijamii. Chuo cha Sayansi ya Jamii cha China kimekisia malalamiko ya ummah kwa mwaka yanazidi 180,000.  Idadi kubwa ya watu duniani inasikia kichache cha yale yanayotokea China kutokana na udhibiti mkali uliowekwa na CCP juu ya kufikiwa taarifa maeneo mengine duniani. China kwa miaka mingi ilijaribu kuziweka pamoja tamaduni pana na taifa lenye watu wa makabila mengi licha ya vipindi vya uwekaji wa uongozi sehemu moja na mgawanyiko wa sehemu sehemu. Lakini tafauti ya tamaduni na lugha imeharibu mambo kutokana na ukuaji usio sawa na ugawanyaji mbovu wa utajiri. Utumiaji mbaya wa nguvu, vifungo, sheria za kizembe za kazi na malipo ya kitapeli na ukweli wa kuwa serikali ya China kuonekana kutoshughulikia mahitaji ya kiuchumi ya idadi kubwa sana ya watu, yote hayo yanasababisha masuala ya mshikamano wa ndani. Uchumi wa China umejengwa juu ya wafanyakazi zaidi ya bilioni moja kutumikia makada milioni 200 wa Chama cha Kikomunisti. Wafanyakazi hawa wanapokea malipo madogo kuliko wafanyakazi katika Afrika na Mexico na wamekuwa ndio kichocheo halisi cha muujiza wa kiuchumi wa China. Wafanyakazi hawa wamekuwa ndio wanaoviweka viwanda vya China kuendelea kufanyakazi kwa masaa 24 kwa siku. CCP ina tatizo halisi la kuunganisha ukuaji wa uchumi na ustawi wa kijamii na hii baada ya kipindi kirefu itapelekea kuondoka kwa utulivu. 

Ripoti ya Wizara ya Elimu ya mwaka 2018 imethibitisha kufungwa kwa shule zaidi ya 13,000 za msingi nchini kote kutoka 2021. Wizara imeliangalia suala hili na mgeuko wa haraka wa taswira ya kidemografia katika kuelezea kufungwa huku kulikoenea kote. Imethibitisha kuwa baina ya 2002 na 2012, idadi ya wanafunzi walioandikishwa shule za msingi imepungua kwa takriban asilimia 20. Sera ya Mtoto Mmoja ambayo China imeifuata kwa kipindi kirefu imeleta uzani usio wa sawa katika idadi yake ya watu huku nguvu kazi yake ikianza kupungua wakati CCP ikihitaji nguvu kazi ya kubeba uzalishaji katika China na kuubakisha uchumi kuendelea kukua. Mabadiliko yalioshuhudiwa karibuni katika sera ya mtoto yamelenga kugeuza muelekeo huu.

Kukosekana kwa mfumo pia kuna maanisha China inacho kidogo tu cha kutoa kwa ulimwengu zaidi ya msingi wa bidhaa rahisi. Huku mpangilio wa (biashara) huria ukihangaika kubakia hai. Wakati utawala wa Wamagharibi wa dunia ukiwa katika muanguko, China ilipaswa kutoa mbadala lakini kukosa kwake mfumo itaondoka mikono mitupu. Hata utamaduni wa Kichina sio wa kuilimwengu; ni wa watu wa China pekee.

Changamoto hizi inazozikabili China haziko tafauti na masuala mengi yaliyopo katika ulimwengu wa Kiislamu. Kukosa kwake mfumo maana yake China haitoweza kushughulikia kwa namna muwafaka matatizo na haitoweza kutatua matatizo bila kuleta matatizo zaidi kwengineko. Wakati China inaweza kupata nafasi kubwa ya kuenea kwa habari zake duniani, inacho kichache tu cha kuonyesha kinachoweza kuigwa. Maendeleo ya China ni ya kipekee kwa uhalisia maalum, na imekuwa na maendeleo ya kiuchumi kwa gharama ya ugawaji wa utajiri na katika kutoa mazingira ya ndani ambayo hayatokubalika kwa wengi. Ummah wa Kiislamu unao Uislamu ambao sio tu unaunganisha watu lakini unatoa muundo wa kuuendesha uchumi na pia muundo wa kuisimamia jamii, na kuwaunganisha watu tafauti. Kile ambacho tunaweza kujifunza kutoka China ni kuwa hakuna mustakbali katika kuyachukua maadili ya Wamagharibi au kujioanisha katika mfumo wa kiulimwengu uliobuniwa na Wamagharibi. Hata hivyo, kuondoa ushawishi wa kigeni na kuwa huru ni jambo ambalo ulimwengu wa Kiislamu unahitaji kuangalia.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Adnan Khan

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu